Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Kenya 2022: Fahamu namna kura zinavyohesabiwa
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Mamilioni ya Wakenya siku ya Jumanne walishiriki katika shughuli ya upigaji kura kuwachagua viongozi wao baada ya kampeni kali iliyotawaliwa na mijadala kuhusu gharama ya maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi.
Lakini bila shaka yoyote jukumu kubwa lipo mikononi mwa mwananchi katika kuamua hatma ya nchi hiyo.
Na katika makala hii tunaangazia jinsi kura zinavyohesabiwa baada ya wananchi kutekeleza wajibu wao wa kujitokeza na kupiga kura kulingana na maagizo na masharti ama ya Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) au Katiba.
Mchakato wa kuhesabu kura baada ya kumalizika kwa upigaji kura
Vituo vya kupiga kura vimefunguliwa saa kumi na mbili asubuhi kwa shughuli ya upigaji kura na punde tu maafisa wa tume wakishasema kuwa shughuli ya kupiga kura imefungwa, atakayekuja baada ya muda huo hataruhusiwa kupiga kura lakini wale wote ambao watakuwa wapo kwenye foleni wataruhusiwa kupiga kura zao.
Afisa msimamizi huchukua hatua zifuatazo za maandalizi (kuhusiana na hesabu):
Huhesabu kura zote ambazo hazijatumika na zilizoharibika na kuzirekodi katika shajara ya kituo cha kupigia kura.
Kulingana na idadi ya kura zilizotolewa kwa kituo cha kupigia kura, hukokotoa idadi ya kura zilizotumika na kurekodi kiasi hiki kwenye shajara.
Pia kinachorekodiwa ni kura ambazo hazijatumika na zilizoharibika.
Kisha, uchaguzi mmoja baada ya mwingine, kwa utaratibu uliowekwa katika kanuni, kazi inaendelea na upangaji: Mbele ya mawakala wa chama au wagombea na waangalizi, nambari za mihuri hutambuliwa na sanduku la kura kufunguliwa.
Kura zimepangwa, kila kura itabainishwa kuwa halali, kukataliwa (maana yake ni batili) au kupingwa.
Kura inayobishaniwa inachukuliwa kuwa halali kwa madhumuni ya kutangaza matokeo katika kituo cha kupigia kura - yaani, kura itaongezwa kwa mgombea mmoja.
Mgombea au wakala wake anaweza kupinga kukataliwa kwa kura.
Katika tukio hili, afisa msimamizi atapiga muhuri kura iliyokataliwa kama ''kukataliwa kunakopingwa''.
Kura zilizo na alama ya ''kukataliwa kupingwa'' na kura zinazobishaniwa zinaweza kukaguliwa na msimamizi wa uchaguzi katika eneo bunge au kituo cha kuhesabu kura cha eneo.
Kura halali lazima zijulikane kwa uwazi na ziwe chini ya taratibu za uwajibikaji.
Baada ya upangaji kukamilika, kura za kila mgombea huhesabiwa na afisa msimamizi.
Kisha kura zisizo sahihi (zilizokataliwa, na zilizopingwa) zinahesabiwa.
Wagombea au mawakala wao wanaweza, si zaidi ya mara mbili, kutafuta kuhesabiwa upya.
Kisha afisa msimamizi atatangaza na kurekodi kwenye fomu ya matokeo:
- Wapigakura waliojiandikisha
- Jumla ya waliojitokeza kupiga kura
- Kura zisizo sahihi
- Kura zitakazopatikana kwa kila mgombea
Kisha fomu za matokeo zitasambazwa kama ifuatavyo: Nakala halisi itatumwa kwa Msimamizi wa Uchaguzi (katika Kituo sahihi cha Kuhesabu kura.)
Nakala itabandikwa katika kituo cha kupigia kura
Nakala halisi ni matokeo rasmi na inaanza safari ya kusafirishwa na Msimamizi wa Uchaguzi katika Kituo cha kuhesabu kura Taifa.
Na kufikia hatua hii, matokeo ya awali sasa yatapitishwa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Kinyume na hapo awali ambapo kura zilihesabiwa katika kituo cha kujumlisha kura, tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC), imesema kuwa kura zitahesabiwa katika kituo cha kupiga kura, ili kuondolea mbali tashwishi zozote.
Kulingana na Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC), mawakala wa vyama vya kisiasa na pia wanahabari wataruhusiwa kupiga picha nakala ya matokeo ya uchaguzi katika kituo cha kupiga kura.
"Kupiga picha nakala hiyo kutawasaidia wawaniaji kuweza kulinganisha matokeo yanayotangazwa katika makao makuu na matokeo yaliyonakiliwa katika kituo cha kupiga kura," alisema Wafula Chebukati mwenyekiti wa tume ya IEBC.
Kuhesabu kura kunafuatia mtiririko wa Rais, Gavana, Seneta, MCA, Mbunge na hatimaye Mwakilishi wa Mwanamke (sawa na jinsi masanduku ya kura yanavyopangwa kwa ajili ya kupiga kura).
Na baada ya mchakato huo kumalizika, maafisa hao wanafaa kuwasilisha fomu 34A (fomu za matokeo katika vituo vya kupigia kura).
Fomu 34A na 34B ni nini?
Chini ya Kanuni za Uchaguzi, Fomu 34A ndiyo fomu ya kwanza inayotumiwa kujumlisha matokeo ya uchaguzi wa urais.
Hujazwa na msimamizi wa chama baada ya kuhesabu kura kwenye kituo cha kupigia kura.
Ina maelezo ya kura alizopata kila mgombea na pia inaeleza jumla ya wapiga kura waliojiandikisha katika kituo hicho, kura zilizokataliwa, zilizopingwa, zinazobishaniwa na zile halali.
Wagombea au mawakala wao basi wanatakiwa kutia saini na kuthibitisha kwamba yaliyomo kwenye fomu hiyo ni sahihi.
Kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi kinatoa masharti kwamba kwa uchaguzi wa urais, IEBC ''itatoa kwa njia ya kielektroniki, katika fomu iliyowekwa, matokeo yaliyoorodheshwa ya uchaguzi wa rais kutoka kituo cha kupigia kura hadi kituo cha kujumlisha kura za eneo bunge na kwa Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha Kura."
Fomu 34A inakabidhiwa msimamizi wa eneo bunge, ambaye anajaza Fomu 34B.
Inatumika kwa ujumuishaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais kutoka kwa vituo vyote vya kupigia kura ndani ya eneo bunge.
Juu yake imeonyeshwa nambari ya kituo cha kupigia kura, jina la kituo, idadi ya wapiga kura waliojiandikisha, nini kila mgombea alipata na idadi ya kura halali zilizopigwa.
Msimamizi wa uchaguzi wa eneo bunge anakabidhi fomu kwa mwenyekiti wa IEBC ambaye pia ndiye msimamizi wa uchaguzi wa urais.
Tangazo la matokeo litatokana na Fomu 34B tutakazopata kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Maafisa wa usalama
Wakati zoezi la kuhesabu kura linaendelea, kunakuwa na maafisa wa usalama wanaohakikisha hali ni shwari kwa kila mshiriki anayefanikisha uchaguzi huo.
Kura iliyoharibika ni ipi?
Kuna sababu nyingi ambazo husababisha kura kuharibika na hivyo kutohesabiwa.
Kuu zaidi huwa ni mpiga kura kuweka alama kwa njia isiyofaa wakati wa kuchagua mgombea au chama anachokitaka.
IEBC inasema mpiga kura anatakiwa kuweka "alama kwenye nafasi iliyotengwa kwa jina la chama/mgombeaji au picha ya chama unachokichagua."
Mpiga kura anafaa "kuweka alama kwa mgombeaji mmoja tu." Hufai kuweka alama yoyote nyingine kwenye karatasi ya kura.
Alama unayoweka inaweza kuwa alama ya ndio (✓), mkasi (✕), au hata alama ya kidole. Hata hivyo, huruhusiwi kuandika jina lako au kuweka sahihi yako kama alama ya kumchagua mgombea unayemtaka. Iwapo utafanya makosa bila kukusudia wakati wa kuweka alama yako kwenye karatasi ya kura na utambue hilo kabla ya kutumbukiza karatasi yako kwenye sanduku, unaweza kupewa karatasi nyingine ya kura. Unaweza kupewa karatasi mpya ya kura mara mbili pekee.
Baada ya kumaliza kuweka alama, unafaa kuikunja karatasi katikati -kutoka kushoto kwenda kulia ili kuweka siri uliyemchagua halafu utumbukize karatasi hiyo kwenye sanduku lifaalo.
Tume ya uchaguzi imepiga marufuku kurandaranda katika kituo baada ya kupiga kura. Vile vile, ni hatia kupiga picha katika kituo cha kupiga kura au kupiga picha karatasi za kura.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma