'Rais Samia alipenda kusoma, baba yetu alimhimiza afaulu’. Familia yake yaeleza

    • Author, Halima Nyanza
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya urais nchini Tanzania, Watanzania wamekuwa na hisia na mitazamo mbalimbali juu yake.

Lakini familia yake na watu wake wa karibu wanamfahamu vizuri kuliko ilivyo kwa watu wengine .

Rashid Suluhu Hassan ni kaka wa Rais Samia anasema jitihada anazozionesha hii leo , alianza tangu akiwa mdogo.

''Alikuwa mtu ambaye ana ari ya kusoma, bidii ya kusoma, alikuwa anapenda kuambiwa soma uwe kama mtu fulani, unamuona kaka yako hapa kwasababu Baba yetu alikuwa mwalimu, hivyo openness alikuwa nayo tangu zamani sana kwa hiyo watoto wake alikuwa akiwaachia nafasi''. Alisema Bw. Rashid.

Kaka yake anasema hakuna yeyote kwenye familia aliyewahi kuwa na ndoto kuwa siku moja atakuwa kiongozi...

''Hakuna mtu alijua.. kama ingewezekana kumfufua marehemu Mzee Suluhu sasa hivi akaamka ukamwambia leo Samia ni rais atakushangaa sana''. Alisema Bw. Rashid

Mgeni Suluhu Hassan ni dada wa Rais Samia anasema hakutarajia mdogo wake kushika nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini Tanzania.

Lakini pia hakushangazwa pia kutokana na rekodi yake ya kushika nafasi mbalimbali akipanda hatua kwa hatua.

''Kapita kwenye nyanja nyingi akianza tangu chini kabisa, mpaka akawa mbunge, kaliongoza bunge la katiba pia, anaweza na anajitahidi kuweza na ataweza''.

Tumsaidie na kumshauri vizuri.'' alisema Bi.Mgeni

Umetimia mwezi mmoja sasa tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipokula kiapo kuitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19 mwaka huu.

Siku zake 31 madarakani zimesababisha gumzo ndani na nje ya nchi yake, akiwa mwanamke wa kwanza kuongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki, pamoja na aina ya utendaji wake wa kazi.

Lakini je, Mama Samia ni nani?

Kwa Watanzania wengi, jina la Samia Hassan Suluhu (61) lilipata umaarufu zaidi wakati alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba lililoteuliwa mwaka 2014.

Tanzania ilikuwa inaelekea kutengeneza Katiba mpya - baada ya kukamilika kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kupitia Tume ya Jaji Warioba na Mama Samia alikuwa amepewa jukumu la kuongoza mchakato huo kupitia Bunge la Katiba.

Kwa sababu bunge lile lilikuwa likionyeshwa moja kwa moja kupitia vituo mbalimbali vya runinga na Watanzania wengi wakiwa na kiu kubwa ya kujua nini kinaendelea - sura ya Samia ilianza kuzoeleka kwenye macho ya wengi na uwezo wa kuongoza ukionekana dhahiri.

Lakini hiyo ilikuwa taswira yake ya hadharani. Katika duru za kisiasa bungeni wakati ule, Samia alikuwa akifahamika kwa uwezo wa kuonyesha utulivu - hata katika nyakati ambazo hali ya hewa katika bunge hilo ikiwa imechafuka na pia kuzungumza na wote.

Muundo wa bunge hilo ulitaka viongozi wake wa juu watoke katika pande mbili za muungano na kwa vile mwenyekiti wa bunge hilo alikuwa ni hayati Samuel Sitta kutoka Tanzania Bara, nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliangukia kwa Mzanzibari Samia.

Hata hivyo, wengi hawakutarajia kwamba angetangazwa na aliyekuwa mgombea urais wa chama cha mapinduzi mwaka 2015, John Magufuli, kuwa mgombea mwenza wake kwenye uchaguzi huo.