Uvamizi Burkina Faso: Wanahabari wa Ulaya wauawa baada ya kutekwa nyara

Iliyochapishwa

Wanahabari wawili wa Uhispania waliotekwa nyara karibu na eneo la hifadhi ya asili mashariki mwa Burkina Faso wameuawa, Waziri Mkuu Pedro Sánchez amesema.

Vyanzo vya usalama vya eneo vimesema kuwa raia wa Ireland pia ameuawa ingawa hilo bado halijathibitishwa rasmi.

Raia hao wa Ulaya walikuwa sehemu ya kundi linaloshika doria kupinga wawindaji haramu waliovamiwa na wanaume wenye silaha karibu na hifadhi ya Pama Jumatatu. Mwanajeshi wa nchi hiyo pia alitekwa nyara.

Bado haijafahamika nani ametekeleza shambulizi hilo.

Nchi hiyo ya Afrika Magharibi inakabiliwa na mgororo wa kiusalama kama nchi nyingine nyingi tu majirani zake huku makundi ya Kiislamu yaliyojihami yakiendelea kutekeleza mashambulizi na utekaji nyara katika sehemu nyingi eneo hilo.

Tunajua nini kuhusu shambulizi hilo?

Ushikaji doria Jumatatu ulijumuisha wanajeshi, walinzi wa misitu na wanahabari wa kigeni.

Wanajeshi wawili waliopata majeraha walizungumza na shirika la habari la AP, na kusema idadi ya wanamgambo ilikuwa imezidi wanaoshika doria.

Mmoja wa wanajeshi hao alipigwa risasi mguuni huku mwingine akijeruhiwa mkononi na hatimaye kukatwa, kulingana na shirika la AP.

Wanajeshi hao walisema walijitahidi kulinda wanahabari wa kigeni lakini baada ya ufyatulianaji wa risasi ndipo walipojua kuwa hawapo.

Magari na silaha za wanamgambo hao pia yalikamatwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Arancha González Laya aliwaambia wanahabari kuwa miili iliyopatikana eneo hilo ilionekana kufanana na ya wanahabari wa Uhispania ambao wamekuwa wakitengeneza makala kuhusu hali ilivyo nchini humo.

Bwana Sánchez baadaye aliandika ujumbe kwenye Twitter: "Taarifa mbaya zimethibitishwa."

Wanahabari hao walitajwa kuwa David Beriain na Roberto Fraile, na kusifu "wale walio kama wao, wanaotekeleza kazi yao na wajibu wao muhimu wa uanahabari katika maeneo ya vita ".

Bwana Beriain alikuwa mwanahabari wa muda mrefu aliyekuwa ameangazia mambo mbalimbali ya dunia na kuanzisha kitengo chake cha habari, huku Bwana Fraile akiwa ameangazia migogoro chungu nzima kama mpiga picha ikiwa ni pamoja na Syria.

Maafisa wa eneo waliambia vyombo vya habari kuwa raia wa Ireland aliyekuwa anashika doria pia naye ameuawa.

Chanzo ambacho ni afisa mwandamizi wa usalama ameliambia shirika la AP kuwa raia watatu wa Ulaya "wameuawa na magaidi".

Katibu mkuu wa kundi moja la kutetea wanahabari amejibu ujumbe wa taarifa hizo katika mtandao wa Twitter na kusema kuwa: "kisa hicho kinathibitisha hatari inayowakabili wanahabari " barani Afrika eneo la Sahel.

Taarifa za kile kilichotokea kwa wanajeshi wa eneo waliokuwa wametekwa nyara hazikujulikana mara moja.

Kipi kimekuwa kikiendelea?

Matukio ya utekaji nyara yamekuwa yakitokea siku za hivi karibuni katika nchi hiyo ambayo ni koloni la Ufaransa ambako hifadhi za wanyama pori ni maarufu sana kwa watalii.

Lakini wengi wao wako katika eneo ambalo sasa hivi linalengwa na wanamgambo wa jihadi.

Wanamgambo wa makundi ya Kiislamu wanaaminika kuwashikilia mateka raia wengi wa kigeni huko Burkina Faso, pamoja na mataifa jirani ya Mali na Niger, shirika la habari la Reuters limesema.

Eneo hilo ambalo nusu ni jangwa la Sahel limekumbwa na wanamgambo tangu walipoteka eneo kubwa la kaskazini mwa Mali mwaka 2012 na 2013.

Ufaransa na washirika wengine wa kimataifa wamepelekwa wanajeshi wao katika eneo hilo lakini wameshindwa kumaliza matukio ya uvamizi wa wanamgambo.

Aidha, mapigano hayo yamesababisha watu karibu milioni tatu kuhama makazi yao.