Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Othman Masoud: Kutoka kuenguliwa Uanasheria Mkuu mpaka kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Jina lake lilianza kugonga vichwa vya habari nje ya Zanzibar wakati Bunge Maalumalipokuwa akijadili rasimu ya katiba mpya mwaka 2014 wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Akiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar chini ya utawala wa Dkt. Ali Mohammed Shein, alitofautiana na msimamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika baadhi ya vifungu vya rasimu hiyo.
Kubwa zaidi ni kuhusu muundo wa Muungano unaopaswa kuwepo kati ya Zanzibar na Tanganyika. Othman Masoud hakukubaliana na muundo wa serikali mbili uliokuwa ukipigiwa debe na CCM na SMZ.
Alisimamia muundo wa muungano wa serikali tatu.
Wadadisi wa mambo wanaamini msimamo huo ndio uliomtia katika kashikashi katika majengo ya Bunge. Na ulifikisha tamati wadhifa wake wa mwanasheria mkuu kwa kuenguliwa Oktoba 2014.
Tukio hilo halikumfanya Othman Masoud asisikike tena, bali kinyume chake ulikuwa ni mlango uliomfungulia njia ya kufanya harakati akiwa huru.
Kipi kimempa umaarufu visiwani?
Ni mpole azungumzapo, wala haina sifa ya kufoka. Lakini anatajwa kuwa na msimamo usioyumba kwa yale anayoamini niya maslahi kwa Zanzibar. Na pia haogopi kuyasema yale yasiyo na maslahi kwa visiwa hivyo.
Moja ya nukuu yake maarufu anahoji, "hivi hatuoni haya kubaki hivi hivi kuwa manispaa wakati Zanzibar ilikuwa empire (dola)."
Akiashiria kuikumbushia historia ya Zanzibar wakati ikiwa ni eneo lote la mwambao wa Afrika Mashariki, na sasa vimebaki visiwa viwili pekee vyenye mamlaka ya ndani tu. Visivyotambulika kuwa nchi kamili kimataifa.
Tangu afukuzwe wadhifa wake ameandika makala nyingi katika tovuti na mitandao ya kijamii. Pia ameshiriki mijadala katika kumbi na mahojiano katika vyombo vya habari.
Nyingi ya shughuli hizo zilikuwa ni harakati za kutumia taaluma yake kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Ambao daima anaamini muundo wake hautendi haki kwa taifa hilo.
Unaweza pia kusoma:
Kwa wengi uzalendo huo ndio umemfanya kuwa maarufu katika medani ya siasa za visiwani. Hadi kuteuliwa kuwa mjumbe katika kamati ya ilani ya chama cha ACT Wazalendo, kabla ya jina lake kupendekezwa kuwa mrithi wa Maalim Seif.
Kwa taaluma yake ya sheria na uwezo mzuri wa kuuchambua Muungano, uwepo wake katika SMZ, huenda ukasaidia kupata was ufumbuzi zile kero za miaka mingi za muungano wa nusu karne sasa.
Othman na viatu vya Maalim
Katika mahojiano yake ya kwanza na chombo kimoja cha habari tangu atangazwe kuwa Makamu wa Kwaza wa Rais, Othman amesema:
"Zanzibar inastahili kuwa inapotakiwa kuwa, sio hapa ilipo sasa. Kulihitajika mashirikiano na uongozi bora. Kwa sasa kuna fursa ya aina yake kulifanikisha hilo."
Katika mahojiano hayo ameashiria kuwa na mtazamo sawa namtangulizi wake Maalim Seif, katika kuafiki aina ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi. Hasa panapohusika umoja wa Wazanzibari na maendeleo ya visiwa hivyo.
Hana historia katika majukwaa ya kisiasa. Hata siasa za upinzani hakuwa mshiriki wa wazi. Kwa maneno mafupi hajawahi kudhihirisha uwezo wake katika majukwaa ya kisiasa mbali yakutumia taaluma yake kuitetea Zanzibar.
Maalim Seif alikuwa mwanasiasa. Kaiogelea bahari hiyo tangu akiwa kijana mbichi. Kapita katika vyama kadhaa vya kisiasa, kuanzia chama tawala CCM, Chama cha Wananchi (CUF), hatimaye ACT Wazalendo .
Ingawa hoja ya kwamba Othman hana mizizi ya kisiasa, haiwezi kuwa kigezo cha kumfanya asiwe mrithi mzuri wa Maalim. Hoja hiyo inaonesha tu ile tofauti ya Maalim na Othman katika muktadha wa historia zao.
ACT Wazalendo ina vigogo wengi wenye historia ya muda mrefu na siasa za Zanzibar.
Nimemuuliza mwandishi wa habari na mchambuzi wa siasa, Abdulfatah Mussa, kwanini chama hicho kilipendekeza jina la Othman?
"Kwa sasa Othman alivyo, unaweza kusema kiutendaji ni chaguo bora kuliko Maalim mwenyewe kwa namna Maalim alivyokuwa kiumri. ACT Wazalendo yumkini wameangalia mbali pia kwa ajili ya urais 2025.
"Mshindani wa Rais Mwinyi anahitaji kuwa na vigezo kama vyake ili avutie wapiga kura. Othman amekidhi kama si zaidi. Na hata yeye Mwinyi hakuondokea kwenye majukwaa ya kisiasa katika nyadhifa za kichama, kwa hiyo Othman hatokuwana upungufu katika hilo."
Kwa hakika miaka yake mitano ya uongozi itaamua pia juu ya uwezo wake wa kisiasa. Kwa sasa ni mapema sana kutabiri ataziendeshaje siasa zake katika serikali ya umoja wa kitaifa.Hilo ni la kusubiri na kuona.
Historia yake ndani ya SMZ
Ni msomi wa sheria na ni nguli katika uwanja huo. Siyo mgeni katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amehudumu katika nafasi mbali mbali chini ya Marais watatu wastaafu.
Alianza kufanya kazi tangu utawala wa awamu ya tano wa Rais mtaafu Salmin Amour, akiwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utawala Bora na Sheria.
Chini ya utawala wa mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Amani Karume, Othman Masoud aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP).
Mwaka 2011, Rais mstaafu Dkt. Ali Mohammed Shein alimteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kabla ya kumtumbua 2014.
Othman Masoud Othman alishiriki kwa kiasi kikubwa katika kuandaa muswada wa marekebisho ya katiba ya Zanzibar. Marekebisho ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Ana shahada tatu za sheria, akianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, Chuo Kikuu cha London, Uingereza na Chuo Kikuu cha Turin, nchini Italia.