Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu ni kwanini kupima ubikira na kurekebisha uke kunapingwa vikali
Kuchunguzwa sehemu ya uke, kuangaliwa ikiwa mwanamke ni bikra na kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha sehemu hiyo kunaweza kupigwa marufuku huko England na Wale hivi karibuni.
Mbunge Richard Holden wa North West Durham kupitia chama cha Conservative, amewasilisha mswada kuhusu afya ambao unatafuta kupiga marufuku kuchunguzwa kama mtu ni bikira pamoja na upasuaji wa kurekebisha sehemu ya uke.
Chini ya mswada huo aliopendekeza, madaktari na wauguzi wanaotekeleza michakato hiyo wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo gerezani.
Hata hivyo, wengine wanahofia kwamba kuharamisha michakato hiyo huenda kusababisha kuendelezwa kwake kinyume na sheria.
Wataalamu wa matibabu wanasema upasuaji wa urekebishaji uke na kurejesha tabaka la utando katika sehemu ya kuingilia ya uke ni sawa na kumvamia mtu, kumnyanyasa na hakuna uhusiano wowote na sayansi.
Haki za binadamu
Bwana Holden aliamua kuchukua hatua baada ya uchunguzi uliofanywa na BBC kubaini kuwa kliniki za Uingereza zinatoa huduma hiyo kwa gharama ya pauni 150-300.
Kuangaliwa ubikira ni ukiukaji wa haki za binadamu, kulingana na Shirika la Afya Duniani na Umoja wa Mataifa.
Utamaduni huo unaofanywa katika karibu nchi 20, hakuna ushahidi wowote kuwa unaoweza kuthibitisha kama mwanamke au msichana amewahi kushiriki ngono, WHO imesema, kwa kuwa ubikira unaweza kuondoka kwasababu nyingine nyingi ikiwemo kutumia kisodo aina ya 'tampon' kwa Kiingereza ambayo huingizwa ndani au hata kwa kufanya mazoezi.
Wanaharakati likiwemo shirika linalotetea haki za wanawake la Iran na Kikurdi wanaunga mkono marufuku hiyo.
Simulizi ya Aisha
Aisha ambaye sio jina lake kamili alilazimishwa kuangaliwa kama ni bikiria au la katika kliniki moja huko London na familia yake, muda mfupi kabla ya kuchumbiwa miaka miwili iliyopita.
Wazazi wake walikuwa wamefanya mipangilio aolewe na binamu yake huko Pakistan kinyume na matakwa yake.
"Nilipofanyiwa vipimo hivyo, ilionekana kwamba mimi sio bikra" amesema.
Na baada ya hapo kaka zake na baba yake walimpiga kweli. Alikuwa amewaletea "aibu", walisema, na kutaka afanyiwe upasuaji wa kurekebisha sehemu yake ya uke ili kurejesha "heshima ya familia".
Lakini baada ya kukataa kufanyiwa upasuaji huo, Aisha alitoroka nyumbani kwao.
Mwanzilishi wa shirika linalotetea haki za wanawake la Iran na Kikurdi (IKWRO) Payzee Mahmod, alianzisha kampeni dhidi ya utamaduni huo baada ya dada yake Banaz kuuawa, alisema: "Wasichana wanakuja kwetu kutufahamisha kwamba wanalazimishwa kuangaliwa ubikira na wanataka kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha uke kurejesha utando… wakiwaza kwamba ikiwa wao sio mabikira wakati wa harusi zao, watakuwa katika hatari ya kunyanyaswa kwasababu ya kukosea wengine heshima na matokeo yake yanaweza kuwa kifo"
Wanaharakati wengine pia wameripoti kuongezeka kwamatukio hayo.
Mwanzilishi wa shirika la Freedom charity Aneeta Prem, ambaye amemuandikia waziri wa mambo ya ndani Priti Patel na waziri wa afya Sajid Javid juu ya upigaji marufuku tabia hii ya "kuchukiza na ya unyanyasaji ", pia amekiri ongezeko la simu za wasichana na wanawake wenye asili za Asia Kusini wanaotaka usaidizi, wengi wao wakilalamikia kwamba wamelazimishwa kuangaliwa ubikira kabla ya ndoa zilizopangwa.
"Tulibaini kwamba familia za waume sio kwamba wanauliza picha za wake wao watarajiwa na kiwango cha elimu tu lakini pia wanataka cheti kuhakikisha kwamba ni bikira," alisema.
Profesa Colin Melville, kutoka Baraza la Tiba, ambalo linachunguza na kuchukua hatua kutokana na malalamishi dhidi ya madaktari alisema: "Madaktari hawastahili kufanya uchunguzi wa sehemu ya uke ambako hakuna tija yoyote kitiba na wanastahili tu kufanya hivyo ikiwa ni lazima na kwa ruhusa ya mgonjwa.
'Tutafuatilia kwa karibu tukisikia kwamba daktari amefanya uchunguzi wowote ule kinyume na matakwa ya mgonjwa au bila ridhaa yake.
"Mwongozo wetu uko wazi; pale ambapo daktari amekanusha mwongozo wetu kweli au kila wakati, tunaweza kuchukua hatua."