Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Kifo cha Maalim Seif na mwamko wa vita dhidi ya corona Tanzania
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Katika historia ya Tanzania, hakuna mwezi ambao taifa hilo limepoteza watu mashuhuri na wenye mchango tofauti ndani na nje ya serikali kuliko Februari 2021.
Huu ni mwezi ambao Tanzania imempoteza Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi, ambaye kitaratibu ndiye Mkuu wa Watumishi wote wa Umma wa taifa hilo. Mwezi huo umeshuhudia pia Tanzania ikimpoteza aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, ambaye Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, amemtaja kama mchumi namba moja wa Tanzania.
Ni mwezi ambao taifa limeshuhudia kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Shariff Hamad - pengine mwanasiasa mashuhuri zaidi wa Zanzibar katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Huu ni mwezi ambao watu ambao wamewahi kuwa mawaziri na watumishi wa ngazi za juu wa serikali kama vile Dk. Servacius Likwelile, Bakari Mwapachu, Arcardo Ntagazwa, Atashasta Nditiye na wengine ambao si mashuhuri kwa Watanzania wamepoteza maisha.
Februari 2021, unaweza kubaki kuwa mwezi mbaya kwa Tanzania kwa maana ya misiba mikubwa ambayo imewahi kutokea. Jambo baya kuliko yote ni kuwa hakuna ushahidi kwamba huu ndiyo mwisho wa upepo huu mbaya au labda ndiyo tunaelekea kubaya zaidi.
Vifo hivi vinatokea katika wakati ambao dunia nzima inatetemeshwa na kuumizwa na ugonjwa wa Corona. Kwa sababu Tanzania si kisiwa, kila anapofariki dunia mtu yeyote katika nyakati hizi na kifo chenyewe kikaonekana kuwa cha ghafla - ni rahisi kwa watu kuhusisha na ugonjwa huu mbaya.
Hata hivyo, miongoni mwa wote waliofariki dunia - kuondoa Nditiye aliyepoteza maisha kwa ajali ya gari, ni Maalim Seif pekee ndiye ambaye ilitangazwa kuwa alikuwa anaugua Corona.
Kuugua kwake kulitangazwa kupitia taarifa rasmi iliyotangazwa na chama chake cha ACT Wazalendo. Hilo halikuwa jambo la kawaida kufanywa na kiongozi wa juu wa serikali si Tanzania pekee bali Afrika nzima kwa ujumla.
Kwa kawaida, jambo la ugonjwa wa viongozi huwa ni jambo linalolindwa kwa usiri mkubwa na ndiyo sababu hatua ya Maalim Seif kujitangaza haikuwa ya kawaida na kuna ambao hawakuipokea taarifa hiyo kwa bashasha.
Jambo pekee la kujadili ni kama hatua hiyo ya Maalim Seif kujitangaza na hatimaye kufariki dunia limesaidia chochote katika namna ambayo Tanzania inapambana na ugonjwa huo.
Upekee wa Zanzibar na janga la Corona
Mmoja wa watu waliokuwa karibu na Maalim Seif katika siku za mwisho hapa duniani aliniambia kwamba uamuzi wake wa kujitangaza ulizingatia hali halisi ya Zanzibar anakotoka.
Katika nyakati hizi za Corona, kuna mambo mawili ya kipekee kuhusu visiwa hivyo ambayo ni muhimu kuyafahamu. Mosi kwamba Zanzibar inategemea sekta ya utalii kwenye uchumi wake.
Takribani theluthi mbili ya mapato ya visiwa hivyo hutegemea utalii na dunia nzima sekta hiyo sasa inahaha kwa sababu ya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya BoT, katika kipindi cha kati ya Julai hadi Desemba mwaka jana, SMZ ilifikia asilimia 60 tu ya malengo ya makusanyo yake katika kipindi hicho kwa sababu ya athari za Corona katika sekta ya utalii.
Makadirio yalikuwa kukusanya shilingi bilioni 492.6 lakini kilichokusanywa ni shilingi bilioni 295.
Namna pekee ya kupambana na ugonjwa huo na kuwapa watalii sababu ya kuchagua Zanzibar - kwa mujibu wa maono ya Seif, ni kuwa na uwazi na kuhakikisha taarifa muhimu kuhusu ugonjwa na wagonjwa zinatoka kwa wakati na kwa usahihi.
Jambo la pili linahusu idadi ya watu. Zaidi ya nusu ya Wazanzibari wote wanaishi Unguja na katika mkoa mmoja wa Mjini Magharibi. Hii maana yake ni kwamba kusambaa kwa ugonjwa huo ni hatari sana kwa sababu watu wengi wataumia.
Tanzania Bara inaweza kuhimili ukosefu wa mapato katika utalii kwa sababu bado ina madini kama dhahabu yanayoweza kuingiza fedha za kigeni.
Pia kuna mazao ya kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi. Zanzibar haina mbadala huo na ndiyo sababu Maalim aliamua kufanya alivyofanya.
Nini kimefuata baada ya vifo vya Maalim Seif na Kijazi?
Saa 48 baada ya kuzikwa kwa Maalim, SMZ kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk. Khalid Salum Mohamed, ilitoa taarifa rasmi kwa Umma kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Hiyo ilikuwa taarifa rasmi ya kwanza kutolewa na SMZ kwa Umma yenye lengo la kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Ni muhimu pia kufahamu kwamba hadi sasa Zanzibar haina Waziri wa Afya kwa sababu nafasi hiyo ilitengwa kwa ajili ya mwakilishi kutoka ACT Wazalendo na Rais Hussein Mwinyi bado hajateua mtu wa kushika wadhifa huo.
Kwenye msiba wa Kijazi - ambaye kifo chake na Maalim vilipishana kwa saa kadhaa; kulitokea jambo ambalo halikuwa limewahi kutokea katika kipindi cha takribani miezi sita nyuma.
Jambo hilo lilikuwa ni tukio la baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu wa wizara za serikali kuonekana hadharani wakiwa wamevaa barakoa.
Kwa Tanzania, ni kawaida kwa viongozi wa juu wa serikali kuonekana wakiwa hawajavaa barakoa na kuonekana kwa wachache kulileta picha tofauti ya uwajibikaji.
Siku moja baadaye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizungumza kwenye mazishi ya Kijazi yaliyofanyika Korogwe mkoani Tanga kwamba hakuna kiongozi aliyekatazwa kuvaa barakoa.
Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliweka mstari kwenye kauli hiyo ya Majaliwa wakati akihutubia waombolezaji kwenye msiba wa Bw.Likwelile aliposema kutoonekana hadharani kwa viongozi wakiwa wamevaa barakoa hakumaanishi kwamba wanamuogopa mtu au la bali kila mtu anachukua tahadhari kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu na kwa kuzingatia hali yake ya kiafya.
Kwa mujibu wa Tulia, wako viongozi ambao hawaonekani hadharani wakiwa wamevaa barakoa kwa sababu wana sababu za kiafya zinazowafanya wasivae lakini wanajikinga na ugonjwa huo kwa namna nyingine.
Tulia ambaye anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasiasa wapya wanawake wanaopanda ngazi kisiasa alikiri hadharani pia kwamba yeye binafsi amewahi kuugua corona mara mbili na hivyo hawezi kusema ugonjwa huo haupo.
Hizi zinaweza kuonekana ni hatua ndogo sana katika mapambano dhidi ya corona lakini katika taifa ambalo kuna wakati kuzungumza kuhusu ugonjwa huu ilikuwa inaonekana kama mwiko - bado ni hatua muhimu kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Ni matarajio ya wengi kwamba yeyote atakayeteuliwa na Dk. Mwinyi kuwa Waziri mpya wa Afya wa Zanzibar - pasi na shaka kutoka ACT Wazalendo, atakuwa na jukumu la kuendeleza pale alipoishia Maalim Seif na pengine kupeleka visiwa hivyo kule alikokuwa anataka iende kwenye jambo hili la vita dhidi ya corona.