Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Larissa Murenzi : "Nilificha siri mbaya kwa miaka mingi, iliniumiza, ikaniua kimawazo, kimoyo na kisaikolojia
Hawezi kukumbuka ni mara ngapi alibakwa na baba wa familia ambamo aliwekwa kama yatima tangu alipokuwa na umri wa miaka minne hadi alipokuwa na umri wa miaka saba. Jeraha alilolipata lilimfanya achukue uamuzi wa kujitoa uhai.
Larissa Murenzi msichana Myarwanda mwenye umri wa miaka 28, anasema hakupata magonjwa hatari ya zinaa lakini jeraha alilolipata moyoni kutokana na ubakaji wa mara kwa mara aliofanyiwa lilikuwa kubwa mno.
Hata hivyo anasema "kwa uwezo wa Mungu" anaweza kusema sasa kwamba amepona na sasa anaweza kusema masaibu aliyopitia baada ya kukaa kimya kwa miaka mingi.
Anasema kwa usaidizi wa madaktari aliweza kuwasaidia watu wengine waliokabiliana na maisha kama aliyoyapitia alipokuwa mtoto mdogo.
"Naweza kusema kuwa jeraha la mwili hupona haraka lakini jeraha la moyoni huwa haliponi kwa urahisi, hasa pale unapokosa usaidizi wa mtu ambaye utakaa umuelezee tatizo ulilo nalo, umlilie na akusikilize masikitiko yako .", alisema katika mazungumzo na mwandishi wa BBC Idhaa ya Maziwa makuu Yvette Kabatesi mjini Kigali.
Nini kilichomtokea?
Wazazi wa Larissa waliondoka mjini Kigali na kuhamia mashariki mwa Rwanda alipokuwa na umri wa miaka minne, wakaamua kumuacha Larissa na kaka yake kwa jamaa yao waliyekuwa na undugu wa karibu wa damu mjini Kigali ili waendelee na masomo.
Mwanaume ambaye alikuwa baba wa familia alimoachwa aliyemchukulia "kama baba " alianza kumbaka, na mara kwa mara alimtishia kuwa atamuua kama angesema kuwa alibakwa. Aliendendelea kumbaka mara kwa mara kwa miaka mingi kitendo kilichokuwa kikifanyika kwa usiri mkubwa.
"Nilificha siri mbaya sana katika maisha yangu kwa miaka mingi, siri hii iliniumiza kila siku, ikaniua kimawazo, kimoyo na kisaikolojia…nilihishi nikijua nimekufa sikuwa na maisha."
Ubakaji wa watoto unaofanywa na watu wazima ni tatizo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara miongoni mwa familia za Wanyarwanda na serikali inasema kuwa imeazimia kupambana na ubakaji huo na kutoa adhabu kali kwa wahusika wa vitendo hivyo.
Hatahivyo watoto bado wanabakwa na watu wazima wanaowalea na mara nyingi taarifa za ubakaji huo hazizungumziwi na ubakaji unapojulikana familia hufanya kila liwezekanalo kuficha taarifa hiyo isitoke ndani ya familia, kwani baadhi ya familia huchukulia kitendo hicho kama balaa na tabia tu.
Hali hii ilidhihirika kwa Larissa Murenzi wakati mzazi wake alipogundua kuwa mtoto wake alikuwa ameingiliwa na kuharibiwa sehemu zake za siri alipokuwa akimuogesha.
"Wakati mmoja tulienda nyumbani kwa wazazi wangu wakati wa likizo, mama aliyekuwa anatulea, aliniogesha akaniuliza 'mbona unanuka wewe ilikuaje? ', alipoendelea kuniuliza kwa kusisitiza nilimwambia lakini akaniambia nisiseme lolote, kwamba katika mila za Kinyarwanda haiwezekani.
"Lakini alinipeleka hospitalini nikatibiwa, akaninunulia dawa, akanijali, akanionesha upendo kwa siku chache nilizokuwa pale za likizo fupi."
Kuwa mtoto tofauti na wengine
Katika kipindo chote cha utoto wake alikuwa mtoto mwenye huzuni kubwa rohoni, lakini hakuweza kudiriki kusema kuwa huzuni alionayo ulitokana na kubakwa na mwanaume ambaye aliyekuwa 'mzazi'.
"Sikuwahi kulia kutokana na kitendo chenyewe cha kunibaka kwasababu nilikua ninajua siwezi kusema kinachoniliza, ila niliposikitishwa au kuumizwa ni kitu kidogo tu niliitumia fursa hiyo kulia sana ili kuondoa huzuni ya kubakwa.
"Hakuna mtu aliyenipenda kwasababu nilikuwa kitoto chenye tabia mbaya kinachojiliza kila mara, ambacho hakitaki kucheza na watoto wengine, ambacho kilikuwa kinalia bila sababu yoyote.
"Lakini kadri nilivyoendelea kukua nilijifunza kutolia mbele ya watu, kwasababu walikuwa mara kwa mara wanasema eti 'machozi yako, machozi yako '.
"Nilifikia wakati nikawa kimtu chenye hofu, kinachonyamaza, kinachozungumza na mtu kinayetaka kuzungumza naye sikuwa naona kitu chochote kizuri, sikupenda chakula, sikupenda kuvaa nguo nzuri, kuwapenda watu wala sherehe…kwa ujumla maisha yalikuw amabaya.", anasema Larissa Murenzi.
Kuwaonesha naweza halafu nijiue
Mienendo hiyo iliifanya familia ya Larissa Murenzi imuone kama mtoto ambaye hatafaulu masomo yake, huku wakimuita ''mjinga'' na kusema hataweza kufanikiwa maishani mwake.
Anasema kuwa aliamua kufanya bidii ili aweze kufaulu mtihani wake wa shule ya sekondari ili awaoneshe kuwa hawako sahihi. Lakini alikuwa ameamua kuwa baada ya kufaulu angejiua.
Anasema "Mungu aliona kuwa nmefikia kiwango cha kufa kabisa. Nakumbuka nilipofika kidato cha sita sekondari nilisema 'lazima nife'.
"Nilihisi ninapaswa kufanya mtihani wa serikali halafu nikimaliza nijiue, hapo ndipo nilipokutana na Mungu."
Bi Murenzi anasema kuwa alienda kanisani, wakasema mtu yeyote mwenye tatizo linalomsumbua aliseme, ''halafu badala ya kusema niombewe nifaulu mtihani , nilisema kilichokuwa moyoni mwangu''.
Baada ya husikiliza matatizo yake kanisani, walimuomba aifahamishe familia Hapo ndipo alipovuta ujasiri akamueleza mama yake ambaye hakusema lolote. Aliongea pia na ''baba'' aliyembaka akamwambia kuwa alisikitishwa na ubakaji aliomfanyia alipokuwa mtoto.
Familia ilitaka kumfuatilia mwanaume huyo, lakini kwasababu miaka mingi ilikuwa imepita tangu abakwe,, Larrissa naye anasema aliamua kumsamehe, na kuendelea na maisha.
"…Kwangu mimi sahii sitaki kuwa na vita naye tena, aende dunia itamfunza ."
Aliyekosewa aligeuzwa kuwa mwenye makosa
Wengi miongoni mwa Wanyarwanda bado wanaogopa kuzungumzia unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa kwasababu bado kuna fikra kwamba watachekwa, kuambiwa ni waongo, na hisia kwamba hilo haliwezekani.
Ingawa Larissa aliweza kufunguka na kutoa huzuni moyoni mwake na kusema kuwa "nahisi nimebadilika" ni dhahiri kuwa bado hajapona jeraha, bali kuzungumzia kubaka kwake kunaweza kumsababishia matatizo zaidi.
Anasema " Niliposema tatizo nililopitia niliona baadhi ya watu ambao walikuja kunitonesha donda langu la moyoni , naweza kusema hivyo…hasa katika familia yangu wengi waliniambia 'kwanini ulisema kuhusu ubakaji?', 'wakati tulikukataza'…
Hatahivyo anasema kuna baadhi ya watu walioishinikiza familia yake wakiiuliza ilifanya nini kuhusu ubakaji aliofanyiwa.
Alishauriwa awaone madaktari wa kisaikolojia, akaenda kuwaona na anasema
"Kusema kweli nilisaidiwa kwasababu ndipo mahala ambapo niliweza walau kuketi nikazungumzia tatizo langu kwa masaa kama manne. Nakumbuka siku ya kwanza niliingia kwa daktari saa nne za asubuhi nikatoka saa kumi na moja jioni.
"Nilisema vitu vyote, ndivyo nilivyoanza kwenda kwa mwanasaikolojia na kusema kweli ilinisaidia sana ."
Kupona na kuwasaidia wengine kupona
Baadaye alikuwa akizungumza na wasichana wengine shuleni akiwaambia maisha yake ya utotoni. Hii iliwafanya pia wafunguke na kumwambia matatizo yake. ''hapo ndipo nilipogundua kuwa wengi wamepitia matatizo kama yangu… nikawa na wazo la kuwasaidia wengine'', anasema.
Aliamua kuanzisha shirikisho la kuwakutanisha wasichana waliopitia ubakaji wa ndani ya familia na mwaka 2020 a alianzisha wakfu wa 'Baho with Larissa Foundation' ,ambao anasema uja wajumbe wengi wakiwemo, wazazi wanawake, wanaume na vijana zaidi ya 300 waliopitia ubakaji sawa na yeye.
Wakfu huo hutoa fursa ya kila mjumbe kufunguka na kuongea kuhusu mambo ya huzuni zao na kuwakiutanisha na madaktari kwa ajili ya kupata tiba na vilevile wakili pale mjumbe anapohitaji usaidizi wa kisheria.
"Ninapoketi na kumsikiliza mtu mwingine mwenye matatizo kama yangu huwa ninahisi huzuni niliyoipitia imeelezewa, ni baraka kubwa."
Kulingana na jamii ya Wanyarwanda umri alionao sasa Larissa ni wa kuolewa, lakini suala hilo humtia hofu kutokana na maisha aliyoyapitia.
"Mwanzoni ilikuwa hata ukiniambia kwamba unanipenda tu kawaida nilikuwa ninahisi umeniambia kitu kibaya sana ",lakini "pamoja na kutibiwa ikifikia muda wa kupata mwenzi nitajaribu kwasababu ni kjambo muhimu ."