Wanaharakati walaani kufungwa kwa mtandao wa X Tanzania
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kusikitishwa kwake na pia kimelaani uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali ya Tanzania wa kufunga mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter).
Hatua hiyo imethibishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia,Jerry Silaa wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni.
Kwa mujibu wa Slaa, uhalali wa serikali kwa hatua hii unatokana na sera za maudhui za jukwaa, ambazo zinadaiwa kuruhusu maudhui yanayokiuka sheria na maadili ya Tanzania.
Wanaharakati hao wamesema ingawa wanaunga mkono umuhimu wa kudhibiti maudhui ya mtandaoni kwa mujibu wa sheria za kitaifa, ''tunasisitiza kwa nguvu zote kwamba hatua hizo lazima ziwe na uwiano, uwazi, na kuheshimu haki za msingi za binadamu hasa haki za uhuru wa kujieleza na kupata habari''.
Wanaharakati wanadai kurejeshwa mara moja kwa X, Clubhouse Telegramu na majukwaa mengine yoyote yaliyowekewa vikwazo
Wameitaka serikali kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika michakato ya udhibiti wa kidijitali kwa kushirikisha wadau katika kuunda sera za udhibiti wa maudhui zinazoheshimu haki za binadamu.
Pia kuzingatia wajibu wa kikatiba na kimataifa kulinda uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari na haki za kidijitali.
''Tunawaomba wadau wote, ikiwa ni pamoja na jumuiya ya kimataifa, kuendelea kuwa macho na kuunga mkono juhudi za kulinda uhuru wa kidijitali nchini Tanzania''. Ilieleza taarifa ya LHRC.
Unaweza kusoma;