Samia Suluhu Hassan: 'Acheni kampeini za mapema za uchaguzi wa 2025'

Iliyochapishwa

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaonya wanasiasa ambao wanadhamiria kuwania viti mbali mbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2025, kuweka kando azma zao na badala yake kuwahudumia wananchi waliowachagua.

Akiongea katika Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma, wakati wa kuwaapisha mawaziri walioteuliwa hiyo jana, Bi Suluhu Hassan amesema kuwa sio jambo la busara ya wanaisasa kuanzisha kampeini za mapema kwani kwa kufanya hivyo kutahujumu juhudi za serikali ya kutoa huduma.

'Nafahamu 2025 iko karibu na kawaida yetu sijui kama Watanzania ama kote ulimwenguni inapoingia kipindi cha pili cha rais aliyepo watu kidogo mnakuwa ma lile na hili kuelekea mbele..nataka kuwaambia acheni.'

Rais Samia kuwakumbusha wanasiasa walio na nia ya kuwania nafasi mbali mbali kwamba rekodi yao ya utendakazi itawafuata katika masiaha yao yote .

''Lakini nalotaka kuwambia jingine ni kwamba rekodi yako inakuafuata katika maisha yako kuna wengine wamekosa hizi nafasi kwa rekodi zao tu ,lakini nataka kuwaambia kila yule mwenye nia ya 2025 aache mara moja'

Rais Samia aliyemrithi hayati John Magufuli wiki mbili zilizopita kama kiongozi wa nchi hiyo aliwaambia wanasiasa wanaolenga kugombea wadhifa huo kuwa watulivu Alisema ilikuwa mapema kwa mtu yeyote kuonyesha nia ya kuwa rais mwaka wa 2025, akionya kuwa atakuwa akiwatazama.

Rais Samia alikuwa makamu wa rais wa Magufuli kutoka Novemba 2015 na kuchukua ofisi ya Rais baada ya bosi wake kufariki dunia mnamo Machi 17, 2021.Kulingana na Katiba, Rais Samia atakamilisha kipindi kilichosalia cha miaka minne ya muhula uliofaa kuwa wa pili kwa hayati Magufuli na atastahiki kugombea muhula mwingine wa miaka mitano mnamo 2025 wakati Tanzania itakapofanya uchaguzi . Ingawaje rais Samia hakumtaja yeyote ,alisema anafahamu kuhusu kuwepo kwa kampeni za mapema.

Wakati huo huo Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba kwenda kupanua wigo wa kodi na kutengeneza walipa kodi wengi zaidi nchini Tanzania

''Mtengeneze walipa kodi wengi zaidi, trendi mnayo kwenda nayo sasa hivi ni kuua walipa kodi. Mnawaua wafanyabiashara mnatumia nguvu zaidi kuliko akili na maarifa kupata kodi

''Sasa wale mnao wakamua mkaenda kuchukua vifaa vyao vya kazi, mkafungia akaunti zao mkachukua pesa kwa guvu kwenye akaunti kisa sheria zina kuruhusu kufanya hivyo, akitoka hapo anakwenda kufunga biashara anahamia nchi ya pili mnapunguza walipa kodi. Nendeni mkatanue wigo wa walipakodi.'' Alisema Rais Samia.

Hapo jana Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya baraza la Mawaziri sambamba na kufanya uteuzi wa wabunge watatu.

Hii leo Mawaziri wanane wateule,na manaibu waziri wamekula viapo hivyo mbele ya Rais Samia

Akizungumza baada ya kiapo hicho Rais Samia amesema teuzi alizozifanya pia amezingatia uwepo wa pande mbili za Muungano wa Tanzania.

Aidha,katika kuhakikisha ufanisi unakuwepo ndani ya serikali Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kufanyia kazi serikali na kuepusha mizozano

''Fanyeni kazi kwa lengo moja kwamba tunawatumikia Watanzania, sisi ni watumishi wa Watanzania, na nitakuwa na kipimo cha mabega, nikiona mtu mabega yanazidi kupanda juu,nitajua huyu sio mtumishi, huyo anaenjoy juu ya kiti chake na ni jambo ambalo siritarajii, natarajia mawaziri nisikie mko huko na huko mkiwatumikia Watanzania'',Alisema Rais Samia.