Afghanistan: Biden alishauriwa kubakisha wanajeshi 2,500 wanasema majenerali

Iliyochapishwa

Majenerali wawili wakuu wa jeshi nchini Marekani wamesema kwamba walipendekeza kubakia kwa wanajeshi 2500 nchini Afghanistan , kabla ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wote mwezi Agosti.

Ushuhuda wa jenerali Mark Milley na Jenerali Frank McKenzie katika bunge la Congress ulionekana kukinzana na tamko la rais Joe Biden aliyesema kwamba hakumbuki kupata ushauri kama huo.

Taliban ilichukuwa madaraka mwezi Agosti baada ya wapiganaji wake kufanikiwa kupiga hatua hadi mjini Kabul na maeneo mengine ya nchi bila upinzani wowote .

Jenerali Milley alisema kwamba Marekani ilishangazwa na kasi ya kuanguka kwa serikali ya Afghanistan. Majenerali hao wawili waliulizwa na kamati ya bunge la seneti kuhusu huduma za jeshi pamoja na waziri wa ulinzi Lloyd Austin siku ya Jumanne.

kikao hicho kinajiri wiki kadhaa baada ya kuondoka kwa ghasia kulikoshuhudiwa katika uwanja wa ndege wa kabul huku mataifa ya kigeni yakijaribu kuwaondosha raia wao huku nao maelfu ya raia wa taifa hilo wakiomba kuokolewa.

Shambulio la kujitolea muhanga liliwau watu 182 wakati wa operesheni hiyo ya kuondoka .

Wanajeshi 13 wa Marekani na raia 169 wa Afghanistan waliuawa katika lango la uwanja wa ndege wa Kabul mnamo tarehe 26 mwezi Agosti.

Kubakisha wanajeshi nchini humo

Jenerali McKenzie , ambaye akiwa mkuu wa majeshi ya Marekani alisimamia kuondoka kwao , alisema chini ya masuali makali kutoka kwa maseneta wa chama cha Republican kwamba alipendekeza kubakishwa kwa kikosi kidogo cha wanajeshi 2,500 nchini Afghanistan.

Tamko lake lilionekana kukinzana na matamshi ya Joe Biden akizungumza na mwandishi wa ABC tarehe 19 Agosti kwamba hakumbuki mtu yeyote akimpatia ushauri kama huo.

Jenerali Milley alisema kwamba alikubaliana na mapendekezo hayo , lakini alipoulizwa na seneta wa Alaska Dan Sullivan iwapo matamshi ya Joe Biden yalikuwa ya uwongo, alikataa kutoa jibu la moja kwa moja.

Baadaye msemaji wa Whitehouse Jen Psaki alisema alizungumzia kuhusu suala hilo.

"Rais anathamini ushauri wa wakuu hao wa jeshi'' , alisema. Lakini hio haimaanishi kwamba anakubaliana nao. Alisema kwamba iwapo wanajeshi wagesalia nchini humo baada ya siku ya mwisho ya kuondoka mwezi Agosti , Marekani hivi sasa ingekuwa katika vita na Taliban.

Uchambuzi wa Anthony Zucher

Mwanahabari wa Marekani ya Kaskazini

Mark Milley, Lloyd Austin na Kenneth McKenzie huenda walikuwa wakitoa ushahidi mbele ya bunge la Congress , lakini matamshi ya Joe Biden mwenyewe ndio yaliomuharibia siku ya Jumanne.

Republican walimkosoa raia huyo kwa matamshi yake ya hivi karibuni kwamba majenerali hao walijikanganya.

Wakati wa mahojiano yaliofanyika mwezi Agosti, Biden alisisitiza kwamba hakukuwa na majenerali waliomwambia kubakisha baadhi ya wanajeshi nchini Afghanistan ili kuzuia utekaji wa Taliban.

Majenerali wote wawili, Milley na McKenzie walisema kwamba walidhani wanajeshi hao walihitajika na wakati mmoja McKenzie alimwambia rais kuhusu hilo.

Maseneta wa Republican pia waliuliza ni kwanini bwana Biden alikuwa ameahidi kuwabakisha wanajeshi hadi raia wote wa Marekani watakapoondoka , kwasababu kulikuwa na raia wa Marekani nchini Afghanistan wiki kadhaa baada ya kuondolewa kwa wanajeshi.

Hatimaye majenerali wote wawili walisema kwamba kundi la al-Qaeda bado lipo nchini Afghanistan -wakikinzana moja kwa moja na taarifa ya awali ya Biden kwamba kundi hilo la kigaidi limeangamizwa.

Hayo yote yaliwapatia wabunge wa Republican silaha ya ,kumshambulia rais kwa kuwadanganya raia wa Marekani.

Joe Biden hakuwa na haja ya kutoa hakikisho hilo. Angesema kwamba alitambua ushauri huo lakini akachukua uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi hao.