Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wasichana zaidi ya 300 wa shule ya sekondari ya Zamfara watekwa nyara Nigeria
Wasichana zaidi ya 300 wa shule ya sekondari wametekwa nyara na wanaume waliokuwa na silaha ambao hadi sasa bado hawajajitambulisha kaskazini magharibi mwa Nigeria jimbo la Zamfara, polisi imesema.
Maafisa wa usalama wamepelekwa katika mji wa Jangebe ambapo wasichana walichukuliwa na kundi la wanaume hao mapema Ijumaa.
Maafisa wa eneo wamethibitisha utekaji nyara huo lakini hawakutoa taarifa zaidi.
Hili ndio tukio la hivi karibuni la utekaji nyara watoto wa shule wiki za hivi karibuni. Mara nyingi magenge ya uhalifu huteka nyara wanafunzi wa shule ili kupewa fidia.
Takriban watu 42 wakiwemo wanafunzi 27 walitekwa nyara wiki jana katika eneo la Kagara jimbo jirani la Niger na bado hawajaachiwa huru.
Mwaka 2014 wasichana wa shule 276 walitekwa nyara kaskazini mashariki mwa Chibok na wanamgambo wa Kiislamu wa kundi la Boko Haram tukio lililovutia hadhira duniani lakini uvamizi wa hivi karibuni unashukiwa kuwa kazi ya magenge ya uhalifu.
Two years after the Chibok girls were kidnapped by Boko Haram militants, the BBC visits a town that lost 25 girl...
Utekaji nyara huo umetokea vipi?
Shambulio hilo lililotokea Ijumaa saa saba usiku saa za eneo, kundi la wanaume waliokuwa na silaha waliwasili katika shule ya sekondari ya serikali mji wa Jangebe wakiwa na magari aina ya pick up na bodaboda, mwalimu wa shule amezungumza na tovuti ya habari ya Punch.
Baadhi ya wanaume hao waliokuwa na silaha walivalia kama vikosi vya usalama vya serikali, ripoti hiyo imeongeza, na kuwalazimisha wanafunzi hao kuingia kwenye magari hayo.
Lakini wengine walioshuhudia wameliambia shirika la BBC kwamba wanaume waliokuwa na silaha waliwasili kwa miguu shuleni humo.
Wazazi waliokuwa wamejawa na wasiwasi walikusanyika nje ya shule hiyo huku wengine wakiwa wamefuata nyayo za watoto wao hadi msituni wakiwa na nia ya kuwaokoa, aliyeshuhudia amesema.
Mwalimu ameliarifu shirika la BBC kuwa wanafunzi 421 walikuwa shuleni wakati huo na ni 55 pekee ambao wamehesabiwa.
Taarifa ya polisi imesema kuwa maafisa wake na wanajeshi wamepelekwa eneo la Jangebe kutafuta wasichana 317 waliotekwa nyara.
Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limesema kuwa ''limekasirishwa na 'kusikitishwa na tukio hilo'' la utekaji tena nyara wanafunzi wengi nchini Nigeria likilielezea kama ''unyama'' na ''ukiukaji wa haki za watoto.''
Unaweza pia kusoma:
Nani amehusika na utekaji nyara huo?
Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na utekaji nyara huo lakini walioshuhudia wamezungumza na BBC Hausa na kuwambia kwamba wanaume waliokuwa na silaha karibu 100 waliingia shuleni humo Ijumaa asubuhi.
"Walivunja lango la shule na kumpiga risasi bawabu. Kisha wakaelekea hadi kwenye mabweni ya kulala ya wasichana hao na kuwaamsha huku wakiwaambia kwamba ni wakati wa kusali. Na kuwakusanya pamoja.
Kipindi hicho wasichana hao walikuwa wanalia na wakawachukua na kuelekea nao msituni. Pia kipindi wanaondoka nao walikuwa wanapiga risasi hewani," aliyeshuhudia amesema.
Makundi yenye silaha yanayoendesha shughuli zake katika eneo la Zamfara mara nyingi huteka nyara wanafunzi wa shule kwasababu ya fidia lakini makundi kama hayo yalipoteka nyara zaidi ya wavulana 300 kutoka eneo la Kankara jirani na jimbo la Katsina Desemba mwaka jana, baadhi ya taarifa zilidai kwamba kundi la Boko Haram, ambalo pia linaendesha shughuli zake kaskazini mashariki, limehusika na utekaji nyara huo.
Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa na baadaye wavulana hao wakaachiwa huru baada ya mazungumzo.