Waridi wa BBC : Nilipofika Gerezani , lilikuwa sio jambo rahisi kumtazama baba ana kwa ana

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Kusikiliza simulizi ya maisha ya Damaris ni sawa kufuatilia simulizi ya filamu au tamthilia
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Damaris Kimani anapoyasimulia maisha yake, unaweza kufikiria kana kwamba unafuatilia sinema ya maisha , lakini ni hali halisi aliyoishi katika maisha ya miaka 21 ya uhai wake.

Ni binti wa kike ambaye amepitia misukosuko mingi ya maisha kuanzia alipoanza kujielewa yeye ni nani .

"Maisha yangu tangu utotoni yamejawa na pandashuka nyingi .Kwani wakati ninakua kati ya wazazi wangu baba na mama walikuwa na changamoto za kiuhusiano na hali hii ilikuwa inaniathiri kama binti wao .Naamanisha kuwa hali ya maisha yetu duni na mahangaiko mengi yalinitaabisha sana , nisijue wa kumgeukia " anasema Damaris.

Simulizi ya Damaris inatupeleka hadi utotoni mwake ambapo anasema kwamba matukio mengi ya maisha yake , ndio ambayo yameathiri pakubwa mtazamo wake wa maisha yake akiwa sasa ni mtu mzima.

Maisha ya utotoni

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Bi Damaris (kushoto) akiwa na umri mdogo na (kulia) muonekano wake kwa sasa

Damaris alizaliwa Kaunti ya Nairobi akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne. Japo anasema kwamba maisha yake ya mwanzo alilelewa na wazazi wake wawili , maisha ya familia yao wakati huo yalijawa na karaha.

"Tatizo kuu katika familia yangu lilianza pale baba mzazi alipoanza kunywa pombe na akawa mlevi wa kupindukia , maisha yetu yalichukua mkondo tofauti kwani ilibidi mama ahangaike usiku na mchana kuhakikisha kama watoto tumekula , tumesoma na kadhalika", anakumbuka Damaris.

Mwanadada huyu anasema kwamba ulevi wa babake uliathiri sana mahusiano katika familia yao hasa kwa kuwa mama yake alikuwa akipigwa mara kwa mara na baba yao.

"Nakumbuka siku mmoja baba alirejea nyumbani usiku wa manane akiwa amelewa chakari , tulikuwa hatuzioni funguo za lango kuu la nyumba na kwa hiyo ilichukua muda kabla hatujamfungulia mlango. Alipoingia alikuwa na ghadhabu kubwa … bidhaa ambazo mama alikuwa anauza katika biashara yake kama mahindi na maharagwe, vyote alimwaga chini ", anakumbuka Damaris.

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Damaris

Ulikuwa usiku wa kiza ambao mwanadada huyu anasema kwamba hawezi kuusahau.

Baada ya siku hiyo biashara aliyokuwa akiifanya mama yake Damaris ilianza kufifia na hivyo changamoto kubwa ya familia hii ikawa ni kukosa mahitaji ya kimsingi ya maisha ya kawaida ya kila siku.

Upande mwingine naye baba alishindwa kukidhi mahitaji ya jamii yake , kwa kuwa pia alifutwa kazi kama dereva wa gari la usafiri wa umma alilokuwa anaendesha.

Mwanadada huyu anasema kwamba tangu wakati huo dhiki nyingi zilianza kuiandama familia na wasiwasi mkuu ulikuwa kwamba hawakuwa wamelipa kodi ya nyumba kwa miezi miwili.

Maisha ya kijijini

Misukosuko yao iliendelea na hali ikageuka kuwa mbaya zaidi pale walipofukuzwa nje ya nyumba walimokuwa wakiishi kama wapangaji kwa kushindwa kulipa kodi ya mwenye nyumba.

"Ilikuwa ni siku ambayo sijawahi kuisahau, nakumbuka tu watu wakiingia nyumbani kwetu kwa fujo na kutupa vitu vyetu vyote nje . Wakati huo ni mama yetu aliyekuwa nyumbani alitizama tu asijue la kufanya …kwa siku mbili tulilala nje kwasababu hatukuwa na suluhu la ni wapi tutaelekea ." Anasema Bi Damaris.

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Baada ya kushindwa kuishi mjini Damaris na familia yake walilazimika kurudi kijijini

Damaris anasema kwamba juhudi zao za kumpigia baba yao simu hazikufua dafu na waliishia kuamua kurudi kijijini, nyumbani kwao mama Damaris.

Kwa miaka miwili walianza maisha ya kijijini na Damaris alianza masomo yake upya huko. Anasema wakati huo baba yao hakuwahi kuwatafuta kujua wako wapi wala kuzungumza nao.

Hatahivyo baada ya kipindi kirefu hatimaye baba yake Damaris alifika kijijini kwa mama Damaris na kuomba msamaha kwa wakwe zake , na kulingana na Damaris mama aliridhia na wakarudi tena na baba mjini Nairobi.

Wakati wamerejea Nairobi maisha yalikuwa bado ni magumu kwani baba yao hakuwa amepata ajira na mahangaiko yao yaliendelea, ila wakati huu yalikuwa ya muda tu.

Kulingana na Damaris mambo yalianza kubadilika pale nyumbani kwani baba alionekana kuwa na pesa na kubadilisha hadhi na maisha ya familia yao .

"Tulianza kufurahi kwa kuwa baba alianza kununua vitu ambavyo hatukuwa tumezoea nyumbani, kwa mfano sisi hatukuzoea maisha ya kuwa na Runinga , na bidhaa mbali mbali za nyumba ambazo husisimuwa watoto wadogo. Basi maisha yetu yalibadilika na kukawa hakuna tena dhiki "Damaris anakumbuka.

Maisha ya ujambazi

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Damaris

Kulingana na Bi Damaris tetesi na masengenyo ya hapa na pale kuhusu alichokuwa anafanya baba yake mzazi zilianza kuenea kila mahali, na haikuchukua muda kwa Damaris na hata mama yake kufahamishwa kwamba baba yao alikuwa ameingia kwenye genge la majambazi sugu ambao walikuwa wanapora watu magari yao.

"Wakati mama anasikia zile tetesi hakuamini na alikuwa anapuuza tu na kusema ni kawaida ya watu kuzungumza asijue ukweli. Lakini ilifikia wakati Damaris pamoja na mama yao waliamini kwamba kilichokuwa kinasemwa ni ukweli, ila walisema kama tunakula ama tunakunywa basi tutatulia tu " anasema Damaris.

Mwanadada huyu anasema kwamba haikuchukua muda pia kwa baba yao kumpeleka mama faraghani na kumfungulia moyo na kukiri kwamba alikuwa ni jambazi.

Ni jambo ambalo familia yake Damaris iliishi nalo kama siri kubwa. Damaris anasema kwamba baba yao alikuwa amewatahadharisha kwamba huenda siku mmoja akatoka nyumbani na asirudi tena kutokana na hatari ya kazi yake .

Mwanadada huyu anasema kwamba sio maisha ambayo aliyachagua kuyaishi ila ndio hali halisi aliyojipata ndani yake asijue la kufanya.

Maisha baada ya kuoa mke wa pili

Maisha yao yalichukua mkondo tofauti wakati baba yao alimuoa mke wa pili , na ikawa kwamba mawazo yake yalitoweka kwenye familia yake ya kwanza na kuyaelekeza maisha yake yote kwa mke wa pili. Damaris anasema kwamba hapo ndipo walitelekezwa na baba yao na ikawa sasa ni mama yao ambaye alikuwa anahangaika kupata mahitaji ya maisha yao ya kila siku.

"Baada ya baba kutoweka ghafla , mara hii akimuoa mke wa pili , ilibidi na sisi tuhame sehemu tuliyokuwa tunaishi kutokana na malimbikizo ya kodi ya nyumba. Mama hangeweza kulipa kodi ya nyumba ile , kwahiyo tulihamia katika mtaa wa makazi duni ya mabanda ", anasema Damaris.

Maisha yaliendelea kuwa magumu sana siku hadi siku, na kwa kuwa ndio wakati alikuwa anahitimu masomo yake ya shule ya msingi, alianza kuingia kwenye makundi ya marafiki ambao walikuwa na mienendo isiyofaa. Kwa mfano anakiri kwamba alianza tabia ya uvutaji wa bangi,unywaji wa pombe wa kupindukia na kukosa maadili kabisa kama akiwa na umri wa miaka 14.

Damaris analaumu hali hii ya misukosuko mingi ya kifamilia kwa kuharibu maisha yake kuanzia utotoni.

"Nilikuwa ninahisi kana kwamba hakuna mtu alikuwa ananijali , nikageukia kuwa mlaji miraa(milungi) wa kipindukia na nikawa mtoto wa kike wa kuingia vilabu hadi chee , mimi hakuna kitu sijawahi kufanya katika dunia hii nikiwa na umri huo. Nilikuwa hata sichani nywele, unawajua wale wanawake wagheto eh nilikuwa hivyo, "anakumbuka Bi Damaris.

Mwanadada huyu anasema kwamba anapoangalia nyuma haamini kwamba ni yeye kwani hata kule mitaani watu walikuwa wameanza kuzungumza kuhusu maisha yake yaliokuwa hayana nidhamu kabisa.

Kumsaidia mama kutafuta ziziki

Damaris anasema kwamba watu hawakuwa wanaelewa kilichokuwa kinafanyika alikuwa na msongo wa mawazo na misukosuko ya ndani ya familia yao iliyokuwa inamuathiri.

Baada ya kuishi maisha ya dhiki Damaris alimua kumsaidia mama yake kutafuta riziki kwa ajili ya kupata mahitaji ya kila siku muhimu ya maisha

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Baada ya kuishi maisha ya dhiki Damaris alimua kumsaidia mama yake kutafuta riziki kwa ajili ya kupata mahitaji ya kila siku muhimu ya maisha

Baada ya kuishi maisha ya shida kwa muda mrefu Bi Damaris aliamua kumsaidia mama yake katika kutafuta riziki kwa ajiliya familia yao kwa hiyo alikuwa anafanya biashara za rejareja za ili kuweza walau kupata mahitaji ya muhimu ya kila siku ya kifamilia.

Wakati akiwa katika pilikapilika za kutafuta riziki, siku moja Damaris alikumbana na baba yake mzazi wakati mmoja alipozuru sehemu waliyokuwa wanaishi. Ila Damaris anasema kwamba mkutano wake na baba yake haukuwa wa furaha bali ulimuwacha na machungu mengi sana .

"Sikufahamu ni kipi kilichomfanya baba kututembelea, ila ziara yake ilikuwa ya kutuacha na huzuni tele. Nakumbuka baba akinionyesha mabunda ya pesa huku akisema kwamba yuko radhi fedha yake ipotee kuliko kunisaidia mimi au mama yangu. Sijawahi kusahau matamshi aliyonieleza wakati huo kwamba ninaweza kuamua kuwa kijakazi wa nyumba au kahaba kujitafutia karo ya shule .", Damaris anasema.

Baada ya kisa hicho Damaris anasema kwamba ilichukua muda kuwasiliana na baba yake mzazi tena hadi pale ilipotokea kwamba baba yake alikamatwa miongoni mwa genge la wezi ambalo lilihusika na wizi wa kimabavu. Mwanadada huyu anasema kwamba mama yao alijulishwa kwamba baba yao alikuwa amewekwa kwenye orodha ya majambazi sugu ambao walikuwa wanasakwa na idara za usalama nchini Kenya .

"Ni kitu cha kusikitisha ila alikuwa ni baba yangu ambaye alikuwa anasakwa usiku na mchana na vyombo vya usalama, iliwadia wakati ambao kati ya genge ambalo baba yangu alikuwa anashirikiana nalo, ni yeye tu alisalia akiwa hai. Wote walikuwa wamepigwa risasi na kuuawa katika akabiliano na polisi hasa wakati mipango yao ya uhalifu ilipotibuliwa."anakumbuka Damaris.

Kukamatwa na kuhukumiwa

Hatimaye baba yake Damaris alishindwa kuepuka mkono wa sheria na alishtakiwa kwa uhalifu wa mauaji na wizi wa mabavu.

Kulingana na Damaris kesi kuhusu mauaji ilitupwa nje kwa ukosefu wa ushahidi, ila baba yake alipatikana na hatia ya wizi wa mabavu na kuhukumiwa kunyongwa. Kwa kuwa sheria ya kunyongwa nchini Kenya imesimamishwa, badala yake alihukumiwa kifungo cha maisha.

Hadi leo baba yake Damaris angali anatumikia kifungo cha maisha katika Gereza la kuu la Kamiti.

"Nilikuwa na uchungu mwingi kutokana na matukio mbali mbali ndani ya familia yangu , hasa kwa kuwa baba yangu alifungwa maisha. Ilikuwa ni hali ngumu kuikubali kwamba huenda sitakuwa na nafasi ya kumuona baba yangu katika mazingira ya nyumbani tena.", Damaris anasema.

Kukutana na baba yake Gerezani.

Bada ya kufikiria sana, Damaris aliona ni muhimu amtembelee baba yake Gereza kuu la Kamiti ili kutafuta msamaha na pia kuzungumzia mengi yaliokuwa yanamkera hasa miaka mingi ya kukulia katika mazingira ya baba aliyekuwa mhalifu.

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Damaris alipomtembelea baba yake katika gereza kuu la Kamiti nchini Kenya

Hatimaye Damaris alipata alipiga moyo konde na kupata ujasiri wa kumtembelea baba yake gerezani, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi , ni hatua anayosema ilimfanya ajihisi mwenye uoga mwingi wa pengine watakuwa na mazungumzo ya aina ipi na pengine watasikilizana na kuombana msamaha au la? ndio mambo aliyokuwa anayafikiria Damaris akiwa njiani kwelekea Kamiti.

"Nilipofika Gerezani , lilikuwa sio jambo rahisi kumtazama baba ana kwa ana kuzungumza , mazingira ya jela unapomtembelea mtu huwa kuna kioo na kuta ambazo huziba mgeni kwa mfungwa - nilipomtazama baba niliangua kilio cha uchungu nisiweze kujizuia ."anakumbuka Damaris

Ilikuwa ni siku ambayo Damaris hatasau maishani mwake , kwani anasema kwamba baba na mwana walipata wasaa wa kuzungimzia machungu na kero zilizogubika uhusiano wao. Damaris anasema kwamba kilele cha ziara yake kumuona baba gerezani kilikuwa ni kusameheana…kila mmoja alimsamehe.

"Nilihisi mzigo mzito umeondolewa juu ya mabega yangu , nilikuwa nimeishi na machungu mengi na ghadhabu kubwa dhidi ya baba , hasa jinsi alivyotutelekeza kama watoto wake. Lakini nilifurahi kwamba tulikuwa na wasaa wakujadiliana na kuelezana ukweli kuhusu matukio hayo . ", Damaris anasema.

Damaris

Chanzo cha picha, Damaris

Maelezo ya picha, Damaris kwa sasa anajishugulisha na utoaji ushauri nasaha kwa watoto ambao hujipata katika maisha ya kutoishi na wazazi

Bi Damaris anasema kwamba kwa miaka mingi alikuwa anawaona watoto wakitangamana na baba zao na kushangaa ni vipi kwao mambo ni tofauti.

Japo baba yake angali anatumikia kifungo Damaris anasema kwamba yeye na ndugu zake wamepata nafasi ya kutangamana na baba na kuwa na mlezi ambayo anafuatilia maisha yao.

Kutokana na hayo Damaris amejitolea sana katika kutoa ushauri nasaha kwa watoto ambao hujipata bila uwepo wa wazazi kufuatia matukio mbali mbali ya maisha.

Vile vile Damaris huzungumza na wazazi hasa haja ya wazazi kuwa na maneno ya kujenga wakati wako kwenye mchakato wa kulea watoto wao. Anasema anaamini kwamba matamshi ya mlezi au mzazi yawe chanya au mabaya huenda yakawa na athari kubwa katika maisha ya watoto baadaye wanapokuwa watu wazima.