WARIDI WA BBC : Petra Bockle msanii wa muziki wa Rap aliyekataa ushirikina ili kujipatia umaarufu na utajiri

.

Chanzo cha picha, Petra Bockle

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Msanii Petra Bockle ni mlimbwende na mama wa mtoto mmoja.

Mbali na kuwa mmoja wa wanamuziki wa kike waliobobea katika mtindo wa muziki wa kufoka au RAP ni mwanamke ambaye amepitia changamoto chungu nzima.

Je ameyapitia yapi mazito?

"Kuwa msanii wa kike kwenye tasnia ya muziki sio kama ngoma za lele mama , kwamba una talanta ila wakati mwingine unajipata katika majaribio mengi ambayo usipokuwa na misimamo mikali na moyo wa ujasiri utajipata kwa mtego "anasema Petra

Na kwa mara ya kwanza kwenye vyombo vya habari msanii huyu amepiga moyo konde na kudhihirisha ari kwa upande mwengine wa ulimwengu wa muziki ambao kwa maoni yake ni wenye kiza kikuu .

Petra anasema kwamba alipoanza muziki wakati huo akiwa na umri wa miaka 10 hivi alikuwa anafikiria kwamba ikiwa msanii ana talanta ingekuwa rahisi kujijenga na kufaulu ila ukweli ulimjia miaka kadhaa baada ya kuanza kutajika nchini Kenya .

"Nilikuwa bado mchanga katika ufahamu wa ulimwengu wa muziki, sikufahamu kwamba kungetokea wakati ambapo ningejipata kwenye majaribu mengi, ambayo yalilenga niongeze umaarufu na pia niwe na ushawishi na utajiri wa haraka"anasema Petra .

Anasema kwamba kulikuwa na jaribio la kumshirikisha na madhehebu ya kishirikina (OCCULT) .

Chanzo cha picha, Petra Bockle

Maelezo ya picha, Anasema kwamba kulikuwa na jaribio la kumshirikisha na madhehebu ya kishirikina (OCCULT) .

Mlimbwende huyu anasema kwamba jaribio moja lilikuwa kupitia watu aliowafahamu vizuri kwa mfano watu waliokuwa na ukaribu naye kama marafiki, wandani wake kimuziki na hata wasanii wengine kutoka nje ya nchi.

Kujiunga na makundi ya kishirikina

Anasema kwamba kulikuwa na jaribio la kumshirikisha na makundi ya kishirikina(Occult)

Kupitia madhehebu haya alikuwa ameahidiwa kwamba angepata utajiri wa haraka na pia umaarufu wake ungekuwa wa ajabu.

Mwanadada huyu anasema kwamba sio mara ya kwanza au ya pili alishuhudia baadhi ya wandani wake wakiwa na pesa nyingi zisizoeleweka ila kwa upande wake yeye alishindwa kushiriki katika ushirikina uliotakikana.

Japo alisita kuzungumzia mengi kuhusu ulimwengu huo wa ushirikina huku akisema kwamba alihofia asiwe ametoboa siri na kujiweka matatani, alikubali kwamba kuna wanamuziki wanaofaidi kupitia ushirikina huo.

Anasema kujiingiza kwake katika madhehebu hayo kungemgharimu utu wake iwapo angeingia kwenye madhehebu hayo haramu .

"Bila kutaka kuzungumzia mengi , sikuwahi kujua kwamba kuna gharama ya kuwa msanii tajika na mwenye hela, kwa akili yangu wakati huo nilidhani talanta ingenifungulia milango kwa urahisi. Ila ninachokijua mimi ni kwamba kwa msanii kama mimi ambaye alikataa kuingia biashara haramu na maswala ya ushirikina lazima nipambambane maradufu ili niafikie malengo yangu"anasema mwanadada huyo.

.

Chanzo cha picha, Petra Bockle

Japo Petra anasema kwamba kama ambavyo kuna ulimwengu wa nuru na giza ni wajibu wa mtu mzima kuchagua anachotaka na kila chaguo lina gharama yake .

Kando na hayo ya majaribio ya ulimwengu wa kisanii Petra pia amejipata akiwa katika mchakato wa kuondokea ndoa ambayo anaitaja kuwa sehemu ya machungu yake yaliopelekea yeye kuwa na sonona.

Mwaka wa 2014 Petra alikutuna na mwanamume na kisha wakapendana . Wawili hao wakafaana na kuwa kama chanda na pete , ni mahaba ambayo yameangaziwa hata kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya , ila hadi mwaka wa 2020 kitumbua cha ndoa kilionekana kuingia mchanga .

" Wanawakei hutamani ndoa , nikiwa binti nilitamani ndoa , ila nilipoingia ndani yake nilianza kuelewa kwamba sio rahisi , mambo mengi yakitendeka na nikawa najipata na msongo wa mawazo uliyopitiliza, sonona ilinikumba nisijue wa kusema naye , njia rahisi ilikuwa kuondoka ."anasema Petra

Petra Bockle (aliyezaliwa 14 Mei 1995) Kaunti ya Mombasa ni rapa, mtunzi wa nyimbo na mwimbaji mwenye asili ya Kenya na Ushelisheli.

Chanzo cha picha, Petra Bockle

Maelezo ya picha, Petra Bockle (aliyezaliwa 14 Mei 1995) Kaunti ya Mombasa ni rapa, mtunzi wa nyimbo na mwimbaji mwenye asili ya Kenya na Ushelisheli.

Kabla ya ndoa yake kupatwa na majaribio anakiri kwamba alishika mimba za kwanza tatu na kujifungua watoto ambao walikufa muda mchache tu baada ya kujifungua , isipokuwa mwanawe wa nne aliyesalia hai.

Je Petra Bockle ni nani haswa?

Petra Bockle (aliyezaliwa 14 Mei 1995) Kaunti ya Mombasa ni rapa, mtunzi wa nyimbo na mwimbaji mwenye asili ya Kenya na Ushelisheli.

Petra Bockle alizaliwa na mama Mkenya na baba kutoka Ushelisheli.

Baba yake alikufa mwaka wa 2004, wakati Petra alipokuwa na umri wa miaka tisa, Alianza kujishughulisha na muziki wakati huu kama aina ya kuondoa sonona ya kumpoteza baba yake mzazi.

Petra amefanya kazi na nyota wa kimataifa kama Bobby Valentino na Vybz Kartel , huku akitazamia kutanua talanta yake ya uimbaji wa kufoka au rap.

Kama msanii wa kike Petra ana maoni kwamba wasanii wa kike hawapaswi kuvaa mavazi yanayoonesha maumbile yao kama njia ya kukubalika.

Hisia zake zinatokana na harakati zake za muziki ambapo amejipata akishauriwa kuvaa nguo zenye kuonesha maumbile yake jambo ambalo hakubakiani nalo.