Makubaliano ya gesi asilia Tanzania - matumaini mapya ama kaa la moto lingine sekta ya nishati?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Juni 11, 2022 Tanzania ilitia saini makubaliano ya awali ya mkataba wa nchi hodhi (HGA) wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kati ya nchi na wawekezaji.
Huu ni mkataba wa kihistoria kwa ukubwa wa thamani yake kuwahi kuingiwa na taifa hilo la Afrika Mashariki, ukigusa eneo hilo la nishati ya gesi, ambayo inazidi kuongezeka thamani kila uchao.
Mkataba huo una thamani ya shilingi za kitanzania zaidi ya trilioni 70, ambazo ni sawa na dola za Marekani bilioni 30, ambazo zinaweza kuleta mageuzi ya uchumi iwapo zitasimamiwa na kutumika ipasavyo. Swali ambalo wengi wanajiuliza makubaliano haya yatainufaishaje Tanzania, je utakuwa kaa la moto kama mingine mikubwa iliyowahi kuingiwa?
Faida na changamoto za mradi huu
Tanzania ina hazina ya futi za ujazo trilioni 57.25 za gesi asilia iliyothibitishwa, kiasi ambacho ni kikubwa kubadili uchumi na Pato la Taifa.
Sehemu kubwa ya gesi hiyo, takribani futi trilioni 49.5 za ujazo, zipo katika kina kirefu chini ya Bahari ya Hindi. Maana yake mitambo ya teknolojia ya juu itahitajika kuichimba.
Mkataba huu na kampuni za Shell ya Uingereza na Equinor ya Norway unakwenda kuiwezesha kuichimba na kuichakata gesi hiyo tayari kwa ajili ya kuuzwa ikiwa katika mfumo wa Liquidfied Natural Gas (LNG).
LNG ni gesi iliyochakatwa na kuwekwa katika mfumo wa kimiminika huku ikiwa imesindikwa kwa zaidi ya mara 600 kutoka katika ukubwa wake wa asili na kuwa katika hali ya ubaridi mkali wa nyuzi joto hasi 162 ili kurahisisha utunzaji na usafirishaji wake.
Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwaka 2025 na kuanza shughuli kati ya mwaka 2029 na 2030 kwenye mtambo wa gesi ya kioevu utakaojengwa katika mji wa Lindi uliopo kusini mwa Tanzania zaidi ya kilomita 450 kutoka jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Ujenzi huo utaenda sambamba na ujenzi wa ukanda wa kiuchumi kwa ajili ya kusaidia huduma kwenye mradi.
Ukiacha miundo mbinu ya barabara, maji na majengo ya kisasa yakiwemo, huduma muhimu za kibinadamu zitazalisha ajira maelfu ya ajira kwa Watanzania.
'Faida za wazi za mradi, ni kutengeneza ajira nyingi na kuongeza mzunguko wa fedha', anasema mchumi Dkt. Barnos William kutoka Chuo kikuu cha Ushirika Moshi.
Lakini uwepo wa ukanda wa kiuchumi haupaswi kwa namna yoyote kuachwa kuhodhiwa na wageni. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni inatia moyo kwamba pengine faida za watu zitajionyesha kupitia ukanda huu, achilia mbali mauzo ya gesi yenyewe.
'Niombe Watanzania tujipange, kuweza kuchukua huduma na kuhudumia mradi, sisi wenyewe ili tuweze kukuza uchumi wetu wa ndani', alisema Rais Samia wakati wa kusaini wa makubaliano ya awali jijini Dodoma.
Pamoja na faida hizo changamoto kubwa inayoikumba Tanzania ni uzoefu wa kuendesha mradi mkubwa wa namna hii.
Ni wazi, inajifunza, haijawahi kufanya, na lazima kutegemea makosa ya hapa na pale. Angalau katika hatua za awali ilianza kuajiri kampuni ya ushauri elekezi ya Baker Botts ya Uingereza ili kuisaidia namna ya kuzungumza na kutekeleza mradi huu. Kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa wa miradi ya aina hii.

Kutokuwa na uzoefu ni jambo ambalo hata Waziri wa Nishati, Januari Makamba anakiri.
'Sisi kama nchi tunafanya hili jambo kwa mara ya kwanza na hatuna uzoefu nalo, na tuna uhaba wa utaalamu na wataalamu wa majadiliano, wa sekta hiii kwa ujumla', alisema.
Nini uzoefu wa nchi nyingine zinazochakata gesi asilia?
Afrika ni Tajiri kwa kuwa na hifadhi kubwa ya gesi asilia, karibu nusu ya nchi zake 55 zina gesi hii inayofikia futi za ujazo trilioni 800.
Lakini kumekuwa na changamoto kwa nchi hizi katika kunufaika na rasilimali hii.
Nigeria, Algeria, Misri na Senegal, ni miongoni mwa nchi zinazojitahidi kwenye sekta ya gesi Afrika, ikijenga miundombinu na usimamizi unaosaidia kuonesha faida yake kwa wananchi.
Nigeria ni mzalishaji mkubwa wa gesi, huku Algeria ikiwa miongoni mwa nchi tano duniani zinazosafirisha na kuuza gesi iliyochakatwa Ulaya.
Kwa mujibu wa umoja wa nchi za Kiarabu zinazouza gesi (OAPEC), Misri ilisafirisha Ulaya tani milioni 1.4 ya gesi asilia iliyochakatwa kwenda Ulaya katika robo ya kwanza ya mwaka 2021.
Kugunduliwa kwa gesi zaidi ya muongo mmoja uliopita kwenye pwani ya Kaskazini mwa Msumbiji, kulileta ndoto na matumaini makubwa ya kuivusha kiuchumi nchi hiyo ifikapo mwaka 2040.
Leo imebaki ndoto. Tuhuma za rushwa, mizozo, utashi wa kiasiasa, vimefifisha ndoto ya mamilioni ya wanamsumbiji. Tanzania inapaswa kujifunza kwao.
'Kinachotuumiza ni ubinafsi na rushwa kwa viongozi, wanapaswa kuweka uadilifu mkubwa kwenye mradi huu, faida zitawafikia wananchi wengi', alisema Raphael Kugesha, mtalaama wa jamii kutoka Moshi.
Msumbiji wananufaika, lakini si kwa kiwango kinachopaswa. Hilo pia linaonekana kwa nchi nyingine kadhaa za Afrika.

Chanzo cha picha, AFP
Mikataba mibovu na hofu ya Watanzania
Kama kuna eneo ambalo, linahitaji maelezo mengi zaidi ni la mikataba. Kashafa nyingi zilizowahi kuzikumba serikali zilizopita zilihusu mikataba mibovu isiyo na maslahi kwa taifa hilo.
Ziliwahi kuundwa Kamati mbili maalumu za bunge kuchunguza masuala ya mikataba mibovu iliyodaiwa kuingizia hasara Serikali, huku wizara ya Nishati nchini Tanzania ikiwa moja ya Wizara zinazohusishwa na kashfa nyingi zitokanazo na miradi mikubwa ya nishati.
Ukiacha uuzwaji wa sehemu yenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe, Kiwira kwa Kampuni ya Tan - Power Resources (TPR), kashfa kubwa ilikuwa mkataba wa ufuaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond, kashfa iliyomfanya Waziri mkuu wakati huo, Edward Lowassa kuachia ngazi.
'Uzoefu kwenye mikataba ya aina hii, unaleta mashaka, ni lazima Serikali ieleze kinagaubaga faida za wazi kwa taifa na wananchi, shilingi trilioni 70, ni nyingi', alisema Amani Maletho mchumi kutoka Arusha.
Waziri wa sasa Januari Makamba, ana kazi kubwa ya kufanya kuwaaminisha watanzania kuhusu faida za mkataba huo na kuuthibitishia umma utofauti wake na mikataba mingine.












