Moja kwa moja, Idadi ya vifo kutokana na Ebola yafikia 506 DR Congo

Kufikia tarehe 4 Julai 2026, katika ripoti iliyochapishwa asubuhi ya leo, jumla ya visa 1,561 vilivyothibitishwa vimerekodiwa tangu mlipuko huo utangazwe tarehe 15 Mei.

Muhtasari

Skip Video and continue reading
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Lizzy Masinga & Rashid Abdallah

  1. Moto wa nyika walazimisha watu 10,000 kuhamishwa Ufaransa

    l

    Chanzo cha picha, Reuters

    Moto wa nyikani umelazimisha maelfu ya watu kuhamishwa kusini mwa Ufaransa huku nchi hiyo ikikabiliana na athari za wimbi la joto la kiangazi ambalo limeikumba sehemu kubwa ya Ulaya.

    Zaidi ya watu 10,000 wameamriwa kuondoka katika miji na vijiji zaidi ya kumi na mbili katika vilima vya Pyrenees huko Ufaransa, karibu na mpaka na Uhispania.

    Moto huo, ulioko Trévillach karibu na Perpignan, umeteketeza hekta 4,600 (ekari 11,366), mkuu wa mkoa Pierre Regnault de la Mothe alisema katika chapisho kwenye X.

    "Asubuhi ya leo hali inazidi kuwa mbaya tena," Waziri wa Mambo ya Ndani Laurent ⁠Nunez alionya kwenye kituo cha televisheni cha Ufaransa TF1. "Leo vita vinaendelea tena."

    Mamlaka zimeonya kwamba upepo mkali unachochea moto zaidi.

    Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alitangaza kwamba EU itatuma ndege nne zilizoko Kupro na Sweden kusaidia katika juhudi za dharura.

    Moto huo pia umeathiri nchi jirani ya Uhispania ambapo zaidi ya hekta 2,200 katika hifadhi ya asili ya Les Gavarres zimeharibiwa.

    Kusini mwa Catalonia, katika jimbo la mashariki la Castellon, watu 500 walihamishwa baada ya moto wa porini kuingia katika mbuga ya kitaifa ya Sierra de Espadan.

    Halijoto inaweza kufikia tena nyuzi joto 40C kusini-magharibi mwa Ufaransa wiki hii na tayari imezidi nyuzi joto 40C katika sehemu za Ureno na Uhispania.

    Wakati wa wimbi la joto lililovunja rekodi la Juni, halijoto ya nyuzi joto 42C katika baadhi ya maeneo, Ufaransa ilishuhudia siku yenye joto kali zaidi kuwahi kutokea kote nchini tarehe 24 Juni.

    Angalau vifo 2,025 vilirekodiwa nchini Ufaransa, 1,222 nchini Ubelgiji na takriban 480 nchini Uholanzi wakati wa wimbi la joto.

    Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza halijoto duniani kote - lakini hasa barani Ulaya. Hii inasababisha kuongezeka joto la kiangazi na moto mkali wa nyikani.

    Pia unaeza kusoma:

  2. Ghasia katika gereza zauwa 26 na zaidi ya 100 wajeruhiwa

    [

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ghasia katika gereza moja magharibi mwa Sri Lanka zimewaua watu 26, saba kati yao wakiwa walinzi, na kujeruhi zaidi ya 100.

    Siku mbili za vurugu katika Gereza la Negombo, katika mji wa pwani kaskazini mwa Colombo, zilianza na mapigano kati ya makundi mawili ya wafungwa.

    Wafungwa wanadaiwa kuchukua bunduki za walinzi siku ya Jumapili. Watu wawili waliuawa siku hiyo, huku makumi wakijeruhiwa. Baadaye, makundi ya wafungwa wanaume, na wanawake kutoka jengo lililo karibu, walipanda juu ya paa za gereza wakidai waachiliwe.

    Vurugu mpya zilizuka Jumatatu wakati wafungwa walipojaribu kuvamia malango ya gereza. Vikosi vya usalama vilitumwa na milio mingi ya risasi ilisikika kutoka ndani ya gereza.

    Vurugu hizo ziliripotiwa kuchochewa na mzozo kuhusu mfungwa mmoja aliyetoa taarifa kuhusu operesheni ya ulanguzi wa dawa za kulevya ndani ya gereza.

    Jumla ya maafisa 23 wa magereza, na wafungwa 54, bado wanapokea matibabu, wanasema maafisa.

    Baadhi ya waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Negombo. Mkurugenzi wa hospitali aliambia shirika la habari la AFP kwamba baadhi yao wana majeraha ya risasi, huku wengine wakipata majeraha na michubuko mikubwa. Wengine walisafirishwa hadi Hospitali ya Kitaifa ya Colombo.

    Polisi wanasema sehemu ya paa la gereza ilianguka na kuwajeruhi baadhi ya wanawake waliohusika, AFP iliripoti.

    Umati wa jamaa wa wafungwa ulikusanyika nje Jumatatu wakati vurugu zikiendele. Baadhi waliiambia BBC Sinhala kwamba hawakupewa taarifa kuhusu mahali walipo jamaa zao, au ni nani alikuwa hai na ni nani aliyefariki

    Maeneo ndani ya gereza bado yanasafishwa, na jeshi limewekwa katika hali ya kusubiri baada ya polisi kuomba msaada, shirika la habari la Reuters liliripoti.

    Msemaji wa vyombo vya habari wa kamishna wa magereza AC Gajanayake alisema hatua zimechukuliwa kuwahamisha wafungwa kwenda magereza mengine.

    Waziri wa Sheria na Magereza Harshana Nanayakkara ameagiza mamlaka kuchunguza na kuwasilisha ripoti.

    Ghasia huzuka mara kwa mara katika magereza yaliyojaa watu, Desemba 2020, watu 11 waliuawa katika gereza moja, huku 117 wakijeruhiwa.

    Magereza ya Sri Lanka yalikuwa na wafungwa 41,250 kufikia Jumapili, ambayo ni mara nne ya uwezo wao, kulingana na AFP.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Uefa yaikosoa Fifa baada ya Trump kuingilia kati kadi nyekundu

    p

    Chanzo cha picha, Gettty Images

    Maelezo ya picha, Gianni Infantino ni rais wa Fifa tangu 2016

    Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa) imekosoa vikali uamuzi wa kushangaza wa Fifa wa kutounga mkono kadi nyekundu dhidi ya mchezaji Folarin Balogun katika Kombe hili la Dunia, na kusema "haujawahi kutokea, haueleweki na haukubaliki."

    Mshambuliaji wa Marekani Balogun, ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu wakati wa mechi dhidi ya Bosnia-Herzegovina, alipaswa kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi ya raundi ya 16 dhidi ya Ubelgiji itakayochezwa siku ya Jumanne.

    Lakini waandaaji wa Kombe la Dunia, Fifa, ambao ni shirikisho linaloongoza soka duniani, walichagua kutotekeleza adhabu hiyo kwa mchezaji huyo wa miaka 25, ikimaanisha kuwa mfungaji bora wa timu hiyo atacheza mechi ijayo.

    Uefa, shirikisho linaloongoza soka barani Ulaya, limesema kuingilia kati ili kufuta kadi nyekundu katika mashindano hayo ni "kuvuka mstari mwekundu".

    Kati ya kadi 188 nyekundu zilizotolewa tangu kuanzishwa kwa Kombe la Dunia, ni mchezaji mmoja tu aliyeondolewa adhabu hiyo.

    Ni Garrincha ya Brazili mwaka 1962, ambapo kulikuwa na tuhuma za kuingiliwa kisiasa.

    CBS News imethibitisha kwamba kurejea kwa Balogun kunakuja baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kumpigia simu rais wa Fifa, Gianni Infantino siku ya Alhamisi na kuzungumza naye kuhusu kadi nyekundu hiyo.

    Rais Donald Trump amethibitisha kuwa aliiomba Fifa kupitia upya adhabu ya kadi nyekundu dhidi ya mshambuliaji wa Marekani Folarin Balogun ya kutocheza mechi moja katika Kombe la Dunia.

    Trump anasema shirikisho linaloongoza soka duniani "limefanya uamuzi sahihi" wa kusimamisha marufuku dhidi ya Balogun, akiongeza kuwa ingeacha "doa kubwa" kwenye mashindano hayo kama ingetekelezwa.

    Balogun, ambaye ndiye mfungaji bora wa nchi yake katika mashindano ya sasa, alitarajiwa kusimamishwa kwa mechi ya 16 bora dhidi ya Ubelgiji huko Seattle Jumanne.

    Akizungumza katika Ikulu ya White House Jumatatu, Trump alisema aliiomba Fifa kupitia upya uamuzi huo kwa sababu "hafikiri kufanya aifanya kosa".

    Trump amethibitisha alizungumza na rais wa Fifa Gianni Infantino, lakini akasema "alichofanya" ni kuomba mapitio na akaongeza kwamba hakumwambia Mswisi huyo kwamba analazimika kusimamisha marufuku ya Balogun.

    Siku ya Jumapili, Rais Trump aliishukuru Fifa kwa kuondoa kadi nyekundu kwa mchezaji huyo.

    Chama cha Soka cha Ubelgiji (RBFA) kilisema katika taarifa Jumatatu kwamba "hakina njia nyingine ila kupinga uhalali wa mchezaji huyo katika mechi ijayo".

    Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Maxime Prevot alisema: "Ikiwa simu ndiyo sababu ya uamuzi huu usioeleweka, itakuwa ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za mpira wa miguu."

    Rais wa zamani wa Fifa Sepp Blatter, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Infantino mwaka 2016 baada ya kashfa ya ufisadi, amenadika kwenye X kwamba "mpira wa miguu haupaswi kamwe kuwa uwanja wa nguvu za kisiasa".

    Uefa imesema kusimamishwa kwa mchezaji "sio chaguo la hiari" bali ni "kanuni iliopo katika kanuni".

    “Sheria zisiposimamiwa na wasimamizi, uadilifu wa mchezo uko hatarini na uaminifu wa shindano hudhoofishwa," Uefa imesema katika taarifa.

    "Tunaeleza mashaka yetu kwa uamuzi huo ambao haujawahi kutokea, usioeleweka na usio na msingi."

    Glenn Micallef, kamishna wa michezo wa Umoja wa Ulaya, amesema maamuzi kuhusu michezo "ni ya mashirika ya michezo, si ya wanasiasa".

    Uefa na Fifa zimekuwa zikizozana kuhusu maamuzi kadhaa katika miezi ya hivi karibuni.

    Baada ya Omar Artan kukataliwa kuingia Marekani kuchezesha Kombe la Dunia, Uefa ilimwalika Msomali huyo kuchezesha Kombe la Super Cup kati ya Paris St-Germain na Aston Villa Agosti 12.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Afrika Kusini kuchunguza mauaji ya raia wawili wa Nigeria

    mmm

    Chanzo cha picha, Sahara Reporters

    Idara ya polisi ya Afrika Kusini, Kurugenzi Huru ya Upelelezi wa Polisi (IPID) wamethibitisha kuwa wanachunguza kesi dhidi ya maafisa wa polisi huko Pretoria, baada ya mauaji ya raia wa Nigeria.

    Ipid inasema malalamiko hayo yalitolewa wiki iliyopita.

    Imeripotiwa kuwa mtu huyo aliuawa wakati wa mabishano na polisi.

    Katika tukio jingine, ambalo pia lilitokea tarehe 28 Juni katika sehemu nyingine ya nchi, polisi wa Mkoa wa Mpumalanga wamethibitisha kesi ya mauaji inachunguzwa baada ya mmiliki wa saluni kuuawa nje ya saluni yake huko Malahleni, zamani Witbank.

    Polisi wanasema mshambuliaji asiyejulikana aliyejihami alimvamia mwanaume huyo kabla ya kumfyatulia risasi kadhaa na kukimbia na gari nyeupe.

    Hakuna mtu aliyekamatwa katika jimbo hili. Sababu ya shambulio hilo haijulikani, polisi wameambia BBC.

    Jeshi la polisi linaomba yeyote mwenye taarifa zinazoweza kupelekea mtu kukamatwa kujitokeza.

    Hakuna taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje nje ya Nigeria kwamba vifo hivyo viwili vinahusishwa na chuki dhidi ya wahamiaji.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Neymar asema safari ya kuitumikia Brazil imefikia ukingoni

    ]

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Neymar amecheza katika mashindano manne ya Kombe la Dunia

    Neymar aliyekuwa akilia amesema safari yake ya kuitumikia Brazil kimataifa "imekwisha" baada ya timu yake kushindwa na Norway katika Kombe la Dunia la 2026.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 aliingia kama mchezaji mbadala dakika ya 67 huku Brazil ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Norway katika mchezo wa raundi ya 16 lakini hakuweza kuzuia Brazil kuondolewa.

    Neymar alifunga penalti ndani ya muda wa ziada katika Uwanja wa MetLife huko New Jersey katika kile kinachotarajiwa kuwa mechi yake ya mwisho kwa nchi yake.

    "Nilijaribu, nilijaribu. Sasa nimefikia mwisho. Nilianza hapa, namalizia hapa," alisema Neymar katika mahojiano na TV Globo baada ya timu yake kuondolewa.

    Neymar alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Brazil katika uwanja huo huo Agosti 2010, alipofunga bao katika ushindi wa 2-0 wa mechi ya kirafiki dhidi ya Marekani.

    Ameendelea kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Brazil akiwa na mabao 80, huku mechi zake 130 akiwa na timu yake ya taifa zikimweka wa pili kwenye orodha ya waliocheza mechi nyingi nyuma ya Cafu aliyecheza mechi 142.

    Neymar hakuwa ameichezea Brazil tangu 2023 huku akikabiliwa na matatizo ya majeraha kabla ya kuchaguliwa katika kikosi cha nchi yake kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2026.

    Ameichezea Brazil katika kombe la dunia kwa mara ya nne, baada ya kuichezea Brazil katika mashindano hayo 2014, 2018 na 2022.

    Pia unaweza kusoma:

  6. China yafanya jaribio la kombora la masafa marefu

    L

    Chanzo cha picha, AA

    China imefanya jaribio la kurusha kombora la masafa marefu kwenye Bahari ya Pasifiki, saa chache baada ya Australia kusaini mkataba mpya wa ulinzi na Fiji.

    Beijing imesema ni "sehemu ya kawaida ya shughuli za kijeshi za kila mwaka za China", lakini jaribio hilo limewakasirisha majirani wakiwemo Japani, New Zealand na Australia.

    Canberra imeishutumu China kwa "kuvuruga" eneo hilo - ingawa maafisa wanasema hawaamini kwamba jaribio hilo ni jibu la makubaliano mapya ya usalama.

    Katika miaka ya hivi karibuni, Australia imekuwa ikijitahidi kuimarisha uhusiano wa ulinzi na majirani zake wa Pasifiki, ili kukabiliana na ushawishi unaoongezeka wa China na upanuzi wa kijeshi katika eneo hilo.

    Waziri wa Ulinzi Richard Marles ameema katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu kwamba Beijing imeifahamisha Canberra kuhusu mipango yake ya kufanya majaribio ya kombora hilo saa chache kabla.

    Marles aliongeza kuwa Australia "ina wasiwasi sana kuhusu vitendo vinavyodhoofisha utulivu, amani, na usalama wa Pasifiki".

    Serikali katika eneo la Indo-Pacific, ikiwa ni pamoja na New Zealand, Japani na Papua New Guinea, ziliarifiwa na maafisa wa China kuhusu nia ya jeshi kufanya mazoezi ya baharini siku ya Jumatatu.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Winston Peters amesema jariobi hilo halikubaliki na linatia mashaka", na serikali yake itafanya mjadala na washirika wa Pasifiki.

    Japani ilisema "imeisihi sana" China kufikiria upya hatua hiyo baada ya kuarifiwa kuhusu urushaji wa kombora dakika 90 kabla haujatokea.

    China imesema jaribio lake la kombora - ambalo linakuja miaka miwili baada ya jaribio la mwisho - lilikuwa sehemu ya mafunzo ya kijeshi ya "kawaida" na "halielekezwi kwa nchi au shabaha yoyote maalum".

  7. Ndege za kivita za Uingereza zazuia ndege ya kijeshi ya Urusi

    ;

    Chanzo cha picha, PA Media

    Ndege za kivita za Uingereza zimeizuia ndege ya doria ya Urusi baada ya kuikaribia meli ya kivita katika Bahari ya Norway, imesema Wizara ya Ulinzi (MoD).

    Ndege ya Urusi aina ya Bear-F ilipita "karibu sana" na meli ya kubeba ndege za kivita ya HMS Prince of Wales na inaaminika kuwa ilidondosha mabiya 10 ya kufuatilia nyambizi ndani ya maji siku ya Alhamisi, Wizara ya Ulinzi iliongeza.

    Wizara ya Ulinzi imesema shughuli za Moscow katika Bahari ya Norway "si salama na zisizo za sawa".

    Hii inakuja wiki kadhaa baada ya wanajeshi wa Royal Marines kupanda meli ya mafuta ya Urusi katika Mlango wa Uingereza, huku mkuu wa jeshi akionya kwamba hatari na vitisho vinavyoikabili Uingereza ni vikubwa zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote tangu Vita Baridi.

    Meli za kivita za Uingereza kwa sasa zimetumwa nje ya Iceland chini ya amri ya Nato, zikiwa na wanajeshi 1,500 wa Uingereza ndani.

    Kundi hilo linajumuisha manowari ya HMS Prince of Wales, manowari ya HMS Duncan, ndege aina ya F-35, helikopta za Merlin na Wildcat, na manowari ya RFA Tidespring ya kujaza mafuta.

    Ni mara ya kwanza kwa Nato kufanya operesheni za ulinzi wa anga kutoka meli ya kivita ya Ulaya.

    Pia unaweza kusoma:

  8. HRW yaishutumu Mamlaka ya Tigray kwa kuajiri watu kwa nguvu jeshini

    p

    Chanzo cha picha, NYT

    Shirika la kutetea hazi za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeri poti kwamba mamlaka za kikanda katika eneo la kaskazini mwa Tigray nchini Ethiopia zimekuwa zikiwateka nyara na kuwaajiri raia kinyume cha sheria, watoto wenye umri wa miaka 15, tangu Aprili 2026.

    Harakati ya kuajiri inafuatia miezi kadhaa ya mvutano unaoongezeka kati ya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

    Katika taarifa iliyotolewa 6 Julai 2026, shirika hilo linasema kwamba jamii katika miji na vijiji zinasema vikosi na maafisa wa Tigray wanawakamata wapiganaji wa zamani na wanaume na wavulana kutoka mitaani, ofisini, majumbani wakati wa upekuzi wa usiku, na maeneo ya kuchimba dhahabu.

    "Kampeni ya mamlaka ya Tigray ya kuwaajiri wanaume na wavulana kwa nguvu katika vikosi vyao inaunda hali ya hofu katika eneo lote," anasema Laetitia Bader, naibu mkurugenzi wa Afrika wa HRW.

    "Mamlaka inapaswa kukomesha kampeni yao mara moja na kuwaruhusu wale walioajiriwa kinyume cha sheria kurudi nyumbani."

    HRW imeekodi visa sita vya kulazimishwa kuajiriwa kupitia mahojiano ya mbali na watu 18 mwezi Juni, wakiwemo mashahidi, jamaa za wapiganaji walioandikishwa jeshini, na wale waliotoroka baada ya kutekwa nyara.

    Waliohojiwa wamesema kuwa msako mkubwa uliongezeka mwishoni mwa Aprili, huku mamlaka za mitaa zikitumia orodha ya wapiganaji wa zamani na watoa taarifa wa maeneo ili kuwatambua wapiganaji walioandikishwa jeshini.

    Inaripotiwa kwamba wapiganaji wapya walishikiliwa katika ofisi za utawala, magereza, au shule kabla ya kuhamishiwa kwenda kwenye kambi za kijeshi kaskazini magharibi na kusini mwa Tigray.

    Kundi hilo la haki za binadamu limetoa wito kwa Umoja wa Afrika, pamoja na serikali zilizounga mkono makubaliano ya Pretoria ya 2022, Marekani, na Umoja wa Ulaya, kuishinikiza mamlaka ya Tigrayan kusitisha kulazimishwa kuajiriwa jeshini, kuwaachilia watoto wote na watu walioandikishwa jeshini kinyume cha sheria, na kuondoa tangazo hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Idadi ya vifo kutokana na Ebola yafikia 506 DR Congo

    p

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamlaka za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) zimetangaza kwamba idadi ya vifo kutokana na Ebola aina ya Bundibugyo imefikia 506.

    Kufikia tarehe 4 Julai 2026, katika ripoti iliyochapishwa asubuhi ya leo, jumla ya visa 1,561 vilivyothibitishwa vimerekodiwa tangu mlipuko huo utangazwe tarehe 15 Mei. Hivi sasa, wagonjwa 628 wametengwa au wamelazwa hospitalini katika majimbo matatu ya mashariki.

    Mkoa wa Ituri unabaki kuwa kitovu cha mlipuko huo, ukichangia zaidi ya 90% ya visa vyote vilivyothibitishwa. Unafuatiwa na Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

    Idadi ya jumla ya watu katika majimbo matatu yaliyoathiriwa inakadiriwa kuwa karibu milioni 15. Maafisa wa afya wana wasiwasi hasa kuhusu maeneo 36 ya afya yenye hatari kubwa, ambayo yanashuhudia uhamaji mkubwa wa watu.

    Uhamaji huu mkubwa unasababishwa hasa na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi wakikimbia mapigano kati ya makundi ya waasi na vikosi vya serikali, pamoja na uhamaji mkubwa unaohusishwa na shughuli zisizo rasmi za uchimbaji dhahabu katika eneo hilo.

    Wiki saba baada ya mlipuko, juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi (IPC), ikiwa ni pamoja na Vifaa vya Kinga Binafsi (PPE) na klorini.

    Kuna visa 96 vilivyothibitishwa miongoni mwa wafanyakazi wa afya, 19 kati yao wamefariki.

    Ufuatiliaji wa watu waliogusana na wagonjwa unaongezeka kwa kasi, huku watu 10,079 wakiorodheshwa.

    Kati ya hawa, 8,221 wanafuatiliwa kikamilifu, ikiwakilisha kiwango cha ufuatiliaji cha asilimia 81.6 huku lengo likiwa 95.

    Katika ishara nyingine nzuri kwa timu ya mwitikio, idadi ya waliopona sasa imeongezeka hadi 254.

    Pia unasoma:

  10. Watu wasiopungua 14 wameuawa katika mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv ndani ya wiki moja

    Huduma za dharura mjini Kyiv zilikuwa zikiwaokoa manusura kutoka kwenye majengo yaliyoharibiwa na mabomu kufuatia mashambulizi yaliyofanyika mapema asubuhi ya Jumatatu.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Watu wasiopungua 11 wameuawa mjini Kyiv kufuatia usiku wa pili wa mashambulizi ya Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine ndani ya wiki moja, kwa mujibu wa mkuu wa utawala wa kijeshi wa jiji hilo.

    Takribani watu 46 wamejeruhiwa, wakiwemo watoto watano, amesema Timur Tkachenko. Maafisa wa huduma za dharura pia walisema watu wengine watatu wameuawa katika eneo kubwa la Kyiv.

    Juhudi za uokoaji zinaendelea katika zaidi ya maeneo 20, Tkachenko aliandika kwenye Telegram, akiongeza kuwa majengo marefu ya makazi yalilengwa katika wilaya mbili za jiji.

    Mashambulizi hayo yametokea siku moja kabla ya mkutano wa kilele wa NATO utakaofanyika nchini Uturuki, ambapo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Saa chache kabla ya mashambulizi hayo ya karibuni, Zelensky alikuwa ameonya kuwa Moscow ilikuwa ikijiandaa kufanya shambulio jingine "kubwa" dhidi ya Kyiv, kufuatia mashambulizi ya Alhamisi yaliyosababisha vifo vya watu 30.

    Ulikuwa ni usiku mwingine wa kutisha kwa wakazi wa mji mkuu, huku milipuko mikubwa na sauti za mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine zikisikika. Kwa mara nyingine, wakazi wengi walikimbilia kujificha kwenye makazi ya chini ya ardhi.

    Meya wa Kyiv, Vitaly Klitschko, alisema makombora ya balestiki ya Urusi yaligonga majengo kadhaa katika maeneo mbalimbali ya jiji, na kusababisha moto kuzuka katika baadhi ya majengo ya makazi.

    Kwa mujibu wa meya huyo, maghala pamoja na karakana ya kutengeneza magari pia viliharibiwa katika mashambulizi hayo.

  11. Jinsi vita vilivyosababisha kuahirishwa kwa mazishi ya Khamenei

    Khamenei aliuawa katika makazi yake mjini Tehran

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kutokana na vita kuendelea kupamba moto, maafisa wa Iran waliokuwa wakipanga mazishi ya mwezi Machi waliamua kuyaahirisha kabisa.

    Wakati huo, afisa mmoja alisema kulikuwa na maombi mengi kutoka kwa watu waliotaka kuhudhuria hafla hiyo ya siku tatu katika ukumbi wa sala ulioko Tehran, na kwamba maandalizi ya miundombinu yalihitajika ili kupokea umati huo.

    Khamenei aliuawa katika makazi yake mjini Tehran katika wimbi la kwanza la mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani na Israel, pamoja na mkwe wake wa kike, mjukuu wake wa mwaka mmoja aitwaye Zahra Mohammadi Golpayegani, na maafisa kadhaa waandamizi.

    Mke wake pia iliripotiwa kuwa aliuawa katika shambulio hilo, ingawa baadaye chombo kimoja cha habari nchini Iran kilidai kuwa bado yuko hai.

    Shughuli ya mazishi ya kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 86 ilikuwa imepangwa kufanyika tarehe 4 Machi, ambapo waombolezaji walitarajiwa kutoa heshima zao huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa katika Msikiti Mkuu wa Grand Mosalla ulioko mji mkuu, Tehran.

    Seyyed Mohsen Mahmoudi, mkuu wa Baraza la Uratibu wa Uenezi wa Kiislamu la Tehran, alisema kuahirishwa kwa mazishi hayo kulitokana na "idadi kubwa ya maombi ya kuhudhuria hafla hii na haja ya kuhakikisha maandalizi yanayofaa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi."

    Unaweza kusoma;

  12. Msafara wa mazishi ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran waanza mjini Tehran

    Waombolezaji

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Msafara wa mazishi ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, umeanza safari yake kupitia mji mkuu, Tehran.

    Khamenei aliiiongoza Iran kwa zaidi ya miaka 35 kabla ya kuuawa katika mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Marekani na Israel mwezi Februari.

    Mazishi yake yalianza Ijumaa na yatafanyika kwa kipindi cha siku saba, yakihusisha shughuli mbalimbali katika maeneo ya Iran na Iraq. Mamlaka za Iran zimesema kuwa kati ya watu milioni 12 na 20 wanatarajiwa kushiriki katika hafla hizo za mazishi.

    Mrithi wa Khamenei, mwanawe Mojtaba Khamenei, hadi sasa hajaonekana hadharani katika mazishi ya baba yake, licha ya kuhudhuriwa na viongozi kadhaa waandamizi wa utawala wa Iran.

    Uvumi kuhusu hali ya Mojtaba umeendelea kuenea, ukichochewa na taarifa zisizothibitishwa kuwa alijeruhiwa katika mashambulizi hayo hayo ya Marekani na Israel yaliyomuua baba yake.

    Hajajitokeza hadharani tangu ateuliwe mapema mwezi Machi.

  13. England yaichapa Mexico katika mechi ya kusisimua na kutinga robo fainali

    England yailaza Mexico katika mechi ya kusisimua na kutinga robo fainali

    Chanzo cha picha, Reuters

    Uingereza ilionesha mchezo wao bora zaidi katika Kombe la Dunia huku kukiwa na shauku na hisia katika Uwanja wa Azteca na kupata ushindi mkubwa dhidi ya Mexico uliowasaidia kutinga robo fainali dhidi ya Norway.

    Huku mechi ikicheleweshwa kwa saa moja kutokana na dhoruba kali, kikosi cha Thomas Tuchel kilinusurika kadi nyekundu ya Jarell Quansah mapema kipindi cha pili na kurekodi moja ya ushindi wao bora zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

    Mexico ilikuwa imepoteza michezo miwili tu kati ya 89 ya ushindani katika ngome yao ya Azteca, lakini mbinu ya Uingereza ya mapema iliwaruhusu kuongoza wakati Jude Bellingham alipofunga mabao mawili katika sekunde 98 kabla ya mapumziko.

    Mlinda lango wa Uingereza Jordan Pickford alikuwa katika hali nzuri sana, akiokoa mara mbili kwa ustadi mpira kutoka kwa Raul Jimenez, lakini hakuwa na nguvu ya kumzuia Julian Quinones akifunga bao la kurudisha kwa Mexico.

    Sauti za mara kwa mara za kelele, ziliongezeka wakati Quansah alipotolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Jesus Gallardo, lakini Uingereza ilirejesha uongozi wao wa mabao mawili wakati Harry Kane alipofunga kwa penalti baada ya Anthony Gordon kuangushwa na mlinda lango Raul Rangel.

    Wakati tu Uingereza ilipofikiri wamerejesha utulivu, Kane alimchezea visivyo Brian Gutierrez katika eneo la hatari, Jimenez akifunga penalti. Wakiwa na shinikizo na katika hali ya wasiwasi, Tuchel aliwaingiza Dan Burn na Djed Spence, wakirejea kwenye ulinzi wa wachezaji watano na kupata ushindi wa dakika 11 za mwisho.

    Unaweza kusoma;

  14. Shambulio la Israel liliua watu wawili huko Gaza, wahudumu wa afya wasema

    Gaza

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Shambulio la anga la Israel liliwaua takribani Wapalestina wawili katika Jiji la Gaza siku ya Jumapili, kwa mujibu wa maafisa wa afya.

    Wahudumu wa afya walisema watu hao wawili waliuawa baada ya shambulio la anga kulenga kundi la watu katika Barabara ya Omar Al-Mokhtar katikati ya jiji hilo, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Watu wengine kadhaa walijeruhiwa, waliongeza.

    Jeshi la Israel halikuzungumza kuhusu tukio hilo.

    Israel imeendelea kutekeleza mashambulizi katika Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kwa upatanishi wa Marekani kati yake na Hamas kufikiwa mwezi Oktoba mwaka uliopita.

    Israel imesema inalenga wanamgambo wanaotishia wanajeshi wake walioko Gaza au wale walioshiriki katika shambulio la mwaka 2023.

    Hamas imeishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Wakati huo huo, Nikolay Mladenov, mjumbe wa Bodi ya Amani ya Gaza aliyeteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa pande zote mbili zimekiuka makubaliano hayo.

    Israel na Hamas bado zimekwama katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu utekelezaji wa awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaanze kutekelezwa miezi minane iliyopita, zaidi ya Wapalestina 1,060, wengi wao wakiwa raia, pamoja na wanajeshi wanne wa Israel, wameuawa mjini Gaza, kulingana na takwimu zilizotolewa na kila upande. Hamas haijatangaza idadi ya wanamgambo wake waliouawa.

    Unaweza kusoma;

  15. Vietnam, kitovu cha kimataifa cha bidhaa bandia za kifahari, yaanzisha msako mkali dhidi ya soko la biashara haramu

    Mikoba yenye chapa ya mbunifu maarufu wa Ufaransa, Louis Vuitton, ni miongoni mwa bidhaa zinazopendwa zaidi katika soko la bidhaa bandia.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mikoba yenye chapa ya mbunifu maarufu wa Ufaransa, Louis Vuitton, ni miongoni mwa bidhaa zinazopendwa zaidi katika soko la bidhaa bandia.

    Mapema mwaka huu, polisi wa Vietnam walipovamia maghala mawili yaliyoko nje kidogo ya mji wa Ho Chi Minh, walikuta zaidi ya jozi 23,000 za ndala zilizokuwa na nembo za Nike, Adidas, Crocs na Gucci.

    Hata hivyo, kampuni hizo hazikuwa na uhusiano wowote na maghala hayo. Ndala zote zilizokutwa zilikuwa bidhaa bandia.

    Operesheni hiyo, iliyosababisha kukamatwa kwa bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola za Vietnam bilioni 2 sawa na dola za Marekani 76,053, ilikuwa sehemu ya kampeni dhidi ya biashara haramu ambayo imeendelea kushamiri waziwazi kwa miongo kadhaa.

    Takriban kilomita 30 kutoka eneo hilo, katika soko la bidhaa za mitumba lililopo katika kitovu cha utalii cha Ho Chi Minh, aina hizo hizo za ndala bandia, zinazoiga bidhaa ambazo huuzwa kwa hadi dola 900 katika masoko ya kimataifa, zinauzwa kwa dola 57 kwa jozi.

    Kando yake kuna bidhaa nyingine nyingi bandia, zikiwemo mikoba yenye chapa ya "Chanel", fulana za "Prada" na saa za "Rolex" zilizopangwa kwenye vibanda vya soko.

    Vietnam inatambulika duniani kama mojawapo ya vituo vikuu vya bidhaa bandia za bei nafuu, hasa bidhaa za kifahari za wabunifu maarufu, na ina baadhi ya masoko makubwa zaidi ya bidhaa hizo duniani.

    Sasa, huku ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, serikali ya Vietnam imeanzisha kampeni ya kuondoa sifa hiyo.

    Mnamo tarehe 7 Mei, serikali ilianzisha operesheni ya kitaifa dhidi ya bidhaa na shughuli zinazokiuka haki za umiliki wa ubunifu, ikiwemo utengenezaji na uuzaji wa bidhaa bandia, uharamia wa maudhui mtandaoni na ukiukaji wa alama za biashara.

  16. Nigeria yasema raia wake wawili wameuawa Afrika Kusini huku mashambulizi dhidi ya wahamiaji yakiongezeka

    Muandamanaji

    Chanzo cha picha, EPA

    Nigeria imesema kuwa raia wake wawili wameuawa nchini Afrika Kusini "wakati ambapo raia wa kigeni wanaendelea kulengwa isivyo haki" nchini humo.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema kuwa Emeka Charles Iroegbu aliuawa tarehe 28 Juni, akidaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi waliotumia "mbinu za kikatili za mahojiano". Pia ilisema kuwa mmiliki wa duka, Musa Yunana Joe, aliuawa siku hiyo hiyo na watu wasiojulikana.

    Hadi sasa, mamlaka za mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, hazijatoa tamko kuhusu matukio hayo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema kuwa matukio haya yanatokea wakati ambapo hisia za kupinga wahamiaji zinaongezeka nchini Afrika Kusini.

    Hali hiyo imesababisha takribani raia 25,000 kutoka mataifa mengine ya Afrika kurejeshwa katika nchi zao, wakiwemo takribani Wanigeria 700.

    Waandamanaji nchini Afrika Kusini wamekuwa wakiiomba serikali kuchukua hatua zaidi kudhibiti uhamiaji haramu. Wanasema kuwa raia wa kigeni wanachukua nafasi za ajira na kunufaika isivyo haki na huduma za umma.

    Nigeria pia imesema itadai fidia kutoka kwa Afrika Kusini kwa raia wake walioondoka nchini humo, ikiongeza kuwa serikali ya Abuja imeanza kuorodhesha biashara na mali zilizotelekezwa na Wanigeria.

    Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ijumaa, Waziri wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Kusini, Khumbudzo Ntshavheni, alisema serikali yake haitalipa fidia na kwamba Wanigeria wanaweza kuuza mali zao zilizosajiliwa walizoacha nchini humo katika soko la Afrika Kusini.

    Unaweza kusoma;

  17. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo