Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Covid: Ufaransa yazidisha vikwazo huku ongeko la Omicron likiripotiwa
Ufaransa imetangaza vikwazo vikali vya Covid huku kukiwa na wasiwasi juu ya kirusi cha Covid,Omicron.
Kuanzia Januari 3, kufanyia kazi nyumbani kutakuwa lazima kwa wale wanaoweza na mikusanyiko ya umma itakuwa na watu 2,000 kwa hafla za ndani.
Habari hizo zinakuja wakati Ufaransa ikirekodi zaidi ya maambukizo mapya 100,000 siku ya Jumamosi - idadi kubwa zaidi iliyoripotiwa nchini tangu janga hilo kuanza.
Lakini waziri mkuu aliacha kutekeleza amri ya kutotoka nje wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya.
Jean Castex aliwaambia waandishi wa habari janga hilo lilihisi "kama filamu isiyo na mwisho" alipokuwa akitangaza hatua mpya katika mkutano wa waandishi wa habari kufuatia mkutano wa baraza la mawaziri .
Waziri wa afya Olivier Véran alisema maambukizo ya coronavirus yalikuwa yanaongezeka mara mbili kila siku mbili, akionya juu ya "wimbi kubwa" la visa vipya.
Sheria mpya pia ni pamoja na mipaka ya mikusanyiko ya nje ya umma - ambayo itazuiliwa kwa watu 5,000 - na marufuku ya kula na kunywa kwenye safari za mwendo mrefu.
Vilabu vya usiku vitasalia kufungwa na mikahawa na baa zitaweza kutoa huduma ya mezani pekee. Wafanyikazi wanaofanya kazi nyumbani watalazimika kufanya hivyo angalau siku tatu kwa wiki. Uvaaji wa barakoa utakuwa wa lazima katikati mwa jiji.
Serikali pia inafupisha urefu wa muda kati ya chanjo ya nyongeza kutoka miezi minne baada ya chanjo ya mwisho hadi miezi mitatu.
Pasi ya chanjo iliyopangwa ya Ufaransa - ambayo itahitaji uthibitisho wa chanjo, sio tu kipimo hasi, ili kuingia kwenye maeneo ya umma - itaanza kutekelezwa kuanzia Januari 15, ikiwa bunge litaidhinisha mswada wa sheria itakayofanikisha utekelezaji wake .
Lakini Bw Castex hakutangaza zuio kamili au amri ya kutotoka nje wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya. Shule pia zitafunguliwa kama ilivyopangwa tarehe 3 Januari.
Kulingana na dashibodi ya nchi hiyo ya coronavirus, Ufaransa kwa sasa ina wastani wa zaidi ya maambukizo mapya 70,000 kila siku.
Siku ya Jumatatu, zaidi ya watu 1,600 walilazwa hospitalini na kuleta jumla ya watu hospitalini kwa sababu ya Covid-19 hadi 17,000, kulingana na data kutoka kwa mamlaka ya afya ya umma ya Ufaransa.
Mahali pengine barani Ulaya, vizuizi zaidi vilitangazwa nchini Ujerumani na Ugiriki huku serikali zikitafuta kukomesha wimbi la kesi chanya.
Mikusanyiko nchini Ujerumani itawekewa kikomo kwa ukubwa kuanzia tarehe 27 Desemba na kumbi za mazoezi, mabwawa ya kuogelea, vilabu vya usiku na sinema zitafungwa kwa umma katika majimbo kadhaa. Mikusanyiko ya kibinafsi ya watu waliochanjwa pia itapunguzwa hadi 10.
Kuanzia tarehe 3 Januari, serikali ya Ugiriki itahitaji baa na mikahawa kufungwa kufikia saa sita usiku na meza zitakuwa na wateja sita pekee. Maeneo ya kumbi hayataruhusiwa kuhudumia wateja waliosimama, na ikiwa hawatatii, muziki utapigwa marufuku katika vituo hivyo, shirika la habari la Reuters liliripoti.
Kinyume chake, nchini Uingereza, Katibu wa Afya Sajid Javid amesema hakuna vizuizi vingine vya Covid vitatekelezwa nchini Uingereza kabla ya mwaka mpya. Lakini alisema watu wanapaswa "kubaki waangalifu" na kusherehekea nje wakati wa Mkesha wa Mwaka Mpya ikiwezekana.
Uingereza na Scotland ziliripoti visa vingi wakati wa Krismasi.