Mkanyagano wa Israel: Watu 44 wafariki katika tamasha la kidini la Lag B'Omer

Iliyochapishwa

Watu wasiopungua 44 wameuawa katika mkanyagano katika sherehe ya kidini iliyojaa watu kaskazini mashariki mwa Israel.

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa katika tamasha la Lag B'Omer, ambalo hufanyika kila mwaka chini ya Mlima Meron.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alielezea kama "janga kubwa" na amesafiri kwenda eneo la tukio.

Makumi ya maelfu ya Wayahudi wa Orthodox walihudhuria sherehe hiyo, na kuifanya kuwa tukio kubwa zaidi nchini Israeli tangu janga la virusi vya Corona lilipoanza.

Programu ya chanjo iliyofanikiwa nchini humo imeiruhusu kuondoa masharti , lakini maafisa wa afya walikuwa bado wameonya juu ya hatari ya virusi vya Corona .

Ripoti za mapema zilidokeza kwamba muundo eneo hilo ulikuwa umeanguka, lakini maafisa wa dharura baadaye walisema mkanyagano ulitokea saa 01:00 saa za kawaida (22:00 GMT Alhamisi).

Vyanzo vya polisi viliambia gazeti la Haaretz kwamba mkanyagano huo ulianza baada ya wahudhuriaji wengine kuteleza,hatua iliyosababisha makumi kadhaa kuanguka.

"Ilitokea haraka sana watu walianguka tu, wakikanyagana. Ilikuwa ni janga," shahidi mmoja aliliambia gazeti hilo.

Video zilizowekwa mtandaoni zinaonyesha maelfu ya watu wakijitahidi kukimbia kupitia njia nyembamba.

Ujumbe wa uliopazwa katika spika uliwahimiza watu kutawanyika, kabla ya polisi kuomba uokoaji kamili katika eneo la mkasa .

"Hakuna mtu aliyefikiria kuwa hii inaweza kutokea hapa," mtu mmoja aliiambia Channel 12 TV. "Shangwe ikawa kuomboleza, nuru kubwa ikawa giza kuu."

Magari kadhaa ya ambulansi yalifika katika eneo la tukio wakati wafanyikazi wa huduma za dharura wilipoweka miili ndani ya mifuko ya plastiki. Helikopta zilipeleka majeruhi hospitalini, wakati jesi likisema kuna wanajeshi waliotumwa kusaidia katika juhudi za kuwaokoa watu

Takriban watu 150 walijeruhiwa, maafisa walisema, pamoja na watu 38 ambao walikuwa katika hali mbaya kwenye eneo la tukio .

'Hakuna eneo la kukimbilia'

Mashahidi wameelezea hofu iliyokuwepo wakati wa mkanyagano huo.

"Kulikuwa na watu wengi na kulikuwa [na] ... hakuna mahali pa kukimbilia ," mtu mmoja aliyehudhuria aliiambia BBC. "Watu walianza kuanguka chini."

"Ghafla tukawaona wahudumu wa afya ... wakikimbia," Shlomo Katz, mmoja wa waliyokuwepo alisema. "Mmoja baada ya mwingine [walianza] kutoka ... Ndipo tukaelewa kuwa kuna jambo linaendelea hapa."

"Zaidi ya watu 1,000 kwa pamoja walijaribu kwenda chini, mahali padogo sana, barabara nyembamba sana na walianguka juu ya kila mmoja," alisema Yanki Farber, mwandishi wa tovuti ya Kiyahudi wa Orthodox Behadrei Haredim.

Sherehe za Lag B'Omer ni nini ?

Makumi ya maelfu ya Wayahudi wa Orthodox hufanya safari ya kwenda Meron kila mwaka kwa Lag B'Omer, likizo ya kidini kuwashwa moto usiku kucha, sala na kucheza.

Mji huo ni mahali pa kaburi la Rabi Shimon Bar Yochai, mwenye hekima wa karne ya pili aliyeheshimiwa, ambaye aliagiza kwamba kumbukumbu ya kifo chake iadhimishwe na sherehe ya maisha yake.

Eneo hilo limetengwa ili kila jinsia kuwa na sehemu yake . Picha na video zinaonyesha mkanyagano ulitokea katika sehemu moja ya wanaume.

Kulingana na Times of Israel, waandaaji walikadiria kuwa watu 100,000 walifika Alhamisi usiku, na zaidi walipaswa kuwasili siku ya Ijumaa.

Idadi ya waliohudhuria ilikuwa kubwa kuliko mwaka jana, wakati tamasha hilo lilifanyika chini ya masharti kwa sababu ya janga la Corona

Lakini bado ilikuwa ndogo kuliko miaka ya nyuma, wakati mamia ya maelfu ya watu walishiriki.