Mzozo wa Israel na Palestina: Uwongo na madai ya kupotosha , ukweli wabainishwa

    • Author, Na BBC Monitoring
    • Nafasi, Essential Media Insight
  • Iliyochapishwa

Wakati mzozo wa Israeli na Palestina ukiendelea, vitu vingi vinachapishwa mtandaoni vilivyo na madai ya kupotosha au ya uwongo .

Tumechunguza mifano ya habari potofu kutoka pande zote mbili ambazo zimesababisha mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii

Video ya moto uliosababishwa na mlipuko wa roketi ni kutoka yria sio Gaza

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliweka kwenye Twitter video ambayo alidai ilionyesha Hamas ikirusha roketi nchini Israeli "kutoka maeneo ya watu wengi".

"1/3 kati ya roketi hizi 250+ zilianguka ndani ya Ukanda wa Gaza, na kuua Wapalestina," Ofir Gendelman alisema kupitia ujumbe huo wa twitter .

Lakini video hiyo ni ya zamani na ni kutoka Syria, sio Gaza.

Ilichukuliwa wakati wa operesheni ya serikali ya Syria dhidi ya vikundi vya waasi katika jiji la Deraa mnamo 2018.

Twitter iliita iliutaja ujumbe huo kama "uliofanyiwa mabadiliko kupotosha ", ikiongeza viungo vya ukaguzi kujua ukweli unaothibitisha kuwa kipande hicho kilitokana na vita vya Syria.

Baada ya kukosolewa, Bwana Gendelman alifuta ujumbe huo wa twitter

Jumbe za twitter zinazosambazwa za 'jeshi la Israeli' ni feki

Watumiaji wengine wa Twitter walieneza kile walichodai kuwa ni picha za jumbe kwenye skrini kutoka kwa akaunti ya Twitter ya Vikosi vya Ulinzi vya Israeli (IDF) wakisema: "Tunapenda tu kuua" na "Tumewalipua watoto kwa mabomu".

Picha hizo ni bandia ambazo zinaweza kufanywa kwa kutumia zana za mitandaoni zinazopatikana bila malipo

IDF haikutoa taarifa hizi kwenye akaunti yao rasmi ya Twitter au mahali pengine popote.

Akaunti ambayo ilitoa jumbe hizo inaegmea upande wa wapalestina na inapinga kabisa utawala wa Israel

Video hiyo haionyeshi 'mazishi feki' huko Gaza

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Israeli waliiweka mtandaoni video moja wakidai ilionyesha Wapalestina wakiandaa mazishi ya mtu anayedaiwa kuuawa na mashambulio ya angani ya Israeli huko Gaza - ili wahurumiwe na ulimwengu

Kwenye video hiyo, ambayo pia ilichapishwa mshauri wa Wizara ya Mambo ya nje ya Israeli, kikundi cha vijana kimebeba kile kinachoonekana kama mwili uliofunikwa na sanda mabegani mwao.

Mara tu wanaposikia sauti ya ving'ora, wanauacha mwili chini na kukimbia. Baadaye kidogo mwili uliobebwa pia huinuka na kukimbia.

Tulipata video hiyo hiyo iliyochapishwa mnamo Machi 2020, na ripoti wakati huo zilionyesha kwamba kundi la wavulana huko Jordan walikuwa wakijaribu kukwepa vizuizi vikali vya Covid-19 kwa kujifanya wanafanya mazishi.

Kipande hiki kilisambazwa chini ya kaulimbiu "Palywood" [Hollywood ya Palestina] na mamia ya watumiaji wa mitandao wanaounga mkono Israeli kwenye majukwaa makubwa ya mitandao ya kijamii

Video haionyeshi msikiti wa al-Aqsa ukiteketea

Watumiaji wengine wa mitandao wanaounga mkono Wapalestina waliweka video ambayo walidai ilionyesha msikiti wa al-Aqsa ulioko Mashariki mwa Jerusalem ukiteketea na wakiishtumu Israeli kwa "kuruhusu Msikiti wa al-Aqsa kuchomeka".

Video ni ya kweli, lakini picha za ziada kutoka kwa pembe zingine zinaonyesha wazi kuwa mti karibu na msikiti huo ndio uliokuwa umewaka moto, sio msikiti wenyewe.

Jumba la msikiti katika Jiji la Kale la Yerusalemu ni moja ya maeneo yenye heshima zaidi kwa Uislamu, lakini eneo hilo pia ni takatifu zaidi kwa wayahudi , ma kujulikana kama Mlima wa Hekalu.

Kwenye video hiyo, umati mkubwa wa vijana wa Kiyahudi wa Kiisraeli wanaweza kusikika wakiimba wimbo wa kupinga Wapalestina nyuma ya Ukuta wa Magharibi, na moto ukionekana kwa mbali.

Sababu ya moto huo haijulikani .

Polisi wa Israeli walisema katika taarifa kwamba ulisababishwa na fataki zilizotupwa na waumini wa Palestina. Lakini Wapalestina wanasema ilisababishwa na maafisa wa Israeli kutupa mabomu ya kuwatawanya.

Kulingana na Reuters, mti huo ulikuwa mita 10 tu kutoka msikitini. Moto ulizimwa baadaye na msikiti haukuharibiwa na moto huo.

Video ya zamani haionyeshi kombora katika barabara ya Gaza

Ujumbe mmoja wa twitter uliosambazwa sana ulidai kuonyesha picha za kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas wakitembeza makombora kwenye barabara huko Gaza. Mtoto anaweza pia kusikika akiongea kwenye video.

Ujumbe huo, kutoka kwa akaunti inayounga mkono Israeli, inadai: "Kwa mara nyingine tena tunaona Hamas ikitumia raia kama ngao kuua Wayahudi wakijua ... kwamba Israeli haitalipa kisasi kwa sababu ya hatari ya kuumiza watu wasio na hatia".

Walakini, tuligundua kuwa video hiyo ilipakiwa kwenye Facebook mnamo 25 Novemba 2018, na nukuu iliyosema ilipigwa katika mji wa Abu Snan huko Galilaya, nchini Israeli.

Aric Toler, mtafiti wa wataalam wa uchunguzi wa Bellingcat, anafikiria kuwa picha hizo zinaonyesha mifano ya makombora yanayotumika kwa mazoezi ya jeshi la Israeli.

Akaunti ya Twitter iliyochapisha video hiyo baadaye ilifutwa, na ikaomba msamaha kwa kuchapisha "data isiyo sahihi".

Na ripoti kutoka kwa Alistair Coleman, Shayan Sardarizadeh, Christopher Giles na Nader Ibrahim.