Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu umuhimu wa ziara ya Rais Samia Ulaya kwa Watanzania
- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
"Tanzania itakuwa sawa na Ulaya ndani ya miaka 6", hii ilikuwa kauli ya Rais wa taifa hilo, Samia Suluhu Hassan mara baada ya kurejea nyumbani mwishoni mwa wiki akitokea barani Ulaya alikokuwa na ziara ya kikazi katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji.
Ni kauli iliyoibua mjadala mkubwa. Wapo wanaojiuliza itawezekanaje? Na wapo wanaoona inawezekana. Lakini hilo halizuii mtazamo wa namna ziara hiyo ilivyoleta sura tofauti kwenye nyanja ya kidiplomasia na fedha za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Siku 10 za ziara hiyo zimefungua milango ya mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na kijami, milango ambayo ilifungwa kwa 'kufuli la chuma' katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.
'Kipindi kile ambacho hatukuwa vizuri walifikia hatua ya kuzuia fedha za miradi ambayo Tanzania iliomba lakini sasa wamefungua kila kitu kiko vizuri", anasema Rais Samia kwenye moja ya mahojiano yake kuhusu ziara hii.
Hasara za kufunga mlango wa mahusiano hasa na nchi za Umoja wa Ulaya zilikuwa kubwa zaidi kuliko faida. Lakini ziara hii ina maana yoyote kwa mtanzania? Jibu fupi na rahisi ni ndiyo, kwa sababu nyingi tu lakini hizi ni miongoni mwao;
Fedha za Miradi
Kwa mujibu wa Rais Samia, amefanikiwa kupata fedha za msaada kiasi cha Euro milioni 450 sawa na Shilingi trilioni1.17 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) ikiwa ni sehemu ya Euro bilioni 55 zilizotengwa na Umoja huo kwa ajili ya Afrika kukabiliana na janga la Covid 19.
Katika kipindi cha cha miaka mitatu ijayo fedha hizo zitatumika kukwamua miradi iliyokwama ya viwanja vya ndege Kigoma, Shinyanga na Pemba, ukarabati wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam (Terminal II), Mafunzo, mradi wa mabasi ya umeme, ukamilishaji wa mradi wa mabasi ya mwendo wa haraka na kilimo.
Euro milioni 450 ni fedha zinazoweza kuchochea maendeleo ya nchi kwa kasi. Uwepo wa fedha hizi mbali na malengo yake ya moja kwa moja, utaongeza pia mzunguko wa fedha mtaani na kuchangamsha shughuli za uchumi kwa wananchi. Shughuli za uchumi zikichangamka, unatengeneza ajira na kuongeza kipato cha watu, mwishowe unaboresha maisha yao kwa sababu wataweza kumudu kununua bidhaa, huduma na mahitaji muhimu kuendesha maisha yao.
Mwishoni mwa mwaka jana Tanzania ilipokea mkopo wa shilingi trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa ajili ya kushughulikia janga la Corona. Mkopo huu umesaidia ujenzi wa maelfu ya madarasa nchi nzima na kutafsiri vyema mpango wa serikali ya Tanzania wa kuinua uchumi wake na wa watu wake. Kama zilivyo kwa fedha hizi, fedha za 'Ulaya' alizozipata Rais Samia kama zitatumika vyema, zitasaidia kuinua sekta lengwa.
'Ziara ya Samia, bila shaka ina faida kubwa, lakini kupata fedha hizi ni jambo moja, japo la pili na la muhimu, lazima fedha hizi zisimamiwe vyema ili zipelekwe kwenye lengo husika lenye faida kwa wananchi', alisema Profesa Balthazari Namwata wa Chuo kikuu cha Ushirika Moshi.
Kusafisha uhusiano wa kiplomasia
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita Tanzania ilisakamwa kwa kutokuwa na mahusiano mazuri kidiplomasia na Jumuia ama nchi zingine. Rais wa wakati huo, Magufuli, alipendelea kutuma wawakilishi katika mikutano mingi mikubwa na hakuwahi kusafiri kwa ziara yoyote ya kikazi nje ya bara la Afrika.
Hata kwa ziara zake ndani ya Afrika, alizuru nchi tisa tu kati ya nchi zaidi ya 50 katika wakati wote huo, akitembelea nchi za Rwanda, Kenya, Ethiopia, Burundi, Uganda, Afrika Kusini, Namibia, Malawi na Zimbabwe.
Lakini katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja Rais Samia ameshatoka kwa uwiano mara nyingi zaidi ya mtangulizi wake. Na safari hii akienda Ulaya ambapo uhusiano wa Jumuia ya bara hilo na Tanzania umedumu kwa miongo zaidi ya mitani.
Rais Samia mwenyewe anakiri kwamba katika kipindi hicho uhusiano wa Tanzania na Jumuia ya Ulaya ulikuwa na changamoto.
"Wakati ule ulikuwa ni mtazamo, tulikuwa tunaangalia mambo ya EPA (Mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi), kulikuwa kuna kugongana gongana kwenye ideology kwenye siasa, labda Ulaya walisema jambo ambalo halikutupendeza, lakini baada ya muda tumezungumza na yote yako sawa sasa", anasema Rais Samia.
Unaweza pia kusoma:
Suala la mapenzi ya jinsia moja, wanafunzi wanaopata mimba kutorejea shuleni na masuala mengine yaliyoonekana kama ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa Jumuia ya Ulaya, yalichochea kuni za moto wa kuyumbisha uhusiano wa pande hizo mbili.
Novemba 2018, Umoja wa Ulaya ulimwita nyumbani Brussels, Ubelgiji mjumbe wake aliyekuwa Tanzania, Balozi Roeland van de Geer ikiwa ni mwezi takribani mmoja, tangu aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutangaza operesheni ya kuwasaka watuhumiwa mapenzi ya jinsia moja jijini Dar es Salaam. Ingawa baadye Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ilisema zoezi hilo halikuwa msimamo wa Serikali.
Katika taarifa rasmi Umoja huo wakati huo ilisema, "Umoja wa Ulaya unajutia kupungua kwa haki za binaadamu na mkondo wa sheria Tanzania na itafanya tathimini pana ya uhusiano wake na Tanzania."
Haki inayotajwa pia kukiukwa wakati wa utawala uliopita ni pamoja na vyama vya siasa kutofanya mikutano siasa kama inavyotakiwa, ingawa hali hiyo inaonekana kuwepo sasa lakini mkazo wake haufanani na sura ya wakati ule.
Mbali na fedha, ziara ya Rais Samia Ulaya, imekwenda kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kidiplomasia baina ya taifa hilo na Jumuia ya Ulaya.
Dhana ya 'mabeberu' ilivyofifisha uhusiano wa pande hizi mbili
Kabla ya kuingia kwa awamu ya tano ya uongozi wa Rais Magufuli, Uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Tanzania, haukuwa na changamoto nyingi. Ni katika awamu hii dhana ya wageni kutoka mataifa ya Marekani na Ulaya kuonekana 'mabeberu' iliposhika kasi na kuonekana kama watu wenye mitazamo ya kunyonya zaidi kuliko kusaidia.
Hata kama dhana hiyo ilikuwepo nyuma, namna ilivyobebwa iliongeza wigo wa utofauti wa mitazamo katika sera, mipango na maoni.
Hapa palikua mwanzo wa kudorora kwa uhusiano huu, na mwishowe Umoja wa Ulaya ukaamua kusitisha fedha za kufadhili miradi mbalimbali, ambayo ilikuwa isaidie mpango wa serikali wa miaka mitano iliyopita. Ilizuia Euro milioni 111.5, ambazo sasa umeziachia baada ya mazungumzo na Rais Samia na umoja huo.
Leo ubeberu, sio hoja, Rais Samia anawakaribisha na anawafuata walipo, na maisha yanaendelea, ikiwa ni tofauti kubwa na mtangulizi wake, Rais Magufuli ambaye katika utawala wake hakuwahi kutoka nje ya bara la Afrika.
"Dhana ya ubeberu na mabeberu, kishabiki unaweza kuiona ni ya maana, lakini kiuhalisia, ubeberu ni falsafa ambayo inakutegemea wewe unawachukuliaji na kulinda rasilimali na watu wako dhidi ya hao unaowaita mabeberu, anasema Martina Mariki Muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
Je huu ni muelekeo wa Rais Samia?
Tangu aingie madarakani, Rais Samia amekuwa akifanya ziara mara kadhaa na kuhudhuria mikutano ya kimataifa ambayo mtangulizi wake, Rais Magufuli mara kadhaa aliwatumia wasaidizi wake akiwemo yeye Samia wakati huo akiwa Makamu wa Rais.
Tumeshuhudia, faida kubwa ya kufanya hivyo katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu aingine madarakani Machi 19, 2021, kufuatia kifo cha Magufuli. Wengi wanajiuliza huu ndio utakuwa muelekeo wake?
'Nadhani tutashuhudia akisafiri sana, kama ilivyokuwa katika kipindi cha Kikwete (Rais wa awamu ya nne), ama atawaalika sana wageni hapa nyumbani, uzuri ni kwamba hakutani tu ama hasafiri tu kama kutembea, vikao na ziara zake zinakuja na faida kwa watanzania', alisema Dkt. Barnos Willium, mchumi kutoka chuo kikuu cha ushirika Moshi.
Liko wazi kwamba Rais Samia anaaamini katika kujenga na kudumisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa na jumuia zingine. Hilo lilionekana dhahiri kwa kumteua Balozi Libarata Mulamula kuwa waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki. Balozi Mulamula ni msomi, na mzoefu wa miaka zaidi ya 30 kwenye diplomasia, akihudumu kama balozi wa Marekani, Canada na balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
Mbali na uteuzi huo, amekuwa akifanya vikao vingi na kukutana na viongozi mbalimbali wa mataifa ya Afrika na nje ya Afrika pamoja na mashirika ya kimataifa.
Pamoja na muelekeo huo, wakosoaji wa ziara zake, wanamuona kama ni mmoja wa viongozi wanaopenda kusaifiri zaidi. Licha ya kutothibitisha madai yao, wanaona safari hizo zinaigharimu Tanzania, kwa kutumia fedha nyingi ili-hali angeweza kutuma wawakilishi ambao wangekuwa na misafara midogo isiyogharimu fedha nyingi za walipa kodi wa Tanzania.
Wanaomtetea wanasema Rais Samia hatapimwa kwa idadi ya ziara zake nje ama amekutana na watu wangapi, atapimwa kwa matokeo ya ziara hizo, ikiwemo hii aliyokutana pia na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, nchini Ubelgiji.