Je ni kwa nini mzaha wa ndizi umeifanya Uturuki kuwafurusha raia wa Syria nchini humo?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Wakicheka na kufanya mzaha mbele ya kamera, raia wa Syria wamekuwa wakishiriki katika vichekesho kwenye mitandao ya kijamii nchini Uturuki.

Kwenye picha hizo za mtandao wa TikTok, wamekuwa wakila ndizi na kuwachochea marafiki zao nao kufanya hivyo.

Video hizo hazionekani zenye madhara kwa viwango vya mtandao wa TikTok. Lakini zimekuwa zenye madhara ya muda mrefu kwa baadhi ya raia wa Syria.

Siku za hivi karibuni, mamlaka nchini Uturuki imewalaumu raia hao wa Syria kwa kuchochea chuki kwa kula ndizi kwa namna ya uchochezi.

Raia kadhaa wa Syria wamekamatwa na huenda wakafukuzwa nchini humo.

Katika mazingira ya kuongezeka uadui dhidi ya jamii kubwa ya Wasyria nchini Uturuki, ndizi zimekuwa ishara ya mgawanyiko

Lakini kuna hadithi ipi kuhusiana na video hizi za ndizi ?

'Siwezi kuzimudu'

Video hiyo ya ndizi ilianza baada ya video nyingine ya mjadala mkali kati ya raia wa Syria na Uturuki kuhusu hali ngumu ya kiuchumi nchini Uturuki. Uchumi wa Uturuki ulikuwa umeathiriwa vibaya kutokana na mfumuko wa bei ambao ulikuwa umezusha viwango vya maisha.

Kwenye video hiyo, maoni tofauti yalitolewa na mwanamke raia wa Syria, aliyezungumza kwa ufasaha lugha ya kituruki, akatetea maadili ya kazi ya wakimbizi. Kujibu hilo raia wa uturuki wakadai kuwa watu kutoka Syria na Afghanistan walikuwa wanawanyanganya ajira zao.

Maoni kama hayo huibuka mara kwa mara nchini Uturuki , nchi inayowahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, wakiwemo milioni 3.6 kutoka Syria. Maoni ya kupinga uhamiaji yamekuwa yakiongezeka huku baadhi ya wanasiasa nchini uturuki wakitaka kuwekwa vikwazo vikali.

Lakini kilichosababisha video hii kupata umaarufu ni wakati mwanamume mmoja raia wa Syria aliposema: "Nimeona raia wa Syria sokoni wakinunua kilo kadhaa za ndizi, mimi mwenyewe siwezi kumudu."

Madai haya yalizua mjadala miongozi mwa jamii ya Wasyria nchini Uturuki na kwa haraka ikageuka kuwa video fupi kwenye mtandao wa TikTok. Wakimfanyia mzaha mwanamume huyu Mturuki, raia wa Syria walijirekodi wakila ndizi, wakizifanyia video hizo mabadiliko na kuzisambaza.

Iwapo mzaha huo kuhusu ndizi ulikuwa ni wa kuchekesha mitandaoni , haukumfurahisha kila mtu.

Picha moja ambapo ndizi ilitumika kama bendera ya uturuki ilizua ghadhabu. Chama kipya cha kisiasa cha nationalist Victory Party kikatoa taarifa na kulalamikia watumia TikTok kutoka Syria kwa kuwatusi watu wa Uturuki na bendera yao.

Wakosoaji wengine kwenye mitandao ya kijamii walikejeli hali ngumu ya kiuchumi iliyokuwa inawakumba watu nchini Uturuki.

Alhamisi iliyopita shirika moja la habari lilisema kuwa polisi nchini Uturuki walikuwa wamewakamata raia 11 wa Syria waliochapisha video za ndizi, "wakiwalaumu kwa kuchochea chuki."

Mamlaka za uhamiaji nchini Uturuki zinasema zitawafukuza baada mipangilio inayohitajika kukamilika.

"Jitihada zinafanyika kutafutia video zote zilizochapishwa na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki katika kampeni hiyo," ailsema mkurugenzi mkuu wa idara ya uhamiaji nchini Uturuki.

Kisha Jumapili, mamlaka za Uturuki zikamkamata mwandishi wa habari raia wa Syria Majed Shamaa, ambaye alifanya ripoti ya televisheni kuhusu video hizo za ndizi mjini Istanbul.

'Hatuwafanyii mzaha waturuki'

Baadhi ya wanasiasa nchini Uturuki walionekana kuunga mkono kamata kamata hizo.

Lakini chama kinachoegemea upande wa watu wachache kinasema hatua hizo ni za kibaguzi.

Mwandishi wa habari raia wa Syria Deema Shullar, anayeishi mjini Istanabul aliiambia BBC kuwa video nyingi hazikuwa na madhara na zilikuwa ni za kuchekesha tu.

Lakini alisema baadhi yazo huenda zilichukuliwa kuwa zenye madhara na za kukera. Nchini Uturuki kuna sheria kali zinazoharamisha matusi kwa taifa, bendera na Rais.

Watengenezaji wa video hizi wanastahili kushtakiwa chini ya sheria hizo, alisema Bi Shullar.

Alisema raia wengi wa Syria wana hofu kuwa huenda watarudishwa nchini mwao nchi ambayo imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muongo mmoja.

Aliitaja hatua ya kuwafukuza raia wa Syria kama vitisho kutoka serikali ya Uturuki.

Video za ndizi zimeondoa macho kutoka kwa tatizo la wakimbizi na changamoto za kiuchumi nchini Uturuki na badala yake kila mtu anaangazia video za TikTok, alisema Shullar.