Uchaguzi kenya 2022: Wakenya wahimili baridi kali alfajiri kupiga kura

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mamilioni ya Wakenya hii leo wamejitokeza katika vituo tofauti nchini kushiriki katika shughuli ya upigaji kura ambapo wanawachagua viongozi wao ikwemo rais mpya.

Wakenya hushiriki katika shughuli hiyo kila baada ya miaka mitano kama ilivyo katika katiba.

Na hii leo Wakenya walirauka alfajiri na mapema kupiga foleni wakiwa na lengo la kuwachagua viongozi wao baada ya kipindi kirefu cha kampeni .

Baadhi ya masuala yaliojadiliwa katika kipindi hicho cha kampeni ni pamoja na Ukosefu wa ajira, gharama ya juu ya maisha na ufisadi.

Zaidi ya Wakenya milioni 22 wamesajiliwa kushiriki katika shughuli hiyo katika zaidi ya vituo 40,000.

Wakati huohuo rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta amekuwa akimuunga mkono kiongozi wa upinzani Raila Odinga dhidi ya naibu wake William Ruto.

Huku Raila Odinga akitafuta uungwaji mkono kwa kushinikiza vita dhidi ya ufisadi katika kampeni yake, naibu wake William Ruto amekuwa akijihusisha zaidi na raia wa tabaka la chini akiwahakikishia kuinua hali yao ya maisha.

Vituo vya Kupiga kura katika maeneo mengi ya nchi vilifunguliwa mwendo wa saa kumi na mbili kamili huku Wakenya wakihimili baridi kali kupiga foleni.

Baadhi ya raia wanadaiwa kulała vituoni ili kuwa katika mstari wa mbele katika shughuli hiyo.

Idara ya hali ya hewa nchini Kenya imesema kuwa sehemu kubwa ya nchi huenda ikawa kavu wiki hii hatua inayotoa fursa nzuri kwa Wakenya zaidi kushiriki katika shughuli hiyo.

Baadhi ya Vituo wanawake walionekana kubeba watoto wao wachanga ili kushiriki katika shughuli hiyo.

Katika Kituo cha Kibra jijini Nairobi , Mwandishi wa BBC Mercy Juma alisambaza picha ya mwanamke ambaye alikuwa amepanga foleni na mtoto wake wa miaka miwili kutoka saa kumi alfajiri saa za kenya, licha ya baridi kali ya asubuhi katika mji mkuu, Nairobi.

Alipoulizwa ni kwanini alikuwa amebeba mtoto wake mgongoni alijibu kwa kusema kwamba hakuwa na mtu wa kumwachia mtoto nyumbani.

Akina mama wajawazito na walio na watoto, wazee na walemavu kwa kawaida hupewa kipaumbele wakati wa kupiga kura.

Kwengineko Wapiga kura katika kituo kimoja cha kupigia kura katika mji mkuu, Nairobi, walijawa na ghadhabu baada ya shughuli ya kupiga kura kukosa kuanza kwa wakati.

Baadhi ya wapiga kura walionya kuzua vurugu iwapo shughuli ya upigaji kura haitaanza. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu Dickens Olewe ulibani kwamba nyenzo za uchaguzi zilichelewa kufika na upangaji ulikuwa ukiendelea.

Wagombea wakuu wapiga kura

Wakati huohuo baadhi ya viongozi wakiwemo wagombea wakuu wa uchaguzi huo Raila Odinga , William Ruto , Waihige Mwaura walitekeleza wajibu wao wa kupiga kura mapema leo.

Naibu rais William Ruto ambaye anagombea wadhfa wa urais kwa tiketi cha ya chama UDA alikuwa wa kwanza kupiga kura.

Ruto aliyeambatana na mkewe Rachael Ruto walikuwa wa kwanza kushiriki katika uchaguzi huo baada ya kupiga kura nyumbani kwake eneo la Sugoi lililopo jimbo la Bonde la Ufa.

'Tatizo kwa kawaida huja wakati, si wakati watu wanapiga kura, lakini wakati watu wanakataa matokeo ya uchaguzi.

Nadhani kwa mara ya kwanza katika historia ya demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya, wagombea wote wamejitolea kwamba watakubali matokeo ya kura

Kwa hivyo nadhani hii itakuwa tofauti na itakuwa ya amani, na ndani ya muda mfupi iwezekanavyo. Tunapaswa kuleta nchi pamoja na kutekeleza ajenda ambayo watu wa Kenya watakuwa wamechagua."

Wa pili Kushiriki katika zoezi hilo alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga Martha Karua ambaye muda mchache tu baada ya Ruto kushiriki katika shughuli hiyo ya Kihistoria, alipiga kura katika eneo bunge la Gichugu , huko Kirinyaga.

Akizungumza muda mfupi baadaye Karua alisema kuwa Wakenya wana nafasi ya kubainisha mwelekeo ambao nchi itafuata.

Martha alitoa wito kwa raia kujitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba.

Naye mgombea mwenza wa William Ruto, Rigathi Gachagua pia naye alipata fursa ya kushiriki katika shughuli hiyo ya kikatiba alipopiga kura katika eneo bunge la Mathira.

Rigathi ambaye alipata mkosi katika kituo cha kupiga kura baada maelezo ya alama zake za vidole kukosekana katika kifaa cha kielektroniki cha kupigia Kura, KIEMS kabla ya jina lake kuidhinishwa kupitia sajili la daftari la wapiga kura ,alisema kwamba ni wakati muhimu na kutoa wito kwa Wakenya kushiriki kwa wingi katika shughuli hiyo.

Mgombea wa chama cha Azimio Raila Odinga aliyeambatana na mkewe Ida Odinga alipiga kura mwendo wa saa nne huku idadi kubwa ya wafuasi wake wakiwasili naye katika kituo cha kupigia kura cha Kibra.Aliambatana na mkewe Ida Odinga aliyesema-

'Wapiga kura wametekeleza jukumu lao,kilichosalia ni IEBC kuhakikisha inatoa matokeo yanayoelezea matakwa yao halisi'

Naye mgombea wa Urais wa Chama cha Roots Prof. Wajakoya amepata hitilafu za kielektroniki za kifaa cha kupigia kura cha KIEMS katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi ya Indangalasia. Amerejea nyumbani kwake na atapiga kura maafisa wa IEBC watakapotatua suala hilo.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma