Virusi vya Corona: Waafrika mashariki walio nchini wanapitia yapi wakati nchi hiyo inaposakamwa na janga la Corona?

Chanzo cha picha, Getty Images
India imelemewa na maambukizi ya virusi vya Corona na taifa hilo limevunja rekodi kwa maambukizi mengi kwa siku za hivi majuzi baada ya watu laki tatu kupata maambukizi ya virusi hivyo .
Hospitali nyingi katika jiji la Delhi pamoja na miji mingine mingi zimezidiwa na wagonjwa wa mlipuko wa corona, hali inayowalazimu watu kufanya mipango ya wagonjwa wao kutibiwa nyumbani.
India imekuwa ikiripoti zaidi ya wagonjwa 300,000 kwa siku, na idadi hiyo kubwa ya wagonjwa imeuzidi uwezo wa mfumo wa matibabu nchini humo. Siku ya Jumapili pekee, watu 2,767 walithibitishwa kufariki.
Kunao watu kutoka Afrika mashariki ambao janga hili limewapata nchini India na wanasimulia jinsi walivyoathiriwa .Kunao walioko nchini humo kwa masomo ilhali wengine wapo India kwa matibabu .

Chanzo cha picha, Edward Onantwa
Dkt. Edward Onantwa
Dkt Edward Onantwa ambaye ni Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Kenyatta nchini Kenya amekuwa nchini India kwa miezi minne akitibiwa saratani . Anasema amefaulu kupata matibabu lakini janga la Corona na hali ya ugonjwa huo nchini India imeathiri ubora wa huduma alizopewa .
Akiwa katika mji wa Calcutta ,Bengal Magharibi ,Dkt Onantwa anasema madaktari wengi nchini India wakiwemo wale waliofaa kumsaidia katika kumpa matibabu wamelazimika kutumiwa pia katika kuwasaidia wagonjwa wa Corona .
Gharama yake ya matibabu imeongezeka kwa sababu ya jinsi janga la Corona linavyoilemea India na hata amepata changamoto ya kununua tiketi ili kuweza kurejea Kenya baada ya gharama ya usafiri kupanda angalau mara tatu ya kiasi cha kawaida .
Mhadhiri huyo anasema hali halisi nchini India inaonekana kuwa mbaya hata kuliko inavyoonekana katika vyombo vya habari . Yeye mwenyewe anasema janga la Corona limemuathiri kwa njia mbali mbali kwa sababu kama mtu mwenye maradhi nyemelea yupo katika hatari ya kuambukizwa Corona na hivyo basi kila anapokwenda kumuona daktari lazima avalie barakoa .
Anasema barakoa inamzuia kupumua vizuri kwa sababu pia ana tataizo la kifua . Dkt Onantwa anaongeza kwamba alifaa kufanyishwa mazoezi ya kila mara lakini hilo sasa haliwezekano ili kumzuia asitangamane na watu wengi .
Madaktari wengi ambao walikuwa wakimshughulikia sasa pia wametakiwa kutoa msaada wao kwa wagonjwa wa Corona .

Chanzo cha picha, Joshua Boit
Joshua Boit -Kiongozi wa wanafunzi
Joshua Boit kutoka Kenya ni mwanafunzi nchini India na anasema kuna wanafunzi wenzake walioambukizwa virusi vya Corona. Amesema wamelazimika kuunda makundi ya whatsapp ili kuweza kuwasiliana .
Boit ambaye ni kiongozi wa wanafunzi anasema hali nchini humo imekuwa mbaya na kote ameshuhudia magari ya kuwabeba wagonjwa yakiwa na mitungi ya hewa ya oksijeni .
Anasema kulikuwa na sherehe ya kidini ya nchini India Kumbh Mela iliyowafanya watu wengi kukusanyika bila kufuata masharti ya mamlaka za afya na imelaumiwa kwa kuchangia kusambaa kwa ugonjwa wa Corona .
Boit anasea amekuwa akitumia usafiri wa pikipiki yake ili kufuatilia jinsi hali ilivyo katika hospitali mbali mbali katika maeneo ambako wakenya na waafrika mashariki wengine walioko India . Anasema wanafunzi wamefaulu kujiandikisha mitandaoni ili kuujulisha ubalozi wa Kenya kuhusu waliko na hali zao .

Chanzo cha picha, Denis Monda
Denis Monda - Mwanafunzi
Denis Monda anasomea katika chuo kuu cha Davangere katika jimbo la Karnataka nchini India ambako amekuwa huko wa miaka minne .Anasema jimbo hilo limetangaza marufuku ya kutotoka na hali imekuwa ngumu kwa raia wote wa kigeni ambao sasa wamelazimika kuhakikisha wanachukua tahadhari kuepuka kuambukizwa virusi vya Corona . Monda amesema pia kuna ubaguzi wa rangi hasa kwa watu weusi kwani wanapopelekwa hospitalini ,hawapewi kipaumbele .
Amesema tayari amewasilisha nambari yake ya mawasiliano kwa ubalozi wa Kenya ili kuweza kuwasiliana na wanafunzi wenzake ambao wapo nchini India . Ubalozi wa Kenya nchini India umewataka Wakenya wote walio nchini humo kujiandikisha na kujiunga na makundi ya whatsapp ili kuweza kuwasiliana kwa haraka panapotokea jambo la dharura .












