Wanajeshi, wanasiasa na waandishi wahukumiwa kwa jaribio la mapinduzi Burundi 2015

Iliyochapishwa

Mahakama ya juu nchini Burundi imeweka hadharani kwa mara ya kwanza hukumu ya kifungo cha maisha jela ya majenerali wa zamani wa jeshi la taifa hilo , wanasiasa , waandishi na wanaharakati kwa jaribio la mapinduzi yaliofeli 2015, hati za mahakama zinasema.

Watu hao 34 walitangazwa kuwa na hatia na kutakiwa kulipa faini ya US$780,000 kwa waathiriwa wanaoshirikisha chama tawala cha CNDD-FDD.

Hii ni kesi ya chuki na siri ya kisiasa, OnesimeNduwimana , waziri wa zamani wa mawasiliano ambaye pia naye amehukumiwa aliambia BBC.

Burundi iliingia katika msukosuko wa kisiasa baada ya jaribio la mapinduzi ya Aprili 2015 dhidi ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza, ambapo maelfu waliuawa huku mamia wakitoroka katika mataifa ya kigeni.

Waliopatikana na hatia

Jenerali Godefroid Niyombare ambaye aliongoza jaribio hilo la mapinduzi , Potien Gaciyubwenge aliyekuwa waziri wa ulinzi na Leonidas Hatungimana ambaye alikuwa msemaji wa rais Nkurunziza ni miongoni mwa wale waliopatikana na hatia, hati hizo za mahakama zinaonesha..

Wengine ni pamoja na makamu wa rais Bernard Busokoza , Muhisani maarufu na mkosoaji mkubwa wa serikali Marguerite Barankitse , Onesime Nduwimana , mwanachama wa upinzani aliye na makao yake Ulaya na waandishi kadhaa ambao walikuwa ni waandishi wakati huo wa mapinduzi.

''Kesi ya kundi moja la watu ambayo haioneshi jukumu la kila mmoja wao huku ikiwa hakuna hata mshukiwa mmoja aliyehudhuria , ni kesi ya chuki na maamuzi ya kisiasa ambayo yalipatiwa majaji kutia saini'', Onesime Nduwimana aliambia BBC Gahuza.

''Hii kesi ya kisiri inaonesha wazi hatua ya seriikali kutotaka kuifungua Burundi. Bob Rugurika, mwandishi na mkurugenzi wa redio ya kibinafsi iliopigwa marufuku nchini Burundi ambaye naye pia amehukumiwa katika kesi hiyo'', aliandika katika Twitter.

''Ni vigumu ,lakini hatutakubali iendelee hivyo'', bwana Nduwimana alisema kuhusu uwezekano wa kukata rufaa