Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
BBI:Mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya yakataa rufaa ya Rais Kenyatta ya kubadilisha katiba
Mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya imeamua kuwa Rais Uhuru Kenyatta alitenda kinyume cha sheria alipoanzisha mchakato wa kufanya mabadiliko mapana ya katiba.
Majaji wa mahakama hiyo ya upeo walikataa rufaa ya serikali iliyotaka kubatilisha maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ambazo zilisema marekebisho ya sheria yalipaswa kuongozwa na raia badala ya kufadhiliwa na mkuu wa nchi aliye madarakani .
Majaji hao pia walisema mapendekezo hayo yamevunja katiba kwa kuunda maeneo bunge mapya bila ushirikishwaji wa wananchi
Serikali hata hivyo iliruhusiwa kukata rufaa kwa masuala mengine matano ambayo yalikuwa yakizingatiwa na mahakama. Hukumu ya mwisho itasomwa Jumanne wiki ijayo.
Rais Kenyatta pia alipata ahueni huku Mahakama ya Juu ikitupilia mbali uamuzi wa mahakama za chini ambao ulikuwa umeamua kwamba anaweza kushtakiwa kama mtu binafsi.
Sheria iliyopendekezwa ambayo inajulikana kama Building Bridges Initiative ililenga kupanua serikali kwa kuleta nafasi za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili . Bunge pia lingepata zaidi ya wabunge wengine 70 hatua ambayo mahakama ilisema ni kinyume cha katiba.
Mjadala kuhusu mpango huo unahusishwa kwa karibu na vita vya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anatazamiwa kuachia ngazi Agosti baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.
Wakosoaji wanaona pendekezo la kupanua wigo wa serikali kuu kama njia ya kuwazawadia wanasiasa.Uamuzi huo sasa utapokelewa kama ushindi na mrengo wa Kenya Kwanza unaoongoza na naibu wa rais William Ruto ambaye amepinga mchakato mzima wa BBI tangia mwanzo ilhali aliyekuwa waziri Mkuu Raila Odinga na rais Kenyattawamekuwa wakiunga mkono mchakato mzima .
Uamuzi wa leo wa mahakama hiyo huenda utakuwa pia na athari kwa kampeni zinazoendelea za uchaguzi wa mwezi Agosti kwani upande mmoja utaonekana kupata ahueni ilhali upande uliokuwa ukiunga mkono utaonekana kushindwa katika jitihada za kurekebisha katia ya nchi hiyo