Aliyekuwa mwanamuziki maarufu Kenya afariki dunia

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 1

Mmoja wa kaka pacha ambao walikuwa wanamuziki maarufu nchini Kenya Christian Longomba amefariki dunia.

Kifo cha Christian kilitangazwa jana usiku na pacha mwenzake Lovy Longomba, ambao kwa pamoja walikuwa wanamuziki wapendwa wakati wao miaka ya 2000 maarufu kama 'Longombas'.

Kaka yake Lovy Longomba alithibitisha kifo chake kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram.

Christian amekuwa mgonjwa tangu mwaka 2015 alipopatikana na uvimbe wa ubongo na kufanyiwa upasuaji nchini Marekani.

Marehemu Christian Longomba na kaka yake Lovy Longomba walivuma na vibao vyao kama Dondosa, Makofi, Shikamoo na Vuta Pumz.

Baada ya mapacha hao kuvuma nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 10, wakati ambao muziki ulikuwa haulipi sana, Longombas walihamia nchini Marekani ambako wameishi kwa miaka kadhaa.

Mwaka 2015, baada ya kupumzika kimuzika kwa muda mrefu wakiwa Marekani, kaka hao walijaribu kurejea tena kwa kuachia kibao kilichofahamika kama 'My Queen' ambacho ndio cha mwisho wao kukiachia kwa mashabiki wao, na Lovy akaokoka na kuwa mchungaji mjini Los Angeles.

Familia ya wanamuziki

Longombas wametoka familia yenye mizizi ya muziki.

Baba yao Lovy Longombas Snr. alikuwa mwanamuziki katika bendi maarufu ya Congo Super Mazembe iliyokuwa na makao yake mjini Nairobi miaka ya 1970 na 80.

Aidha, babu yao, Vicky Longombas alikuwa mmoja wa bendi ya TPOK Jazz.

Mwanamuziki maarufu wa muziki aina ya Soukouss katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Awilo Longomba ni mjomba yao na aliyekuwa mwanamuziki wa Deux Vulture, Nasty Thomas ni binamu yao.