Tamasha la Sauti za Busara laja kitofauti mwaka huu

    • Author, Munira Hussein
    • Nafasi, Reporter
  • Iliyochapishwa

Tamasha la sauti za busara limeanza visiwani Zanzibar, tamasha hili kwa kawaida hufanyika karibu wiki nzima, lakini kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, kwa mwaka huu linafanyika kwa siku mbili pekee.

Hata hivyo watazamaji wa tamasha hili hujuimisha watalii na wenyeji, kwa mwaka huu shamra shamra zinaonekana kupungua kutoka na idadi ndogo ya watalii.

''kwa upande wa watalii kwa mwaka huu si wengi kutokana na athari za corona na mazuio yaliyowekwa, hata kwa upande wa wanamuziki ambao walitakiwa kuja kutoka mataifa mengine ya Afrika imeshindikana kutoka na kufungwa kwa mipaka nchini kwao, kwa hiyo kuna wanamuziki kutoka maeneo matatu tuu nje ya Tanzania.'' Anasema Yusuph Mahmoud mmoja wa waanzilishi wa tamasha hili.

Tamasha lilopita, zaidi ya watu 29,000 walihudhuria kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Jitihada zipi zimefanyika kujilinda na maambukizi ya virusi vya corona?

''Kwanza tumeweka vitakasa vya mikono kila mahali ukiwa unafika kwenye tamasha hili, lakini pia tumepunguza siku za ufanyikaji wa tamasha ambao kwa mwaka huu ni siku mbili tuu.'' Anasema Yusuph.

Kwa upande wa wafanyabiashara wanasema kuwa tamasha la mwaka huu huwezi kulinganisha na miaka iliyopita, huku corona ikiwa ni sababu kubwa ya kuzorotesha biashara.

''Nadhani hali inaonekana kabisa, watu si wengi, ingawa kuna wageni wachache lakini kwa upande wa biashara si sana kama wakati uliopita, na corona imeathiri sana, kwa sasa kuna watalii wengi kutoka urusi na Ujerumani kidogo , zamani walikua wageni kutoka nchi nyingi duniani'' anasema Suleiman mfanyabisha.

Vikundi na wanamuziki 11 kutoka Tanzania bara na visiwani watashiriki katika tamasha hili, huku kutoka nje ya Tanzania kukiwa na wanamuziki kutoka nchi tatu, ambayo ni Algeria, Lesotho na Uganda.