Mawakili wasema wafuasi wa Trump walivamia bunge 'kwa hiari yao'

Donald Trump aliwashawishi wafuasi '' kuvamia Capitol'' tarehe 6 mwezi Januari

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Mawakili wa Donald Trump wamejibu mashtaka dhidi yake, wakisema wafuasi wa rais huyo wa zamani wa Marekani walivamia Bunge huko Washington DC tarehe 6 mwezi Januari kwa hiari yao.

Kesi ya Bw Trump katika Seneti inatarajiwa kuanza Jumanne baada ya kushtakiwa kwa mara ya pili na Baraza la Wawakilishi mwezi uliopita.

Ameshtakiwa kwa "kuchochea vurugu" katika hotuba kwa wafuasi kabla ya vurugu kutolea

Bw Trump anasema hatatoa ushahidi.

Watu watano, pamoja na afisa wa polisi, walifariki wakati kundi la wafuasi wa Trump liliposhambulia jengo la Capitol, na kulazimu wanasiasa na wafanyakazi kujificha kwenye ofisi.

Bwana Trump ndiye rais pekee wa Marekani katika historia aliyewahi kushtakiwa mara mbili na mmoja kati ya watatu tu ambao walishtakiwa kabisa.

Katika muhtasari wa kabla ya kesi uliotolewa Jumatatu, mawakili wa rais huyo wa zamani walisema kwamba nyaraka za FBI zimeonesha kuwa maandamano hayo yalipangwa siku chache kabla, ikimaanisha kwamba Bw Trump hakuweza kuhimiza vurugu hizo.

Wanasisitiza pia kuwa kesi hiyo ni kinyume na katiba kwa sababu Bw Trump ameacha kazi na sasa ni raia.

Wafuasi wa Trump nje ya jengo la Capitol

Chanzo cha picha, Getty Images

Mawakili walielezea kesi hiyo kama "ukumbi wa michezo ya kisiasa na maigizo ya Democrats ambayo yalikusudiwa "kumnyamazisha mpinzani wa kisiasa na chama cha wachache".

"Utaratibu huu wa mashtaka haukuwahi kutafuta haki," waliandika.

Democrat wanasema kukataa mara kwa mara kwa Bw Trump kukubali matokeo ya urais mwezi Novemba mwaka jana vile vile kauli kali katika hotuba yake kwa wafuasi tarehe 6 mwezi Januari - zilihimiza vurugu.

Mawakili wake wanasema kwamba Bwana Trump alikuwa akitumia haki yake ya uhuru wa kuzungumza.

Kundi la watu lilishambulia bunge tarehe 6 mwezi Januari

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika jibu lao wenyewe baadaye Jumatatu, wasimamizi wa kesi hiyo walisisitiza kwamba Bwana Trump "amewasaliti Wamarekani".

"Uchochezi wake wa uasi dhidi ya serikali ya Marekani- ambao ulivuruga ukabidhiwaji wa madaraka kwa amani ni jinai mbaya zaidi kikatiba kuwahi kufanywa na rais," ilisema taarifa yao.

Kitakachotokea Jumanne

Kesi hiyo inatarajiwa kuanza na mjadala wa saa nne na kisha kupiga kura ikiwa kesi hiyo ni kinyume na katiba.

Ikiwa itaendelea - kama inavyotarajiwa - midahalo ya wazi itaanza Jumatano alasiri na pande zote kuruhusiwa hadi saa 16 kila moja kwa uwasilishaji.

Hatahivyo, kwa Seneti kumtia hatiani Bw Trump theluthi mbili inahitajika ikimaanisha Warepublican 17 watahitaji kujiunga na wanachama wa Democratic 50 katika kura hiyo.

Tarehe 26 Januari, ombi la kutupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa ni kinyume cha katiba iliungwa mkono na Warepublican 45 kati ya 50 wa bunge la seneti