Waridi wa BBC: Kazi ya malkia wa video sio ukahaba, asema Official Lynn

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Irene Jefrey Luis almaarufu Official Lynn ni mojawapo ya wasanii na malkia wa video 'videovixens' ambao ni maarufu nchini Tanzania.

Umaarufu wake unaibua hisia mseto. Hasa kwa kuwa amehusishwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasanii tajika nchini humo. Japo wasanii ambao amewataja tayari wamekanusha hayo.

Lynn ni kijana wa kike anayefwatiliwa mno hasa na vijana kutokana na mtindo wake wa maisha.

Ameshiriki kwenye video za wasanii wa Tanzania na Kenya mbali na kuwa kwa wakati huu ameanza kutunga na kuimba nyimbo zake.

"Ninapenda kuwa malkia wa video za muziki, na sitishwi na fikra za baadhi ya watu kuhusu kazi yangu, kuna watu wanasoema kuwa kazi hii ni njia ya ukahaba lakini sivyo," anasema Lynn.

Lynn anakiri kuwa kazi ya kuwa malkia wa video inatoa taswira kuwa wasichana kama yeye huenda wanatumia urembo na muonekano wa miili yao kujiuza, swala ambalo anakanusha kwa nguvu zake zote.

Swala hili la malkia wa video sio geni , katika nchi nyingi gumzo limekuweko kuhusu nafasi yao katika miziki wanayoshiriki kama modo au wanenguaji. Kwake Lynn kazi ni kazi na hii yake anatamani pia kila mtu aiheshimu kama kazi rasmi.

"Sina hela nyingi, ila ninajitajhidi kuishi maisha mazuri na maisha haya nayagharimikia. Faida ni kuwa nimejulikana, pili ninatambulika kama balozi wa bidhaa kadhaa hapa Tanzania "anasema Lynn.

Maisha ya kuwa yatima

Ni mzaliwa wa eneo la Buguruni jijini Daresalam, akitokea katika familia ambayo Lynn anasema ilikuwa na maisha ya kawaida.

Akiwa na miaka miwili baba yake mzazi aliaga dunia na baadae alipotimu miaka 13 mama naye alifariki na hapa aliikuta akiuingia ulimwengu wa kuwa yatima.

Licha ya kuwa na kaka na dada zake anasema kuwa aliukosa sana uwepo wa mama yake.

Lynn anaeleza kuwa maisha yake yaliingia katika mazingira magumu hasa kwa kuwa baadhi ya ndugu zake walikuwa tayari wamo katika maisha yao mengine aidha kuwa katika ndoa au shughuli nyengine.

"Baada ya mama kuondoka duniani, nilikuwa naishi na dada, ila nilikuwa sina ujasiri, mara nafokewa, wajua mali ya wazazi wangu zilikuwepo ila sikuwa na usemi kwani nilikuwa binti mdogo, yale maneno mabaya yalinisukuma nje ya mazingira ya kwetu," anakumbuka Lynn.

Lynn aliamua kutoroka nyumbani kwao na kuanza kuishi pekee yake, yaani kujilea.

"Nilianza kupanga nyumba, nikawa naishi maisha yangu pekee yangu, mara nyingi sikuwa na hela na nikaamua sitaki kuomba chochote, kule kukaa pekee yangu kulinikomoza , sio kwamba nilikuwa sina kwa kwenda ila nilichagua maisha hayo," anakumbuka Lynn.

Mwanadada huyu anasema haikuwa kawaida kwa msichana wa umri mdogo kama wake kuishi pekee yake na kulikuwa na ugumu, ila anasema kuwa aling'ang'ana. Alifanya biashara ndogo ili kujikimu, akianza na kuuza viatu na mapochi.

Wakati anashiriki video ya kwanza ya 'Kwetu' ya msanii Rayvanny alipata umaarufu wa kiasi chake, wakati huo alikuwa na miaka 18, anakiri alikutana na mwanamume mmoja na wakaanza urafiki wa kimapenzi, ni mwanamume aliyemchumbia na hata kutoa mahari kule kwao nyumbani.

Kipindi hicho aligundua alikuwa ameshika ujauzito, na alikuwa tayari anaishi kwa mchumba wake.

Lynn anasema kuwa haikuchukua muda kwao kuanza mikwaruzano katika uhusiano wao, anasema kuwa mahusiano yanayoleta watu wawili wenye umri mdogo pamoja hautakosa hali kama hiyo.

Mwanadada huyu anasema wakati wanakosana, mimba yeke iliharibika.

Kwa maoni yake nimuhimu, aendelee kujitafutia maisha mazuri kwa mana awe na mali na pesa zake kwa kuwa anamawazo ya kuwa baadhi ya wanaume hubadilika baada ya kuingia kwenye ndoa au mahusiano ya kimapenzi, yeye hataki kujipatakujikuta kwenye pandashuka ya kukosa chochote maishani mwake .

Kuhusu haya ya mahusiano anadai kuwa amekuwa mahusiano ya kimapnezi na wasanii tajika, lakini kwa sasa anajipatia muda akomae na ajijue kabla ya kuanza mahusiano mengine.

Wimbo wa kuhuzunisha

Ni wimbo kuhusu maisha yake- wimbo huu ujulikanao kama 'Maneno' unazungumzia hasa shida na magumu ambayo ameyapitia kama yatıma.

Wimbo wenyewe Lynn anasema kuwa aliuimba ili kuhimiza wasichana wasikate tamaa licha ya ugumu wa maisha ambao unawakabili.

Official Lynn anadokeza kuwa mtazamo wa baadhi ya watu unaeza kuwa amefanikiwa, kutokana na kutizama shughuli zake kaaika mitandao ya kijamii hasa Instagram, ila hali sivyo na ndio sabubu kuwa wimbo huu ni wa maana kwake kwani unaeleza bayana maisha yake halisi

"Yule mama ambae anauza nazi, ifikapo jioni atakuwa amepata faida, kwa hiyo huwezi kukaa hivi hivi bila kufanya chochote na utarajie mafanikio. Licha ya kwamba utamuomba Mwenyezi Mungu kwa mafanikio maombi hayo hayawezi kutimia hadi uwe na malengo na ujishughulishe kila siku. Huo ndio upeo wangu "anasema Lynn.