Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Sura zilizotumika kumtangaza Vladimir Putin mitandaoni
ER Yamini msichana mwenye ushawishi katika mitandao ya kijamii nchini India, hajawahi kuchapisha kitu chochote katika mtandao wa Twitter maishani mwake - anapendelea kuongeza wafuasi wake wakubwa kwenye mtandao wa Instagram na YouTube.
Lakini mapema mwezi Machi, akaunti moja ya Twitter ikatumia picha yake na kuandika: "#IStandWithPutin. Urafiki wa Kweli" ikiambatana na video inayoonesha wanaume wawili wakikumbatiana - mmoja akiwakilisha India, mwingine, Urusi.
Yamini anasema haungi mkono nchi yoyote katika vita vya Urusi na Ukraine, na ana wasiwasi kuhusu mashabiki wake.
"Ikiwa wataona tweet hiyo, watanifikiriaje?" anauliza, "Laiti wasingetumia picha yangu kwenye akaunti hiyo."
Akaunti hiyo ghushi ni sehemu ya mtandao unaomtangaza rais wa Urusi Vladimir Putin kwenye Twitter, ambayo ilitumia alama za reli #IStandWithPutin na #IStandWithRussia tarehe 2 na 3 Machi. Hii ilisababisha kuwa mada zinazo ongelewa sana katika maeneo tofauti - ikionesha kuunga mkono vita, katika nchi kama India, Pakistan, Afrika Kusini na Nigeria.
Sehemu ya akaunti zilizofuatiliwa zilikuwa halisi kwa maneno mengine ziliandaliwa na watu halisi - inayoonesha uungwaji mkono wa kweli katika baadhi ya nchi kwa Bw Putin na Urusi.
Lakini akaunti nyingine nyingi zinaonekana kuwa si halisi. Walituma ujumbe tena kwa wingi, wakatoa ujumbe mchache wa kweli asili na zilitengenezwa kipindi cha hivi karibuni.
"Inawezekana zilitengenezwa na roboti, wasifu bandia au akaunti zilizoathiriwa, zikihamasisha uungwaji mkono wa Putin katika nchi hizi," anasema Carl Miller, mwanzilishi mwenza wa CASM Technology, kampuni inayotafiti madhara na habari potofu mtandaoni.
Ilifuatilia maelezo mafupi 9,907 yaliyotangaza uungwaji mkono kwa Urusi tarehe 2 na 3 Machi, katika lugha kadhaa tofauti. CASM ilipata zaidi ya akaunti 1,000 kati ya hizo zilikuwa na sifa kama barua taka 9 (Spam).
BBC ilichunguza mamia ya akaunti hizi zilizoonekana kuwa zisizo sahihi. Utafiti wetu unathibitisha mawazo ya Bw Miller - wanajaribu kuangalia kama ukweli, lakini kwa kweli ni bandia.
Kupitia utafutaji wa picha za nyuma, tumegundua kwamba picha zilizotumiwa kama utambulisho wa akaunti zilinakiliwa kutoka kwa watu mashuhuri, wenye ushawishi na watumiaji wa kawaida, ambao hawakujua kama picha zao zilikuwa zikitumiwa kuunga mkono Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
Hatujaweza kubainisha ni nani aliyefungua akaunti, au kama zina uhusiano wowote na serikali ya Urusi.
Kwamfano akaunti inayoitwa Preety Sharma, inasema katika wasifu wake kwamba ni "mwanamitindo na mjasiriamali" asili yake ni India na sasa yupo Miami. Ilitengenezwa tarehe 26 Februari, siku mbili baada ya uvamizi wa Urusi. "Putin ni mtu mzuri", inasema moja ya retweets zake.
Lakini mwanamke aliyeoneshwa kwenye picha ya utambulisho wa akaunti yuko upande mwingine wa dunia. Nicole Thorne ni mshawishi wa mitandao ya kijamii wa Australia ambaye ana wafuasi milioni 1.5 kwenye Instagram, na mara chache tu hutumia picha ya asili kwenye akaunti ya Twitter.
Akaunti nyingine inajaribu kumtumia mwimbaji wa Kihindi Raja Gujjar. Tweet yake ya kwanza ilitumwa tarehe 24 Februari, siku ya kwanza ya uvamizi huo. Na machapisho yote 178 na akaunti ni zilizotumwa tena retweets, kiashiria kikubwa cha akaunti zinazojiendesha automatisering.
BBC iliwasiliana na Bi Thorne na Bw Gujjar, na wote wawili walithibitisha kuwa akaunti hizi si zao.
Ingawa ni kama akaunti bandia za Roboti, sio akaunti zote zilizochunguzwa hazikuwa halisi.
Chukua akaunti ya mmoja, uliyotengenezwa Februari 2022 kwa kuanza kushapisha tweets kuanzia tarehe 2 Machi. Haina wafuasi. Wakati wa utafutaji wa picha za nyuma BBC ilikutana na akaunti ya kijana wa kihindi kwenye mtandaop wa LinkedIn.
Lakini ni halisi, na imeanzishwa na Senthil Kumar, mhandisi wa angani. Tuliuliza kwa nini alifungua akaunti ili tu kutuma ujumbe wa wanaounga mkono Urusi.
"Kawaida, mimi hufungua Twitter na kuona kile kinachovuma mitandaoni. Kwa hivyo niliona machapisho haya na kuyatuma tena," alisema. Anaamini kuwa Urusi iliungwa mkono na India hapo awali, na Wahindi sasa wanapaswa kuunga mkono Urusi. Na akaunti yake ilikuwa mpya, alisema, kwa sababu alikuwa amesahau neno la siri la akaunti yake ya awali.
Si Magharibi
Akaunti hizo kwenye Twitter zina ukosoaji wa nchi za Magharibi, zinaonesha mshikamano kati ya mataifa yanayoitwa Brics (Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini), na kutoa uungaji mkono wa moja kwa moja kwa Bw Putin.
"Hatukubaliani na wazo kwamba taarifa za kampeni zitaelekezwa Magharibi. Hata hivyo hakuna akaunti yoyote iliyokuwa ikiangazia nchi za Magharibi wala kudai kuwa inatoka Magharibi," anasema Bw Miller.
Ili kutambua kitu gani kinachoweza kuiweka akaunti katika kundi la akaunti bandia, watafiti wanaangalia tarehe za kuunda akaunti, muundo wa kuchapisha tweet "usio wa kawaida" (kama vile akaunti kuchapisha ujumbe kwa kutuma saa 24 kwa siku), na aina ya mada zilizotumwa kwenye twita.
Ukosefu wa picha halisi ya wasifu pia inaweza kuwa kiashiria.
Kati ya sampuli za akaunti 100 zilizofuatiliwa na CASM, BBC iligundua kuwa 41 hazikuwa na picha za utambulisho (Profile). Wengine 30 walikuwa na vielelezo au picha za watu binafsi kama Bw Putin au afisa mkuu mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg. Robo pekee walikuwa na picha zinazoonyesha watu - na baadhi yao ziliibiwa.
Twitter inakataza kuiga taarifa za "watu binafsi, vikundi au mashirika ili kuwapotosha, kuwachanganya, au kuwahadaa wengine".
Kampuni hiyo ilituambia kuwa tangu vita hivyo vilipoanza, imeondoa zaidi ya akaunti 100,000 kwa ukiukaji wa matumizi mabaya ya sera ya jukwaa hilo na ujumbe usiofaa ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kwa akaunti nyingi zinazohusiana na alama za reli #IStandWithRussia na #IStandWithPutin.
Twitter inasema imechunguza na kusimamisha mamia ya akaunti zilizoonyeshwa na utafiti wa CASM na kutumwa kwa jukwaa na BBC, ikiwa ni pamoja na akaunti 11 kati ya 12 ambazo zimeripotiwa mahsusi na BBC kwa kutumia picha za kwenye akaunti za watu wengine.
Lakini ilisema hakukuwa na ushahidi wowote wa kuratibu ukuzaji wa maoni kwa njia isiyo halali kuhusu vita vya Ukraine.