Pandora Papers: Wamiliki wa siri wa mali ya thamani ya mabilioni ya pesa nchini Uingereza

London property traced to offshore firms
    • Author, Na Timu inayoripoti kuhusu Nyaraka za Pandora
    • Nafasi, BBC Panorama
  • Iliyochapishwa

Wamiliki wa siri wa zaidi ya mali 1,500 za Uingereza zilizonunuliwa kwa kutumia kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa kulipa kodi wamefichuliwa na uchunguzi wa BBC.

Maelezo hayo yameonyeshwa katika nyaraka maalum za kifedha kwa jina Pandora Papers zenye orodha ya mali na thamani inayokadiriwa kuwa zaidi ya Pauni 4bn.

Wamiliki hao ni pamoja na wanasiasa mashuhuri wa kigeni, watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi na wafadhili wa kisiasa wa Uingereza.

Mawaziri wanasema wataleta sheria mpya watakapokuwa na muda bungeni.

Serikali za Conservative moja baada ya nyingine zimekuwa zikiahidi kuanzisha sheria ya kulazimisha kutajwa kwa wanaomiliki mali kupitia kampuni za kigeni kwa lengo la kumaliza utakatishaji fedha .

Miongoni mwa ufichuzi uliotolewa ni:

• Mke wa bwenyenye Sir Philip Green alianza kununua mali ya London wakati milki ya wenzi hao iliouzwa hivi karibuni ilipokaribia kuporomoka.

• Familia tawala ya Qatar ilinunua nyumba mbili ghali zaidi London kupitia kampuni za kigeni ili kuokokoa mamilioni ya pauni kama ushuru

• Bilionea wa Kiukreni Gennadiy Bogolyubov, ambaye anachunguzwa na FBI na alikuwa na mamia ya mamilioni ya mali zilizobanwa katika kesi ya udanganyifu, anamiliki mali ya zaidi ya pauni milioni 400 Uingereza

•Jengo la ofisi London lenye thamani ya pauni milioni 40 linamilikiwa na mtoto wa bwenyenye wa Urusi aliyewekewa vikwazo Mikhail Gutseriev

BBC ilifanya kazi na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ), the Guardian, Finance Uncovered na vyombo vingine vya habari kutambua katika faili zilizovuja watu wanaomiliki kampuni za nje ambazo zilikuwa na mali nchini Uingereza na Wales.

Kumiliki mali isiyohamishika kupitia kampuni kama hizo ni halali, na hakuna maoni ya makosa kwa kutumia tu kampuni ya kigeni kununua mali.

Walakini, serikali ya Uingereza hivi karibuni ilileta tathmini yake juu ya hatari ya utapeli wa pesa kutoka "kadri" hadi "juu".

Kiwango kikubwa cha hatari ni pale ambapo kuna "ugumu katika kuamua wamiliki wa faida ", kulingana na ripoti ya Ofisi ya masuala ya ndani mnamo Desemba 2020.

Inakuja wakati viongozi kadhaa wa ulimwengu - pamoja na Mfalme wa Jordan na familia inayotawala ya Azabajani - wametajwa katika uvujaji wa Pandora Papers baada ya kununua mali nchini Uingereza kwa kutumia kampuni za kigeni .

Familia ya Green

Sir Philip na Tina Green

Mke wa tajiri wa biashara ya bidhaa za rejareja Sir Philip Green alinunua mali ya mamilioni ya pauni London wakati BHS, msururu wa duka ambazo walikuwa wanamiliki, zikielekea kuanguka.

Utambulisho wake kama mnunuzi wa mali huko London ulifichwa kwa sababu walifanya ununuzi kupitia kampuni zisizojulikana zilizo katika Visiwa vya Virgin ,eneo lenye unafuu wa kulipa ushuru .

Ununuzi huo ulijumuisha nyumba ya pauni milioni 15 huko Mayfair na nyumba mpya ya binti yao karibu na Jumba la Buckingham, iliyonunuliwa kwa pauni milioni 10.6 mnamo 2016.

Msururu wa ununuzi huo ulifanyika zaidi ya miezi 12 baada ya Sir Philip kuuza BHS .

Biashara hiyo ilianguka na kusababisha kupotea kwa nafasi 11,000 za ajira na kuacha maeneo mengi ya biashara kuwa wazi katika vituo vya miji.

Kuanguka huko pia kulisababisha kilio ilipoibuka kuwa biashara ilikuwa imeacha pengo kubwa la hadi pauni milioni 571 katika mfuko wake wa pensheni.

Kupitia wanasheria wao, Sir Philip na Lady Green walikataa kujibu maswali ya kina, wakidokeza kuwa haya yalikuwa mambo ya kibinafsi.

Familia inayotawala Qatar

Uvujaji wa Pandora Papers pia unafichua mali ya familia inayomilikiwa na familia tawala ya Qatar kupitia mtandao mwingine wa makampuni.

Familia ya kifalme ya Al-Thani ilinunua majumba mawili kwenye moja ya maeneo ya bei ghali zaidi ulimwenguni, inayoangalia Hifadhi ya Regent huko London. Zilinunuliwa kupitia kampuni za kigeni ili kuokoa mamilioni ya pauni ambayo yangelipwa kama ushuru.

Uchambuzi wa BBC uligundua mali zingine nyingi zinazomilikiwa na wanafamilia kupitia miundo hii, inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya pauni milioni 650.

Serikali ya Qatar haikujibu maswali juu ya ilichopata BBC.

Gennadiy Bogolyubov

Gennadiy Bogolyubov ni bilionea wa Kiukreni ambaye anachunguzwa na FBI kwa utakatishaji wa pesa.

Yeye na mshirika wake wa kibiashara wanatuhumiwa kwa ulaghai wa benki waliyoanzisha wa zaidi ya Pauni 1bn.

Nyaraka za korti zilizojumuishwa kwenye Nyaraka za Pandora zinamfichua kuwa mmiliki mkuu wa mkusanyiko wa mali za Uingereza ambazo zinaweza kuwa na zaidi ya pauni milioni 400, pamoja na jengo la Trafalgar Square.

Zinashikiliwa kupitia mtandao wa kampuni, zingine za kigeni , ambazo zinaficha utambulisho wa wamiliki.

Bwana Bogolyubov ndiye mwanzilishi mwenza wa PrivatBank, mkopeshaji mkubwa wa Ukraine.

Benki hiyo ilitaifishwa mnamo 2016 baada ya wasimamizi kupata pengo la $ 5.5bn kwenye hesabu zake

PrivatBank imekuwa ikimfuata Bwana Bogolyubov na mshirika wake wa kibiashara Igor Kolomoisky kupitia hatua ya korti huko England na Marekani wakijaribu kurudisha zaidi ya $ 3bn zinazohusiana na pesa zilizopotea wakati wa uongozi wao.

Mnamo mwaka wa 2020 Idara ya Sheria ya Marekani ililenga kuchukua mali za kibiashara huko Texas, Ohio na Kentucky kutoka kwa wawili hao, ikishuku kuwa "zilipatikana kwa kutumia pesa zilizoporwa kutoka kwa Privatbank". Kesi za kortini zinaendelea.

Mali ya Bwana Bogolyubov kwa sasa iko chini ya zuio la kubanwa ulimwenguni

Mnamo 2016 aliamua kuondoka nchini na kukaa Uswizi, kwa "sababu za ushuru".

Mawakili wa Bw Bogolyubov walikataa kutoa maoni yao kwani hatua za kisheria zinaendelea.

Mikhail Gutseriev

Mikhail Gutseriev ni bwenyenye wa Urusi ambaye aliwekewa vikwazo na Uingereza mnamo Agosti kwa uhusiano wake wa karibu na Rais wa Belarusi Alexander Lukashenko. Nyaraka za Pandora zinafichua kuwa mtoto wake anamiliki kitita cha mamilioni ya pesa kupitia kampuni ya siri ya kigeni , iliyonunuliwa kwa zaidi ya pauni milioni 40.

Picture of commercial property in London

Bwana Gutseriev ndiye mwanzilishi wa Safmar Group, kampuni ya Urusi inayohusika na biashara ya mafuta, makaa ya mawe na mali za majengo .

Kufuatia kukandamizwa kwa haki za binadamu na demokrasia huko Belarusi mnamo 2020, Uingereza na EU hivi karibuni zimeleta vikwazo dhidi ya Rais Lukashenko, pamoja na Bwana Gutseriev na washirika wengine wao wa karibu.

Serikali ya Uingereza imeushutumu utawala wa Belarusi kwa kuendelea "kuponda demokrasia na kukiuka haki za binadamu".

Ilielezea Bwana Gutseriev kama "mfanyabiashara mashuhuri wa Urusi ambaye ni mmoja wa wawekezaji wakuu wa kibinafsi huko Belarusi na mshirika wa muda mrefu wa Alexander Lukashenko". Iliongeza kuwa "alikuwa ametoa msaada kwa serikali ya Belarusi, pamoja na matumizi ya biashara yake".

Bwana Gutseriev hahusiki tena katika Safmar, ambayo sasa inamilikiwa na mwanawe, Said, raia wa Uingereza.

Wawakilishi wa Said Gutseriev waliambia BBC kwamba hakuwa na "uhusiano wowote wa kibiashara na baba yake" .Harusi yake ya kifahari iligonga vichwa vya habari mnamo 2016 - ilihusisha maonyesho ya muziki ya wasanii Jennifer Lopez na Enrique Iglesias na iliripotiwa kugharimu $ 1bn.

Je Serikali ya Uingereza inafanya nini?

Mipango wa kuwa na orodha ya kampuni za kigeni zinazomiliki mali za Uingereza ilitangazwa kwa mara ya kwanza mnamo 2016 na Waziri Mkuu wa wakati huo David Cameron, ili "watu mafisadi na nchi hazitaweza tena kuhamisha , kutakatisha na kuficha pesa haramu kupitia soko la mali la London, na haitaweza kufaidika na fedha zetu za umma ".

Rasimu ya sheria ilichapishwa miaka miwili baadaye na "hatua " juu ya kubadilisha sheria iliahidiwa katika Hotuba ya Malkia ya 2019.

Mapema mwaka huu, kufuatia mkutano wa kilele wa G7, serikali ilirudia kujitolea kwake kuunda daftari la umma la mashirika ya nje ya nchi ambayo yanamiliki mali Uingereza.

Walakini, sheria hiyo bado haijaletwa Bungeni na haikuorodheshwa kama moja ya vipaumbele vya sheria vya serikali katika Hotuba ya Malkia ya mwaka huu.

Mbunge wa Labour Margaret Hodge aliiambia BBC kwamba wakati akiwa serikalini David Cameron na waziri wake wa Fedha George Osborne "walituahidi kwamba wataunda rejista ya umma ya wamiliki wanaofaidika na kampuni hizo hapa Uingereza ... lakini tumekuwa tukingojea tangu 2016 kwa ahadi hiyo'

Aliongeza: "Iko tayari, imekaa pale, sio ngumu ... lakini bado haijaibuka ... kwa hivyo ni kashfa ambayo haijatokea."

Serikali inasema inadhibiti utapeli wa pesa na sheria kali na utekelezaji, na kwamba itaanzisha rejista ya kampuni za kigeni zinazomiliki mali Uingereza muda wa bunge utakaporuhusu.

.

Viongozi wa ulimwengu

Mali za Uingereza zinazomilikiwa na viongozi wa kigeni

Mali za Uingereza za Mfalme wa Jordan na familia inayotawala ya Azabajani ilifichuliwa na BBC Panorama Jumapili.

Mawakili wa Mfalme Abdullah walisema alitumia utajiri wake wa kibinafsi kununua nyumba hizo na hakuna kitu kibaya juu yake kutumia kampuni za kigeni kufanya hivyo.

Ufichuzi mwingine kutoka kwa Pandora Papers unaonyesha uhusiano zaidi kati ya viongozi wa kigeni na umiliki wa mali nchini uingereza kupitia kampuni za siri ambazo pia ni za kigeni

Familia ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ambayo imetawala siasa za nchi hiyo tangu uhuru, ilimiliki kwa siri kampuni za kigeni kwa miongo kadhaa.

Moja ya kampuni hizi ilinunua nyumba katikati mwa London, kulingana na rekodi za Usajili wa Ardhi.

Kampuni hiyo ilianzishwa na Ngina Kenyatta, mama wa rais, na binti zake wawili Kristina na Anna.

Mnamo 2018, Bwana Kenyatta aliambia kipindi cha BBC Hardtalk kwamba utajiri wa familia yake unajulikana kwa umma, na kama rais alikuwa ametangaza mali zake kama inavyotakiwa na sheria.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alihusishwa na mtandao wa kampuni za kigeni zinazomilikiwa na marafiki wake wa muda mrefu na washirika wa biashara ya Runinga, Guardian ilifichua Jumapili.

Kampuni hizi zilishikilia mali pamoja na vyumba karibu na Hifadhi ya Regent ya London.

Viongozi kadhaa wa ulimwengu wametoa taarifa kukana makosa baada ya kuhusishwa na uvujaji huo

Wafadhili wa Tory

Nchini Uingereza , wafadhili wakuu wa kisiasa kwa chama cha Conservative wamewekeza katika mali kupitia kampuni za kigeni

Wafadhili wa Conservative

Mohammed Amersi, alinunua majumba mawili kwa kutumia kampuni za kigeni: nyumba ya mji ya Mayfair na nyumba nyingine huko Gloucestershire. Alifichuliwa na Panorama kuhusika katika moja ya kashfa kubwa za ufisadi barani Ulaya. Anakanusha makosa yoyote.

Lubov Chernukhin ametoa zaidi ya pauni milioni 1.8 kwa chama hicho tangu mwaka 2012. Nyaraka za Pandora zilizovuja zilifichua kiwango cha utajiri wa siri wa nje ambao anamiliki na mumewe, waziri wa zamani wa Urusi. Inajumuisha nyumba karibu na Hifadhi ya Regent huko London yenye thamani ya pauni milioni 38, na jumba moja huko Oxfordshire lililonunuliwa kwa pauni milioni 10. Mali hizo zilinunuliwa kwa siri kupitia mtandao wa kampuni za kigeni. Mawakili wa Bi Chernukhin wanasema yeye ni raia wa Uingereza na ana haki ya kufanya apendavyo na pesa zake

Kampuni za mfanyabiashara wa Urusi Victor Fedotov zimewapa Pauni 900,000 wabunge. Alinunua nyumba ya Hampshire kupitia mtandao wa kampuni za kigeni . Faili katika nyaraka za Pandora zinaonyesha alitengeneza mamilioni ya pesa kutoka kwa mradi ambao ulijaa madai ya ufisadi. Mawakili wa Bw Fedotov walisema "hakuna ushahidi wowote" alifanya kosa.

BBC ilitafuta habari kuhusu wafadhili kwa vyama vyote vya kisiasa kati ya nyaraka za Pandora Papers lakini zilitokea kwenye faili hizo zilikuwa juu ya wafadhili wa chama cha Conservative

Pandora Papers banner

Nyaraka za Pandora ni uvujaji wa hati na faili karibu milioni 12 zinazoonyesha utajiri wa siri na shughuli za viongozi wa ulimwengu, wanasiasa na mabilionea. Takwimu hizo zilipatikana na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi huko Washington DC na imesababisha moja ya uchunguzi mkubwa zaidi ulimwenguni. Zaidi ya waandishi wa habari 600 kutoka nchi 117 wameangalia utajiri uliofichwa wa watu wenye nguvu zaidi duniani. BBC Panorama na Guardian wameongoza uchunguzi nchini Uingereza.

Picha kutoka : BBC, London News Pictures, Central News, Shutterstock

Pandora Papers coverage: follow reaction on Twitter using #PandoraPapers, in the BBC News app.