Mwai Kibaki: Fahamu mchango wa Rais Kibaki katika siasa za 2022

- Author, Joseph Kioko
- Nafasi, Mchambuzi Kenya
- Iliyochapishwa
Mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki yanafanyika leo katika mojawapo ya shughuli za mwisho za kumpa safari ya mwisho kiongozi huyo aliyeongoza Kenya kwa miaka 10.
Siku ya Ijumaa, Aprili 22, 2022 itaishia kuwa moja ya siku za giza, huzuni kubwa maishani mwetu kama Wakenya.
Kifo cha Rais wa awamu ya 3 Jamhuri ya Kenya, Mhe. Emilio Mwai Kibaki kilishangaza taifa ilipotangazwa na rais wa 4 wa jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta katika ikulu ya Nairobi. Kibaki aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90.
Jinsi alivyonza siasa nchini Kenya
Rais Kibaki binafsi, amekuwepo katika enzi zote za kisiasa ambazo zimefafanua mwelekeo wa demokrasia ya nchi yetu. Akiwa mhadhiri mchanga katika Chuo Kikuu cha Makerere wakati wa enzi za kabla ya kupatikana kwa uhuru, Mwai Kibaki "alichukuliwa " na marehemu Tom Mboya ili kuja kuongoza chama kipya kilichoanzishwa cha Kenya African National Union (KANU) kama Mkurugenzi Mtendaji wake wa kwanza na pia kusaidia katika uandishi wa katiba ya kwanza ya uhuru huko Lancaster Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kazi ya kisiasa ya Kibaki ilianza mwaka wa 1963 kama Mbunge wa Donholm wakati huo (sasa Makadara jijini Nairobi) kabla ya kuhama katika uchaguzi uliofuata hadi eneo bunge la sasa la Othaya, ambako alihudumu kama Mbunge hadi 2001.
Wakati wa baraza la mawaziri la kwanza baada ya uhuru chini ya uongozi wa Rais Jomo Kenyatta, Kibaki aliwahi kuwa Waziri Msaidizi kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha kuanzia 1969 hadi 1982.
Ni katika kipindi chake kama Waziri wa Fedha, ambapo gazeti la Times lilimtaja kuwa miongoni mwa watu 100 wakuu duniani waliokuwa na uwezo wa kuongoza.
Kifo cha rais Jomo Kenyatta
Wakati wa mabadiliko ya kwanza ya kisiasa/uongozi katika ngazi ya ofisi ya Rais yalipotokea kwa sababu ya kifo cha Rais Jomo Kenyatta na hatimaye Rais Moi kuwa Rais wa 2 wa Kenya mwaka 1978, Kibaki alipandishwa cheo hadi Makamu wa Rais akiwa bado anashikilia wadhifa wa Fedha ,hadi wadhfa huo ulipobadilisha hadi ule wa Mambo ya Ndani mwaka wa 1982. Kibaki alihudumu kama Makamu wa Rais wa Moi kuanzia 1978-1988.
Wakati wa msukosuko wa kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini, Kibaki aliendelea kuwa mtetezi mwaminifu wa KANU hadi alipomshangaza kila mtu mnamo Desemba 1991 kwa kujiuzulu kutoka kwa serikali ya KANU na kuunda chama cha upinzani kilichoitwa Democratic Party.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa kutumia chama hiki, Kibaki aligombea na kushindwa katika chaguzi zote mbili za urais za 1992 na 1997 na Rais aliyekuwa madarakani Moi, hata hivyo aliweza kuimarisha sifa yake ya kidemokrasia kama mshiriki aliyekuwa mbele katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa 2002.
Moja ya mafunzo muhimu yaliyopatikana katika uchaguzi wa 1992 na 1997 ni kwamba upinzani uliogawanyika haungeweza kamwe kushinda dhidi ya chama cha KANU na mgombea wake ambaye angeungwa mkono na Rais aliyekuwa w madarakani wakati huo Daniel Moi.
Uchaguzi wa 2002
Utambuzi huo ndio uliozaa Muungano wa Kitaifa wa Upinde wa mvua (NARC) uliowaleta pamoja viongozi wa zamani wa upinzani na wanachama wa ngazi za juu waliochukizwa na chama tawala cha KANU ulioongozwa na Raila Odinga na marehemu George Saitoti miongoni mwa vinara wengine wa KANU.
Muungano huu ndio uliomsukuma Mwai Kibaki kuwa Rais wa 3 wa Jamhuri ya Kenya. Ushindi huu uliimarisha umuhimu wa ujenzi wa miungano katika mjadala wa kisiasa wa taifa letu, yaani, hakuna mtu hata mmoja angeweza kuwa na njia ya kuingia madarakani bila kuingia katika miungano ya kisiasa/na watu wengine wenye nia kama yake.
Wahusika wa kisiasa nchini Kenya
Uchaguzi wa 2002 wa Kibaki kama rais ulileta kipindi cha matumaini katika mfumo wa kitaifa wa siasa zetu. Nchi iliamini kuwa utawala mpya wa NARC ungeondoa mtindo mbaya wa KANU wa kuendesha shughuli za serikali.
Katika nyanja ya kisiasa, istilahi mpya ilikuwa imeanzishwa kwa jina la 'Mkataba wa Maelewano' (MoU) ambayo ilifafanua jinsi washirika wa muungano wangepaswa kufanya mara tu wanaposhika mamlaka.

Chanzo cha picha, AFP
Kuheshimiwa kwa MoU kati ya mrengo wa Rais Kibaki wa muungano wa NARC na mrengo wa Raila Odinga lilikuwa jambo la wasiwasi mkubwa ambalo lilitishia na hatimaye kufanikiwa kuisambaratisha serikali ya NARC katikati.
Rais Kibaki alishutumiwa kwa kupuuza ahadi zilizotolewa katika MoU, muhimu miongoni mwao ilikuwa ni kuanzishwa kwa ofisi ya Waziri Mkuu na pia kupitishwa kwa katiba mpya miongoni mwa masuala mengine.
Mgogoro huu uliibua swali la uwezekano na utekelezwaji wa mikataba ya kabla ya uchaguzi mara tu vyama/mtu binafsi anaposhinda chaguzi.
Katika masuala ya kiuchumi, Rais Kibaki hakulaumiwa kwani maono yake yalikuwa hayajawahi kuonekana awali nchini Kenya; urithi wa kidemokrasia wa Kibaki hata hivyo ulitiliwa shaka kutokana na masuala pacha ya uaminifu wa kisiasa kama inavyofafanuliwa na MoU katika uwanja wa kisiasa na uwasilishaji wa katiba mpya na faida zake kwa kenya mpya.
Siasa ni kama mtiririko wa maji kwa asili yake; mambo yanayozua ugomvi leo labda huenda yakakubalika kesho na yanayokubalika leo labda kesho huenda yakazua ugomvi.
Hali kama hiyo ilijiri wakati wa kutekelezwa kwa MoU ya 2002 kati ya washirika wa muungano wa NARC. Wakati wa mazungumzo, wahusika wote walijiendesha kwa njia ya heshima, kulikuwa na imani ya kweli kwamba MoU ingeheshimiwa, hata hivyo mara tu mgombea wa NARC Kibaki alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, uwezo wa kutekeleza MoU uligonga mwamba.
MoU haikuwa na nguvu ya sheria lakini ilitegemea nia njema kutoka kwa Rais Kibaki na wenzake.
Tangu wakati huo hali hii imejirudia kwa miaka mingi na viongozi mbalimbali wa kisiasa, hivi majuzi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Uhuru alikuwa ametangaza hadharani kwamba "kumi yangu, kumi ya Ruto"; hata hivyo Kenya inapokaribia uchaguzi wa 2022, Rais Uhuru ametangaza waziwazi kumuunga mkono Raila Odinga na kuamua kupuuza barua ya ahadi aliompatia naibu wake William Ruto.
Kwa upande mwingine wa muungano wa NASA wa 2017, chama cha ODM kiliamua kwa upande mmoja kuwanyima washirika wengine wa muungano huo sehemu yao ya haki kutoka kwa hazina ya vyama vya kisiasa kwa msingi kwamba uchaguzi wa 2017 ulibatilishwa.
Kwa hivyo kile kilichoanza kama ukiukaji mdogo kati ya washirika wa muungano ndani ya muungano wa Rais Kibaki wa NARC umezua tabia mbaya ya kisiasa, ambayo baadaye ililazimu kupitishwa kwa Sheria ya vyama vya kisiasa iliyorekebishwa ya 2022, kufafanua na kutunga sheria jinsi miungano ya kabla na baada ya uchaguzi inapaswa kusimamiwa.
Katiba Mpya
Mtu hawezi kutenganisha msukumo wa kutaka katiba mpya na urithi wa kidemokrasia wa Rais Kibaki. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 90, Wakenya walikuwa wakipigania kupitishwa kwa katiba mpya ambayo ilikuwa na msukumo wa raia na isiyo na marekebisho kidogo.
Pamoja na uchaguzi wa 2002 wa Rais Kibaki, Wakenya wengi waliamini kuwa katiba mpya inaweza kupatikana. Hata hivyo utumizi mbaya wa MoU ya kisiasa ndani ya NARC ya Rais Kibaki ulikuwa umeunda mazingira ya sumu ambayo hayakuwa na uaminifu na hivyo basi kile ambacho kingekuwa zoezi la kupendeza katika uundaji wa katiba kiligeuka kuwa jaribio la kuchukiza na la kuleta migawanyiko katika uundaji wa katiba.
Mgawanyiko kubwa katika serikali ya NARC ulidhihirika katika kampeni ya kura ya maoni ya katiba ya 2005, ambapo nusu ya upande wa serikali iliunga mkono rasimu ya katiba huku nusu nyingine ya serikali inayoongozwa na Raila Odinga ikipinga rasimu ya katiba.
Rasimu ya katiba hatimaye ilishindwa, nusu ya baraza la mawaziri lililopinga rasimu hiyo likafutwa kazi na Rais Kibaki, na chama kipya cha kisiasa kilichoitwa Orange Democratic Movement (ODM) kikaundwa, kikiongozwa na Raila Odinga.
Msukumo wa kisiasa ambao ulitokana na kushindwa kwa rasimu ya katiba ya serikali ya Rais Kibaki uliendelezwa hadi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2007, huku chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kikiwa kifua mbele.
Ingawa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) ilimtangaza Mwai Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali wa 2007, matokeo yake yalipingwa na chama cha ODM, hatua iliozidisha maandamano ya Wakenya wengi ambao walihisi kuwa Kibaki hakushinda uchaguzi.
Hili ndilo lililosababisha ghasia za baada ya uchaguzi ambazo zilishuhudiwa mwaka wa 2007. Katika juhudi za kuhakikisha amani na utulivu, serikali ya umoja wa kitaifa iliundwa huku Kibaki akiwa bado amebakia kama Rais na Raila kama Waziri Mkuu, na kwa ushirikiano wa pamoja wakiwa na dhamira ya kuuundwa na hatimaye kuidhinishwa kuwa katiba mpya.
Huku wahusika wote wakuu wa kisiasa wakikubaliana, Kenya iliweza kupata na kutunga katiba mpya mwaka wa 2010 na hivyo kumaliza kelele na hamu ya katiba mpya nchini Kenya. Hivyo Rais Kibaki hatimaye aliweza kuwapa Wakenya katiba mpya.
Viongozi aliowaacha katika ulingo wa kisiasa
Kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (2007-2013), ndiko kulikozaa kwa namna nyingi zao la viongozi wa sasa; huku Raila Odinga akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta na Musalia Mudavadi waliteuliwa kuwa manaibu waziri Mkuu, Kalonzo Musyoka aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais na William Ruto aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo; watu hawa watano wameendelea kutawala siasa nchini Kenya hata baada ya Rais Mwai Kibaki kustaafu mwaka 2013.
Uchaguzi mkuu wa 2013 ulikuwa mchuano kati ya muungano wa Waziri Mkuu Raila Odinga na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka (CORD) dhidi ya muungano wa Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na Waziri William Ruto (TNA/URP).
Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi pia aliwania wadhifa huo katika uchaguzi huo. Wakati wa kampeni za 2013 nambazo zilikuwa tofauti kabisa na kipindi cha mpito cha kisiasa cha 2002 kilichosimamiwa na mtangulizi wake, Rais Mwai Kibaki alichagua kuchukua msimamo wa kutoegemea upande wowote na kwa msisitizo mkubwa katika kuhakikisha kuna mpito wa amani kwa yeyote atakayeshinda.
Na kwa hili, uchaguzi wa 2013 ulikuwa wa amani kwa kiasi kikubwa, wale ambao walisikitishwa na matokeo ambapo walihimizwa kupinga matokeo kupitia mahakama kuu mpya iliyoanzishwa kama ilivyoainishwa katika katiba na hivyo mabadiliko ya amani yalifanyika.
Siasa katika maisha ina changamoto nyingi, kupanda na kushuka, ushindi na hasara, furaha na huzuni; Rais Mwai Kibaki, kama mwanasiasa kwa ubora alipitia yote haya .
Pamoja na mafanikio yake mengi pia alikuwa na mapungufu yake, lakini yote kumi , Kenya ilipata mojawapo ya nyakati zake bora za ukuaji wa uchumi wakati wa uongozi wa Rais wa 3 wa Jamhuri ya Kenya; huku pia ikipitia kipindi kigumu cha msukukosuko wa kisiasa uliotokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007.
















