Kwanini suala la kutambulisha kabila limeleta gumzo Tanzania?

Iliyochapishwa

Oktoba 12 mwaka 2021, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizungumza hadharani akiwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma kwamba yeye hana kabila.

Chini ya miezi sita baada ya kauli hiyo, serikali imewataka watumishi wake kutaja makabila na dini zao katika taarifa zao rasmi. Watanzania, sirini na hadharani kupitia mitandao ya kijamii., wamepigwa na butwaa.

Tayari baadhi ya taasisi za kitaaluma, watumishi wa serikali na wanahabari wameanza kuhoji nini hasa ni lengo la serikali katika kulazimisha watumishi wake kuweka taarifa za namna hiyo kwenye mafaili yao.

Swali kubwa ambalo linaulizwa ni je, kama Rais ambaye kikatiba ni Mkuu wa Serikali na Watanzania walimwamini kushika wadhifa huo mkubwa kuliko wote ndani ya Jamhuri ya Muungano pasipo kujua kabila lake, nini hasa serikali inakitafuta kwa kuuliza dini na makabila ya watumishi wake?

Akizungumza na mojawapo ya magazeti ya Tanzania wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, alieleza hatua hiyo kuwa ni ya kawaida na ina lengo la kuwa na taarifa zaidi za watumishi wao na pia kurahisisha mawasiliano wakati wanapotakiwa kutumika katika maeneo mengine nje ya utumishi wa serikali.

Katika kitabu chake mashuhuri cha Why Leaders Lie, Profesa John Mearsheimer wa Chuo Kikuu cha Chicago, Marekani anazungumzia namna mbili ambazo serikali inaweza kutoa taarifa ambazo si halisi; ama kutoa nusu ya taarifa au kutoa taarifa ambayo inaweza kukubalika kirahisi kwa watu (spinning). Maelezo ya Tutuba yanaangukia zaidi katika sababu ya kwanza kuliko ya pili. Lakini kwanza ni muhimu kueleza kwa nini Watanzania wameshtushwa na hatua hii.

Watanzania na ukabila

Hakuna kiongozi ambaye anajulikana kwa kukemea udini na ukabila nchini Tanzania kumzidi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius. Mwalimu Nyerere anaheshimika duniani kwa sifa ya kuwa mtu aliyeifanya nchi hiyo kuwa mojawapo ya nchi chache za Kiafrika zisizo na tatizo la ukabila.

Katika mojawapo ya hotuba zake mashuhuri, Mwalimu alisikika akisema; "Ukisikia Watanzania wanaulizana makabila yao ujue wanataka kutambika". Kwa maana moja au nyingine, aliamini kwamba Watanzania wameshavuka hatua ya mtu kujua kabila la mwingine katika masuala yanayohusu maslahi ya umma kama utumishi wa serikali.

Hata katika hotuba yake niliyoinukuu katika aya ya kwanza ya makala hii, Rais Samia alieleza kwamba Zanzibar anakotoka, watu wanajuana zaidi kupitia mahali walikozaliwa kama vile Tumbatu, Pemba, Makunduchi na kwingine kuliko makabila yao. Rais huyo alikuwa akijibu watu aliodai alikuwa 'akitumbua' watu kutoka makabila na dini fulani huku akiteua na kubakisha watu wa dini na maeneo fulani ya Tanzania.

Serikali ya Mwalimu Nyerere, kuanzia siku za mwanzo za Uhuru, ilifanya jitihada kubwa za kuunganisha makabila nchini kwa kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kote nchini humo, kuvunja tawala za uchifu, kuweka mfumo wa Watanzania kupitia mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa sheria na hata kuchagua viongozi wakubwa wa chama na serikali pasipo kujali udogo au ukubwa wa makabila yao. Hadi hii leo, kupitia jitihada hizo za kisera za kujenga taifa lisilo na udini wala ukabila, hakuna sensa iliyowahi kufanyika Tanzania na kusema idadi ya Wakristo na Waislamu au kabila moja moja miongoni mwa zaidi ya 120 yaliyopo.

Kwa sababu ya maneno ya Baba wa Taifa katika miaka ya nyuma na kutokana na ukweli kwamba pengine Tanzania ndiyo nchi pekee ya Afrika Mashariki na Kati yenye mchangamano mkubwa zaidi wa kidini na kikabila miongoni mwa watu wake - jambo lolote linalogusa au lenye viashiria vya kuweka mbele mambo hayo huwa linapokewa tofauti na jamii.

Nchi Jirani kama Rwanda na Burundi zilikuwa na utaratibu wa kuweka makabila yao hadi katika vitambulisho vyao vya utaifa lakini utaratibu huo uliondolewa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbari yaliyotokana na ukabila; hivyo kulazimisha kufanyika jitihada za makusudi kuondoa taratibu hizo za kutaja makabila katika maeneo ya utumishi wa umma na maisha ya kila siku.

Utafiti katika mtandao wa internet unaonyesha kwamba nchi nyingi duniani zimeachana na taratibu za kutaja makabila na kimsingi hivi sasa watu wanashauriwa kuacha hata kuandika jinsi zao, kama wameoa au kuolewa, dini zao na kadhalika kwa sababu inaonekana taarifa hizo zimeanza kutumika kubagua zaidi kuliko sababu nyingine yoyote ya msingi.

Kwanini waajiri hutafuta taarifa za dini na makabila?

Miaka mitatu iliyopita, kampuni moja nchini Kenya ilitoa tangazo la nafasi za kazi lakini ikaeleza kwamba wanaoomba kazi ni lazima wataje makabila yao katika maombi yao. Jambo hilo lilizua mjadala mkubwa kiasi kwamba mtandao wa careerpointkenya ulimhoji mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu kutoka shirika la Corporate Staffing Services, Kennedy Munyendo, ili atoe maoni yake kuhusu nini hasa inaweza kuwa sababu.

Mtaalamu huyo alitoa sababu tatu zinazoweza kumfanya mwajiri kutaka kujua dini au kabila la anayeomba kazi. Sababu hizo ni; endapo mwajiri anaona shirika lake limejaa watu wa kabila au eneo fulani na anataka kuingiza watu wengine, hataki kuajiri watu wa sehemu fulani na anatumia fursa hiyo kutimiza lengo lake na la tatu linahusu aina ya kazi inayotaka kufanyika. Katika jambo la tatu alitoa mfano wa kazi ambayo kwa mfano inahitaji mtu anayejua lugha fulani kwa sababu inahusu kufanya kazi na jamii hiyo.

Kwa maelezo hayo ya Munyendo, sababu ya tatu haiwezi kuwa ndiyo inayotakiwa na serikali ya Tanzania kwa sababu inahusu watumishi wote. Sababu ya kwanza inaweza kujibu swali la kwanini serikali inataka kufanya inachofanya sasa.

Hakuna ukabila lakini kuna makabila

Kitabu cha Profesa Mearsheimer kinaeleza sababu mojawapo ya serikali kutotoa taarifa halisi na kamili wakati fulani. Kama kutoa taarifa rasmi kunaweza kuleta mjadala mkubwa zaidi kuliko kutoa taarifa kidogo, hilo limefanyika mara nyingi ikiwamo wakati wa mgogoro wa baina ya Marekani na Urusi kuhusu makombora ya Cuba (Cuban Missiles Crisis).

Yapo malalamiko kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na tatizo la watu kupewa vyeo na ajira serikalini bila kuzingatia uwiano walau wa maeneo na dini. Mwanahistoria maarufu wa Tanzania, Mohamed Said, hivi karibuni alitoa chapisho mitandaoni lililoonyesha kwamba katika miaka sita iliyopita; uteuzi katika nafasi za mawaziri, wakurugenzi, viongozi wa halmashauri na wengine ulikuwa na uwiano wa asilimia 80 kwa Wakristo na 20 Waislamu. Yapo pia malalamiko kwamba kuna makabila yalinufaika zaidi na uteuzi kuliko mengine.

Kuna uwezekano kwamba serikali inataka kujiridhisha na kufahamu ukubwa wa jambo husika. Hoja hii inatiwa nguvu na ukweli kwamba walau kwa sasa, wanaotakiwa kutoa taarifa hizi ni wale ambao tayari wako serikalini na si wanaoomba. Huenda zoezi hili litaipa serikali nafasi ya kufahamu kama kuna tatizo na namna ya kubadilisha mwelekeo. Hii ni kama sababu za kutaka watu wataje makabila na dini ndiyo zile za Munyendo.

Na kama hii ndiyo sababu halisi, kama ambavyo Mearsheimer aliandika miaka michache iliyopita, sioni namna ya serikali kutoka hadharani na kusema sababu halisi ndiyo hiyo. Ikifanya hivyo, itakuwa imefungua mlango wa mjadala ambao pengine moto wake ni mkali kuliko huu wa kusema "hii ni hatua ya kawaida".