Mahojiaono ya Meghan na Harry: Familia ya Kifalme 'haina ubaguzi' - Mwanamfalme William.

Duke wa Cambridge amesema kuwa "familia ya kifalme haina ubaguzi" katika maoni yake ya kwanza baada ya madai ya Duke na Duchess wa Sussex kupitia mahojiano ya kwenye televisheni.
Mwanamfalme William pia amesema kwamba bado hajazungumza na kaka yake lakini atazungumza naye.
Mwanamfalme Harry na mke wake Meghan walisema kuwa mtu katika familia hiyo alikuwa na wasiwasi juu ya vile mtoto wake Archie atakavyokuwa mweusi.
Kasri la Buckingham awali lilitoa taarifa kwamba limesikitishwa na madai hayo na litayashughulikia.
Taarifa hiyo ilisema, huenda "matukio yakatofautiana" lakini wanandoa wa Sussexes wataendelea kupendwa.
Wakati wa ziara yake katika shule ya Stratford, mashariki mwa London, Alhamisi, Mwanamfalme William aliulizwa na mwanahabari: "Je Familia ya Kifalme ina ubaguzi?"
Mwanamfalme huyo akajibu: "Sisi sio familia ya kibaguzi."
Alipoulizwa ikiwa amezungumza na Mwanamfalme Harry tangu alipofanya mahojiano na Oprah Winfrey, Mwanamfalme William alisema: "Hapana, Sijazungumza naye lakini nitazungumza naye."
Ziara ya Mwanamfalme William sio ya kwanza kujitokeza kwa waandamizi wa familia hiyo ya Kifalme tangu kufanyika kwa mahojiano - Mwanamfalme wa Wales pia alikuwa anaendesha shughuli zake mapema wiki hii.
Katika mahojiano ya kwenye televisheni, Meghan alimwambia Oprah kulikuwa na "mazungumzo yaliyoonesha wasiwasi juu ya vile mtoto wake [Archie] atakavyokuwa mweusi".
Wote Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan walikataa kumtaja kwa jina aliyetoa matamshi hayo - lakini Harry baadaye akaweka wazi kwamba sio Malkia waka Duke wa Edinburgh.
Wakati wa mahojiano hayo pia, Harry pia alisema kwamba ilimuumiza moyo kuona kwamba familia yake haikusema lolote kuhusu hilo.
Alipoulizwa na Oprah ikiwa wawili hao waliondoka Uingereza kwasababu ya ubaguzi wa rangi wa vyombo vya habari, Harry alijibu: "Hilo lilichangia pakubwa."

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mahojiano pia, Harry pia alizungumza kuhusu uhusiano wake na familia yake - hasa baba yake, Mwanamfalme wa Wales na kaka yake Mwanamfalme William.
Wakati fulani baada ya kuachana na majukumu ya kifalme, Harry alisema Charles "aliacha kupokea simu zangu".
Na kuhusu William, Harry alisema: "Uhusiano sasa hivi una 'pengo'. Na bila shaka mambo yatakuwa sawa kadiri muda unavyokwenda, nina matumaini."
Makazi ya Kifalme ya Buckingham yalitoa taarifa baada ya mahojiano ya mapema wiki hii kufuatia mkutano wa dharura uliohusisha waandamizi wa familia ya kifalme.
Takwimu kutoka Shirika la CBS nchini Marekani zaonesha kuwa karibu watu million 50 kote duniani walikuwa wanafuatilia mahojiano ya Oprah na wanandoa hao wawili.












