Mzozo wa Israeli na Palestina: Jinsi makombora yalivyokatiza maisha ya watoto wadogo

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kati ya watu 219 ambao wamepoteza maisha katika Ukanda wa Gaza, watoto ni 63, inaeleza wizara ya afya iliyopo chini ya wanamgambo wa Hamas. Na kwa upande wa Israeli, watoto wawili ni kati ya watu 10 waliopoteza maisha kwa mujibu wa wizara ya afya ya nchi hiyo.

Haya ni baadhi ya tunayoyafahamu kuhusu watoto hao na familia zao.

Watoto wa familia ya al-Kawalek

Pale kombora kutoka ndege ya kivita ya Israeli lilipotua katika mtaa wa al-Wihda katikati ya jiji la Gaza mapema Jumapili, watu 13 kutoka familia al-Kawalek 'walizikwa' katika kifusi cha nyumba yao.

Wengi kati yao walikuwa ni watoto, mmoja akiwa ni mchanga kabisa wa umri wa miezi sita.

"Hatukuona chochote zaidi ya moshi," ameeleza moja ya mwanafamilia hiyo, Sanaa al-Kawalek, ambaye alinusurika katika shambulio hilo. "Sikumuona mtoto wangu japo nilikuwa nimemkumbatia, sikuweza kuona chochote."

Jeshi la Israeli (IDF) limejitetea na kueleza kuwa shambulio hilo "halikuwa la kawaida" na kuwa halikuwa lengo lao kuwadhuru raia wa kawaida. Msemaji wa jeshi ameeleza kuwa shambulio hilo lilisambaratisha handaki ambalo lilisababisha nyumba za karibuni kuanguka pia.

Kati ya waliouawa ni dada wawili Yara, 9, na Rula, 5. Wote wawili walikuwa wanapata matibabu ya 'kiwewe' kutoka kwa madaktari wa Shirika la Wakimbizi la Norway (NRC).

Mabinti hao wawili walikuwa wapole, ambao walikuwa wakifanya kazi za shule kwa muda unaotakiwa, moja ya walimu wao ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia BBC.

Picha ya mtoto wa miaka 10, Aziz al-Kawalek, ambaye ndiye pekee aliyenusurika katika familia yake akiwa amekumbatia mwili wa mama yake imesambazwa sana mtandaoni.

Ido Avigal, 5

Mtoto mdogo zaidi aliyeuawa kwa upande wa Israeli anadhaniwa kuwa ni Ido Avigal, mvulana wa miaka mitano ambaye ameuawa Jumatano ya wiki iliyopita katika mji wa kusini wa Sderot.

Ido aliuawa akiwa katika chumba chenye ulinzi maalumu na jeshi la Israeli linasema tukio hilo ni la kipekee.

Mama yake alimnyakua na kukimbia nae katika chumba chenye ulinzi dhidi ya mabomu baada ya kusikia ving'ora vya tahadhari katika mki wa Sderot, gazeti la Times of Israel linaripoti.

Vyuma venye ncha kali kotoka kwenye kombora la roketi vilipenya kwenye dirisha ambalo limetengenezwa maalumu kwa chuma ambacho kinazuia mabomu na kumuumiza mama yake na adada yake mwenye miaka saba. Ido alifariki kutokana na majeraha yake baada ya saa chache.

"Samahani sikuwepo ili nikukinge na roketi," Baba wa Ido, Bwana Asaf Avigal alisema wakati wa mazishi ya mwanawe. "Siku chache zilizopita uliniuliza: 'Baba, nini kitatokea kama king'ora kitalia tukiwa nje ya nyumba?' Nikakwambia, madhali nipo na wewe nitakulinda. Nilikudanganya."

Mama yake Ido bado yupo hospitali akiendelea na matibabu.

Nadine Awad, 16

Nadine Awad, a msichana wa miaka 16 wa kiarabu raia wa Israeli alikuwa na baba yake mwenye miaka 52 mapema asubuhi ya Jumatano wakati roketi ilipoangukia kwenye gari lao na nyumba yao na kuwaua wote wawili. Mama yake, ambaye alikuwa kwenye gari pia aliumizwa vibaya, madaktari wameeleza.

Binamu wa Nadine, Ahmad Ismail, anasema alisikia mngurumo wa roketi ukiangukia ndani ya nyumba yao katika jiji la Lod, karibu na Tel Aviv, ambapo Waarabu na Wayahudi wanaishi pamoja.

"Ilitokea kwa haraka sana," Ahmad ameliambia shilika la habari la Kan."Hata tungelitaka kukimbilia sehemu, hatuna chumba salama cha kujikinga."

Nadine alikuwa "binti wa kipekee sana" na alikuwa na ndoto za kuwa daktari, wanaomjua wanasema.

Watoto wa familia ya al-Hadidi

Ijumaa, watoto wanne wa Muhammad al-Hadidi - Suhayb, 13, Yahya, 11, Abderrahman, 8, na Osama, sita - walivaa nguo zao mpya kabisa wakaenda kusherehekea Siku Kuu ya Eid kwa kuwatembelea ndugu zao katika kambi ya wakimbizi nje kidogo ya jiji la Gaza.

"Watoto walivalia nguo zao za Eid, wakachukua wanasesere wao na kwenda kwa baba yao mdogo kwa ajili ya sherehe," baba yao mwenye miaka 37 ameeleza.

"Kufika usiku wakanipigia simu na kuniomba walale huko na nikawakubalia."

Siku iliyofuata, nyumba waliyokuwamo ikashambuliwa na makombora. Ni mdogo wao tu mwenye miezi mitano, Omar, ndiye aliyenusurika kifo baada ya kuibuliwa kutoka kwenye kifusi pembeni ya mwili wa mama yake aliyekufa katika shambulio hilo.

"Walikuwa salama ndani ya nyumba yao, hawakuwa na silaha, hawakurusha makombora ya roketi," amelalamika Bw Hadid juu ya kilichoikumba familia yake. "Wamefanya nini mpaka kustahili kilichowakuta? Sisi ni raia tu."

Ibrahim al-Masry, 14

Ibrahim al-Masry alikuwa akicheza na ndugu zake mbele ya nyumba yao kaskazini mwa Gaza wakati kombora lilipowaangukia, kwa mujibu wa ripoti.

Ibrahim, kaka yake Marwan pamoja na ndugu wengine kadhaa waliuawa pao hapo.

"Kila siku mwezi wa Ramadhan walikuwa wanacheza mtaani wakisubiri muda wa futari," baba yao, Youssef al-Masri, ameliambia gaazeti la The Independent.

"Hatukuliona shambulio lilipokuwa linatokea, tulisikia milipuko miwili tu... Kila mtu akawa nakimbilia mtaani, watoto walikuwa wakimiminika damu, akina mama walikuwa wakilia, damu ilikuwa imetapakaa kote."

"Niliwashuhudia ndugu zangu wakiungua na kukatika vipande vipande."

Hamza Nassar, 12

Hamza Nassar aliondoka nyumbani kwao Jumatano iliyopita mjini Gaza kwenda kununua mboga ili mama yake atengeneze futari, kwa mujibu wa ripori. Hakurejea tena nyumbani.

Hamza alikuwa mtoto mwema na mwanafunzi bora, baba yake ameiambia Al Jazeera.

Tala Abu al-Ouf, 13

Shambulio ambalo liliipiga nyumba ya familia ya al-Kawalek pia lilikatiza maisha ya jirani yao na binti wa miaka 13 Tala Abu al-Ouf, na kaka yake Tawfik, 17.

Baba yao, Dkt Ayman Abu al-Ouf, pia aliuawa katika shambulio hilo. Alikuwa ni mkuu wa kitengo cha matibabu ya magonjwa ya ndani katika hospitali kuu ya al-Shifa ya jijini Gaaza ambapo alikuwa ni mkuu wa mapambano dhidi ya corona.

Mwalimu wake anamuelezea Tala kuwa alikuwa binti mchangamfu na mwanafunzi bora.