Rais Samia atoa onyo dhidi ya waliochochea vurugu

Rais Samia akemea vikali vitendo vya uvunjifu wa sheria vilivyotokea wakati wa Uchunguzi Mkuu.

Moja kwa moja

Na Waandishi wa BBC

  1. Maandamano, Uhaba, hofu na Ukimya - Upi mustakabali wa Tanzania

    Ni siku ya tano sasa tangu huduma za intaneti nchini Tanzania zikatwe, hatua iliyoathiri upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hali ya kiusalama kufuatia maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa kati ya Jumatano na Ijumaa wiki iliyopita.

    Chanzo cha kidiplomasia kimeiambia BBC kuwa kuna ushahidi wa kuaminika unaoonyesha kuwa angalau watu 500 wameuawa katika ghasia hizo.

    Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Thabit Kombo, ameeleza kuwa serikali haiwezi kuthibitisha idadi hiyo rasmi. Wengine wanasemekana kukamatwa au hawajulikani walipo, huku mashuhuda walioko Dar es Salaam wakieleza kusikia milio ya risasi katika siku mbili za mwanzo za maandamano.

    Hali hiyo imekuja sambamba na amri ya kutotoka nje katika baadhi ya maeneo, huku Mkuu wa Majeshi jenerali Nkunda akionya kuwa JWTZ halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayevunja amani.

    Wakati huo huo, Tume Huru ya Uchaguzi INEC imemtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa Rais mteule wa Tanzania na kumkabidhi cheti cha ushindi — hatua iliyozua maoni mseto katika mitandao ya kijamii kabla ya mitandao hiyo kufungwa.

    Hali ya maisha kwa raia wengi imezorota. Mafuta yamepanda bei mara nne kwenye soko la magendo, vituo vya mafuta vimefungwa, na usafiri wa umma umesimama. Ni bodaboda wachache pekee wanaoendelea kufanya kazi, wakitoza bei kubwa. Ukosefu wa mafuta na usafiri unakwamisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kama chakula.

    Maduka mengi yamefungwa, mengine yakiishiwa bidhaa. Wakati huo huo, huduma za benki na malipo ya kidijitali zimevurugwa kutokana na kukosekana kwa intaneti. Uingereza imetoa onyo kwa raia wake, ikitaja uhaba wa chakula, mafuta, fedha taslimu na intaneti, na kuwataka wasafiri kuepuka safari zisizo za lazima.

    Kwa sasa, kukosekana kwa intaneti kumezidisha ukosefu wa taarifa zilizothibitishwa. Mitandao ya kijamii kama X, Instagram, TikTok na Telegram nchini Kenya imefurika video na madai kuhusu kinachoendelea Tanzania, lakini wachambuzi wanasema si zote ni za ukweli. Mfano mmoja ni video iliyosambaa ikionyesha watu wakikimbia katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere — tukio lilihusiana na mapokezi ya mwili wa hayati Rais John Magufuli mwaka 2021.

    Wataalamu wa usalama wa kidijitali wanatahadharisha kwamba kufungwa kwa mitandao kunazidisha uwezekano wa upotoshaji wa habari. Mtaalamu George Musalama ameiambia BBC: “kukosekana kwa intaneti kunazidisha taharuki na kutoa nafasi kwa propaganda kuenea bila uthibitisho wowote.”

    Kuhusu intaneti WaziriKombo alisema kuwa serikali ilichukua hatua ya kuminya mitandao ili kukomesha mawasiliano kati ya, kwa maneno yake, “vijana wahuni waliokuwa wanaitumia kupanga vitendo vya uvunjifu wa amani.”

  2. Idadi ya waliofariki kutokana na maporomoko Kenya yafikia 26

    .

    Chanzo cha picha, Ministry of Interior

    Maelezo ya picha, Waziri wa usalama Kipchumba Murkomen

    Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Kipchumba Murkomen ametangaza kwamba idadi ya waliofariki kwenye maporomoko ya ardhi katika bonde la Kerio imepanda hadi watu 26.

    Shughuli za uokoaji zimeingia siku ya pili huku jeshi la Kenya KDF likishirikiana na polisi na shirika la msalaba mwekundu kuwatafuta watu zaidi ya 20 ambao walikuw ahawajulikani walipo.

    Majeruhi wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi ilijyopo Jijini Eldoret.

    Majeruhi ambao wako katika hali mbaya wamekuwa wakihamishwa kwa ndege aina ya helikopta tangu Jumamosi mchana kwa kuwa hospitali ya Chesongoch ambayo pia iliharibiwa upande mmoja na maporomoko ya ardhi.

    Wakati huohuo waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen amesema kwamba shughuli ya uokoaji imesimama hadi Jumatatu mchana huku ndege za jeshi la Kenya KDF zikisalia katika eneo la ajali kwa pamoja na zile za idara ya polisi.

    “Waziri mwenzagu wa barabara na uchukuzi wa umma, Davis Chirchir anahangaikia kutolewa kwa fedha za ziada zitakazokarabati barabara zilizoharibiwa na mafuriko na tope la maporomoko ya ardhi.

    'Waziri wa kawi Opiyo Wandayi amewatuma wahandisi wa kampuni ya umeme kukarabati milingoti ya umeme iliyoharibika na kurejesha umeme katika eneo hilo,’ alisema Waziri.

    Ndege za jeshi zinatarajiwa kubeba karatasi za mitihani kuwafaa watahiniwa wa kidato cha nne ambao wanaendelea na mitihani yao ya mwisho.

    Shule 15 zimeathirika na maporomomko hayo ya ardhi .

    Serikali ya Kenya imesema kwamba mapormoko hayo yaliyotokea mwendo wa saa nane – usiku wa manene – kuamkia Novemba Mosi, baada ya mvua kubwa kunyesha usiku kucha. Vijiji vya Moror na kituo cha kibiashara cha Chesongoch ndivyo viliathirika pakubwa.

    Wizara ya usalama wa ndani imesema kwamba majumba zaidi ya 1000 yalifunikw ana maji na tope huku serikali ikiwataka waathiriwa kuhamia maemeo ya juu kwa sasa wakiahidi pia kutoa chakula, malazi na dawa kwa familia husika. Milima ya Chesongoch iliyopo katika bonde la Kerio imeshuhudia ajali mbaya ya maporomoko ya ardhi katika miaka ya hivi maajuzi.

    Watu zaidi y amia mbili wameuawa baada ya kufunikwa na ardhi au kusombwa na maji katika ajali ziizlotokea 2010, 2012 na 2020.

  3. Jumuiya ya Madola yaeleza wasiwasi kuhusu hali ya usalama Tanzania

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jumuiya ya Madola imeeleza masikitiko makubwa kuhusiana na hali ya usalama ilivyo nchini Tanzania.

    Katika taarifa iliyoichapishwa kwenye tovuti ya jumuiya hiyo na pia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, katibu mkuu wa jumuiya hiyo Shirley Botchwey amesema kwamba ,

    “Nimefuatilia kwa karibu matukio nchini Tanzania na kusikitishwa na jinsi hali ya usalama ilivyo. Nimetiwa wasiwasi na ripoti za maafa, majeruhi mengi, watu kutekwa na kupotea wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi. Ningependa kuwaomba kuwa na utulivu huku nikipendekeza kwamba kuwepo na mazungumzo ya kutafuta suluhu. Pia kuna haja ya uchunguzi kufanyika kuhusu niliyoyataja kwa ajili ya kurejesha Imani ya watu na amani na vile vile kuweka misingi bora ya Demokrasia nchini humo. ‘

    Hali ya taharuki bado ipo katika mji wa Dar es Salaam japo tangu jana hakuna ripoti zozote za maandamano zilizotolewa.

    Hata hivyo chama kikuu cha upinzani CHADEMA kimesema kwamba kitaitisha maandamano makubwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa Urais ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa kura hiyo baada ya kujizolea kura zaidi ya milioni 31 ikiwa ni asilimia 97.66 ya jumla ya kura zote zilizopigwa.

    Baadhi ya wagombea wa Urais walioshindana na Samia wamekubali matokeo na kushindwa na kusema kwamba wako tayari kushirikiana na Rais Samia kwa ajili ya uwiano wa kitaifa na pia kuhakikisha kwamba matakwa ya raia waliokuwa wakishabikia kupitia manifesto zao zitaangaziwa kwa kina.

    Huku Samia akisubiriwa kuapishwa, wengi ndani ya nchi wanahofia kuwa kuendeea kuzimwa kwa mtandao wa intanenti kunachangia pakubwa katika hali ngumu ya maisha ambayo wanajipata ndani kutokana na uhaba wa chakula na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli huku umeme ukikatizwa mara kwa mara katika mji mkuu wa kibishara- Dar es Salaam. Katika taarifa yake,

    Katibu wa Jumuiya ya Madola Shirley Botchwey amesema kwamba anaiomba mamlaka nchini Tanzania kuhakikisha kwamba kuna hali salama ya kuwaruhusu wenye kutaka kuandamana kufanya hivyo, huku akiwataka wanadamanaji kuwa wenye utulivu wakati wanapo tekeleza haki hiyo ya kikatiba na kuwataka kuheshimu sheria za nchini wanapofanya hivyo. ‘

    Mamlaka zinapaswa kuanzisha uchuguzi kuhusu madaia ya matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa upande wa polisi,’ alisema mheshimiwa Botchwey.

    Amevitaka vyama vya kisiasa nchini humo na washikadau wengine kuchukuwa hatua za haraka kuanzisha mazungumzo yatakayoangazia masuala ama chanzo cha maandamano na hali tete ambayo inashuhudiwa katika baadhi ya miji ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha denmokrasia nchini humo.

    Hapo jana alipopokezwa cheti cha ushindi, Rais Samia alilaani vurugu zilizoshuhudiwa nchini humo akisema kwamba ni juhudi za kuvunja amani ambayo muungano wa Tanganyika na Zanzibar imefurahia tangu 1961.

    “Nitahakikisha kwamba ninafanya kila iwezekanalo kulinda amani ya nchi na nitatumia asasi zote za kiuslama kukabiliana na wale wote ambao wanataka kuharibu amani ya nchi.” Alisema Rais Hassan.

  4. Uchaguzi Tanzania 2025: Viongozi wa Afrika wampongeza Rais Suluhu kwa ushindi wake

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Viongozi wawili wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika MAshariki wamempongeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kama Rais wa kwanza wa kike wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

    Samia ambaye ni kiongozi wa awamu ya sita amehifadhi kiti alichokirithi mwaka wa 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli.

    Katika ujumbe wake wa pongezi kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alisema : ‘Ndugu Dada Mheshimiwa Suluhu Samia, kwa niaba ya raia wa Burundi na kwa niaba yangu binafsi, ninakutolea hongera zangu za dhati kwa ajili ya uteuzi wako kw a mara nyingine, nikikutakia heri na fanaka. Burundi na Tanzania zitaendelea na ushirikiano bora kwa ajili ya maendeleo ya pamoja.’

    Naye Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mahmoud katika ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X amesema: ‘Ninatuma salamu zangu za kheir kwakwe mheshimiwa Suluhu Samia kwa kuchaguliwa kama Rais wa Jamuhuri ya muungano ya Tanzania.

    Ushindi wake unaashiria Imani ya watu wa Tanzania katika uongozi wake. Somalia inatazamia kupanua uhusiano kati ya mataifa yetu mawili ya undugu na kuendeleza juhudi za amani na uwiano katika ukanda huu.’

    Hapo jana mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC -Mahmoud Ali Youssuf alimpongeza Rais Samia kwa niaba ya Muungano wa Afrika kwa ushindi wake kwenye uuchaguzi mkuu wa Tanzania.

    Na japo alitaja kwamba AU iko tayari kushirikiana na Tanzania katika juhudi zake za kuboresha maisha ya raia wake, taarifa ya Youssuf ilisisitiza kwamba AU imesikitishwa na hali ya ghasia zilizochangia maafa nchini humo na kutuma risala za rambi rambi kwa jamaa na marafiki wa waliofariki.

    Hadi sasa Tanzania haijatangaza idadi ya waliofariki kwenye maandamano ya siku tatu mfululizo katika miji mbali mbali huku shirika la Amnesty International likisema kwamba hospitali hazitoi takwimu za majeruhi wa ghasia hizo ambazo polisi nchini humo wamedaiwa na kulaumiwa kutumia risasi za moto kukabiliana na waandamanaji.

    Maoni ya AU yameungwa mkono na jumuiya ya maendeleo ya mataifa ya Afrika kusini SADC ambayo imeeleza wasiwasi wake kuhusiana na ghasia zilizoshuhudiwa nchini humo.

    Kwa sasa, wengi wanasubiria mtandao wa intaneti kurejeshwa nchini humo kwa kuwa imezimwa tangu Jumatano.

    Naye Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissoco Embalo, amempongeza Rais Samia kwa ushindi wake, akiandika kwenye ukurasa wake wa X : ‘ Ningependa kutuma ujumbe wa heri njema kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kwake.

    Ushindi huu ni ishara kwamba watu wa Tanzania wana imani katika uongozi wake ambao ameuthibitisha kwa kuangazia masuala ya maendeleo na ustawi wa Tanzania.

  5. Hali ya utulivu yashuhudiwa Tanzania

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Utulivu warejea Tanzania

    Kwa siku ya pili sasa hali ya utulivu kiasi imeshuhudiwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania – Dar es Salaam baada ya siku tatu za maandamano yaliyosababisha uharibifu wa mali, wengi kujeruhiwa na hata baadhi kuripotiwa kufariki.

    Haya yanajiri wakati ambapo mtandao wa intaneti bado umezimwa nchini humo hali ambayo Waziri wa mambo ya kigeni balozi Mahmoud Thabit Kombo alitaja kama hatua iliyochukuliwa na serkali kudhibiti hali ya kiusalama nchini humo.

    Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Jumamosi Novemba mosi, Balozi Thabit alipongeza nchi yake kwa kuandaa uchaguzi ulio wazi na kuwashukuru raia kwa kujitokeza kwa amani na kumchagua kiongozi wanayemtaka.

    Aidha alilaani maandamano ya wiki nzima kama alivyotaja awali Rais Samia alipokuwa akipokezwa cheti cha ushindi katika makao makuu ya tume ya uchaguzi INEC jijini Dodoma.

    Kuhusu hali ya usalama na maamuzi ya serikali kudhibiti mambo Balozi Thabit amesema: ‘ Kutokana na hali ambayo ni ya kusikitisha kura ilipokuw ainaendelea kupigwa, kulitokea matukio ya hapa na pale ya watu kujaribu kuvunja sheria katika baadhi ya maeneo ya nchi.

    Vitengo vyetu vya usalama vilijukumika kwa haraka kukabiliana na watu hao na kudhibiti hali kuhakikisha kwamba hali hiyo haikusambaa zadi ya palipotokea maandamano na kuathiri uchaguzi uliokuwa ukiendelea,’ alisema Waziri huyo wa mambo ya kigeni.

    Huku serikali ikisema kwamba imedhibiti hali, amri ya kutotoka nje kati ya saa 12 jioni na saa 12 asubuhi bado inaendelea kutekelezwa jijini Dar Es Salaam huku taasisi mbali mbali za serikali kama vyuo vikuu vikiashirisha siku ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuingia vyuoni hadi mwishoni mwa mwezi Novemba.

    Wiki jana msemaji wa serikali Gerson Msigwa alitangaza siku mbili za wafanyakazi wa umma kutakiwa kufanya kazi nyumbani ikiwa majukumu yao ya kikazi sio ya dharura. Aliwataka waajiri katiak sekta ya binafsi kuwaacha wafanyakazi wao kusalia nyumbani huku wanafunzi wanaofanya mitihani ya kitaifa wakiombwa kujisomea nyumbani.

    Wengi wanasubiri kujuwa ni hatua gani serikali ya Tanzania itachukuwa ikizingatiwa wiki mpya inaaza Jumatatu, na wengi wanaofanya kazi na biashara jijini Dar Es Salaam wakitaka kujua hali itakuwa vipi Jumatatu.

    Vyanzo ndani ya Tanzania vimeieleza BBC kwamba bei ya bidhaa muhimu kama vile vyakula na mafuta ya petroli imepanda na inatia hofu kwamba ikiwa hali itasalia kama ilivyo, basi wengi watahangaika.

    Hapo jana chama cha upinzani cha CHADEMA kililaani hali inayoshuhudiwa nchini Tanzania na kusema kwamba hakitambui matokeo yaliyotangazwa Jumamosi na mwenyekiti wa INEC Jaji Jackobs Mwambegele.

    Aidha wamesema kwamba huenda wakaitisha maandamano makubwa kupinga matokeo ya uchaguzi.

  6. Matokeo ya Uchaguzi Tanzania ni kejeli kwa demokrasia - Upinzani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ushindi wa asilimia 98 wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi ni "kejeli ya mchakato wa kidemokrasia", msemaji wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema amesema . "Tunatoa wito kwa chombo kinachoaminika kuingilia kati kusimamia uchaguzi mwingine mpya," alisema John Kitoka.

    "Hilo ni kofi kwenye uso wa raia, na watu wamekasirika sana, na hivi karibuni tutatangaza hatua yetu ambayo inaweza pia kujumuisha kuitisha maandamano ya kitaifa," alisema.

    Wachunguzi wa Chadema katika hospitali na kliniki za afya wameripoti "watu wasiopungua 800" waliouawa na vyombo vya usalama katika maandamano yaliyotokea siku ya uchaguzi, Kitoka alisema.

    Takwimu hizi hazikuweza kuthibitishwa kwa kujitegemea, kwa kiasi fulani kutokana na kuzimwa kabisa kwa mtandao na kupigwa marufuku kwa wanahabari wanaofanya kazi kote nchini.

    Kitoka alisema takwimu za tume ya uchaguzi za asilimia 87 ya waliojitokeza katika uchaguzi huo ni mzaha tu.

    "Kilichotokea tarehe 29 Oktoba haikuwa uchaguzi kwa hiyo chochote kitakachotoka ni kinyume cha sheria," alisema.

    Waziri wa Mambo ya Nje Mahmoud Thabit Kombo alisema Ijumaa kuwa serikali yake "haina takwimu" kuhusu waliofariki.

  7. Karibu tena katika matangazo yetu ya moja kwa moja, hii leo ikiwa siku ya Jumapili

  8. Tunapumua kidogo tutaendelea na matangazo haya mubashara kadri tutakavyopokea habari zaidi kuhusiana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025. Endelea kuwa nasi.

  9. Matokeo ya uchaguzi wa Tanzania 2025: Watanzania mpakani Namanga wanasema nini?

    Raia wa Tanzania wanaoishi katika mpaka wa Namanga wametoa hisia za mchanganyiko kuhusu ushindi wa Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa Tanzania.

    Namanga ni moja ya sehemu zilizoshuhudia vurugu la maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu Tanzania

    Hawa hapa chini ni baadhi yao.

    CHARLES MASAI, Dereva wa malori ya uchukuzi, Namanga

    ''Ni bora tuunge mkono matokeo ya uchaguzi ili maisha yaendelee hata kama uchaguzi huo ulikuwa na utata. Kama vyama vyote vingeshiriki, ingekuwa vizuri zaidi.''

    MZEE MADIKO, Fundi wa magari Namanga

    ''Familia yake inateseka sana kufuatia virugu hizi, Badala ya vurugu, hebu Mama aapishwe. Kwa nini? Kwa sababu mimi ni mzazi. Je, unapenda vita? Je, unapenda kulala nje? Je, unataka askari watawale nchi yetu ya Tanzania? Tunaomba Mama aapishwe ili tupate amani hiyo.''

    HUSSEIN JAFFAR

    ''Nimepokea matokeo ya uchaguzi kwa masikitiko. Hakukuwa na upinzani wa kweli, Sio mimi tu niliyekasirishwa na matukio ya ukandamizaji wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu — watu wengi hawalitaki.''

    Pia unaweza kusoma:

  10. INEC ilindesha vyema uchaguzi - Jumuiya ya uangalizi wa uchaguzi wa EAC

    Mkuu wa ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk. Speciosa Wandira Kazibwe amesema Tume Huru ya uchaguzi ya Tanzania INEC imeendesha vyema mchakato wa uchaguzi kuanzia mwanzo hadi mwisho.

    ''Tumekuja hapa na kushuhudia jinsi mnavyosimamia uchaguzi huu na tumejiridhisha kwamba utaratibu wote ulifuatwa,''Dkt Wandira alisema.

    Pia aliongeza kwamba walikutana na wagombea wote waliowania urais na wameufahamisha ujumbe huo kupitia wawakilishi wao kwamba wanafahamu kilichofanyika wakati wa uchaguzi na wamekubaliana na matokeo ya uchaguzi huo.

    Akihutubia hafla ya INEC ya kumkabidhi chetu mshini wa uchaguzi huo Rais Mteule Samia Suluhu Hassan, Dkt Wandira aliitaja Tanzania kama mfano wa kuigwa katika eneo la Afrika Mashariki kwa kuendesha mchakato huo kwa njia ya amani.

    Soma pia:

  11. Samia akabidhiwa cheti cha cha ushindi katika makao makuu ya INEC

    Rais Samia Suluhu Hassan akabidhiwa cheti cha ushindi wa uchaguzi wa 2025 na Tume Huru ya Taifa nchini Tanzania (INEC) uliofanyika tarehe 29/10/2025.

    Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa INEC amesema kwamba kulingana na Katiba ya Tanzania mshindi anahitaji tu kuwa na kura nyingi kuliko washindani wengine.

    INEC ikitangaza mshindi mtokeo hayawezi kubatilishwa ama mahakamani au kupitia mahakama ya utatuzi wa mizozo ya INEC.

    Rais Samia alipata ushindi kwa kupata kura 31,913,866 kati ya 32,678,844 zilizopigwa.

  12. Watanzania waliojeruhiwa katika maandamano watibiwa Kenya

    Picha ya muandamanaji aliyebebwa baada ya kujeruhiwa
    Maelezo ya picha, Picha ya muandamanaji aliyebebwa baada ya kujeruhiwa

    Hospitali tafauti nchini Kenya zimeanza kuwapokea raia wa Tanzania waliojeruhiwa katika maandamano, hususan katika miji ya mpakani ya Isebania - Sirari,

    Kufikia Ijumaa tarehe 31 Oktoba, takriban raia 25 wa Tanzania waliovuka mpaka na kuingia Kenya walikuwa wametibiwa katika hospitali tofauti za Kaunti ya Migori magharibi mwa nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa gazeti la The Standard, taarifa kutoka Kituo cha Polisi cha Isebania inaonyesha kuwa waathiriwa hao waliingia nchini kupitia njia zisizo rasmi za mpakani, ambapo sita kati yao walikuwa na majeraha ya risasi.

    Hospitali ya BNM iliwahudumia na kuwaachilia wagonjwa wanne waliokuwa na majeraha ya kipigo, huku ikimlaza mgonjwa mmoja aliyepigwa risasi.

    Hospitali ya Jamii ya Emalia iliwapokea wagonjwa wawili wenye majeraha ya risasi na kuwapeleka katika Hospitali ya Migori kwa matibabu maalumu.

    Hospitali ya Getontira ilipokea wagonjwa sita, watatu wakalazwa na watatu wakapelekwa hospitali nyingine, ilhali Hospitali ya Queen Easter ilimlaza mgonjwa mmoja aliyepigwa risasi ambaye baadaye aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya hali yake kuimarika.

    Hospitali ya Bwana Mifupa ilishughulikia visa tisa vya wagonjwa wenye mifupa iliyovunjika, ingawa haikurekodi majeraha yoyote ya risasi.

    Maafisa wa afya na usalama katika Kaunti ya Migori wanaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo, huku kukiwa na hofu kwamba idadi ya majeruhi watakaovuka mpaka huenda ikaongezeka endapo machafuko nchini Tanzania yataendelea.

    Soma pia:

  13. Habari za hivi punde, Hussein Mwinyi aapishwa kuwa Rais wa Zanzibar kipindi cha Pili

    Dr. Hussein Ali Mwinyi ameapishwa kwa Rais wa Zanzibar kwa muhula wa pili.

    Hafla ya kuapishwa kwake iliongozwa na Jaji Khamis Ramadhan Abdhallah katika uwanja wa Amaan.

    "Mimi Hussein Ali Mwinyi naapa ya kwamba kwa Jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa muaminifu kwa Zanzibar na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba nitaihifadhi, nitailinda, nitaitii na… Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na watu wake kwa mujibu wa sheria iliyowekwa. Nakuomba Mwenyezi Mungu unisaidie."

    Hafla hii ya uapisho inafanywa katika uwanja wa Amaan Complex na imehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, mabalozi na viongozi wa kisiasa.

  14. Rais Mteule wa Zanzibar Hussein Mwinyi anakagua Gwaride la Heshima

    Tayari Rais Mteule wa Zanzibar Hussein Mwinyi amewasili uwanjani kwa ajili ya kuapishwa.

    Wanajeshi wameshaanza kuongoza sherehe hizo na risasi za heshima zimepigwa.

    Hussein Mwinyi anakagua gwaride lake la mwisho kwa kuwa ni kipindi chake cha mwisho.

    Wakati anaingia, alikaribishwa kwa shangwe, nderemo na vifijo na wenyeji.

  15. Habari za hivi punde, Hafla ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zanzibar inaendelea

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Hafla ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zanzibar Hussein Mwinyi inaendelea.

    Dr. Mwinyi alishinda uchaguzi mkuu wa asilimia 74.8 na amegombea kwa tiketi ya chama tawala cha CCM, ambacho hakijawahi kushindwa uchaguzi tangu uhuru.

    Dr. Mwinyi anaapishwa leo kuwa Rais wa awamu ya nane kipindi cha pili.

    Hafla hii ya uapisho inafanywa katika uwanja wa Amaan Complex. Na imehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, mabalozi na viongozi wa kisiasa.

    Soma zaidi:

  16. Katibu wa masuala ya nje wa CHADEMA aitaka EAC, SADC, AU kuingilia hali ilivyo Tanzania

    .

    Katibu wa masuala ya nje wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Deogratias Munishi, ametoa wito kwa EAC, SADC, AU pamoja na vyombo vingine kuingilia kati hali ilivyo nchini humo.

    Katika mahojiano na BBC, Munishi alisema kutangaza matokeo ya uchaguzi kutaongeza 'ghadhabu' miongoni mwa wananchi.

    Munishi alipoulizwa na mwandishi wa BBC ikiwa CHADEMA imepanga kupinga rasmi matokeo ya uchaguzi, alisema hata kama pengine wangeshiriki uchaguzi, kulingana na ‘mfumo wa uchaguzi nchini, huwezi kupinga matokeo ya uchaguzi yaliotangazwa na Tume katika mahakama yoyote’.

    Tume ya Taifa ya Uchaguzi INEC hapo jana ilikuwa inaendelea na shughuli ya kuhesabu kura huku serikali ikiendelea kusisitiza kuwa usalama umeimarishwa.

    Soma zaidi:

  17. Serikali ya Tanzania: Hatuwezi kuthibitisha idadi ya watu waliouawa katika maandamano

    Thabit Kombo

    Chanzo cha picha, Thabit/FB

    Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Thabit Kombo amezungumza na BBC kueleza kinachoendelea nchini Tanzania

    Serikali ya Tanzania imesema kwamba haiwezi kuthibitisha idadi ya watu waliouawa katika maandamano baada ya uchaguzi uliofanyika Jumatano wiki hii, vurugu za uchaguzi zikiingia siku ya tatu.

    'Kwa sasa hakuna mtu anaweza kusema ni watu wangapi wamefariki au kuumia. Tunaendelea kupokea ripoti kuhusu mali binafsi ya watu iliyoharibiwa, magari, mali ya umma, magari ya TANESCO ambayo ni kampuni yetu ya umeme yalichomwa. Kwa sasa hakuna hesabu kamili, mpaka serikali itakapopokea ripoti kamili na itatoa idadi kamili,' alisema Mahmoud Thabit.

    Baadhi ya makundi ya upinzani yalidai kuwa mamia ya watu waliuawa, huku umoja wa mataifa ukisema kuwa watu kumi wameuawa, madai ambayo Thabit Kombo amekanusha.

    Vile vile serikali ya Tanzania imeeleza kuwa hatua za kuminya intaneti hazilengi kuwakandamiza wananchi bali ni za kuwalinda huku wakiwahakikishia huduma za intaneti zitarudi hivi karibuni.

    'Wakati tulipowasha mtandao wa intaneti ilileta shida kwa watu wachache wahuni ambao walikuwa wakitumia mtandao kuleta vurugu. Sasa kwa mujibu wa sheria za mamlaka ya kusimamia mawasiliano Tanzania kuna sheria ambazo zinatumiwa wakati kuna wasiwasi wa usalama wa kitaifa kuhusu mtandao wa intaneti ndani ya nchi. Haya si mambo ya haki au ukosefu wa haki, tunazungumzia maisha ya watu, mali ya watu na usalama wa nchi yetu.'

    Akizungumza na BBC, Waziri wa mambo ya kigeni Balozi Mahmoud Thabit Kombo alitetea jinsi serikali ilivyokabiliana na waandamanaji baada ya uchaguzi wa Jumatano wiki hii.

    Soma pia:

  18. Karibu tena msomaji wetu. Ni siku nyingine tena tunapokutana katika matangazo yetu ya moja kwa moja kukujuza kile kinacoendelea nchini Tanzania. Tarehe ni 01/11/2025 na Hii ni BBC SWAHILI

  19. Mwanasiasa wa Upinzani Tanzania adai maisha yake yako hatarini

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanasiasa mwandamizi wa chama cha upinzani nchini Tanzania amedai kuwa anahofia maisha yake kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano, ambao umeibua utata na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu.

    Bw. John Kitoka, Mkurugenzi wa Masuala ya Nje na Diaspora wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ameiambia kipindi cha BBC Newshour kwamba kuna taarifa zinazoonyesha kuwa takribani watu 500 wameuawa na maafisa wa polisi pamoja na watu wanaodaiwa kuwa ni mamluki wa kigeni akionya kuwa idadi hiyo huenda ni kubwa zaidi.

    Kwa mujibu wa Bw. Kitoka, mauaji hayo yanafanyika nyakati za usiku, wakati hakuna mashuhuda, jambo linalozidisha hofu miongoni mwa wananchi.

    “Nina hofu kubwa kwa maisha yangu,” amesema akiwa mafichoni ndani ya nchi. “Wanawafuatilia viongozi wetu mmoja baada ya mwingine; baadhi wamekimbia nchi. Watu hawa wanaua bila hofu wala kuwajibishwa,” ameongeza.

    Aidha, amesema kuwa viongozi wakuu wa upinzani walizuiwa kugombea dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa mchakato huo haukustahili kuitwa uchaguzi huru na wa haki, bali “sherehe ya kumtawaza kiongozi mmoja.”

    Hadi sasa, mamlaka za serikali hazijatoa tamko rasmi kuhusu tuhuma hizo, huku jumuiya ya kimataifa ikiripotiwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kisiasa nchini Tanzania kufuatia uchaguzi huo wenye utata.

    Soma pia:

  20. Bunge la Ulaya laiomba INEC kutotangaza matokeo ya uchaguzi Tanzania

    Bunge la Ulaya

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bunge la Ulaya limetoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC kutotangaza matokeo ya uchaguzi hadi pale uchunguzi wa kina utakapofanyika.

    Bunge hilo pia limetoa wito kwa Jeshi la taifa hilo la Afrika Mashariki kuwa tu washikilizi wa madaraka iwapo watachukua jukumu la kudhibiti maandamano yanayoendelea nchini humo.

    ''Iwapo Jeshi la Tanzania litaamua kuchukua hatua yoyote ya udhibiti iwe ni ya kudumisha amani na kuleta utulivu na sio kung'ang'ania mamlaka', ilisoma taarifa hiyo ya Bunge la Ulaya.

    Wakati huo huo,bunge hilo limesema kuwa linawaunga mkono waandamanaji na kuongeza kuwa maandamano hayo ni ya kupigania haki na uwajibikaji na sio vurugu kama inavyotajwa na wengi.

    Haya yanajiri baada ya mkuu wa Jeshi la Tanzania Jenerali Jacob Mkunda kulaani vitendo vya vurugu vinavyoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini humo na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria.

    ''Tunashirikiana na vyombo vingine vya usalama kurejesha hali ya utulivu,''alisema Jenerali Mkunda Alhamisi usiku katika taarifa iliyopeperushwa kupitia televisheni ya taifa nchini humo TBC.

    Soma pia: