Uchaguzi Kenya 2022: Ukweli wabainishwa kuhusu kauli za Naibu wa Rais William Ruto katika mdahalo wa urais

    • Author, Na Peter Mwai
    • Nafasi, BBC Reality Check
  • Iliyochapishwa

Huku uchaguzi nchini Kenya ukiwa umesalia wiki chache tu, nchi hiyo imekuwa na mdahalo wa kwanza wa televisheni kwa wagombea urais katika uchaguzi huu.

Mmoja wa wagombea wawili wakuu, William Ruto, alishiriki peke yake kwa sababu mwanasiasa mkongwe - na waziri mkuu wa zamani - Raila Odinga, aliamua kutohudhuria.

Kwa sasa Bw Ruto ndiye naibu wa rais, na tumetathmini baadhi ya majibu aliyotoa kwa maswali aliyoulizwa.

'Tuna vijana milioni tano ambao hawafanyi kazi'

Madai ya Bw Ruto kwamba vijana milioni tano hawana kazi ni ya juu zaidi kuliko takwimu rasmi zinavyopendekeza.

Taarifa za hivi punde kutoka kwa ofisi ya kitaifa ya takwimu ni kwamba kuna Wakenya milioni 2.5 wenye umri wa kufanya kazi (miaka 15 hadi 64) ambao hawana kazi kwa sasa.

Haijabainika haswa ni rika gani ambalo Bw Ruto alikuwa akimaanisha, ingawa ufafanuzi rasmi wa vijana nchini Kenya ni umri wa miaka 18-34.

Kulingana na sensa ya mwaka wa 2019 nchini Kenya, kulikuwa na watu milioni 1.6 pekee wasio na ajira katika kundi hilo la umri wakati ambapo sensa ilifanywa.

Tumepata marejeleo ya zaidi ya watu milioni tano wasio na ajira na "wenye ajira ya chini" katika ripoti ya 2015 kuhusu nguvu kazi nchini Kenya.

Idadi hii ilikuwa ya rika zote (sio vijana tu), na inajumuisha sio tu wale ambao hawana kazi kabisa, lakini pia wale ambao walisema saa zao hazitoshi, ujuzi wao haukutumiwa ipasavyo au hawakuwa na tija kadri walivyoweza .

'Tuna Wakenya milioni 15 ambao leo wameorodheshwa katika CRBs [Mashirika ya kuweka taarifa za waliokosa ama kushindwa kulipa mikopo]'

Bw Ruto anarejelea hapa vyombo vinavyoidhinisha Wakenya kuwa wanastahili kupewa mikopo.

Tulipata nakala ya gazeti kutoka Februari 2021, ambayo ilitaja idadi ya chini kidogo - milioni 14 - lakini kwa akaunti za mkopo zilizodaiwa mwezi uliopita, sio watu wenye malimbikizo.

Sam Omukoko kutoka Metropol, mojawapo ya mashirika matatu ya CRB nchini Kenya, alithibitisha kwenye kituo cha runinga cha KTN News kwamba idadi hiyo ya milioni 14 mwaka wa 2021 ilikuwa ya malimbikizo ya akaunti.Hatujapata takwimu za hivi majuzi zaidi.

"Wakenya wana wastani wa takriban akaunti tano," alisema, akiongeza walikopa kutoka kwa benki, taasisi ndogo za fedha na vyama vya kuweka akiba.

Inayomaanisha kuwa idadi ya watu halisi walio na madeni inaweza kuwa ndogo sana, ikizingatiwa kuwa kwa ujumla wana zaidi ya akaunti moja.

Aidha, idadi ya malimbikizo ya akaunti huenda ikapungua katika kipindi cha miezi sita iliyopita, baada ya Rais Kenyatta kuagiza kusitishwa kwa muda kuorodhesha wale ambao wamekosa kulipa kiasi cha chini ya shilingi milioni tano za Kenya ($42,000; £34,800).

'...karibu asilimia 80 ya mikopo yetu yote ni ya ndani'

Naibu rais Ruto alisema nchi imekuwa ikikopa pesa zaidi kutokea ndani "hiyo ina maana kwamba pia tunadhuru biashara zetu mashinani."

"Upatikanaji wa mikopo unakuwa changamoto kubwa [na] lazima tufikirie jinsi tunapaswa kupunguza kasi ya kukopa ndani ya nchi," aliongeza.

Lakini kiasi cha deni wanalodaiwa wakopeshaji wa kimataifa, na kiasi kinachodaiwa na wakopeshaji wa ndani (kama vile benki za biashara) kimesalia takribani sawa katika miaka ya hivi karibuni, huku deni la nje kwa ujumla likiwa juu kidogo kama sehemu ya jumla ya deni.

Takwimu za Benki Kuu ya Kenya zinaonyesha kuwa mnamo Desemba 2021, wakati jumla ya deni la umma lilikuwa shilingi trilioni 8.2, deni la ndani lilikuwa trilioni 4 na deni la nje trilioni 4.2.

Ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika mwaka jana ilibainisha kuwa "idadi ya deni la nje (kama asilimia ya deni lote) ilipanda kutoka 44.5% mwaka 2013 hadi 52.5% mwaka 2020."

Ni kweli kwamba wakati wa muhula wa kwanza wa Bw Kenyatta na Bw Ruto kati ya 2013 na 2017, ukopaji wa ndani ulikuwa mkubwa kwa muda kabla ya deni la nje kuanza kuongezeka.

'Asilimia 50 ya gharama ya mafuta ni kodi'

Bw Ruto alisema nchi inahitaji kuangalia upya ushuru wa mafuta, akiulaumu kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa bei.

"Jambo la kwanza tunalohitaji kufanya ni kuangalia ushuru kwa sababu karibu 50% ya gharama ya mafuta nchini Kenya ni ushuru," alisema, akiongeza kuwa kuna ushuru aina 15 tofauti wa mafuta.

Lakini data kutoka kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) inaonyesha ushuru na tozo unajumuisha takriban 40% ya gharama ya jumla ya mafuta.

Katika mapitio ya hivi majuzi zaidi ya bei ya petroli, kati ya shilingi 159.12 za Kenya kwa lita moja ya petroli, 64.06 kati ya hizo huenda kwa serikali kama kodi.

Na kodi na ushuru ni asilimia tisa - si 15. Zinajumuisha ushuru wa bidhaa, ushuru wa matengenezo ya barabara, ushuru wa usafirishaji wa mfanyabiashara na Kodi ya Ongezeko la Thamani(VAT).

Ripoti ya ziada kutoka kwa Victor Komen,Nairobi

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma