Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais Samia awaonya wanaharakati dhidi ya kuchochea vurugu
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewakosoa wanaharakati kwa kutegemea vurugu ili kuendesha maisha yao kwa maslahi ya wengine.
Muhtasari
- Iran yasema imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya vituo vya Marekani Mashariki ya Kati
- Watu 130 wakamatwa Tanzania kwa tuhuma za kupanga vurugu za Julai 7
- Kombe la Dunia 2026: FIFA yakataa malalamiko ya Misri kuhusu waamuzi
- Ubalozi wa Marekani nchini Jordan wawataka raia wake kutafuta hifadhi haraka
- Mwili wa Khamenei kuzikwa leo katika mji alikozaliwa wa Mashhad, Iran
- DRC yadai Somalia na Kenya zinaunga mkono waasi wa M23
- Ripoti yasema Kenya iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu za uchaguzi wa 2027
- Iran yadokeza Kenya na Nigeria huenda zikahusika kijeshi katika mzozo wake na Marekani
- CCM na ACT Wazalendo zakubaliana kuanza mazungumzo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar
- Rais Samia aonya wanaharakati dhidi ya kuchochea vurugu
- Iran yawasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga mashambulizi ya Marekani
- Mkuu wa NATO aiambia BBC kuwa matamshi ya Trump ni kama "mabishano ya kifamilia"
- Trump asema Ukraine itapewa leseni ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Patriot
- Rais wa Nigeria ataka kujua jinsi taasisi feki ilivyoanzishwa ndani ya ofisi yake
- Mahakama ya ICC imesema imepata ushahidi katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Sudan
- Marekani na Iran zashambuliana kwa siku ya pili,afisa mkuu wa Iran asema "kukiuka makubaliano kutakuwa"na gharama
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga & Mariam Mjahid
Iran yasema imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya vituo vya Marekani Mashariki ya Kati
Iran imesema imeanzisha awamu mpya ya mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika Mashariki ya Kati, saa chache baada ya Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyoko kusini mwa Iran.
Shirika la habari la Mehr, linalohusishwa na serikali ya Iran, limesema mashambulizi hayo ni jibu kwa mashambulizi ya Marekani yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa Mehr, makombora yaliyofyatuliwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yalilenga maeneo yanayotumiwa na Marekani nchini Kuwait.
Shirika hilo pia limedai kuwa vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Jordan vililengwa kwa mashambulizi ya makombora. Hata hivyo, mamlaka za Jordan zimesema jeshi la nchi hiyo lilitungua makombora manane yaliyoingia katika anga yake.
Aidha, Mehr imeripoti kuwa milipuko ilisikika katika Kituo cha Kijeshi cha Victory Base mjini Baghdad, Iraq, ambacho kinatumiwa na vikosi vya Marekani.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema hana uhakika kama bado kuna sababu ya kufikia makubaliano na Iran.
"Sijui kama Iran bado inafaa kufanya makubaliano nayo," Trump amesema, siku moja baada ya kutangaza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalikuwa "yamekamilika."
Madai ya Iran kuhusu mashambulizi hayo hayajathibitishwa kwa njia huru, na hadi sasa Marekani haijatoa tamko rasmi kuhusu madai ya kulengwa kwa vituo vyake vya kijeshi katika nchi hizo.
Mshawishi wa mitandao kutoka Ghana apelekwa Marekani kujibu tuhuma za ulaghai wa dola milioni 8
Mtengeneza maudhui katika mitandao ya kijamii kutoka Ghana, Frederick Kumi, maarufu kama Abu Trica, amepelekwa Marekani kujibu tuhuma za kufanya ulaghai wa kimapenzi mtandaoni uliodaiwa kuwaibia Wamarekani wazee zaidi ya dola milioni nane za Marekani.
Kumi, ambaye anakanusha tuhuma zote, alisafirishwa kwenda Marekani Alhamisi kwa ndege ya Delta Airlines, huku mawakili wake wakidai walikuwa wamewasilisha ombi mahakamani la kusitisha hatua hiyo hadi uhalali wa kurejeshwa kwake Marekani uamuliwe.
Mwakilishi wake wa kisheria, Oliver Barker Vormawor, amesema serikali ilichukua hatua kabla mahakama haijatoa uamuzi.
"Mchakato wa mahakama ulizidiwa na hatua za mamlaka za serikali. Hili linaibua maswali makubwa ya kikatiba kuhusu iwapo usimamizi wa mahakama unaweza kuwa na maana ikiwa serikali inaweza kuchukua hatua kabla mahakama haijaamua," amesema.
Mamlaka za Marekani zilimshtaki Kumi mwezi Desemba mwaka jana kwa makosa ya kula njama za kufanya ulaghai wa kielektroniki, kula njama za utakatishaji fedha na makosa mengine yanayohusiana. Akipatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela.
Kumi mwenye umri wa miaka 28, ambaye anatoka Swedru kusini mwa Ghana, alikamatwa katika operesheni ya pamoja kati ya Ghana na Marekani.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanadai Kumi na mshukiwa mwenzake, Emmanuel Kojo Baah Obeng, walitumia zana za akili bandia kuunda utambulisho wa watu wasio halisi mtandaoni, kujenga mahusiano ya kimapenzi na waathiriwa na baadaye kuwaomba fedha kwa visingizio mbalimbali.
"Walijenga uaminifu kupitia mazungumzo ya mara kwa mara kwa simu, barua pepe na programu za ujumbe. Kisha waliomba fedha au vitu vya thamani kwa visingizio vya uongo kama mahitaji ya matibabu ya dharura, gharama za usafiri au fursa za uwekezaji," wamesema waendesha mashtaka wa Marekani.
Waendesha mashtaka wanadai fedha hizo zilielekezwa kwa washirika waliokuwa wakijifanya watu wengine, huku Kumi akidaiwa kuzisambaza kwa washirika wake nchini Marekani na Ghana.
Kesi hiyo inasikilizwa chini ya sheria ya Marekani inayolenga kuzuia na kuwafungulia mashtaka wahusika wa unyanyasaji na ulaghai dhidi ya wazee, wakati mamlaka za Marekani zikiendelea kuongeza juhudi za kuvunja mitandao ya uhalifu inayolenga kuwaibia wazee kupitia mtandao.
Watu 130 wakamatwa Tanzania kwa tuhuma za kupanga vurugu za Julai 7
Jeshi la Polisi Tanzania limesema linawashikilia watu 130 wanaotuhumiwa kuhusika katika kupanga na kuhamasisha vitendo vya kihalifu Julai saba mapema wiki hii.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi na Msemaji wa Jeshi la Polisi, jeshi hilo limesema watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia uchunguzi uliofanywa baada ya tahadhari za usalama zilizotolewa Juni 19 na Julai 5 mwaka huu.
Polisi wamesema uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakitumia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine kuhamasisha watu kushiriki katika vitendo vinavyokiuka sheria.
Taarifa hiyo imeorodhesha vitendo vinavyodaiwa kupangwa kuwa ni pamoja na kupanga, kutamka, kuandaa na kusambaza taarifa za uchochezi, kuhamasisha wananchi kushiriki katika vitendo vya kihalifu vinavyoweza kusababisha madhara kwa raia, kuchoma moto, kulipua transfoma za umeme, kuharibu miundombinu ya umma na mali za watu binafsi, pamoja na kushambulia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupora silaha.
"Kufuatia utafiti huo, jumla ya watuhumiwa 130 waliokuwa wanapanga, kushiriki katika vikao vya ndani, wakiandaa na kusambaza taarifa za kuhamasisha vitendo hivyo vya kihalifu visivyokubalika wamekamatwa katika mikoa mbalimbali nchini. Uchunguzi unakamilishwa ili hatua zingine za kisheria zifuate," imesema taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha, limewataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa kuwajibika na kuepuka kushiriki katika kuandaa au kusambaza taarifa zinazoweza kuchochea vitendo vya kihalifu au ambazo hazijathibitishwa.
"Tunaendelea kutoa wito kwa watu wote kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa kuepuka kushiriki katika kuandaa na kusambaza taarifa zenye kuhamasisha vitendo vya kihalifu au kusambaza taarifa zinazozushwa na ambazo hazina uhakika nazo wala kujua chanzo chake," imeongeza taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kufuatilia hali ya usalama nchini na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kuhusika na vitendo vinavyokiuka sheria.
Pia unaweza kusoma:
Ali Khamenei alikuwa nani, ambaye mazishi yake ya kitaifa yanafanyika leo?
Shughuli za mazishi na maombolezo ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, zinaendelea mjini Tehran na maeneo mengine nchini humo.
Anatarajiwa kuzikwa alikozaliwa Mashhad huko Iran.
Mazishi yake yanaendelea sambamba na mashambulizi kati ya Iran na Marekani yakishamiri hasa katika maeneo yaliyo karibu na mlango wa Hormuz.
Khamenei aliuawa katika mashambulizi ya kwanza kati ya Marekani na Iran yaliyolenga Iran.
Soma historia na safari ya maisha ya Ayatollah Ali Khamenei kupitia kiungo kilicho hapa chini.
Kombe la Dunia 2026: FIFA yakataa malalamiko ya Misri kuhusu waamuzi
Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA, limekataa malalamiko yaliyowasilishwa na Chama cha Soka cha Misri kuhusu uamuzi wa waamuzi katika mechi ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Argentina.
Misri ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2 kwa 0, lakini Argentina, mabingwa watetezi, walifanikiwa kurejea mchezoni na kufunga mabao matatu ndani ya dakika 13, na kutinga hatua inayofuata ya mashindano huku safari ya Misri ikifikia tamati.
Chama cha Soka cha Misri kilisema hakiwezi kunyamaza kutokana na kile kilichokiita makosa ya wazi na yasiyo ya haki yaliyofanywa na mwamuzi wa mechi hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Waamuzi wa FIFA, Pierluigi Collina wa Italia, ametetea maamuzi ya waamuzi hao.
"Si haki kuwashutumu waamuzi wakati walifanya maamuzi waliyoamini kuwa sahihi na walifanya kila walichoweza kuhakikisha mechi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria," amesema Collina.
Kauli hiyo inaashiria msimamo wa FIFA kwamba hakukuwa na sababu ya kubadili matokeo ya mechi hiyo licha ya malalamiko yaliyowasilishwa na upande wa Misri.
Soma Zaidi:
Ubalozi wa Marekani nchini Jordan wawataka raia wake kutafuta hifadhi haraka
Ubalozi wa Marekani nchini Jordan umewataka raia wa Marekani walioko nchini humo kutafuta hifadhi mara moja, ukisema kuna taarifa zinazoashiria kuwa makombora, ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu yanapita katika anga ya Jordan.
Katika taarifa yake, ubalozi huo umesema unafuatilia kwa karibu maendeleo ya hali ya usalama na utaendelea kutoa taarifa na maelekezo mapya kadiri yatakavyohitajika.
"Taarifa zinaonyesha kuwa makombora, ndege zisizo na rubani au makombora ya masafa marefu yako katika anga ya Jordan," taarifa ya ubalozi huo imesema.
Onyo hilo linatolewa wakati mvutano wa usalama katika eneo la Mashariki ya Kati ukiendelea kuongezeka, huku nchi mbalimbali zikiendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya hali hiyo.
Mwili wa Khamenei kuzikwa leo katika mji alikozaliwa wa Mashhad, Iran
Mwili wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, unatarajiwa kuzikwa leo katika eneo takatifu la Imam Reza, iliyoko mjini Mashhad, mji alikozaliwa kaskazini mashariki mwa Iran.
Mazishi hayo yanahitimisha takriban siku sita za shughuli za maombolezo na ibada za kumuaga zilizofanyika katika miji mbalimbali nchini Iran na Iraq.
Makao makuu ya kamati inayosimamia mazishi ya Khamenei yamesema ndege iliyobeba jeneza lake pamoja na miili ya baadhi ya wanafamilia wake waliouawa katika mashambulizi ya Marekani imewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hasheminejad mjini Mashhad ikitokea Iraq.
Shughuli ya mwisho ya mazishi na maziko inatarajiwa kufanyika leo katika mji huo wa Mashhad, ambao ni kitovu cha kidini na nyumbani kwa Haram ya Imam Reza, moja ya maeneo matakatifu zaidi kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Mazishi ya Khamenei yalianza Ijumaa iliyopita, huku maelfu ya waombolezaji wakishiriki katika shughuli mbalimbali za kumuaga.
Siku ya Jumamosi, Julai 4, majeneza ya Khamenei na wanafamilia wake wanne yaliwekwa katika Uwanja wa Msikiti wa Mosalla jijini Tehran ili wananchi waweze kutoa heshima zao za mwisho kabla ya kusafirishwa kwenda Mashhad kwa maziko.
DRC yadai Somalia na Kenya zinaunga mkono waasi wa M23
Mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinadai kuwa Somalia na Kenya zimetuma wanajeshi kupigana bega kwa bega na waasi wa M23 katika jimbo la Kivu Kusini, kwa mujibu wa taarifa zilizofuatiliwa na BBC Monitoring.
Msimamizi wa eneo la Fizi, lililoko Kivu Kusini, alisema tarehe 5 mwezi huu kuwa wanajeshi kutoka Somalia na Kenya walionekana wakipigana pamoja na waasi wa M23 katika eneo la Hauts Plateaux.
Samy Kalonji Badibanga alisema wanajeshi hao walikuwa wakisaidiwa na vikosi vya Rwanda, wanamgambo wa Twirwaneho, kundi la Red Tabara kutoka Burundi na waasi wa M23 katika mapambano dhidi ya vikosi vya serikali.
"Wanajeshi hao wanasababisha vifo na kuwafanya maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao katika eneo hilo," alinukuliwa akisema.
Hapo awali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikiishutumu Kenya kwa kuunga mkono M23 na makundi yanayoshirikiana nayo. Hata hivyo, hii ni mara ya kwanza kwa madai kama hayo kuelekezwa dhidi ya Somalia.
BBC Somali haijaweza kuthibitisha madai hayo kwa njia huru.
Kufikia sasa, Kenya na Somalia hazijatoa tamko kuhusu tuhuma hizo, ingawa Kenya imewahi kukanusha kuhusika katika mzozo huo.
Madai hayo yanatolewa wakati vikosi vya serikali ya DRC na washirika wao, wakiwemo wanamgambo wa Wazalendo, vikidai kupata mafanikio katika mapigano dhidi ya M23 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Mnamo Julai 6, vikosi vya serikali pamoja na wanamgambo wa Wazalendo vilisema viliteka tena vijiji vitatu vilivyo karibu na mji wa Minembwe, katika jimbo la Kivu Kusini.
M23 ni kundi la waasi lililojitenga na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo karibu miaka 20 iliyopita. Kundi hilo linasema linapigania kulinda jamii ya Watutsi, ambayo linadai imekumbwa kwa muda mrefu na mauaji na ubaguzi.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakisema kuwa M23 inaungwa mkono na Rwanda, madai ambayo serikali ya Rwanda imeendelea kuyakanusha.
Kwa upande wake, Rwanda imekuwa ikiishutumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kushirikiana na baadhi ya makundi yanayohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi na Wahutu nchini Rwanda.
Soma Pia:
Ripoti yasema Kenya iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu za uchaguzi wa 2027
Kenya inakabiliwa na uwezekano wa asilimia 84.1 wa kutokea kwa aina fulani ya vurugu zinazohusiana na uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Taasisi ya Kofi Annan.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia hiyo ni tathmini ya kiwango cha hatari na si uhakika kwamba vurugu zitatokea. Hivyo, inatoa wito kwa serikali, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia na wananchi kuchukua hatua mapema ili kuimarisha juhudi za kudumisha amani na kuzuia vurugu kabla hazijatokea.
"Takwimu hizi ni tathmini ya hatari, si uhakika wa kitakachotokea. Zinapaswa kuwa mwito wa kuchukua hatua mapema ili kuimarisha juhudi za amani na kuzuia vurugu kabla hazijatokea," imeongeza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kofi Annan, uchaguzi unaweza kuwa fursa ya kuimarisha demokrasia, lakini pia unaweza kuongeza mvutano iwapo kutakuwa na mgawanyiko wa kisiasa, taasisi dhaifu au kupungua kwa imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa Kielezo cha Hatari ya Uchaguzi kinatumia viashiria vya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutawala kutathmini mazingira ya uchaguzi na kutoa tahadhari ya mapema kwa watunga sera, wasimamizi wa uchaguzi na wadau wengine.
Kenya ni miongoni mwa nchi 10 zilizofanyiwa uchambuzi wa kina katika ripoti hiyo, ambao unachanganya tathmini ya takwimu na uchambuzi wa mazingira ya kisiasa, changamoto za uchaguzi na hatua zinazoweza kuchukuliwa kupunguza hatari ya vurugu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Iran yadokeza Kenya na Nigeria huenda zikahusika kijeshi katika mzozo wake na Marekani
Kituo cha habari cha serikali ya Iran, IRIB, kimechapisha ujumbe kwenye mtandao wa X ukidai kuwa Kenya na Nigeria zina akiba za kimkakati za kijeshi ambazo zinaweza kutumika kwa wakati unaofaa.
Katika chapisho hilo, IRIB iliandika: “Kenya na Nigeria pia zina akiba za kimkakati za kijeshi ambazo zitaingia uwanjani kwa wakati unaofaa,'' wakirejelea ni mtaalam wa masuala ya kitaifa alisema.
Hata hivyo, chapisho hilo halikutoa maelezo yoyote kuhusu akiba hizo za kijeshi, wala halikufafanua jinsi nchi hizo mbili zinavyodaiwa kuhusika katika mzozo unaoendelea.
Mpaka sasa, serikali za Kenya na Nigeria hazijatoa tamko rasmi kujibu madai hayo.
Vile vile, haijabainika ikiwa kauli hiyo iliyochapishwa na IRIB inaakisi msimamo rasmi wa serikali ya Iran au ni maoni ya mchangiaji aliyekuwa akizungumza na kituo hicho.
Wanadiplomasia na wachambuzi wanaendelea kufuatilia iwapo kutakuwa na majibu rasmi kutoka Nairobi, Abuja au Tehran kuhusu kauli hiyo.
Unaweza kusoma;
Rais Samia awaonya wanaharakati dhidi ya kuchochea vurugu
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaonya wanaharakati kwa matendo yao ya kigaidi.
Samia amesema kundi hili la watu huwa linatumia njia ya uanaharakati kujitambulisha duniani lakini ni wenye nia tofauti kulingana na matendo yao.
"Watu au kundi hilo linakuwa na kauli zinazovaa sura ya kizalendo lakini kwa undani ni maslahi binafsi," amesema Rais Samia.
Amewakosoa wanaharakati kwa kutegemea vurugu ili kuendesha maisha yao kwa maslahi ya wengine.
"Niwaonye wale wote wanaojishuhulisha na vitendo hivyo, kwamba taifa lolote duniani hutumia nguvu ya dola kuhami raia wake na kulinda heshima yake," amesema Rais Samia.
Rais Samia ameonyesha kuwa tofauti zimekuwepo lakini sio kwa nia ya kubomoa wala uvunjifu wa amani.
Aidha, amesihi Tanzania kushikamana kwa ajili ya taifa wala sio kulidhalilisha kwa sababu ya matwaka ya watu binafsi.
Rais Samia amewahikikishia raia kuwa serikali iko imara kuwalinda pamoja na mali zao.
Soma Zaidi:
CCM na ACT Wazalendo zakubaliana kuanza mazungumzo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na ACT Wazalendo wamekubaliana kuanza mchakato wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, wakisema hatua hiyo inalenga kupata suluhisho la kudumu na endelevu kwa changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiutawala zinazoikabili Zanzibar.
Tamko hilo la pamoja limesomwa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansura Mosi Kassim, ambaye amesema vyama hivyo viwili vinavyostahili kikatiba kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa vimeamua kuendeleza ushirikiano kwa maslahi ya Zanzibar.
"Pande mbili zinakubaliana kuwa mazingira ya Zanzibar, kiusalama, kiuchumi na kisiasa, yanahitaji pande mbili husika kuendelea kushirikiana, kujenga umoja, ushikamano na maridhiano ya dhati yatakayowezesha Zanzibar kuendelea kuwa na amani na utulivu endelevu," amesema Mansura.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kamati ya pamoja ya majadiliano itaundwa kusimamia mchakato huo kwa kuzingatia ratiba itakayokubaliwa na pande zote mbili, huku marais wastaafu waliosimamia awamu ya kwanza ya mazungumzo wakitarajiwa kutoa mwongozo.
Pande hizo mbili pia zimekubaliana kuchukua hatua za kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wa biashara na uwekezaji kwa kujenga taasisi imara na kuendeleza misingi ya demokrasia, utawala bora, uwajibikaji na utawala wa sheria.
"Viongozi wa kisiasa wana nia ya dhati ya kujenga mfumo na taasisi zitakazosaidia kujenga na kuimarisha demokrasia, utawala bora, uwajibikaji na utawala wa sheria, ambapo uendeshaji wa uchaguzi huru na wa haki, na utoaji wa haki kwa ufanisi, utakuwa kielelezo cha kufanikisha malengo haya," amesema Mansura.
Tamko hilo linaeleza pia kuwa mchakato huo utakuwa shirikishi kwa kuwahusisha wananchi, vyama vya siasa, asasi za kiraia na makundi mengine mbalimbali kadiri itakavyohitajika.
Aidha, pande hizo mbili zimesema mazungumzo yataongozwa na ukweli, nia ya dhati na uaminifu, huku maslahi ya Zanzibar yakipewa kipaumbele kuliko maslahi ya vyama, makundi au watu binafsi.
Vile vile, ajenda zilizokubaliwa zitatekelezwa hatua kwa hatua kupitia kamati ya pamoja, huku chombo maalumu kitakachoundwa kwa mujibu wa sheria kikiratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Pande hizo mbili zimesema utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza mara moja baada ya kutolewa kwa tamko hilo.
"Pande zote mbili zinatoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono hatua hii, kwa kutoa ushirikiano wa dhati, kwa lengo la kujenga mustakabali mwema wa nchi na wananchi wake," amesema Mansura.
Viongozi hao wamewahakikishia wananchi kuwa watausimamia mchakato huo kwa dhati na kuyaweka mbele maslahi mapana ya Zanzibar na Tanzania.
Haya yanajiri baada ya chama cha National League for Democracy kupongeza vyama hivyo viwili kutia saini ya makubaliano kikisema hatua hiyo huenda ikarejesha utulivu Zanzibar.
Soma Zaidi:
Iran yawasilisha malalamiko kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga mashambulizi ya Marekani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema imewasilisha barua za malalamiko kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani.
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Saeed Iravani, amesema Marekani imeanzisha tena "mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya mamlaka na mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," akidai kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na wajibu wake chini ya sheria za kimataifa.
Iravani pia alisema mashambulizi hayo yanakiuka kifungu cha makubaliano ya hati ya Maelewano ya Islamabad iliyosainiwa kati ya Iran na Marekani.
Katika hatua nyingine, jeshi la Marekani limetangaza kuwa lilishambulia malengo 170 nchini Iran katika mawimbi mawili ya mashambulizi yaliyofanyika kwa siku mbili mfululizo.
Katika ujumbe uliotumwa kupitia mtandao wa kijamii wa X, ukiambatana na video ya mashambulizi ya anga, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema lengo la operesheni hiyo lilikuwa "kuendelea kudhoofisha uwezo wa Iran wa kushambulia meli za kibiashara na mabaharia raia katika Mlango wa Hormuz."
Kwa mujibu wa CENTCOM, mashambulizi hayo yalilenga mifumo ya ulinzi wa anga, vifaa vya ufuatiliaji na uangalizi wa maeneo ya pwani, maghala ya kuhifadhi makombora na ndege zisizo na rubani , uwezo wa vikosi vya majini, pamoja na miundombinu ya kijeshi na usafirishaji wa vifaa vya kijeshi katika ukanda wa pwani wa Iran.
Unaweza kusoma;
Mkuu wa NATO aiambia BBC kuwa matamshi ya Trump ni kama "mabishano ya kifamilia"
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amesema muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi una nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Alitoa kauli hiyo katika mahojiano na BBC wakati wa mkutano wa kilele wa NATO uliofanyika mjini Ankara.
Kauli hiyo imekuja licha ya matamshi makali ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alisema amesikitishwa na kile alichodai kuwa NATO haikuungana na Marekani katika vita vyake dhidi ya Iran.
Hata hivyo, NATO haikushirikishwa rasmi katika operesheni hiyo, ingawa baadhi ya nchi wanachama, ikiwemo Uingereza, ziliruhusu majeshi ya Marekani kutumia kambi zao kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya makombora ya Iran.
Katika mahojiano hayo, mwandishi wa BBC alimwambia Rutte kuwa kuna tofauti kati ya kauli za matumaini zinazotolewa na viongozi wa NATO na matamshi ya wakati mwingine yanayoonekana kugawa yaliyotolewa na Trump.
Katika mkutano huo, Trump alirudia msimamo wake kwamba Marekani inapaswa kuichukua Greenland na pia aliitaja Hispania kuwa "mshirika mbaya". Hata hivyo, alisema viongozi waliokutana Ankara walionesha umoja na kwamba kulikuwa na "upendo mkubwa" katika kikao hicho.
Akijibu, Rutte alisema hali hiyo ni kama ilivyo katika familia.
"Ni kama familia. Kuna familia ambazo hazigombani kabisa, na nyingine huzozana mara kwa mara, lakini bado hubaki familia," alisema.
Rutte alisisitiza kuwa Trump anaendelea kuunga mkono NATO kikamilifu.
"Trump ameijitolea kabisa NATO," alisema.
Alipoulizwa ni kwa nini ana uhakika huo, ikizingatiwa kwamba Trump aliwahi kusema siku za nyuma kuwa kuiondoa Marekani ndani ya NATO ni jambo linaloweza kuzingatiwa, Rutte alijibu:
"Nina uhakika kwa asilimia 100 kwamba Trump anaunga mkono NATO. Anaelewa kuwa operesheni za kijeshi za Marekani, ikiwemo Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran, zisingeweza kufanyika kwa kiwango hicho bila kutumia Ulaya kama jukwaa la kuendeshea operesheni za kijeshi."
Rutte alisema kuwa katika kipindi cha wiki sita kati ya mwisho wa Februari na katikati ya Aprili, kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa, zaidi ya ndege za kijeshi 5,000 ziliondoka katika vituo vya kijeshi vya Ulaya kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili ya matumizi ya kambi hizo.
Akizungumzia umuhimu wa nchi za Nordic zilizo wanachama wa NATO, ambazo ziko karibu na Rasi ya Kola nchini Urusi ambako kuna vituo vikubwa vya manowari zenye silaha za nyuklia, Rutte alisema eneo hilo lina mchango muhimu katika usalama wa Marekani kwa kutoa tahadhari za mapema kuhusu vitisho vinavyoweza kutokea.
Unaweza kusoma;
Trump asema Ukraine itapewa leseni ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Patriot
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema yuko tayari kuipa Ukraine leseni ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Patriot, hatua ambayo inaweza kusaidia nchi hiyo kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya makombora ya masafa marefu kutoka Urusi.
Akizungumza na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wakati wa mkutano wa NATO uliofanyika Ankara Jumatano, Trump alisema: "Tutawapa leseni ya kutengeneza Patriot. Nafikiri wanaweza kuanza kuzalisha kwa haraka mara tu tutakapowapa maelekezo."
Trump alisema bado hajawafahamisha watengenezaji wa mifumo hiyo ya ulinzi, kampuni za Lockheed Martin na Raytheon, kuhusu uamuzi huo, lakini aliongeza kuwa anaamini suala hilo litashughulikiwa vizuri.
Mfumo wa Patriot hutambua na kuharibu makombora yanayolengwa angani na unachukuliwa kuwa miongoni mwa mifumo bora zaidi ya ulinzi wa anga duniani.
Hata hivyo, pia ni miongoni mwa mifumo ghali zaidi, ambapo betri moja kamili yenye makombora yake hugharimu takriban dola bilioni moja za Marekani.
Aidha, uzalishaji wake huchukua muda mrefu, huku takribani makombora 600 pekee yakizalishwa kwa mwaka, kwa mujibu wa wizara ya Ulinzi ya Marekani.
Marekani imekuwa na tahadhari kuhusu kutoa mifumo hiyo kutokana na kuwa ilitumia zaidi ya nusu ya akiba yake ya makombora ya Patriot wakati wa vita vyake na Iran mapema mwaka huu, kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Center for Strategic and International Studies (CSIS).
"Tunayo mifumo ya Patriot, lakini si mingi. Tunaihitaji pia kwa ajili ya kujilinda sisi wenyewe," alisema Trump.
Hata hivyo, Ukraine inahitaji kwa dharura mifumo ya ulinzi ya Patriot ili kujikinga dhidi ya mashambulizi ya Urusi.
Katika miezi ya hivi karibuni, Moscow imeongeza mashambulizi ya makombora ya masafa marefu dhidi ya Ukraine, na kusababisha vifo vya watu kadhaa, hususan katika mji mkuu, Kyiv.
Katika kipindi cha wiki iliyopita pekee, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya makumi ya watu mjini humo.
Unaweza kusoma;
Rais wa Nigeria ataka kujua jinsi taasisi feki ilivyoanzishwa ndani ya ofisi yake
Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi baada ya madai kwamba taasisi ya serikali isiyokuwepo kisheria iliundwa ndani ya ofisi yake na kupewa fedha za umma zenye thamani ya dola za Marekani 950,000.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Nigeria, barua iliyodaiwa kutolewa na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais ya kuanzisha Presidential Foreign Intervention Promotion Council (PFIPC) ilikuwa ya kughushi.
Polisi wameanzisha msako dhidi ya Adeniyi Adeyemi Matthew, ambaye alikuwa akijitambulisha kama Mkurugenzi Mkuu wa PFIPC, kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kujifanya afisa wa umma na makosa mengine yanayohusiana.
Kabla ya kutoweka, Adeyemi aliviambia vyombo vya habari vya nchini humo kuwa hana hatia na kwamba ana hofu kuhusu usalama wa maisha yake.
Aliahidi kufika mahakamani kuthibitisha kutokuwa na hatia, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria. Pia aliwashutumu baadhi ya maafisa waandamizi serikalini kwa kudai rushwa wakati wa mchakato wa uteuzi wake na baadaye kujaribu kudhibiti fedha za taasisi hiyo. Ikulu imekanusha tuhuma hizo.
Adeyemi alisema PFIPC ilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini Nigeria, lakini hakuna rekodi yoyote inayoonesha kuwa ilifanikiwa kufanikisha uwekezaji wowote.
Taasisi hiyo ina wafanyakazi watatu pekee, ambao tayari wamehojiwa na polisi.
Jumanne, Rais Tinubu aliiagiza Tume Huru ya kupambana na vitendo vya rushwa (ICPC) kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti kamili ndani ya siku 30.
Uchunguzi wa BBC News Pidgin umebaini kuwa taasisi hiyo ilikuwa imepata ofisi ndani ya Federal Secretariat, jengo kubwa la serikali linalohifadhi wizara nyingi za Nigeria katika mji mkuu, Abuja.
Pia ilifungua akaunti za benki katika Benki Kuu ya Nigeria (CBN) na iliorodheshwa katika Sheria ya Bajeti ya mwaka 2026 ikiwa na mgao wa naira bilioni 1.3, sawa na dola za Marekani 950,000.
Hata hivyo, Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali imesema PFIPC haikuwahi kuwa na akaunti inayofanya kazi katika Benki Kuu ya Nigeria, na haijawahi kupokea fedha za umma wala kulipa mishahara.
Ikulu ya Rais imesema uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na polisi umethibitisha kuwa saini ya Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais, Femi Gbajabiamila, iliyokuwa kwenye barua inayodaiwa kuanzisha taasisi hiyo, ilighushiwa.
Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa katika Mahakama Kuu, mjini Abuja, Adeniyi Adeyemi pamoja na washtakiwa wengine wawili wanatuhumiwa kutumia nyaraka za serikali zilizoghushiwa kuanzisha na kuendesha taasisi hiyo inayodaiwa kuwapo, kufungua akaunti kadhaa za benki kwa jina lake na kutafuta kutambuliwa rasmi kwa taasisi ambayo serikali inasisitiza kuwa haipo.
Rais Bola Tinubu ameiagiza Tume Huru ya Kupambana na Vitendo vya Rushwa na Makosa Mengine Yanayohusiana (ICPC) kuchunguza tuhuma mbalimbali, zikiwemo:
- Kughushi barua za uteuzi na nyaraka rasmi za serikali;
- Kutumia madai ya uongo kutafuta utambuzi rasmi na uungwaji mkono wa kidiplomasia, ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa visa;
- Kufungua akaunti nyingi za benki kwa kutumia nyaraka zinazodaiwa kughushiwa; na
- Kuchunguza nafasi ya mtumishi yeyote wa umma, mtu binafsi, taasisi ya kifedha au mpatanishi ambaye huenda alihusika katika kuwezesha njama hiyo.
Rais pia ameagiza wachunguzi kuchunguza mazingira yaliyoifanya taasisi inayodaiwa kuwa ya kubuniwa ionekane kuwa halali, pamoja na kubaini udhaifu katika mifumo na taratibu za serikali ambao unadaiwa kutumiwa kufanikisha mpango huo.
Kashfa hiyo imezua shinikizo kubwa kutoka kwa mashirika ya kiraia, wanasiasa wa upinzani na mawakili waandamizi, ambao wamekuwa wakitaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu suala hilo.
Mahakama ya ICC imesema imepata ushahidi katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Sudan
Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Nazhat Shameem Khan, amesema mahakama hiyo imepata "ushahidi thabiti" unaowahusisha viongozi wa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) na uhalifu wa kivita uliofanyika hivi karibuni katika jimbo la Darfur, Sudan.
Akizungumza na BBC, Khan alisema ICC imepata "mafanikio makubwa" katika uchunguzi wake kuhusu mauaji ya raia yaliyotokea katika miji ya El-Fasher na El-Geneina.
"Huenda ikachukua muda kabla haki haijapatikana na kesi kufikishwa mahakamani, lakini tutafika huko," alisema Khan, akiongeza kuwa ushahidi pia unawahusisha viongozi wa RSF na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Kuzingirwa na hatimaye kutwaliwa kwa mji wa El-Fasher kulikuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi katika vita vinavyoendelea kati ya RSF na jeshi la Sudan.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 6,000 waliuawa mjini El-Fasher wakati RSF ilipouteka mji huo mwezi Oktoba mwaka jana.
Aidha, kikundi hicho kinatuhumiwa kutekeleza mauaji ya halaiki kama hayo katika mji wa El-Geneina.
RSF imeendelea kukanusha mara kwa mara tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu wengi katika eneo lolote la Darfur.
Hata hivyo, hakutaja ni lini mashtaka yanaweza kufunguliwa dhidi ya wale wanaodaiwa kuhusika na ukatili uliotekelezwa katika vita hivyo, vilivyoanza mwezi Aprili 2023.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), yenye makao yake makuu mjini The Hague nchini Uholanzi, ni mahakama ya kimataifa yenye mamlaka ya kushtaki watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.
Khan alizungumza na BBC baada ya kutembelea kambi za wakimbizi mashariki mwa Chad, ambako watu waliokimbia mapigano huko Darfur walimweleza kuhusu ukatili walioupitia.
Makumi ya maelfu ya watu walilazimika kuyahama makazi yao mjini El-Fasher, huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa ghasia zilizotokea huko zilikuwa na "viashiria vya mauaji ya kimbari."
RSF imekanusha madai yaliyoenea kwamba mauaji yaliyotokea El-Fasher yalichochewa na misingi ya kikabila na kwamba yalifuata mtindo wa wanamgambo Waarabu kuwashambulia makundi yasiyo ya Kiarabu.
Kikundi hicho kimesisitiza kuwa kiwango cha ukatili kilichoripotiwa kimezidishwa, ingawa kimekiri kwamba baadhi ya ukiukaji wa haki za binadamu ulitokea katika mji huo.
Unaweza kusoma;
Marekani yaanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya Iran huku milipuko ikiripotiwa kusini mwa nchi
Marekani imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, huku milipuko ikiripotiwa katika maeneo ya kusini mwa nchi, ikiwemo karibu na Bandar Abbas na maeneo mengine ya pwani.
Maafisa wa Marekani wamesema mashambulizi hayo yanalenga kupunguza uwezo wa Iran wa kutishia usafiri wa majini katika Mlango bahari wa Hormuz, kufuatia mashambulizi yaliyodaiwa kufanywa na Iran dhidi ya meli za kibiashara.
Iran imekosoa mashambulizi hayo na kuyataja kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku ikidai kujibu kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba.
Mvutano huo umeongeza hofu ya kuenea kwa mzozo katika Mashariki ya Kati na kusababisha bei za mafuta kupanda katika masoko ya dunia.
Milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Iran, ikiwemo miji ya Konarak na Chabahar.
Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa milipuko minane imetokea katika mji wa Bandar Abbas, huku ikidai kwamba makombora mawili yalipiga bandari za Sirik na Jask, ambazo zote ziko kusini mwa Iran.
Vyombo vya habari vya serikali pia vilisema kuwa makombora mawili yalilipiga kisiwa cha Abu Musa, eneo ambalo limekuwa likizozaniwa umiliki kwa muda mrefu kati ya Iran na Falme za Kiarabu.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya serikali ya Iran, mifumo ya ulinzi wa anga imewashwa katika mji wa Bandar Abbas kufuatia mashambulizi hayo.
Kiwango halisi cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Marekani bado hakijajulikana. Hata hivyo, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kukatika kwa umeme katika mji wa Chabahar na kuzuka kwa moto katika kambi ya Jeshi la Iran mjini Bushehr.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One, Jumatano jioni, Rais Donald Trump alisema Iran ilikuwa imewasiliana na Marekani muda mfupi uliopita na ilikuwa "inataka kufikia makubaliano kwa udi na uvumba."
Trump aliongeza: "Sijui kama wanafaa kufanya makubaliano. Sijui kama watayaheshimu makubaliano hayo, hilo ndilo tatizo."
Unaweza kusoma;
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo