Mapambano yaendelea kuchachamaa licha ya mataifa makubwa kuzitaka Israeli, Palestina kushusha silaha

Iliyochapishwa

Mashambulizi yanaendelea katika ukanda wa Gaza, Palestina na kusini mwa Israeli leo Jumanne licha ya mwito wa kusitisha vita ukitolewa na mataifa mengi zaidi duniani.

Ripoti kutoka jeshi la Israeli zasema kuwa ving'ora vimesikika katika baadhi ya sehemu za Israel baada ya yile ambacho kilisemekana ni ukimya wa karibu "saa sita".

Ving'ora hivyo vya tahadhari vimesikika katika miji ya Kfar Aza, Nahal Oz, na Zimrat karibu na kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kusababisha watu kukimbilia usalama wao.

Ving'ora hivyo vilionya wakaazi kuwa kuna maroketi yanayorushwa kuelekea Israel kutoka Gaza.

'Israeli ina maeneo elfu ya kushambulia Gaza'

Jeshi la Israeli (IDF) limejibu mapigo kwa kuendeleza mashambulizi kutoka angani kwa kutumia ndege vita zake huku Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Benny Gantz akitangaza kuwa IDF "lina zaidi ya maeneo ya elfu moja ya kushambulia katika ukanda wa Gaza."

"Jeshi linapanga kuendelea kuishambulia Hamas na mapigano hayatasitishwa mpaka tulete mpango kamilifu na wa muda mrefu wa amani," Bwana Gantz amenukuliwa akisema na gazeti la Times of Israel.

"Jeshi limeshatumwa katika mipaka yote na lipo tayari kuzima jaribio lolote la kutoka nje ya nchi ambalo litalenga kuwadhuru raia wa Israeli au uhuru wa nchi yetu," ameongeza Gantz.

Jumanne asubuhi, Israel iliendelea kufanya mashambilizi ya anga katika ukanda wa Gaza. Jeshi lake lilisema makumi ya roketi yalirushwa katika eneo lake usiku kucha na kundi la Hamas.

Mapigano hayo sasa hivi yanaingia wiki ya pili huku ishara za mgogoro huo kusitishwa zikiwa finyu mno.

Takriban watu 212 wakiwemo wanawake 100 na watoto wameuawa katika eneo la Gaza, kulingana na wizara ya afya. Nchini Israel watu 10 wakiwemo watoto wawili wameuawa, huduma zake za matibabu zimesema.

Pia, hii leo Israel imedungua ndege isiyokuwa na rubani katika mpaka wake na Jordan.

Hata hivyo, haikusema ndege hiyo imetoka wapi hasa.

Israel ina mpaka na Jordan upande wa mashariki. Wakati huo huo, katika historia Jordan imekuwa mshirika wa karibu sana wapalestina, lakini ilirejesha uhusiano na Israeli mnamo mwaka 1994.

Biden atoa wito wa amani

Hayo yamejiri licha ya Rais wa Marekani Joe Biden kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano baada ya siku nane za mapambao kati ya Israel na Palestina huko Gaza.

Bwana Biden alimuambia Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kwamba Marekani inashirikiana na Misri na nchi zingine kusitisha uhasama uliopo kati yao.

Lakini pia Marekani kwa mara nyengine tena imezuia tamko la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutaka vita hivyo visistishwe.

Hata hivyo, katika wito wake, Rais Biden alimuambia Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa kwa mara ya kwanza anaunga mkono kusitishwa kwa mapigano na kwamba ataongeza shinikizo kwa Israel kumaliza mgogoro huo.

Rais Putin atoa wito wa kusitishwa kwa vita

Rais wa Urusi Vladimir Putin pia naye ametoa wito wa kusitishwa kwa vita hivyo mara moja kati ya Israel na Palestinians na kusema kuwa "vimesababisha idadi kubwa ya waathirika miongoni mwao ni wasio kuwa chuki na mtu kama vile watoto".

"Tunaamini kuna umuhimu wa kusitishwa kwa vurugu hizi kati na pande zote mbili na kutafutwe suluhu ya kudumu kwa kuzingatia maazimio ya msingi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - na kutambua kanuni za sheria ya kiataifa kwa ujumla," Bwana Putin aliongeza.

Macron kuungana na wengine katika juhudi za kusitisha vita

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia naye ameahidi kuungana na wengine katika mazungumzo na Rais wa Misri na Mfalme wa Jordan, ofisi yar ais imesema.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujadili njia mbalimbali za kuwezesha kusitishwa kwa mapigano hayo.

Mwanahabari wa BBC Rushdi Abualouf huko Gaza amekuwa akiandika ujumbe kwenye Twitter kuhusu matukio ya jana usiku, wakati ndege za kivita za Israeli zilipotekeleza mashambulizi ya anga zaidi ya 60 na wanamgambo wa Palestina nao wakirusha zaidi ya roketi 90 kuelekea kusini mwa Israel .

Israel yatetea mkakati wake ghadhabu ikindelea kuongezeka

Hasira inaendelea kuogezeka kimataifa kwasababu ya raia wanaoendelea kupoteza maisha huko Gaza, na Israel inaendelea kujaribu kuonesha umuhimu wah atua inazochukua, ameandika mwanahabari wa BBC wa masuala ya kidiplomasia Paul Adams.

Miongoni mwa taarifa ambazo imekuwa ikitoa, afisa mwandamizi wa jeshi ameelezea oparesheni hiyo kuwa yenye uwezekano wa "kuendelea kwa muda".