Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashariki ya kati: Jinsi Ufaransa na Uingereza zilivyoigawanya karne moja iliyopita
Asubuhi ya Aprili 1920, Ufaransa na Uingereza walianza mkutano katika mji mdogo wa Italia wa Riviera, lengo likiwa ni kurasimisha kugawaywa kwa eneo la Ottoman Mashariki ya kati.
Paris ingesalia na Lebanon na Syria, huku London ikichukua udhibiti wa Iraq na Palestina, kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano uliofanyika San Remo, Aprili 19-26, 1920, miaka 101 iliyopita.
Kugawanywa kwa eneo hilo kati ya nchi zilizokuwa na nguvu kubwa wakati wa ukoloni wakati huo kulifikiwa makubaliano miaka minne ya nyuma katika mkutano wa siri ambapo pamoja na ruhusa ya Urusi, mwanadiplomasia wa Ufaransa François Georges-Picot na Muingereza Sir Mark Sykes walijadiliana na kufikia makubaliano ya mkataba maarufu wa Sykes-Picot.
Na mkutuno huo sio tu kwamba ulikuwa msingi wa mipaka ya sasa Mashariki ya Kati, lakini pia chanzo cha matatizo mengi yanayoendelea kujitokeza hadi hii leo.
"Athari ya kilichotokea San Remo ni kubwa mno. Miaka mingi iliyopita Ufaransa na Uingereza zilifanya maamuzi ambayo yaliishia kuunda maeneo bila utaifa kwasababu nchi nyingi hazikuwa na haki ya kujieleza," amezungumza na BBC World Jean-Paul Chagnollaud, Profesa wa somo la sayansi ya siasa chuo kikuu cha Cergy-Pontoise na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati.
"Matatizo mengi tunayoshuhudia hii leo huko Palestine, Lebanon, Iraq au Syria yanahusishwa na kilichotokea mwaka 1920 na miaka ya 1921, 1922 na 1923", anaendelea kusema mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti na Masomo ya Mediteranea na Mashariki ya Kati.
Ahadi za Uingereza
Waarabu walipuuza kwa miaka mingi kwamba Paris na London zilikuwa zinapanga mkataba ambao ulididimiza ahadi waliyopewa na Uingereza kwamba ikiwa wataasi dhidi ya Waottomani, kuanguka kwa utawala huo kutawafanya kuwa huru na wenye kujitegemea.
Ushindi wa washirika wa Mashariki ya Kati wakati wa vita vya kwanza vya Dunia ilikuwa moja ya vichocheo vya kuanguka kwa Utawala wa Ottoman.
Kufuatia tukio hilo, wajibu wa Ufaransa kwa Syria na wajibu wa Uingereza kwa Iraq na Palestina ukaundwa, kama ilivyopangwa, wote ukiwa chini ya Shirikisho la Mataifa (bodi ambayo ilitangulia Umoja wa Mataifa).
"Uingereza ilisaidia Waarabu katika eneo hilo kuasi dhidi utawala wa Ottoman lakini wakati wa vita waliweka ahadi kwa makundi mbalimbali," Priya Satia, mtaalamu wa historia katika utawala wa Uingereza na Profesa wa chuo kikuu cha Stanford, ameielezea BBC Mundo.
"Waliwaahidi Waarabu kuwa watatawala wenyewe Palestina, waliahidi Wafaransa kuwa watagawanya baadhi ya maeneo nao, na pia kuna ahadi walioweka wakati wa azimio la Balfour," amesema.
"Hawakuwa tayari kujitawala"
Lakini katika mkutano wa San Remo, aliyekuwa wakati huo Waziri Mkuu wa Uingereza David Lloyd George, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ufaransa Alexandre Millerand, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia Francesco Nitti na balozi wa Japani Keishirō Matsui walikubaliana kuwa sio eneo lote lilikuwa tayari kwa na uhuru kamili.
"Huko San Remo, mazungumzo hayo yaliangazia majukumu ya maeneo ambayo Ufaransa na Uingereza tayari zilikuwa zimeyagawanya. Hususan, kulikuwa na mjadala uliofanyika kwa muda mrefu kuhusu Palestina na azimio la Balfour," amesema Jean -Paul Chagnollaud.
Makubaliano yalitiwa saini Novemba 2, 1917, vita vya dunia vikiwa vinaendelea, azimio la Balfour lilikuwa ni nyaraka ambayo serikali ya Uingereza iliahidi raia wa Kiyahudi "makazi" katika eneo la Palestina.
Uingereza na Ufaransa zikapanga kugawanya eneo ambalo linafahamika kama Mediterania ambako pia kunachukuliwa kama eneo la kidini.
Lebanon ikachukuliwa kama eneo la hifadhi ya Wakiristo na Wadruze.
Kulingana na kikao cha San Francisco Palestina itakuwa nyumbani kwa jamii ndogo ya Wayahudi huku bonde la Bekah karibu na mpaka wa Lebanon na Syria likitengwa kuwa eneo la Waislamu wa Shia.
Syria itakuwa eneo la Waislamu wa Sunni.
Mipaka "ilichorwa kwa penseli na rula"
Ingawa jiografia ilisaidia kuhalalisha mipaka hiyo, wataalamu wengi wanakubali kuwa ilichorwa kwa "penseli na rula" tu, bila ya ufahamu mkubwa wa eneo, na kwamba mipaka hiyo iliyochorwa na Ufaransa na Uingereza haikuzingatia dini, kabila au makundi ya asili ya watu.
Pia kulikuwa na mapungufu fulani katika mkutano wa San Remo. Mfaransa Alexandre Millerand na Mwingereza David Lloyd George hawakukubaliana baadhi ya mambo.
Jukumu la Marekani
"Uingereza ilikubali mamlaka ya Ufaransa kwasababu walibaini kwamba hawakuwa sawa kifedha kudhibiti eneo lote la Mashariki ya kati, " maelezo ya Henry Laurens, Profesa wa historia ya Uarabuni duniani katika chuo cha Collège de France na mwandishi wa kazi zingine kubwa juu ya historia ya Ulaya na Ottoman karne za 19 na 20.
Wamarekani kwa upande wao, walijiondoa kwenye majadaliano baada ya seneta wao kukataa makubaliano ya mkataba wa Versailles, ambayo yaliwakilisha mwisho wa vita vya kwanza vya dunia.
Mkutano huo pia ulizungumzia Armenia na vile mipaka yao inaweza kuwa (Marekani ilikataa kuundwa kwa mamlaka ya Armenia), pamoja na uwezekano wa jimbo la Kurdi na kwa ujumla hatma na uhamisho wa baadhi ya maeneo chini ya utawala wa Ottoman.
Kukiwa na mkataba wa Sèvres, uliotiwa saini miezi minne baadaye, Agosti 1920, Ottoman ikakubali rasmi kuachia maeneo yaliyokubaliwa kwa pamoja na mamlaka za Uingereza na Ufaranasa.
Na hiyo ikawa hatua moja ya kuanguka kwa Milki ya Ottoman na kuundwa kwa Uturuki ambayo ingeanza kuchukua nafasi yake miaka mitatu baadaye.
Kanuni tatu za kugawanya mipaka
Awali, mkataba wa Sykes-Picot ulipanga kugawanya Mashariki ya Kati kuwa eneo huru kwa kutegemea ushauri wa London na Paris na kuanzisha maeneo ya kudhibitiwa huko Iraq.
Lakini mpango huo ukatupiliwa mbali huku kukiitishwa dharura ya kuundwa kwa mamlaka mwaka 1919.
Baada ya kufikiwa uamuzi wa hilo, kilichobakia pekee kikawa ni kuundwa kwa mamlaka hizo, cha msingi kikiwa kujua Palestina inaishia wapi na Syria inaanzia wapi.
Katika mkutano wa San Remo, mataifa yenye nguvu yalitegemea kanuni tatu kuweka mipaka.
Walitetea uhusiano kati ya Palestine na Bibilia, kwahiyo, Lloyd George alitumia kitabu cha ramani cha historia ya kijiografia ya eneo hilo iliyochapishwa mwaka 1915 na mchungaji wa Scotland George Adam Smith, kuweka mipaka ya eneo.
"Kanuni ya pili ilikuwa Ufaransa kukataa mamlaka yake kujumuisha koloni la Wayahudi," ameelezea Henry Laurens wa chuo cha de France.
"Na hivi ndivyo vile eneo dogo kati ya Syria na Lebanon, linalofahamika kama Galilee, lilivyoishia kujumuishwa kwenye mamlaka ya Uingereza 'Palestina' na wala sio katika mamlaka ya Ufaransa 'Syria' kwasababu huko kulikuwa na makazi ya Wayahudi," amesema mtaalamu wa masuala ya dunia ya Uarabuni.
Na mwishowe, Uingereza ilitaka hapo kuendelea kuwa eneo kati ya mamlaka za Palestina na Iraqi.
"Kuanzia mwanzo, watu waliohamia maeneo mengine walichukuliwa kuwa wageni. Na wakimbizi wa Palestina walipowasili Syria, Lebanon au Jordan mwaka 1948, pia nao walichukuliwa kama raia wa kigeni. "
Mkutano mwingine wa San Remo
Wiki hiyo hiyo kukafanyika mkutano wa pili juu ya ugawanaji wa raslimali za mafuta huko San Remo.
Hitaji kubwa la nishati wakati wa vita ulionesha nchi zenye nguvu kubwa umuhimu kuwa na raslimali zao wenyewe za mafuta.
Kama walivyokubaliana, Ufaransa ingepokea robo ya mtaji kutoka kwa kampuni ya petroli ya Uturuki, ambayo baadaye iligeuka na kuwa kampuni ya Petroli ya Iraq.
Walioibuka na ushindi
Jean-Paul Chagnollaud, kutoka chuo kikuu cha Cergy-Pontoise, amesema kuwa baadhi katika eneo hilo waliridhika na kugawanywa kwa maeneo hayo.
"Kiasi kikubwa, Walebanon walifurahia hata kama imewasababishia machungu mengi sana."
" Israel pia ilikuwa na furaha hhasa na azimio la Balfour kuanzisha 'nyumba za taifa' huko Palestina. Nafikiri wao walikuwa washindi wakubwa."
Wakati huo huo, Iraq kukawa na mvutano kati ya Waislamu wa Shia na waliokuwa wengi Wasunni alikotoka aliyekuwa Rais Saddam Hussein - na Wakurdi waliotaka kujitangazia uhuru wao.
Leo hii, Syria, licha ya kuwepo kwa mamlaka Ufaransa, imejumuisha Wasunni walio wengi wakifuatiwa na Alawite walio wachache - kunakotoka familia ya utawala wa Assad - lakini pia inajumuisha Wakiristo, Wadruze na jamii za Wayahudi.
Miaka 101 baadaye, athari za mkutano wa San Remo bado zinashuhudiwa kote duniani.