Uchaguzi wa Kenya2022:Ratiba na tarehe muhimu kuelekea uchaguzi wa Kenya 2022

    • Author, Odhiambo Joseph
    • Nafasi, BBC Africa, Nairobi
  • Iliyochapishwa

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya tayari imetoa ilani ya ya mchakato mzima kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumanne tarehe 9 Agosti , 2022.

Katika ilani hiyo kuna baadhi ya tarehe ambazo zinajumuisha viti vyote na kuna nyingine inayohusu viti fulani tu.

Tarehe za jumla

•Jumatano , Februari 9, 2022 - Afisa yeyote wa umma anayetaka kugombea kiti chochote katika uchaguzi huu mkuu atalazimika kujiuzulu ifikapo Jumatano , Februari 9, 2022 ( miezi sita kabla ya uchaguzi)

•Alhamisi , Juni 9, 2022 - Mapingamizi au kesi zinazohusu uteuzi wa wagombea ndani ya vyama ni sharti ziwasilishwe mbele ya tume kabla ya siku ya Alhamisi , Juni 9, 2022.

•Saa za kampeni ni kuanzia saa moja asubuhi hadi kumi na mbili jioni - katika kipindi cha kampeni.

•Jumatatu , Julai 25, 2022- Vyama vya kisiasa pamoja na wagombea watahitajika kuwateuwa na kuwasilisha majina ya mawakala wao kwa tume kabla ya Jumatatu , Julai 25, 2022.

•Jumapili Mei 29, 2022 -Kipindi rasmi cha kampeni za uchaguzi huu mkuu ni kuanzia Jumapili Mei 29, 2022 na kumalizika jumamosi , Agosti 6, 2022, yaani saa 48 kabla ya siku ya kupiga kura.

•Jumanne tarehe 9 Agosti , 2022- Siku ya kupiga kura

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma

Masharti na tarehe zinazohusu vyama vya kisiasa

Vyama vyote vya kisiasa vinalazimika kuwasilisha sajili zao za wanachama kwa tume ya uchaguzi ifikapo Jumamosi , Aprili 9, 2022.

•Chama chochote kinacholenga kushiriki katika uchaguzi huu ni sharti kiwasilishe majina ya wale wote wanaonuia kushiriki katika mchakato wa uteuzi wa vyama kwa njia ya mchujo, tarehe ya shughuli yenyewe na mahali penyewe ifikapo Jumamosi , Aprili 9, 2022, ikiwa ni siku 21 kabla ya uchaguzi mkuu.

•Chama kinachopanga kushiriki katika uchaguzi mkuu nisharti washughulike mapingamizi yeyote kwa kutumia mfumo wa ndani wa chama ifikapo Ijumaa Aprili 22, 2022.

•Chama kinachopanga kumteuwa mgombea au wagombea kwa mfumo wa moja kwa moja bila ya mchujo kiwasilishe majina hayo kwa tume ifikapo Alhamisi Aprili 28, 2022.

Masharti na tarehe zinazohusu wagombea huru

•Jumatatu Mei 2, 2022 - Wagombea wanapanga kushiriki katika uchaguzi huu kama wagombea huru ni sharti wasiwe wanachama wa chama chochote cha kisiasa kabla ya Jumatatu Mei 2, 2022, hii ikiwa ni angalau miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu .

•Jumatatu Mei 2, 2022.- Wagombea wanaolenga kushiriki katika uchaguzi huu kama wagombea huru ni sharti wawasilishe majina yao pamoja na nembo zao wanazonuia kutumia katika uchaguzi ifikapo Jumatatu Mei 2, 2022.

•Ijumaa Mei 13, 2022 -Tume ya Uchaguzi itachapisha katika gaezeti rasmi la serikali majina pamoja na nembo ambazo wagombea huru wanapanga kutumia angalau siku 14 kabla ya tarehe rasmi ya uteuzi iliyowekwa na tume, yaani kabla ya Ijumaa Mei 13, 2022

Masharti na tarehe zinazohusu wagombea urais

Jumatatu Mei 23, 2022 - Wagombea Urais kuwasilisha orodha ya angalau wapiga kura 2000 kutoka zaidi ya nusu ya Kaunti zote 47 kufikia Jumatatu , Mei 23 , 2022

Jumatatu , Julai 25, 202 - Vyama vya kisiasa pamoja na wagombea urais kuteuwa na kuwasilisha majina ya mawakala wake wakuu wa kitaifa na wa maeneo bunge kwa tume ifikapo Jumatatu , Julai 25, 202.

Jumapili , Mei 29 - Zoezi la uteuzi wa Tume kwa wagombea wote wa Urais kupitia vyama vya kisiasa na hata wagombea huru utaanza Jumapili , Mei 29 na kulamilika Jumatatu, Juni 6, 2022

Jumanne Agosti 9 , 2022- siku ya uchaguzi Mkuu wa Kenya