Wakimbizi wa Afghanistan 'waliosahaulika' wanaojiua

Iliyochapishwa

Akiwa ametenganishwa na wapendwa wake, Ali Joya alimchukulia rafiki yake Mujtaba Qalandari kama familia yake.

Raia wawili wa Afghanistan ambao wamekuwa Indonesia kwa muda mrefu tu.

"Alikuwa mtu mwerevu," Mujtaba amesema kumhusu Ali. "Siku zote alikuwa ametamani kuishi ughaibuni aweze kumsaidia mama yake. Kila wakati alikuwa akisema, nataka kujitengenezea maisha yangu ya baadaye - niwe na mke na watoto'."

Lakini alikuwa amesubiri kwa muda mrefu - Ali alijiua mwishoni mwaka jana. Akiwa bado kwenye umri wa miaka ya 20, alikuwa amesubiri kupata hifadhi kwa miaka minane.

Ali ni mmoja katika ya raia 13 wa Afghanistan nchini Indonesia ambao wamejitoa uhai katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kulingana na Mohammad Yasin Alemi, ambaye ni mwakilishi wa raia wa Afghanistan katika mji wa Tangerang.

'Tumesahaulika'

Afghanistan ina watu milioni 2.7 ambao ni miongoni nwa wakimbizi waliosajiliwa na UNHCR kote duniani.

Ukosefu wa uthabiti wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi baada ya Marekani kuingilia Afghanistan mwaka 2001 kulichangia kuondoka kwao.

Karibu wakimbizi wa Afghanistan 8,000 na wanaotafuta hifadhi walisajiliwa na shirika la UNHCR nchini Indonesia kufikia Desemba 2020 lakini nchi hiyo bado haijasajili mkataba wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa na kusitisha uhifadhi wao wa kudumu.

Kwa maana hiyo basi, ni kinyume cha sheria kwa raia hao kufanyakazi, na hivyo basi hawawezi kupata bima ya afya wala elimu.

Wengi wao wanaishi kambini huku wengine wakisubiri zaidi ya miaka 10 kupata hifadhi katika nchi za nje kupitia mchakato unaosimamiwa na UNHCR.

Ni bahati na sibu, Mujtaba Qalandari, 42, anajua hilo vizuri sana. Yeye, mke wake na kijana wake walihamia Indonesia mwaka 2015 kutoroka vita nchini Afghanistan nia yao ikiwa ni kutafuta maisha mazuri ya siku za usoni.

Mke wake anasema kuwa kusubiri kufanikiwa kumesababisha msongo wa mawazo kwake na mume wake.

"Tulijisajili na UNHCR UNHCR. mwaka 2015. Lakini hatujawahi kuambiwa lolote tangu wakati huo. Tumesahaulika," mama huyo, 34, amesema.

Bwana Alemi anasema ameona visa vya kujitoa uhai vikiongezeka.

"Sababu kubwa ni mchakato mrefu wa UNHCR wa kuwapa watu hifadhi. Muda mfupi zaidi mtu anasubiri sio chini ya miaka 6," amesema.

"Matatizo ya kifedha, hofu ya hatma ya baadaye na wasiwasi ni miongoni mwa yale yanayochangia wao kujitoa uhai."

'Aliniacha peke yangu'

Kote duniani, kulikuwa na wakimbizi milioni 26 na wengine zaidi ya milioni 4 wakiwa wanatafuta hifadhi mwaka 2019, kabla ya kuanza kwa janga la virusi vya corona.

Mujtaba Hossain ni raia mwingine wa Afghanistan ambaye alimpoteza rafiki yake wa karibu. Abdul, 22, ambaye alikuwa akiishi naye chumba kimoja amekuwa Indonesia kwa miaka saba - mwaka mmoja zaidi yake.

Wakati huo wote, Abdul, 36, amekuwa na matumaini ya kuungana tena na mke wake na watoto wake wawili, ambao hakuweza kusafiri nao Indonesia. Lakini Mujtaba anasema ilipofika Desemba, alikata tamaa na kujitoa uhai".

Athari yake ilikuwa kubwa kwa Mujtaba - walikuwa marafiki wa karibu sana nchini Indonesia.

"Alikuwa mtu mcheshi, kila wakati alikuwa anatania na alichopenda zaidi ni kwenda kwenye chumba cha mazoezi," amesema Mujtaba. "Tulikuwa tumeahidiana kuwa, liwe liwalo tutakutana tena siku za usoni. Lakini aliniacha peke yangu katikati ya safari."

Mujtaba bado anaishi Tangerang, katika chumba kidogo chenye dirisha moja alilokuwa analitumia kwa pamoja na Abdul. Anasema kuwa theluthi moja ya maisha yake yamepotea akiwa tu anasubiri hifadhi.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Indonesia, Ann Maymann, ameelezea vyombo vya habari kuwa idadi ya wanaojitoa uhai inasikitisha sana lakini akaongeza: "Ni kidogo sana yanayoweza kufanywa na serikali, wenyeji au kupitia usaidizi wa kimataifa."

Bi. Maymann anasema kuwa wakimbizi wanastahili kutangamana na wengine wanapoishi, lakini Indonesia haikutia saini mkataba wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa.

'Siku mbaya zaidi maishani mwangu'

Raia wengi wa Afghanistan wanaoishi Indonesia wana matarajio ya kupewa hifadhi katika nchi nyingine, hasa Australia. Lakini nchi zilizowapa hifadhi kipindi hiki zinakubali maombi kidogo tu.

Hiyo ndio sababu watu wengi nchini Indonesia bado wanasubiri, wizara ya mambo ya nje nchini humo imesema.

Mwaka 2016, wakimbizi 1,271 waliokuwa Indonesia walipata hifadhi kwenye nchi zingine idadi ambayo mwaka uliofuata ilipungua kwa nusu yake.

Musa Sazawar, 42, mwanahabari kutoka Afghanistan, anahisi vibaya kila anapoangalia takwimu hizo.

Machozi yanamtiririka hasa akikumbuka kuwa alimuacha mke wake akiwa mjamzito katika kusini magharibi mwa Afghanistan.

"Kijana wangu anatimiza miaka minane na bado sijawahi kumuona. Sijawahi hata kumkumbatia," Musa anasema.

Mwaka mmoja baada ya kuondoka, Nato ilisitisha mapigano yake nchini Afghanistan, Marekani ikapunguza idadi ya wanajeshi wake nchini humo na ghasia zikaongezeka kote nchini humo.

Mamia ya raia wa Afghanistan wakalazimika kutoroka makazi yao.

Anasema, baada ya kuondoka nchi yake akiwa na matarajio ya kuboresha maisha ya familia yake, amefikia kidogo sana zaidi ikiwa ni majonzi na msongo wa mawazo.

"Siku mbaya zaidi maishani mwangu ni zile ambazo nimekuwa mbali na nyumbani," amesema.