Mpenda senene, mwenye Vitz na maana ya wateule wa Rais Samia

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi
  • Iliyochapishwa

Mwaka 2007, Wakuu wa nchi 11 za Maziwa Makuu walifanya uamuzi wa kuunda chombo kitakachotazama masuala ya Amani na Usalama katika eneo hilo. Kilitakiwa kuongozwa na mwanadiplomasia ambaye sifa zake hazina shaka.

Nchi mbalimbali zilituma watu wake kwenda kuwania nafasi ya Katibu Mtendaji ambaye ndiye hasa angekuwa kiongozi wa chombo hicho ambacho kwa lugha ya Kiswahili kinajulikana kama Taasisi ya Kongamano la Nchi za Maziwa Makuu.

Tanzania nayo ilipeleka jina. Hata hivyo, siku chache baadaye, zikaja taarifa kwamba mgombea kutoka taifa hilo hakuwa na mvuto na nchi jirani zilidai kwamba mgombea wa awali alikuwa "hatoshi".

Serikali ya Tanzania ikaamua kubadili mgombea na kumpeleka Balozi Liberata Mulamula. Upepo ukabadilika ghafla na mgombea huyo akawashinda wenzake kwa mbali sana.

Hivyo ndivyo namna Mulamula - ambaye ameteuliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wiki hii, anavyoheshimika katika duru za kimataifa.

Uteuzi wake kushika wadhifa huo - akiwa mwanamke wa pili tu kufanya hivyo katika historia ya Tanzania, una maana kubwa katika namba na katika mwelekeo wa taifa hilo kubwa la Afrika Mashariki chini ya Rais Samia.

Balozi Mulamula amezaliwa pacha na mwenzake na jambo moja ambalo rafiki zake wanalijua kuhusu mtumishi huyu ni mapenzi yake kwa senene -chakula maarufu kwa watu wa mkoa anaotoka wa Kagera.

Mabadiliko ya namba na mwelekeo

Katika Baraza la Mawaziri la hayati John Magufuli ambapo Samia alikuwa Makamu wa Rais , baraza zima lilikuwa na mawaziri wanawake wanne kati ya 23.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 17 ya mawaziri wote lakini kwa kumuongeza Mulamula, sasa kiwango hicho kimeongezeka kufikia takribani asilimia 22.

Katika taifa ambalo linapigania suala la kuwa na uwakilishi sawa baina ya wanawake na wanaume katika vyombo vya maamuzi, hatua hii - japo ni ndogo, ni mwendelezo wa safari ya kupanda juu kuelekea kunakotakiwa.

Wizara ya Mambo ya Nje pia ni mojawapo ya wizara zenye nguvu kubwa na uamuzi huo unaonyesha Rais Samia hatasita kuwapa wanawake wanaostahili nafasi kubwa wakati fursa zitakapojitokeza.

Balozi Mulamula anajulikana kwa uwezo na sifa yake kubwa kama mwanadiplomasia mbobezi na mnyenyekevu na uteuzi wake unaonyesha Rais Samia atakuwa tofauti na mtangulizi wake kwa kutumia wanadiplomasia katika maeneo ambako wanahitajika na si kutumia watu wanaoaminika na kiongozi.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kabla ya Mulamula, Profesa Palamagamba Kabudi ni mmoja wa wasomi mashuhuri wa sheria nchini Tanzania na sasa amepelekwa Wizara ya Katiba na Sheria.

Waziri mpya wa Fedha, Mwigulu Nchemba ni mchumi aliyesomea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Inaonekana, mwelekeo wa Samia utakuwa ni kuwaweka samaki katika maji badala ya kuwafundisha ndege kuogelea au samaki kupaa.

Ni akina nani wanawake wengine kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Samia?

Kuondoa Mulamula, wanawake wengine katika baraza la mawaziri ni Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu - Bunge, Vijana, Walemavu), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Ummy Mwalimu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -Tamisemi) na Dk. Dorothy Gwajima (Afya).

Jenista ni mwalimu kitaaluma lakini sasa anachukuliwa kama mmoja wa wanasiasa waandamizi wanawake hapa nchini.

Hiki ni kipindi chake cha nne bungeni na ingawa amekuwa machoni kwa umma kwa muda wa takribani miaka 20 sasa, si mwanasiasa mashuhuri ingawa kipaji chake kinaelezwa kuwa ndani ya siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Profesa Ndalichako ni msomi wa kiwango cha Shahada ya Uzamivu (PhD) na mwalimu kitaaluma na hana muda mrefu sana katika siasa - hiki kikiwa ni kipindi chake cha pili bungeni; akiingia kwa mara ya kwanza kwa kuteuliwa na Rais Magufuli.

Ummy Mwalimu ni mwanasiasa mwanamke ambaye heshima na nyota yake inaonekana kupaa kwa kasi.

Anatajwa kama mmoja wa wanasiasa wanaopendwa na Samia - yeye mwenyewe akizunguka naye katika maeneo mengi kumwombea kura wakati akiwania Umakamu wa Rais kwa mara ya kwanza mwaka 2015.

Gwajima ni daktari wa binadamu, akiwa amesomea taaluma hiyo Ulaya Mashariki na hii ndiyo mara yake ya kwanza kuwa mbunge kwa kuteuliwa kwake na Magufuli pia.

Kurejeshwa kwake katika nafasi hiyo na Samia kumewashangaza wakosoaji wake wengi ambao hawakufurahishwa na namna anavyopambana na janga la ugonjwa wa Corona.

Katika mabadiliko ya mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia wiki hii, hakuna aliyeondolewa katika baraza na badala yake kuna waliohamishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine.

Inaonekana Gwajima amepewa nafasi nyingine ya kuonyesha uwezo wake na Samia - kama ilivyokuwa kwa wengine na muda utaeleza namna gani atabadilika katika utawala mpya.

Bosi asiye na makuu

Uamuzi mkubwa zaidi uliofanywa na Samia katika mabadiliko hayo ni kumtoa Dk. Bashiru Ally kutoka nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi na nafasi yake kuchukuliwa na Balozi Hussein Katanga.

Bashiru, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM aliteuliwa na Magufuli kushika wadhifa huo takribani mwezi mmoja tu uliopita na wengi hawakutaraji kama mabadiliko hayo yangekuja mapema namna hii.

Hata hivyo, uamuzi huo umepokewa vema na wale walioamini kwamba yalikuwa ni makosa kumteua mtu aliyewahi kuwa mwanasiasa wa kiwango cha Bashiru - pasipo historia ya utumishi ya umma, kushika wadhifa huo.

Katanga, kwa upande mwingine, ni mtumishi wa umma ambaye amepita katika mfumo unaotakiwa na hajawahi kuhusishwa na chama chochote cha siasa.

Kwa wanaomfahamu, Katanga anafahamika kwa sifa ya uadilifu, msimamo na anayependa mambo kufanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Wakati akiwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, Katanga alijijengea heshima kwa watumishi wake kwa tabia yake ya kutokuwa na makuu na mara nyingi akitumia gari yake binafsi ya gharama nafuu kwenda au kurudi nyumbani wakati wa siku au saa zisizo za kazi.

Kama Bashiru alikuwa alama ya utawala wa Magufuli na maamuzi yake katika utumishi wa umma, Katanga ni alama ya Samia na ujio wake katika utumishi huo.