Tel Aviv umetajwa kuwa mji ghali zaidi kwa mtu yeyote kuishi

Iliyochapishwa

Mji huo wa Israel ulichukua nafasi ya kwanza kote duniani katika utafiti uliofanywa na Economist Intelligence Unit EIU.

Mji huo wa Israel ulipanda kutoka nafasi ya tano mwaka uliopita na kuusukuma mji wa Paris katika nafasi ya pili sawa na ule wa Singapore.

Mji wa Damascus, katika taifa lililozongwa na vita la Syria ndio mji wenye gharama ya chini duniani .

Utafiti huo unalinganisha bei za bidhaa na huduma kwa dola ya Marekani katika mataifa 173.

EIU imesema kwamba data iliokusanywa mwezi Agosti na Septemba ilionesha kwamba bei za wastani ziliongezeka kwa asilimia 3.5 kulingana na sarafu za mataifa hayo - ikiwa ndio mfumuko wa hivi karibuni uliorekodiwa katika kipindi cha miaka mitano.

Sekta ya uchukuzi imeshuhudia kupanda kwa bei , huku bei ya lita moja ya mafuta ya petroli ikipanda kwa sailimia 21 kwa wastani katika utafiti huo wa miji.

Gharama ya Maisha Duniani ya EIU ilionyesha hasa kupanda kwa thamani ya sarafu ya Israel, shekeli, dhidi ya dola. Bei za ndani za karibu 10% ya bidhaa pia ziliongezeka sana, haswa mboga.

Utafiti huo uligundua kwamba mji wa Tel Aviv ulikuwa mji wa pili wenye gharama za juu kwabidhaa kama vile pombe na usafiri, wa tano kwa vitu vya utunzaji wa kibinafsi, na wa sita kwa burudani.

Meya wa Tel Aviv, Ron Huldai, alionya katika mahojiano na gazeti la Haaretz kwamba kupanda kwa bei ya bidhaa - ambazo hazijajumuishwa katika hesabu za EIU - kunamaanisha kuwa jiji hilo lilikuwa linakaribia "mlipuko" wa gharama.

"Tel Aviv itazidi kuwa ghali zaidi, kama vile nchi nzima inavyozidi kuwa ghali," alisema.

"Tatizo la msingi ni kwamba Israel hakuna mji mkuu mbadala. Marekani kuna New York, Chicago, Miami na kadhalika. Uingereza kuna Greater London, Manchester na Liverpool. Huko unaweza kuhamia mji mwingine. ikiwa gharama ya maisha ni ngumu sana."

Mwaka jana, Paris, Zurich na Hong Kong zilishiriki nafasi ya kwanza katika utafiti wa EIU. Zurich na Hong Kong walikuwa wa nne na wa tano mwaka huu, wakifuatiwa na New York, Geneva, Copenhagen, Los Angeles na Osaka.

Tehran ilipanda zaidi katika viwango hivyo, ikiruka kutoka nafasi ya 79 hadi ya 29, huku vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vikiendelea kusababisha uhaba wa bidhaa na kupanda kwa bei ya bidhaa kutoka nje ya Iran.

EIU ilisema viwango vinaendelea kuwa nyeti kwa mabadiliko yanayosababishwa na janga la corona.

"Ijapokuwa uchumi mwingi sasa unaimarika huku chanjo za Covid-19 zikitolewa, miji mikuu ya ulimwengu bado inakabiliwa na ongezeko la mara kwa mara la kesi, na kusababisha vikwazo vipya vya kijamii. Katika miji mingi hii imetatiza usambazaji wa bidhaa, na kusababisha uhaba wa bidhaa na bei ya juu. "

Iliongezea: "Kubadilika kwa mahitaji ya watumiaji pia kumeathiri tabia ya ununuzi, wakati imani ya wawekezaji imeathiri sarafu, na hivyo kuchochea kupanda kwa bei."

EIU ilisema inatarajia kupanda kwa bei hadi wastani mwaka ujao huku benki kuu zikiongeza viwango vya riba kwa uangalifu ili kupunguza mfumuko wa bei.

Miji mitano ghali zaidi duniani

•1 Tel Aviv

•2= Paris

•2= Singapore

•4 Zurich

•5 Hong Kong

Miji mitano yenye gharama za chini duniani

•169 Almaty

•170 Tunis

•171 Tashkent

•172 Tripoli

•173 Damascus

Chanzo: EIU's World Cost of Living indexMji mkuu wa Tel Aviv umetajwa kuwa mji ghali zaidi kwa mtu kuishi duniani , huku kupanda kwa mfumuko na matatizo ya ugavi yakisababisha kupanda kwa bei za bidhaa duniani.