Rais Samia atoa onyo dhidi ya waliochochea vurugu

Rais Samia akemea vikali vitendo vya uvunjifu wa sheria vilivyotokea wakati wa Uchunguzi Mkuu.

Moja kwa moja

Na Waandishi wa BBC

  1. Waandamanaji 10 wamefariki dunia katika vurugu inayoshuhudiwa Tanzania - UN

    Upinzani umeishutumu serikali kwa kuhujumu demokrasia, jambo ambalo inakanusha
    Maelezo ya picha, Upinzani umeishutumu serikali kwa kuhujumu demokrasia, jambo ambalo inakanusha

    Umoja wa mataifa kitengo cha haki za kibinadamu umesema kuwa idadi ya waandamanaji waliofariki dunia kufikia sasa tangu maandamano yaanze sambamaba na siku ya uchaguzi nchini Tanzania ni kumi pekee.

    ''Ripoti tulizopokea zinaashiria kwamba watu takribani 10 wameuawa," yasema Umoja wa Mataifa.

    Umoja wa Mataifa pia imetoa wito kwa vikosi vya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

    "Tumetamaushwa na idadi ya vifo na majeruhi yaliyoshuhudiwa katika maandamano yanayoendelea nchini Tanzania''.Shirika la habari la Reuters lilimnukuu msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu Seif Magango akisema.

    Kauli yao inatolewa wakati fununu zimesambaa kuwa ni takriban watu 700 wamefariki katika maandamano yaliyogeuka kuwa vurugu huko Tanzania bara.

    Wakati huo huo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Kenya limeiambia BBC kuwa mawasiliano yamekatizwa katika nchi jirani ya Tanzania na halijaweza kuthibitisha ripoti za vifo.

    ''Hospitali nchini humo hazikubali kutoa taarifa kwa waandishi wa habari au mashirika ya kutetea haki za binadamu wanapoulizwa kuhusu visababishi.''

    Pia unaweza kusoma:

  2. Watalii wakwama katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar

    Watalii wakwama katika uwanja wa ndege wa Al Ubeid

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Watalii wakwama katika uwanja wa ndege wa Al Ubeid Zanzibar

    Saa chache baada ya Ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari kwa raia wake wanaoishi nchini Tanzania na kuwataka wasalie majumbani mwao, watalii waliokuwa wamefika katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar wamekwama kutokana na safari za ndege kusitishwa.

    haya yanajiri siku moja baada ya uchaguzi mkuu wenye utata nchini Tanzania, huku kukiripotiwa machafuko na maandamano yenye vurugu katika maeneo ya bara, wakati huduma za intaneti na mawasiliano mengine zikiwa zimekatizwa.

    Kupitia taarifa iliotolewa kwenye tovuti ya ubalozi wa Marekani iliwajulisha raia wake kuthibitisha safari zao kwanza kwa njia ya simu kabla ya kusafiri kuelekea uwanja wa ndege kwani safari za ndege nyingi za kimataifa zimefutwa

    Aidha, imeongeza kuwa kusafiri kwa barabara kuna hatarisha maisha yao na kuwataka wasalie majumbani mwao na wajiepushe kushiriki maandamano yanayoendelea Tanzania bara.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Upinzani wapinga matokeo ya uchaguzi wa urais Zanzibar

    Othman Masoud

    Chanzo cha picha, ACT-Wazalendo

    Maelezo ya picha, Othman Masoud aligombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha upinzani cha ACT - Wazalendo

    Chama cha upinzani, ACT-Wazalendo, kimepinga matokeo ya uchagauzi wa urais visiwani Zanzibar baada ya Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC kumtangaza mshindi Hussein Mwinyi,

    "Wananchi wameibiwa sauti yao... Suluhu pekee ya kupata haki ni uchaguzi mpya," kilisema chama hicho.

    Afisa mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo aliiambia shirika la habari la AFP kwamba masanduku ya kupigia kura yalikuwa mengi, watu waliruhusiwa kupiga kura mara kadhaa bila kitambulisho na mawakala wao wa uchaguzi walifukuzwa kwenye vyumba vya kuhesabia kura.

    Wakati huo huo, Chama tawala (Chama Cha Mapinduzi: CCM) kinatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari baadaye hii leo.

    Wafuasi wa upinzani Zanzibar, waliionekana wakitoa malalamishi yao kwa hofu.

    "Hakujawa na uchaguzi wa kuaminika tangu mwaka 1995," alisema mzee mmoja mwenye umri wa miaka 70, akiashiria kura ya kwanza ya Tanzania ya vyama vingi.

    Hakuna hata mmoja wa waliohojiwa aliyetaja jina lake.

    "Tunaogopa kuongea kwa sababu wanaweza kuja nyumbani kwetu na kutuchukua," alisema mmoja.

    Othman Masoud aliyegombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT- Wazalendo ni mwanasheria mwenye taaluma ya juu na uzoefu mpana serikalini.

    Kabla ya kuingia rasmi katika siasa za upinzani, aliwahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa mashtaka (2002–2011) na baadaye mwanasheria mkuu wa Serikali wa Zanzibar.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Mufti wa Tanzania aomba Waislamu kuswali adhuhuri nyumbani

    .

    Chanzo cha picha, Muftitanzania/Instagram

    Mufti wa Tanzania Dk. Abubakar Zubeir bin Ally ameomba Waislamu kuswali swala ya adhuhuri nyumbani badala ya kwenda msikitini.

    Kama Sheikh mkuu, yeye ndiye mamlaka ya kidini kwa Waislamu nchini Tanzania.

    Mara kwa mara huwa anatoa taarifa kwa umma kwa niaba ya jamii ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na kutoa wito wa umoja na amani wakati wa uchaguzi.

    Msemaji wa serikali Gerson Msigwa, hapo jana 30/10/2025, alitoa taarifa inayowataka watumishi wa umma kuendelea kufanyia kazi nyumbani isipokuwa kwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawahitaji kuwa katika vituo vyao vya kazi.

    Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa ni kufuatia angalizo la kiusalama lililotangazwa Jumatano 29,Oktoba, 2025 na Jeshi la Polisi.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2025: Matokeo ya awali yaendelea kutangazwa

    .

    Chanzo cha picha, NEC

    Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania inaendelea kutangaza matokeo ya awali ya urais ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika 29 Oktoba, 2025.

    Matokeo hayo yamepokelewa kutoka maeneo bunge mbalimbali.

    Kulingana na matokeo ya awali yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, yanaonyesha kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan yuko kifua mbele.

    INEC ilikuwa imesema kuwa itamtangaza mshindi wa urais ndani ya saa 72 baada ya uchaguzi kufanyika 29/10/2025.

  6. Uchaguzi Tanzania 2025: Mtandao waendelea kuminywa kwa siku ya tatu mfululizo

    .

    Mtandao umeendelea kuminywa nchini Tanzania kwa siku ya tatu na kufanya mawasiliano kuwa magumu.

    Hapo jana, ulionekana kurejea kwa muda kidogo tu kama takriban saa moja hivi kabla ya kuanza tena kuminywa.

    Hatua hii imefanya hata mawasiliano katika mitandao ya kijamii kuathirika na hivyo kufanya iwe vigumu vile vile kujua hali inavyoendelea nchini humo.

    Jana, 30/10/2025, maandamano yalishuhudiwa kwa siku ya pili mfululizo na kusababisha vurugu na ghasia.

    Baaadhi ya barabara pia zilikuwa zimewekwa vizuizi.

    Nchi kama vile Marekani na Uingereza zilitoa tahadhari ya usafiri kwa raia wake wanaoishi nchini humo.

    Soma zaidi:

  7. Ubalozi wa Marekani waonya raia wake kuwa usafiri wa barabarani unahatarisha maisha yao

    .

    Ubalozi wa Marekani umetoa tahadhari kwa raia wake wanaoishi nchini Tanzania.

    Taarifa hiyo imetolewa kwenye tovuti ya ubalozi huo na kusema kuwa Tanzania imekumbwa na maandamano ya nchi nzima na kusababisha "vurugu na vizuizi vya barabarani."

    Aidha, imeongeza kuwa kusafiri kwa barabara kuna hatarisha maisha yao.

    Ufikiaji wa mtandao bado umekuwa na jambo gumu na kufanya mawasiliano yote kuwa magumu.

    Aidha, ubalozi huo umesema kuwa safari za ndege nyingi za kimataifa zimefutwa na kushauri raia wake kuthibitisha safari zao kwanza kwa njia ya simu kabla ya kusafiri kuelekea uwanja wa ndege.

    Ubalozi huo umewataka raia wake kuepuka maandamano, maeneo yenye mkusanyiko wa watu, kuepuka kujitokeza hadharani, kufuatilia taarifa za vyombo vya habari pamoja na kufahamu mazingira walioko.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Baadhi ya wasanii wafuta maudhui yanayoegemea CCM Tanzania

    .

    Vurugu ambazo zimeshuhudiwa nchini Tanzania zimeonekana kulenga watu mashuhuri kama vile wasanii na wanamitindo wanaodaiwa kuunga mkono serikali ba kusababisha kuvamiwa na kuharibiwa kwa biashara zao.

    Kufuatia hatua hiyo, baadhi yao wamefuta picha na video walizochapisha kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram zakumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

    Wakiongozwa na msanii wa nyimbo za bongo Naseeb Abdul almarufu Diamond Platnumz wamefuta maudhui hayo waliokuwa wakiyachapisha wakati wa kampuni za uchaguzi mkuu.

    Miongoni mwa waathirika wa kwanza ni mwimbaji Shilole, ambaye mgahawa wake maarufu wa Shishi Foods, ulichomwa moto katika machafuko hayo.

    Mkuu wa jeshi nchini Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda alitoa taarifa akilaani vurugu zinazoendelea na kusema kuwa ni 'lazima utawala wa sheria uzingatiwe' na kuonya kuwa wahusika watachukuliwa hatua.

    Soma zaidi

  9. Serikali yaonya Wakenya dhidi ya kushiriki maandamano ya Tanzania

    .

    Chanzo cha picha, PS Omollo Raymond/ FB

    Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Raymond Omollo amewaonya Wakenya dhidi ya kushiriki maandamano kinyume cha sheria mpakani mwa Kenya na Tanzania, akionya kuwa yeyote atakayepatikana akisababisha fujo atakabiliwa na sheria.

    Onyo lake linafuatia ripoti za maandamano katika vituo kadhaa vya mpakani, ikiwa ni pamoja na Namanga, ambapo baadhi ya wakazi waliripotiwa kuingia barabarani kwa mshikamano na Watanzania kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumatano.

    Akizungumza na vyombo vya habari mjini Mombasa, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Kenya ina sheria na kanuni wazi zinazosimamia maandamano na kuwataka raia kuendesha shughuli zao ndani ya mipaka ya kisheria.

    "Kama nchi, tuna sheria na kanuni zinazoongoza maandamano. Wito wangu ni kwamba yeyote anayetaka kushiriki katika shughuli kama hizo lazima afanye hivyo kwa mujibu wa sheria," alisema Omollo.

    Hakutaka kuzungumzia hali nchini Tanzania, akibainisha kuwa ni suala la ndani kwa nchi hiyo jirani.

    "Nisingependa kuzungumza na kile kinachotokea Tanzania. Ni majirani zetu marafiki na tunawatakia kila la kheri wanapopitia michakato yao ya kidemokrasia," alisema. Waziri pia aliwahimiza wakazi na wafanyabiashara wanaofanya kazi kando ya mpaka kushirikiana na mamlaka ili kuepuka usumbufu wakati wanaendesha shughuli zao.

    "Ikiwa kuna usumbufu wowote…, maafisa katika vituo vyetu vya kuingia na kutoka mpakani watatoa mwongozo ili kuhakikisha usalama wa maisha na mwendelezo wa biashara", aliongeza.

    Soma zaidi:

  10. Habari za hivi punde, Hussein Mwinyi ashinda uchaguzi wa urais Zanzibar

    Mwinyi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imemtangaza Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais katika visiwa hivyo.

    Dk.Mwinyi aligombea kwa tiketi ya chama tawala cha CCM, ambacho hakijawahi kushindwa uchaguzi tangu uhuru.

    Zanzibar, eneo linalojitawala ndani ya Tanzania, lilipiga kura siku ya Jumatano.

    Mwinyi, aliye na umri wa miaka 59, ameingia kwenye uchaguzi huu wa 2025 akibeba bendera ya CCM kwa mara ya pili mfululizo.

    Tangu kuingia madarakani, ameelekeza juhudi zake katika maeneo matatu makuu: utalii, uwekezaji na huduma za kijamii.

    Pia amesifiwa kwa kuendesha Zanzibar yenye hali ya utulivu na mshikamano zaidi kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tofauti na misuguano ya kisiasa iliyoshuhudiwa kabla ya hapo.

    Soma pia:

  11. Mkuu wa jeshi Tanzania alaani vurugu zinazoendelea

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkuu wa jeshi nchini Tanzania amelaani vitendo vya vurgu vinavyoendelea kote nchini humo na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria.

    Katika hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa, Jenerali Jacob John Mkunda alisema ni 'lazima utawala wa sheria uzingatiwe' na kuonya kuwa wahusika watachukuliwa hatua.

    Aliongeza kuwa jeshi linashirikiana na vyombo vingine vya usalama kudhibiti hali ya usalama huku akiwataka wanaoendesha vurugu hizo kuyakomesha mara moja.

    Taarifa hiyo imetolewa wakati maandamano yakizidi kuongezeka katika miji mikubwa.

    Mkunda alisema jeshi na vyombo vingine vya usalama vilikuwa vinashirikiana kudhibiti hali hiyo.

    Mvutano uliongezeka baada ya matokeo ya uchaguzi kuonyesha Rais Samia Suluhu anaongoza katika maeneo kadhaa.

    Waandamanaji wanashutumu serikali kwa kunyamazisha upinzani huku waangalizi wa Umoja wa Ulaya wakisema uchaguzi 'haukuwa huru na wa haki'.

    Soma Pia:

  12. Ufunguzi wa Vyuo Vikuu Tanzania waahirishwa

    Wazara ya Elimu Sayansi naTeknolojia nchini Tanzania imetangaza kuahirishwa kwa ufungui wa vyuo vikuu,vyuo vya elimu ya juu na kati hadi itakapotangazwa tena.

    Vyuo hivyo viliatarajiwa kufunguliwa tarehe 3 mwezi Novemba.

    Tangazo hilo pia linawajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo ambao walipaswa kujiunga tarehe moja Novemba.

    Soma pia:

  13. Raia wa Uingereza walioko Tanzania watakiwa kuchukua tahadhari

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Raia wa Uingereza wanaoishi nchini Tanzania wameshauriwa kuchukua tahadhari na kujilinda kufuatia ghasia na maandamano yanayoendelea kuripotiwa nchini humo.

    Kulingana na taarifa ya ubalozi wa Uingereza iliotolewa tarehe 30 Oktoba, ubalozi huo aidha umewashauri raia wake wafuate amri zinazotolewa na serikali ya Tanzania kipindi hiki.

    'Zingatieni amri ya kutotoka nje, fuata ushauri wa serikali za mitaa na pia epukeni maandamano', yasema taarifa hiyo.

  14. Vurugu za uchaguzi Tanzania: Hali ikoje Mwanza?

    Hali ya sintofahamu iliendelea kushuhudiwa mjini Mwanza usiku wa kuamkia leo kutokana na hali ngumu iliyotokana na maandamano ya vijana maarufu Gen Z wakipita katika maeneo mbali mbali ya mji na kuzua hali ya taharuki hasa walipokuwa wakipambana na vikosi vya usalama.

    mali Milio ya risasi na mabomu ya machozi ilisikika katika maeneo kadha wa kadha ya jiji hilo.

    Kituo kikuu cha mabasi cha Nyegezi kuelekea eneo la Buhongwa waandamanaji wameripotiwa kufukuzana na polisi baada ya kituo cha polisi kuteketezwa.

    Katika barabara kuu kutoka Mwanza mjini kuelekea eneo la uwanja wa ndege waandamanaji walipambana na polisi wamekuwa wakipambana vilivyo na ofisi ya kata na kituo kidogo cha polisi nacho kikachomwa moto. Katika eneo la Nyamanolo mkabala na Fwatiati hali sio shwari kwani huko pia kituo cha polisi na ofisi ya kata ya CCM kilichomwa moto.

    Waandamanaji pia walivamia duka kubwa la jumla yaani Super Market na kulipora.

    Soma pia:

  15. Watumishi wa umma Tanzania kuendelea kufanya kazi nyumbani

    G

    Chanzo cha picha, Msigwa/X

    Msemaji wa serikali Gerson Msigwa ametoa taarifa inayowataka watumishi wa umma kuendelea kufanyia kazi nyumbani isipokuwa kwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawahitaji kuwa katika vituo vyao vya kazi.

    Taarifa hiyo inaendelea kusema kuwa ni kufuatia angalizo la kiusalama lililotangazwa jana Jumatano 29,Oktoba,2025 na Jeshi la Polisi.

    Aidha wanafunzi wote wa shule na vyuo wameombwa kuendelea kujisomea manyumbani na waajiri katika sekta binafsi wameshauriwa kuzingatia tahadhari hiyo na kuwaruhusu wafanyakazi wao kufanyia pia kazi majumbani.

    Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania Camillius Wambura jana alitangaza amri ya kutotoka nje mjini Dar es Salam kuanzia saa kumi na mbili jioni.

    Hatua hizo zinafuatia maandamano ya umma yaliyoshuhudiwa katika miji mbali mbali nchini Tanzania,kupinga uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano 29,Oktoba, 2025.

    Soma pia:

  16. Maandamano yashuhudiwa Namanga mpaka wa Kenya na Tanzania

    Waandamanaji waingia mtaani mpakani Namanga
    Maelezo ya picha, Waandamanaji waingia mtaani mpakani Namanga

    Mtu mmoja anahofiwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mapambano makali kati ya waandamanaji na polisi katika mpaka wa Namanga, kituo kikuu cha usafiri kinachounganisha Kenya na Tanzania.

    Makabiliano hayo yalianza mapema asubuhi na kuendelea kutwa nzima huku waandamanaji wakiingia barabarani kupinga uchaguzi mkuu wa Jumatano nchini Tanzania, ambao wanadai haukuwa huru na wa haki.

    Polisi walijibu kwa kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira katika kujaribu kuwatawanya waandamanaji hao.

    Machafuko hayo yalisitisha shughuli zote za kibiashara katika mji huo wa mpakani wenye shughuli nyingi.

    Malori ya kusafirisha bidhaa kutoka na kuingia nchini humo yamekwamba mpakani.

    Mamlaka bado hazijatoa tamko rasmi kuhusu idadi ya waliopoteza maisha, lakini hali ya wasiwasi bado imetanda, huku vikosi vya usalama vimetumwa kwenye mpaka huo.

    .
    Waandamanaji wakipita kando ya moto unaowaka
    Maelezo ya picha, Waandamanaji wakipita kando ya moto unaowaka
  17. Habari za hivi punde, Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Tanzania

    Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wa taifa hilo wanaoishi nchini humo .

    Kulingana na tahadhari hiyo ubalozi huo umewataka raia wa taifa hilo kuepuka maandamano yanayoendelea, kuepekuka mikusanyiko ya watu kufuatialia kwa karibu taarifa za vyombo vya habari ili kujifahamisha yanayoendelea mbali na kuchukua tahadhari ya juu katika maeneo waliopo.

    Hatua hiyo inajiri kufuatia maandamano yanayoendelea nchini humo.

    Kulingana na taarifa hiyo kuna ripoti za maandamano kote nchini ambayo yamesababisha kuzuka kwa ghasia na kufungwa kwa baadhi ya barabara.

    Ripoti hiyo imeelezea kwamba baadhi ya barabara kama ile ya kuelekea katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere imefungwa.

    Aidha taarifa hiyo imeongeza kuhusu kuzimwa kwa mtandaohali ambayo imeathiri pakubwa mawasiliano.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Uchaguzi Tanzania 2025: Tume ya Uchaguzi Tanzania yaanza kutangaza matokeo

    .

    Chanzo cha picha, Tume ya Uchaguzi Tanzania INEC

    Maelezo ya picha, Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndugu Ramadhani Kailima

    Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC imeanza kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.

    Hadi kufikia sasa ni mikoa minne pekee iliofanikiwa kuwasilisha matokeo yake.

    Kulingana na matokeo hayo Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama tawala cha CCM Samia Suluhu Hassan anaongoza kulingana na kura zilizohesabiwa.

    Aidha maandamano yameripotiwa katika eneo la Meriwa lililopo barabara ya jiji kuu la Dodoma na Dar es Salaam ambapo polisi wamewatawanya waandamanaji.

    Polisi vilevile wameripotiwa kufunga barabara ya Singida - Arusha kwa hofu ya kuzuka maandamano zaidi.

    Soma zaidi:

  19. Habari za hivi punde, Maandamano yaendelea kwa siku ya pili mjini Dar es Salaam

    .

    Polisi katika mji wa Dar nchini Tanzania wamefyatua risasi na vitoa machozi siku ya Alhamisi kutawanya waandamanaji waliorejea barabarani siku moja baada ya uchaguzi uliogubikwa na maandamano yenye vurugu, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Reuters.

    Maandamano yalizuka mjini Dar es Salaam na miji mingine kadhaa wakati wa upigaji kura siku ya Jumatano, huku waandamanaji wakilalamikia kukamatwa kwa viongozi wakuu wa upinzani na kuzuiliwa kushiriki katika uchaguzi wa Urais mbali na madai ya ukandamizaji wa wakosoaji wa serikali.

    Kwa mujibu wa Reuters baadhi ya maeneo ambayo maandamano hayo yameripotiwa kufanyika hii leo ni pamoja na Mbagala, Gongo la Mboto and Kiluvya.

    Soma zaidi:

  20. Habari za hivi punde, Hali ya wasiwasi yaendelea kuripotiwa Tanzania

    .

    Hali ya wasiwasi inaendelea kushuhudiwa nchini Tanzania kufuatia maandamano ya ghasia yaliofanyika hapo jana.

    Hatahivyo baadhi ya barabara ambazo zilikuwa zimefungwa hapo jana sasa zimefunguliwa.

    Baadhi ya raia ambao walikuwa wamekwama kutokana na maandamano yaliosababisha amri ya kutotoka nje kuwekwa hapo jana wamefanikiwa kufika makwao.

    Aidha kuna ripoti za maandamano kuzuka katika mji wa kaskazini wa Mwanza.

    Taarifa mjini humo zinasema kwamba waandamanaji walifanikiwa kupenya hadi katikati ya jiji na kusababisha makabiliano ya umwagaji damu dhidi ya polisi.

    Mwanza ni jiji la pili kwa ukubwa kwa idadi ya watu na biashara baada ya Dar Es Salaam na liko kwenye mwambao wa kusini mwa Ziwa Victoria.

    Aidha kuna madai kwamba baadhi ya waandamanaji mjini Dar, Mbeya na Dodoma wamekuwa wakiwashambulia walioshiriki katika shughuli ya kupiga kura hapo jana

    Vilevile huku mitandao ikiendelea kuminywa kwa siku ya pili mfululizo ni simu za kawaida pekee zinazotumika kwa mawasiliano.

    Soma zaidi: