Mpishi huyu hajawahi kula chochote kwa kipindi cha miaka sita iliyopita

Iliyochapishwa

Loretta Harmes hajawahi kula chakula chochote kwa kipindi cha miaka sita lakini hilo halikumfanya kupoteza shauku yake ya kupika. Hata ingawa hawezi kuonja vyakula vyake, ana wafuasi wengi kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, ambako anafahamika kama 'nil-by-mouth foodie'.

Loretta alikula viazi vilivyookwa vyenye ladha tamu. Yeye na mama yake, Julie, walijua kuwa huu ndio mlo wake wa mwisho na kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.

Lakini punde si punde akaanza kusikia uchungu usio wa kawaida tumboni, kitu hivi kinamsokota tumboni kama ilivyokuwa kawaida anapokula au kunywa kitu. Na kitakachofuata ni maumivu kweli na kuwa mgonjwa huku akihisi kana kwamba tumbo lake litapasuka.

Lakini akaamua kusahau yote hayo na kufurahia na familia yake akiwa jikoni ambako amekuwa stadi wa mapishi tangu akiwa mdogo.

"Kukaa chini na kula pamoja na mama yake na dada yake alihisi kuwa kitu kigeni cha kufurahisha," amesema. "Kwa mara ya kwanza tukajitahidi kukiona kama ni kitendo cha kawaida."

Ulikuwa mwaka 2015 na Loretta, 23, alikuwa tayari akiishi kwa kunywa vinywaji tu kwa miaka kadhaa. Wakati huo anasema hata kushika kijiko na uma alihisi kuwa jambo lisilo la kawaida licha ya kutafuna kiazi na supu ya kuku iliyotiwa limau na kitunguu saumu.

Simulizi zake nyingi kuhusu chakula zilileta kumbukumbu ya familia kuwa pamoja.

Kila Alhamisi familia yake yote ingeenda kwa Mavis kula chakula.

Loretta anamkumbuka akiketi katika meza kubwa ya kula chakula wakifurahia mlo wao.

Loretta akiwa na miaka 11 tayari alikuwa anapikia familia yake chakula kila Jumanne usiku wakati ambapo mama yake alikuwa anafanyakazi usiku.

Alikuwa akifanya biashara ya kutengeneza watu nywele na wateja wake wakaanza kumzoea Loretta akiwa kila mara yuko saluni na kijiko chake akimpa mama yake chakula alichopika amuonjee.

Akiwa shule ya sekondari, alishinda mashindano ya upishi. Wakati wanafunzi walikuwa wanakwama katika mapishi yao, Loretta angepika bila matatizo yoyote kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Mama yake, Julie, anasea Loretta alikuwa na bado ni mpishi hodari. ''Alikuwa akitumia vyombo vyote jikoni lakini sikusema lolote kwasababu nilijua anavyofurahia kupika.''

"Alichokuwa anapenda kufanya Loretta, ilikuwa ni kutengeneza mlo kutokana na viambato vyovyote atakavyopata jikoni - alikuwa mbunifu sana," mama yake, Julie, amesema.

Alipokuwa na umri wa miaka 15, alipata ugonjwa wa anoreksia ambao unahusisha kukosa hamu ya kula lakini ulikuwa kwa chini ya mwaka mmoja. Pia akiwa kijana alikuwa akilalamikia sana matatizo ya tumbo mara kwa mara. Lakini kipindi hicho, bado aliweza kupika na kula.

Lakini akiwa na miaka 19, mambo yalianza kuwa mabaya.

"Hali ilibadilika ghafla - sikuweza kula chakula au kwenda msalani kabisa na katika kipindi cha miaka mitano iliyofuata hali ikawa mbaya hata zaidi, sikuweza hata kutoka kitandani," amesema.

Tatizo lilianza pale daktari aliposema kuwa kupungua mwili kwa Loretta huenda kumesababishwa na kurejea kwa tatizo la kutokula.

Kuna wakati uzito wake ulikuwa kilogramu 25 pekee na hapo ikawa ni lazima ajilazimishe kula ili kuongeza uzito hata ingawa kulimsababishia machungu kupita kiasi.

Kama haitoshi alijipata akipewa huduma za afya ya akili kwa kipindi cha miezi 18.

"Niliwaeleza mara kadhaa kuwa sababu ya mimi kupata msongo wa mawazo ni kwasababu ya matatizo yangu ya tumbo lakini hawakuniamini," amesema.

Pia msichana huyo alijaribu kujiua mara kadhaa kwasababu ya kukosa matumaini maishani na kuhisi kuwa hakuna dawa inayoweza kuponya machungu aliyo nayo.

Vyakula wanavyopewa hospitali walitakiwa kumaliza ndani ya kipindi fulani. Lakini baada ya muda huo kukamilika, Loretta alikuwa bado amesalia na chakula chake.

Wagonjwa walikuwa wanaketi kwenye chumba cha kula chakula na wengine wote wangeondoka na Loretta angesalia peke yake huku wahudumu na wagonjwa wengine wakimzomea kama njia moja ya kumharakisha kula.

Loretta alihisi kupiga mayowe hasa wakati wahudumu wamemzunguka.

"Nilitamani sana kupata amani moyoni mwangu," amesema.

"Nilipona kabisa tatizo la kutokuwa na hamu ya kula, lilikuwa somo maishani ambalo liligeuka na kuwa kifungo cha maisha."

Miaka mingi baadaye, Loretta akaja kubainika na ugonjwa wa kijenetiki ambao unaweza kujitokeza kwa namna mbalimbali.

Kilichobainika ni kuwa tumbo la Loretta lilikuwa limepooza kwa kiasi fulani na haliwezi kumeng'enya au kujitoa uchafu inavyotakikana. Na hivyo basi kumlazimisha kula ilikuwa kazi bure.

Dalili zingine za ugonjwa huo zilikuwa ni kipandauso, uchovu, moyo kupiga kwa haraka anaposimama au anapoketi, maumivu ya shingo na hatimaye akatakiwa kufanyiwa upasuaji.

Kwa wastani, inachukua miaka 10 hadi 14 mtu kubainika kuwa na ugonjwa huo, amesema daktari Alan Hakim kwasababu dalili zake zinatofautiana na huenda hata zisioneshe kuwa na uhusiano na ugonjwa huo.

Miaka sita tangu alipokula chakula chake cha mwisho, Loretta anajua kuwa hatawahi kula tena maishani mwake au hata kunywa maji tena.

Sasa hivi anatumia mfumo maalum wa lishe unaomaanisha kuwa kwa saa 18 kwa siku anakuwa kwenye lishe ambayo ipo kwa njia ya majimaji yanayopita kwa mpira kwenye mfumo wa kumeng'enya chakula na kuingia moja kwa moja hadi kwenye mfumo wa mzunguko wa damu. Mrija huo unapita kwenye kifua chake hadi katika mishipa mkubwa na unapitishwa hadi kwenye moyo.

Anaonekana katika akaunti yake ya Instagram ya the.nil.by.mouth.foodie, akizungusha kifuko chenye majimaji ambayo ni lishe maalum anayotumia. Inasemekana kwamba huwa anaomba wengine wamshikie lishe yake acheze densi usiku.

Lakini hakuna kisichokosa makosa. Hata uchafu kidogo tu unaweza kuharibu laini ya kupitisha lishe hiyo. Pia mara nyingi amekuwa akipata maambukizi yanayoweza kusababisha kiungo cha mwili kushindwa kufanya kazi au hata kifo.

Hata hivyo kabla Loretta kuwa mgonjwa, pia alikuwa kitandandani kwa kipindi kirefu. Mwili wake haukuwa na nguvu kabisa kiasi kwamba mifupa yake ilianza kuwa laini na dhaifu na siku zake za hedhi zikakoma kabisa. Lakini kibaya zaidi ilikuwa ni machungu yasiyo na kikomo.

"Mfumo huu wa lishe maalum umerejesha uzito wa mwili na kunipatia nguvu. Nilifurahi sana nilipoanza tena kuvaa nguo zangu kama kawaida wala sio kununua nguo za watoto," amesema.

Afueni aliyopata kumemfanya kuanza tena kuwa na ndoto yake ya kupika na wakati mwingine huingia jikoni akiwa na kiti chake cha magurudumu.

Kuwa mpishi ambaye hata hali chakula kumemfanya kuwa wa kipekee katika mtandao wa Instagram.

"Sababu inayonifanya sihisi vibaya kwasababu sili chakula ni kuwa nimepata afueni kubwa, na niko huru kutokana na maumivu niliyokuwa nikipitia kwa miaka mingi," Loretta amesema.

"Kupika ndio Faraja yangu - na kuwa jikoni ndio njia yangu ya kuwa mbunifu.

Karibu kumbukumbu zake zote wakati wa kupika chakula, dada yake, Abbie ndiye anayemkumbuka zaidi.

Abbie alishangazwa sana na machungu aliyokuwa akipitia kwasababu ya tatizo la kutokula kiasi kwamba akaamua kufanyakazi katika hospitali ya afya ya akili kwa ajili ya watoto.

Wakati wa chakula cha mwisho cha Loretta, Abbie alikuwa hapo na alipiga picha kwa kutumia simu yake akisaidia ionekane kuwa tukio la kipekee.

Mwaka 2019, mama yao, Julie na Abbie walimtembelea Loretta hospitali ambako alikuwa akipata nafuu. Lakini kwa bahati mbaya Abbie alifariki dunia kwa ajali ya barabarani akiwa anarejea nyumbani. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 23 pekee.

"Alikuwa amebadilisha maisha ya wengi na maisha yake ndio tu yalikuwa yameanza kung'ara," amesema Loretta.

Loretta anahisi kuwa dada yake alistahili kuishi kwasababu yao wote na hilo linamfanya awe na shauku ya kubadilisha maisha ya wengi.