Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afghanistan: Jenerali wa jeshi la Marekani Mark Milley yuko kikaangoni
Jenerali mkuu wa majeshi ya Marekani na Waziri wa Ulinzi wanahojiwa na Bunge la Congress kuhusu uondoshaji wa vikosi vya kijeshi Afghanistan mwezi uliopita.
Vikosi vya Marekani vililazimika kuharakisha kuondoka - awali operesheni zilipaswa kukamilika tarehe 31 Agosti - baada ya Kabul kuangukia kwenye mikono ya Taliban tarehe 15.
Mwenyekiti wa kamati ya huduma ya silaha Jack Reed alisema kuwa wabunge wanataka kuelewa ikiwa Marekan'' haikuona viashiria" vya kuanguka kwa serikali.
Marekani imesema sasa itajielekeza kwenye operesheni dhidi ya ugaidi.
Mahojiano hayo yanakuja wiki kadhaa baada ya kuondoka Kabul wakati mataifa ya kigeni yalipotaka kuwarudisha raia wao nyumbani na maelfu ya Waafghan waliokata tamaa waliomba kuokolewa.
Shambulio la kujitoa muhanga liliua watu 182 wakati wa operesheni ya kuondoka. Wafanyakazi 13 wa Kimarekani na takribani Waafghan 169 waliuawa wakati mshambuliaji alipojilipua kwenye lango la uwanja wa ndege tarehe 26 mwezi Agosti.
Mahojiano ya Jumanne yalianza na ushuhuda kutoka kwa Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin. Jenerali Mark Milley amepangwa kutoa ushahidi baadaye.
Jenerali mwingine wa Marekani, Kenneth McKenzie, pia ni miongoni mwao. Kama mkuu wa aliyesimamia mchakato wa kujiondoa Afghanistan.
Wanajeshi wa Marekani waliingia Afghanistan kwanza mwishoni mwa 2001, muda mfupi baada ya mashambulizi ya 9/11. Wakati wanaondoka, Marekani ilikuwa imetumia karibu dola za Marekani bilioni 985 na kupeleka maelfu ya wanajeshi, wakifikia 110,000 mnamo mwaka 2011.
Katika wiki kati ya kuanguka kwa Kabul na tarehe ya mwisho ya kuondoka Agosti 31, Marekani ilihamisha wanajeshi wake 4,000 waliosalia. Ilichukua pia wakimbizi wapatao 50,000 wa Afghanistan ambao walisafirishwa kwa ndege kutoka Kabul.
Watu wapatao 20 walifariki katika umati uliokusanyika katika uwanja wa ndege siku chache baada ya Taliban kuutwaa mji wa Kabul.
Jenerali Milley huenda akakabiliwa na maswali magumu Jumanne, haswa kutoka kwa wafuasi wa Republican, ambao wametaka afukuzwe kazi.
Yeye na Jenerali McKenzie wataulizwa kuhusu shambulio la droni ya Marekani huko Kabul tarehe 29 mwezi Agosti ambalo liliwaua watu 10 wasio na hatia wa familia moja.
Baada ya shambulio hilo, Jenerali McKenzie alisema intelijensia ya Marekani ilifuatilia gari la mtu mmoja wa familia hiyo, mfanyakazi wa misaada, ikiamini anahusishwa na tawi la kundi la wanamgambo wa Islamic State (IS).
Mwanzoni Milley alielezea shambulio hilo kama "shambulio la haki". Baada ya Pentagon kugundua kuwa waliopoteza maisha wote ni raia.
Iliibuka hivi karibuni kwamba alifanya mazungumzo ya simu na jeshi la China kufuatia wasiwasi juu ya Rais wa wakati huo Donald Trump.
Simu hizo zilifunuliwa katika kitabu na mwandishi wa habari Bob Woodward, ambaye pia alisema Jenerali Milley aliwaambia wafanyakazi wake kwamba ikiwa Bwana Trump ataamuru shambulio la nyuklia, basi atalazimika kuthibitisha kabla ya kutekelezwa.
Msemaji wa Jenerali Milley alitetea simu hizo, akisema zilikuwa sehemu ya jukumu lake kudumisha "utulivu wa kimkakati".
Seneta wa juu wa Republican Marco Rubio alielezea kitendo hicho kuwa "uhaini".