Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Waziri Mkuu Abiy ana tatizo na msaada wa ngano?
- Author, Na Peter Mwai
- Nafasi, BBC Reality Check
- Iliyochapishwa
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amedai kuwa matatizo mengi ya nchi hiyo ikiwemo kuingia kwa magonjwa kutoka nje ya nchi yanatokana na msaada wa ngano kutoka nje.
"Tatizo la Ethiopia ni msaada wa ngano. Msaada wa ngano huja na magonjwa," alisema Bw Abiy. "Tukiisimamisha, matatizo mengi yatatatuliwa."
Je, Bw Abiy yuko sawa kuhusisha uagizaji wa ngano na magonjwa na changamoto nyingine zinazoikabili Ethiopia?
Utegemezi wa Ethiopia kwenye ngano
Ngano haijawahi kuwa zao kuu nchini Ethiopia, lakini imekuwa ikikua kwa umaarufu katika miaka ya hivi karibuni, haswa katika maeneo ya mijini.
Sasa ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa ngano Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini uzalishaji umekuwa ukipungua mara kwa mara.
Nchi hiyo pia imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa chakula na ukame, huku mamilioni ya watu wakihitaji msaada wa chakula.
Ili kukabiliana na upungufu huo, Ethiopia kwa sasa inaagiza takribani robo moja ya ngano yake, na takribani robo ya hiyo inafika kama msaada wa chakula, sehemu kubwa yake kutoka Marekani.
Kuagiza ngano kutoka nje kunaweza kusababisha maradhi?
Bw Abiy alikuwa akizungumza na wakulima katika eneo la Oromia alipozungumzia magonjwa yanayosababishwa na ngano kutoka nje.
Moja ya magonjwa yanayosumbua wakulima nchini Ethiopia ni kutu ya ngano, inayosababishwa na fangasi wanaobebwa na upepo.
Mlipuko wa mwaka 2010 uliathiri 30% ya maeneo yaliyolimwa na kupunguza uzalishaji kwa zaidi ya 15%.
Njia bora zaidi ya kudhibiti kutu ya ngano ni kwa kuzalisha aina za ngano sugu, lakini aina mpya za fangasi huwa tishio linaloendelea.
Mnamo 2013, aina mpya ya kutu ya shina iliweza kushambulia aina ya ngano iliyostahimili hapo awali (inayojulikana kama digalu), na kusababisha hasara kubwa.
Utafiti uliochapishwa mwaka wa 2017 unaonesha aina hii ya fangasi labda ilitoka Yemen kabla ya kuvuka, kwa ndege, hadi Ethiopia. Hata hivyo, haiondoi kwamba huenda pia ilitoka katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati au Afrika Mashariki.
Kwa hakika kuna uwezekano kwamba magonjwa na wadudu wa mazao wanaweza kuingia nchini kupitia misaada au mazao yanayoagizwa kutoka nje, anasema Wuletaw Tadesse Degu, mtaalamu wa uzalishaji wa ngano katika Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Kilimo.
Hili linawezekana hasa katika nchi ambazo vifaa vya karantini ni dhaifu.
"Kumekuwa na madai kuwa magugu na wadudu waharibifu wengi waliopo kwa sasa waliingizwa nchini humo," anasema.
"Mito na maziwa yetu, mashamba na maeneo mbalimbali yanatishiwa na magugu ambayo hayakuwepo hapo awali nchini Ethiopia."
Wataalamu wameiambia BBC kwamba nafaka yoyote inayokuja nchini inahitaji kuchunguzwa kwa uangalifu ili kuhakikisha haina magonjwa.
Ulimwenguni kuna matukio ambapo ugonjwa umeenea kupitia uagizaji wa bidhaa kutoka nje. Mfano mmoja ni mlipuko wa ngano ambao husambazwa kwa mbegu, na hivi karibuni ulihamishwa kutoka Amerika Kusini hadi Bangladesh na Zambia kupitia biashara ya nafaka.
Kwa kutu ya ngano, hata hivyo, ambayo hupeperushwa na kubebwa na mbegu, sio mara zote kwamba aina mpya hutoka nje ya kanda.
Kuna ushahidi kwamba baadhi ya aina mpya za kutu zimeibuka ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kama vile vilivyotoka kwingineko.
Shirika la maendeleo la kimataifa la Marekani liliiambia BBC: "Msaada wa chakula wa Marekani uko chini ya udhibiti mkali wa ubora ili kufikia viwango vyote vya kimataifa." Iliongeza msaada huo unazingatia kanuni za usalama wa chakula na ubora wa ndani.
Serikali ya Ethiopia inasema nini?
Tuliuliza serikali ya Ethiopia kwa maelezo zaidi juu ya magonjwa ambayo Waziri Mkuu alikuwa akimaanisha. Msemaji wake, Billene Seyoum, alituambia Bw Abiy amekuwa akizungumza kwa ujumla zaidi kuhusu hitaji la kuachana na ngano na kuelekea kwenye mazao ya ndani yenye afya.
"Unene, kisukari, kwa mfano, vinahusishwa na ulaji mwingi wa wanga. Hivyo ujumbe wake kwa ujumla unajikita katika haja ya kupunguza utegemezi wa misaada kwa kuongeza tija ya kilimo," alisema.
Jibu hili, hata hivyo, halielezi ni kwa nini serikali ina tatizo na ngano inayoagizwa kutoka nje na sio zao linalozalishwa nchini.
Bi Billene pia alisema kuwa matokeo ya moja kwa moja ya kuacha kutegemea ngano kutoka nje itakuwa kuokoa fedha za kigeni.
Ethiopia inafadhili uagizaji wa ngano kutoka nje ya nchi, na kuwapa wasambazaji wakubwa ambao nao huuza unga kwa viwanda vya kuoka mikate kwa bei iliyodhibitiwa.
Kukomesha uagizaji wa bidhaa kutoka nje kunamaanisha kuwa serikali haitumii tena pesa kufadhili ununuzi huu wa ngano.
"Utegemezi wa misaada umewarudisha nyuma Waethiopia wengi, na kwa jambo hilo Waafrika, kutumia rasilimali ipasavyo," anasema Bi Seyoum.
"Pia fedha za kigeni zikitumika kuagiza ngano kutoka nje zitaanza kuingia katika sekta nyingine za uzalishaji."
Ethiopia inaweza kuzalisha ngano zaidi?
Ngano nyingi nchini Ethiopia hulimwa na wakulima wadogo.
Kwa kuongezeka kwa mitambo, mavuno yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kulingana na data za serikali.
Hata hivyo, tija inabakia kuwa ndogo na pato bado ni pungufu ya mahitaji.
Kijadi, Ethiopia imekuwa ikilima ngano katika nyanda za juu na kutegemea mvua.
Sasa inaongeza kwa kukuza ngano katika nyanda za chini, ambazo mara nyingi huwa kavu, kwa njia ya umwagiliaji.
Ethiopia inashinikiza kuacha kabisa kuagiza ngano kutoka nje ifikapo 2023.
"Ni lengo la kweli na linaloweza kufikiwa, kwa kuwa tuna ardhi ya hekta 500,000 ya kumwagilia ambayo haijalimwa kwa sasa," asema Bw Tadesse.