Kenya yapiga marufuku ununuzi wa mahindi kutoka Tanzania na Uganda

Chanzo cha picha, NTV
Kenya imepiga marufuku mara moja ununuzi wa mahindi kutoka mataifa jirani ya Tanzania na Uganda.
Kulingana na barua ilioandikwa na Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kilimo na chakula, Kello Harsama kwa Pamela Ahago ambaye ni Kamishna wa forodha katika mamlaka ya ushuru nchini Kenya KRA, ununuzi huo umesitishwa baada ya uchunguzi kubaini kwamba mahindi kutoka mataifa hayo mawili sio salama kwa matumizi ya chakula cha binadamu.
Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya uchunguzi kuhusu usalama wa chakula kinachoingizwa nchini Kenya .
''Matokeo kutoka kwa mahindi yalioagizwa kutoka Tanzania na Uganda yamefichua kwamba kuna viwango vya juu vya sumu ya mycotoxins na hivyobasi kufanya bidhaa hiyo kutofikia viwango vyake vya usalama wa chakula cha binadamu'', ilisema barua hiyo ikinukuliwa na gazeti la The Ciitizen Tanzania.
Milolongo mirefu ya malori ya kubeba bidhaa hiyo siku ya Jumamosi ilishuhudiwa katika mpaka wa Namanga baada ya mamlaka ya ushuru nchini Kenya kuyazuia kuingia nchini Kenya.
Kulingana na The Citizen Tanzania, akiwa katika wilaya ya Longido hii leo , naibu waziri wa kilimo nchini Tanzania Bashe alisema kwamba serikali ya Tanzania inachukulia marufuku hiyo ya mahindi kwa umuhimu mkubwa.
''Serikali inachunguza kwa makini marufuku na naweza kuwahakikishia kwamba serikali ya Tanzania itaendelea kutetea maslahi yake, Bashe alinukuliwa na gazeti hilo akisema.

Kulingana na bodi ya Kenya inayohusika na udhibiti, ukuzaji wa mimea , ununuzi wa bidhaa hiyo umesitishwa mara moja huku ikiendelea kuwasiliana na mataifa hayo mawili.
Habari hiyo itaumiza sana wafanyabiashara wanaotegemea kipato kutokana na mahindi hayo yanayouzwa Kenya.












