Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump atishia Iran usitishaji mapigano "umefutiliwa mbali"; Iran yaonya kuwa "watajibu bila uwoga"

Trump alipokuwa akiuita uongozi wa Iran kuwa "wakihuni" na "unaougua", Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: "Hatulipizi matusi kwa matusi, bali kwa vitendo."

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Jeshi la Iran limesema limeshambulia maeneo 85 ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait na Bahrain

    Jeshi la Iran limetangaza kuwa limeanzisha mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika kile lilichokitaja kuwa ni jibu la mashambulizi yaliyofanywa na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) dhidi ya zaidi ya malengo 80 kusini mwa Iran.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Julai 8, IRGC ilidai kuwa Marekani ilikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na makubaliano ya Islamabad kwa kufanya mashambulizi ya anga mapema asubuhi dhidi ya vituo vya pwani na maeneo ya kiraia katika mikoa ya Hormozgan na Mahshahr.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika "hatua ya awali ya kujibu uchokozi huo," vikosi vya majini na anga vya IRGC vilifanya mashambulizi ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni), yakidai kulenga na kuharibu vituo 85 muhimu vya kijeshi vya Marekani, vikiwemo eneo la Port Salman, Makao Makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani nchini Bahrain, pamoja na Kambi ya Anga ya Ali Salem nchini Kuwait.

    IRGC pia ilidai kuwa ilidungua ndege moja isiyo na rubani aina ya MQ-9 ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuingilia operesheni hiyo.

    Kabla ya tangazo hilo, jeshi la Kuwait lilisema lilikuwa limewasha mifumo yake ya ulinzi kutokana na kile lilichokiita mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani, huku pia kukiwa na ripoti za ving'ora vya tahadhari kusikika nchini Bahrain.

    Tangazo la IRGC kuhusu mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait na Bahrain limetolewa wakati Iran imeendelea kukanusha kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli tatu za kubeba mafuta katika Mlango wa Hormuz yaliyotokea Jumanne, Julai 6.

    Mashambulizi hayo yamezua mzozo mpya wa kijeshi kati ya Iran na Marekani. Wakati Iran ikikanusha kuhusika, Qatar, Saudi Arabia na Marekani zimeilaumu IRGC kwa kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli hizo.

    Unaweza kusoma;

  2. Wafanyakazi wa bandari wanavyohofu kupoteza kazi kutokana na maatumizi ya AI

    Wafanyakazi wa bandari nchini Australia wanadai wiki ya kazi ya saa 28 bila kupunguziwa mishahara, huku matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia ya otomatiki yakizidi kuongezeka katika bandari za nchi hiyo.

    Shinikizo la kuanzishwa kwa AI linaongozwa na kampuni kubwa ya usafirishaji na uendeshaji wa bandari, DP World, ambayo Chama cha Wafanyakazi wa Baharini cha Australia (MUA) kinasema kimeweka ajira za wafanyakazi "kwenye hatari kubwa."

    Chama hicho kilisema: "Ikiwa DP World inataka kutumia AI na otomatiki, basi lazima ilipe faida za kijamii zinazotokana na teknolojia hiyo. Teknolojia mpya haipaswi kuwagharimu wanachama wetu ajira zao au kuhatarisha maisha yao ili tu kampuni iongeze faida."

    BBC imewasiliana na DP World kuomba maoni yao na pia imeiomba MUA kutoa maelezo zaidi kuhusu madai hayo.

    DP World, yenye makao makuu yake Dubai, imekuwa ikijaribu kutumia zana za AI kusimamia wafanyakazi na kupanga ratiba za kazi katika shughuli zake, kwa mujibu wa utafiti wa Kituo cha Kimataifa cha Uwajibikaji na Utafiti wa Kodi za Makampuni, uliofanywa kwa agizo la MUA.

    Utafiti huo unasema mpango wa kuongeza matumizi ya otomatiki ni sehemu ya mwenendo wa kuingiza AI katika shughuli za kampuni "bila mashauriano ya kweli," na kwamba unaweza kuhatarisha ajira za hadi wafanyakazi 1,000, sawa na zaidi ya asilimia 60 ya wafanyakazi wa bandarini na wa matengenezo.

    Pia ilielezwa kuwa kampuni hiyo imependekeza matumizi ya kreni zinazoendeshwa kwa udhibiti wa mbali kwa msaada wa AI pamoja na magari yanayojiendesha yenyewe.

    Chama cha MUA kimesema teknolojia hiyo "inapaswa kutumika kuboresha maisha ya wafanyakazi, si kuyaharibu," huku kikisisitiza wito wake wa kuanzishwa kwa wiki ya kazi ya saa 28.

    Kwa mujibu wa gazeti la Australian Financial Review, ambalo lilikuwa la kwanza kuripoti kuhusu mazungumzo hayo, wafanyakazi wa DP World kwa sasa wanaaminika kufanya kazi kati ya saa 32 na 35 kwa wiki, kutegemea eneo walipo.

    DP World, kampuni inayomilikiwa na serikali ya Dubai, ni miongoni mwa waendeshaji wakubwa zaidi wa bandari duniani na iko chini ya usimamizi wa mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum.

    Nchini Australia, kampuni hiyo husafirisha mamilioni ya makasha ya mizigo kila mwaka kupitia bandari zake zilizopo Sydney, Melbourne na maeneo mengine ya nchi.

    Ikiwa na shughuli katika nchi 84 na zaidi ya wafanyakazi 126,000 duniani kote, DP World hushughulikia takriban asilimia 10 ya usafirishaji wa makasha ya mizigo duniani.

    Unaweza kusoma;

  3. Misri yakerwa na 'dhuluma' na kudai Messi alipendelewa

    Zikiwa zimesalia dakika 12 kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida wa mchezo, Misri ilikuwa karibu kuandika historia kwa kupata ushindi wake mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika Kombe la Dunia.

    Mafarao walikuwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Argentina, mabingwa watetezi wa dunia, kwenye Uwanja wa Atlanta.

    Nafasi ya kufuzu kwa robo fainali kwa mara ya kwanza ilikuwa karibu kutimia kwa taifa hilo la Afrika linalopenda sana soka.

    Lakini mambo yalibadilika kwa kasi kubwa.

    Cristian Romero alipofunga bao la kwanza la Argentina katika dakika ya 79, Misri ilihitaji tu kujilinda hadi mwisho wa mchezo. Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla wakati nahodha Lionel Messi aliposawazisha matokeo kuwa 2-2 dakika nne baadaye.

    Kisha Enzo Fernandez alifunga bao la ushindi kwa kichwa katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza, na kuwafanya mashabiki wa Argentina kushangilia kwa furaha.

    Misri ilitoka uwanjani ikiwa imevunjika moyo na yenye hasira, hasa baada ya Mfumo wa Usaidizi wa Waamuzi kwa Video (VAR) kulifuta bao la pili la Mostafa Zico kutokana na faulo iliyodaiwa kufanywa na kiungo Marwan Attia, aliyepatikana amemkanyaga kidogo Lisandro Martinez mwanzoni mwa shambulizi hilo wakati Misri ikiwa inaongoza kwa bao 1-0.

    Wachezaji wa Misri pia walisisitiza kuwa Mohamed Salah alifanyiwa faulo ndani ya eneo la penalti la Argentina sekunde chache kabla ya mabingwa hao wa dunia kuanzisha shambulizi lililozaa bao la ushindi.

    Mwamuzi wa Ufaransa, Francois Letexier, alipopuliza filimbi ya mwisho, wachezaji wengi wa Misri walianguka chini kwa mshangao na huzuni kutokana na kilichotokea.

    Katika mahojiano makali baada ya mchezo, kocha wa Misri, Hossam Hassan, alisema timu yake "haikutendewa haki" na kwamba "ilidhulumiwa." BBC Sport imesema imeiomba FIFA kutoa maoni kuhusu madai hayo.

    "Kuna mambo mengi ya kuhojiwa ndani na nje ya uwanja," alisema Hassan.

    "Kulikuwa na mambo mengi yasiyoridhisha. Kinachozungumziwa hapa ni uaminifu na namna mchezo ulivyochezeshwa.

    "Huenda walitaka mabingwa wa dunia waendelee kubaki kwenye mashindano. Huenda walitaka Messi aendelee kushiriki.

    "Mabingwa wa dunia walipata msaada katika kila namna. Inaonekana kulikuwa na shinikizo kutoka upande wa Argentina kuhusu matokeo haya."

    Mchezo huo ulikuwa na kila aina ya drama: penalti iliyookolewa, bao lililofutwa na VAR, kadi nyekundu, pamoja na kurejea kwa kushangaza kwa Argentina kutoka nyuma kwa mabao mawili na kushinda bila kuhitaji muda wa nyongeza.

    BBC Sport imechambua mechi hiyo, ambayo itaingia kwenye historia ya Kombe la Dunia kama mojawapo ya mechi za kusisimua zaidi, baada ya timu iliyokuwa nyuma kwa mabao mawili hadi dakika za mwisho kuibuka na ushindi ndani ya muda wa kawaida.

    Unaweza kusoma;

  4. Marekani yaanzisha mashambulizi dhidi ya Iran baada ya meli za mafuta kushambuliwa katika Mlango wa Hormuz

    Marekani imeanzisha mashambulizi makali dhidi ya Iran kujibu mashambulizi yaliyolenga meli tatu za kubeba mafuta katika Mlango wa Hormuz.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) ilisema Jumanne kuwa ilishambulia zaidi ya malengo 80, yakiwemo zaidi ya boti ndogo 60 za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) zilizokuwa katika mlango huo wa bahari.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema mashambulizi ya Marekani ni ukiukaji wa makubaliano ya maelewano kati ya Marekani na Iran yaliyotiwa saini mwezi uliopita, na kuonya kwamba Tehran "itachukua hatua madhubuti."

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema mashambulizi yalilenga Kisiwa cha Qeshm, Bandar Abbas na Sirik, ambapo baadhi ya watu walijeruhiwa. Iran haijatangaza rasmi kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli tatu za mafuta yaliyosababisha Marekani kuanzisha mashambulizi hayo.

    Centcom ilisema mbali na kushambulia boti hizo ndogo zaidi ya 60, pia ililenga maeneo ya kurushia makombora na vituo vya uongozi vya Iran, lakini haikutaja maeneo halisi ya mashambulizi hayo.

    Marekani ilikuwa imeonya kwamba kungekuwa na madhara kufuatia kile ilichokiita mashambulizi "yasiyokubalika kabisa" dhidi ya meli hizo tatu za mafuta.

    Kabla ya mashambulizi hayo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilifuta msamaha uliokuwa umesitisha kwa muda vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran. Msamaha huo ulikuwa sehemu ya makubaliano ya maelewano yaliyotiwa saini kati ya Washington na Tehran mwezi uliopita.

    Unaweza kusoma;

  5. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo