Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Vitisho na wito wa kuwaua "wauaji wa Khamenei" katika mazishi Tehran

Picha zilizotolewa kutoka kwenye maandamano hayo, ikiwa ni pamoja na kurushiwa mawe picha ya Donald Trump na wito wa "kuwaua wauaji'', zilikuwa miongoni mwa mambo yaliyojitokeza.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Zaidi ya watu 1,000 wakamatwa katika operesheni ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu

    Zaidi ya watu 1,000 wamekamatwa katika operesheni ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu iliyofanyika katika nchi 59.

    Operesheni hiyo, iliyoratibiwa na Interpol na kujulikana kama Operation Global Chain, iliwalenga wahusika wa biashara haramu ya binadamu kwa madhumuni ya unyonyaji wa kingono, ajira za kulazimishwa, uhalifu wa kulazimishwa na kuwalazimisha watu kuombaomba.

    Kwa mujibu wa mamlaka, mtandao uliokuwa ukiwasafirisha waathiriwa kwenda Cambodia kwa ajili ya ulaghai wa mtandaoni ulivunjwa, pamoja na mtandao mwingine uliokuwa ukiwalazimisha wasichana wenye umri mdogo waliopatikana kupitia mitandao ya kijamii kujiingiza katika biashara ya ngono barani Ulaya.

    Kwa jumla, waathiriwa 2,070 au watu wanaoshukiwa kuwa waathiriwa walitambuliwa, wengi wao wakiwa wanawake. Kati ya waliokamatwa, watu 334 wanakabiliwa na tuhuma za biashara haramu ya binadamu, huku 690 wakikabiliwa na makosa mengine yanayohusiana na uhalifu huo.

    Interpol, ambayo iliratibu operesheni hiyo kwa kushirikiana na Europol na Shirika la Ulaya la Kulinda Mipaka (Frontex), ilisema matokeo ya operesheni hiyo yamebaini njia na mbinu mpya zinazotumiwa na mitandao ya biashara haramu ya binadamu.

    Operesheni hiyo iligundua mwenendo mpya ambapo waathiriwa kutoka Amerika ya Kusini wanasafirishwa kwenda Ulaya kwa ajili ya kazi za kulazimishwa. Takribani asilimia 10 ya waathiriwa waliotambuliwa walikuwa watoto kutoka bara la Amerika waliolazimishwa kufanyiwa unyonyaji wa kingono.

    Katika hatua nyingine, mamlaka nchini Colombia zilianzisha kampeni ya uhamasishaji katika viwanja vya ndege ili kuwaonya wasafiri kuhusu hatari ya matangazo ya ajira za ulaghai nje ya nchi.

    Interpol pia ilisema Polisi wa Brazil walitambua waathiriwa 406, raia 83 wa Brazil na raia 323 wa kigeni, waliokuwa sehemu ya mtandao wa kimataifa uliokuwa ukiwasafirisha watu kwenda Cambodia, ambako walilazimishwa kushiriki katika ulaghai wa mtandaoni.

    Unaweza kusoma;

  2. ‘Maandamano Saba saba’: Ulinzi mkali waendelea Dar Es Salaam

    Hali ya ulinzi imeonekana kuimarishwa zaidi katika jiji kuu la kibiashara la Tanzania Dar es Salaam, huku mamia ya maafisa polisi na jeshi wakionekana kutanda katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

    Hatua hii inafuatia wito wa maandamano kutoka kwa baadhi ya wanaharakati wa mitandaoni, wakidai mabadiliko na uwajibikaji kwa serikali.

    BBC imeshuhudia doria za vyombo vya usalama katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.

    Hata hivyo, maafisa hao hawajaweka vizuizi vya barabarani na wananchi wapo huru kuendelea na shughuli zai za kawaida. Hata hivyo kuna idadi ndogo ya magari na watu barabarani, leo ikiwa ni sikukuu nchini humo.

    BBC imeshuhudia uwepo wa maafisa usalama waliojihami kwa silaha makutano ya barabara za Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma eneo la Mwenge na Makutano ya Ali Hassan Mwinyi n Barabara ya Kawawa/Mwai Kibaki eneo la Kinondoni Morocco.

    BBC pia imeshuhudia uwepo wa Askari wenye silaha katika vituo vingi vya mabasi ya mwendokasi jijini humo. Maafisa hao pia wameonekana katikati ya jiji eneo la Posta ambapo walikuwa wamejihami na gari ambayo humwaga maji ya kuwasha.

    Kumeshuhudiwa ulinzi mkali pia katikati njia za kuingia katika bandari kuu ya Dar Es Salaam pamoja na eneo la bandari lenye maghala ya kuhifadhia mafuta upande wa Kigamboni.

    Hata hivyo duru zinzonesha kuwa hofu ya ghasia na kumbukumbu za mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba mwaka jana pamoja na kushindikana kwa maandamano yaliyoitishea Desemba 9 mwaka jana huenda kukapungunga matarajio ya kufanyika kwa maandamano hayo siku ya leo.

    Makundi kadhaa ya haki za binadamu na upinzani yanasema maelfu ya watu waliuawa katika machafuko yaliyotokana na uchaguzi wa Oktoba 2025, huku takwimu rasmi za serikali zikisema ni takribani watu 500 ndio waliofariki.

  3. Siku ya Saba Saba: Polisi waweka vizuizi vya usalama kote jijini Nairobi

    Polisi imeimarisha vizuizi vya usalama kwenye barabara kuu za Nairobi huku Wakenya wakiadhimisha Siku ya Saba Saba.

    Polisi imesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kudumisha usalama, amani na utulivu wakati wa maadhimisho ya kila mwaka ya Saba Saba. The Star imeripoti

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Msemaji wa Polisi, Michael Muchiri, alisema hatua za kuimarisha usalama zimechukuliwa kutokana na uzoefu wa miaka iliyopita ambapo baadhi ya maandamano yaligeuka kuwa ya vurugu, na kusababisha uvunjifu wa amani pamoja na kuvurugika kwa shughuli za kawaida za biashara.

    “Huduma ya Kitaifa ya Polisi inapenda kuwafahamisha wananchi wote kwamba, kutokana na yaliyoshuhudiwa wakati wa maadhimisho ya Saba Saba katika miaka iliyopita, baadhi ya watu wamehusika katika vitendo vya kuvunja amani, jambo lililoathiri shughuli za kawaida za wale ambao hawashiriki maandamano,” ilisema taarifa hiyo.

    Muchiri alisema vizuizi hivyo vinatumika kudhibiti mienendo ya watembea kwa miguu na magari ndani ya jiji, huku polisi wakilenga kuzuia vurugu na kuhakikisha usalama wa umma.

    Ripoti zinaonesha kuwa maafisa wa polisi wamepelekwa katika maeneo mbalimbali ya Nairobi na miji mikuu kama Kitengela, Mlolongo, Rongai, Githurai, Waiyaki Way na maeneo mengine.

    Baadhi ya sehemu za katikati mwa jiji la Nairobi zimetangazwa kuwa maeneo yasiyoruhusiwa kufikiwa.

    Muchiri aliwataka wananchi kushirikiana na maafisa wa polisi na kufuata maelekezo ya usalama ili kusaidia kudumisha amani na utulivu siku nzima.

    Polisi pia wameonya kuwa mtu yeyote atakayepatikana akijihusisha na vitendo visivyo halali atachukuliwa hatua za kisheria.

    Maadhimisho ya Saba Saba, yanayofanyika kila mwaka tarehe 7 Julai, yamekuwa yakihusishwa kihistoria na maandamano yanayodai mageuzi ya kisiasa na kiutawala, huku mamlaka mara nyingi zikiongeza idadi ya maafisa wa usalama kwa matarajio ya mikusanyiko mikubwa ya watu.

  4. Safari ya Ronaldo katika Kombe la Dunia yafikia mwisho kwa machozi

    Mmoja wa wasakata kabumbu mahiri kuwahi kutokea duniani Cristian Ronaldo wa Ureno amelazimika kuimaliza kazi yake bila kutwaa tuzo kubwa zaidi duniani baada ya mechi yake ya mwisho kwa Ureno kumalizika kwa kushindwa 1-0 na Hispania katika hatua ya 16 bora.

    Ronaldo alibubujikwa machozi huku hadithi yake ya Kombe la Dunia ikimalizika jijini Dallas baada ya kushuhudia goli la dakika za majeruhi la Mikel Merino likiwapa majirani zao nafasi ya kutinga robo fainali.

    Mshindi huyo wa Ballon d'Or mara tano, mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano na bingwa wa Euro 2016 mwenye umri wa miaka 41, ana rekodi ya dunia ya kufunga mabao 976 kwa vilabu na nchi yake.

    Amefunga mabao sita kwa rekodi ya Kombe la Dunia. Lakini ushindi wake wa karibu zaidi ya kombe la dunia ni wakati Ureno ilipocheza nusu fainali katika fainali zake za kwanza mwaka 2006 huko Ujerumani.

    Leo usiku ni Misri dhidi ya Argentina na Uswisi ikicheza na Colombia kukamilisha hatua ya 16 bora.

    Unaweza kusoma;

  5. Zelensky kuishinikiza NATO kuipatia Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga baada ya mashambulizi makali ya Urusi

    Rais wa Ukraine anapanga kutumia mkutano wa NATO nchini Uturuki kuwahimiza washirika wa Kyiv kuipatia mifumo ya ulinzi wa anga inayohitaji kwa dharura ili kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi yanayozidi kuongezeka.

    Wito wa Volodymyr Zelensky wa kuomba msaada umeongezeka uzito baada ya makombora ya Urusi kushambulia mji mkuu wa Ukraine mara mbili ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja, yakipiga majengo ya makazi na kusababisha vifo vya zaidi ya raia 50.

    Mkutano huo mjini Ankara pia utampa Zelensky fursa ya kukutana na Donald Trump katika mazungumzo muhimu na kusisitiza hoja yake kwamba mashambulizi ya "kikatili" ya Urusi yanaonesha udhaifu badala ya nguvu, na kwamba Vladimir Putin anapaswa kushinikizwa kuingia katika mazungumzo yatakayolenga kufikia amani yenye "heshima."

    Mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Ukraine yanakuja wakati nchi hiyo imekuwa ikiongeza mashambulizi yake ya masafa marefu kwa kutumia ndege zisizo na rubani dhidi ya Urusi, ikilenga viwanda vya kusafisha mafuta na maeneo ya kijeshi, hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa mafuta na kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo ya Urusi.

    Unaweza kusoma;

  6. Vitisho na wito wa kuwaua "wauaji wa Khamenei" katika mazishi Tehran

    Shughuli rasmi za mazishi ya aliyekuwa kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu katikati mwa Tehran, pamoja na mabadiliko na hali ya kutokuwepo kwa mwafaka iliyowachanganya maelfu ya watu, iliambatana pia na kauli kali dhidi ya Masoud Pezeshkian, Abbas Araqchi na wajumbe wa mazungumzo na Marekani.

    Picha zilizotolewa kutoka kwenye maandamano hayo, ikiwa ni pamoja na kurushiwa mawe picha ya Donald Trump na wito wa "kuwaua wauaji" wa Ali Khamenei, zilikuwa miongoni mwa mambo yaliyovutia katika hafla hiyo, ambayo ilifanyika kwa uratibu na maandalizi makubwa ya serikali.

    Donald Trump ametoa tena vitisho vipya dhidi ya Iran, akisema kwamba ikiwa makubaliano hayatapatikana na Iran, "atakamilisha kazi."

    Akijibu tishio hilo, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kwa Rais wa Marekani: "Zungumza kwa heshima na watu wa Iran, la sivyo tutakujibu kwa lugha tofauti."

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi,katika taarifa zetu